Wednesday, November 8, 2023

WANUFAIKA MRADI WA KLIC WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA TEHAMA-TET

 

Na Andrew Chale,Dar es Salaam.

Shule zote nchini zilizonufaika na vifaa vya mradi wa KOREAN E-LEARNING IMPROVEMENT COOPORATION(KLIC) ulio chini ya Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan ya nchini Korea ya Kusini, wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA, wametakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri , kiusahihi na kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti,Habari na Machapisho waTaasisi ya Elimu Tanzania(TET), Bw. Kwangu Masalu leo tarehe 8/11/2023 katika shule ya Sekondari Kimbiji iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam katika ziara ya ujumbe wa watu kutoka korea ulipofika shuleni hapo kwa ajili ya kugawa vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia masomo pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo ya namna ya kuvitumia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo .

Mwakilishi wa walimu waliopo kwenye ziara hiyo kutoka nchini Korea Kusini, Bwana.Kim Chi Gon ameeleza kuwa , wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanakuza utumiaji wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini na kwani kwa sasa ulimwengu umebadilika sana hasa katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Twidike Ntima ameeleza kwamba shule hiyo kuwa moja ya shule za mfano wa kupata vifaa vya TEHAMA ni jambo kubwa ambapo imesaidia sana kwa walimu kuweza kufanya kazi kwa urahisi na kuwa endapo masuala ya TEHAMA yataendelea kusambaa nchi nzima basi wanafunzi nchini na walimu wataweza kupiga hatua katika masuala ya elimu.

Naye Mkuu wa shule hiyo Bi. Joyce Ndaona amesema kuwa kwa sasa walimu wa shule hiyo wamepata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa nchini Korea ya Kusini ambapo wameweza kupata ujuzi wa kurahisishiwa kazi hasa katika eneo la ufundishaji na kuwapa nafuu wanafunzi kutumia TEHAMA kwenye ujifunzaji tofauti na awali.

Hata hivyo ugeni huo wa walimu na wanafunzi ukiwa katika shule hiyo ya Kimbjiji, uliweza kujionea namna wanafunzi wanavyoonesha uelewa katika masomo yao ambapo waliweza kuonesha utaalamu wao kupitia masomo ya fikizia na Uchoraji na baadae wanafunzi hao kuweza kufanya mafunzo kwa vitendo.






WAFANYABIASHARA MKURANGA, KIBITI WAMSIFU SAMIA UHURU WA BIASHARA.

 

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

WAFANYABISHARA wilayani Mkuranga na Kibiti, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuliza dhorobu ya hali ya biashara nchini.

Wamesema kwenye wilaya hizo biashara zinafanyika kwa amani na utulivu bila usumbufu tofauti na miaka ya nyuma.

Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwenye mkutano kati ya wafanyabishara wa wilaya hizo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) inayoendelea mkoani Pwani yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wafanyabishara.

Mfanyabiashara Hassan Mbwana Kambangwa, amesema wafanyabiashara kwa asilimia kubwa wilayani humo wananufaidika sana tangu kuingia kwa utawala wa Rais Samia.

Amesema "Kimsingi namshuruku Rais Samia kwa kutuletea ugeni uliotupa fursa ya kuzungumza changamoto zinazotukabili, lakini sisi tangu kuingia kwa utawala huu wa Mama Samia tunafaidika nao kwa asilimia kubwa."

Mfanyabiasha huyo ametolea mfano wa mambo wanayofaidika nayo kuwa ni mikopo, uhusiano mazuri na halmashauri lakini pia taasisi mbalimbali za kifedha ziko huru kuwasaidia wafanyabiashara.

Amesema serikali imezingatia suala la amani na utulivu na kwa mikoa mingi ilikua inapata changamoto nyingi lakini hapa wilaya ya Mkuranga wafanyabiashara wako huru na wanafanyabiashara bila bugudha.

"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan tunafanyabiashara kwa amani lakini pia tunashukuru ujio huu wa leo umefanya tuweza kufunguka yale ambayo yako ndani ya moyo na tunaamini mtayafikisha," Kambangwa.

Naye mfanyabishara Wilaya ya Kibiti, Salim Juma, amempongeza Rais Samia kwa kuona sekta ya wafanyabishara ni sehemu ya uchumi wa Taifa na kuamua kuungana kwa pamoja kutatua kero zao.

"Ili kuwa na ustawi tumefanikiwa kumpa Rais Samia, ambaye ameona umuhimu wetu na kutambua mchango wetu ndio maana leo viongozi mpo hapa," amesema Juma.
Mwisho




BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA BAGAMOYO LAFANYA KIKAO CHAKE CHA KWANZA CHA ROBO MWAKA 2023

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo leo tarehe 8 Novemba 2023 limekutana na kufanya Kikao chake cha kwanza katika mfululizo wa vikao viwili vya Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, vikao ambavyo vimepangwa kufanya tarehe 8-9 Novemba 2023.

Katika Kikoa hicho Baraza lilipokea Taarifa za Utendaji kwenye ngazi ya Kata kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023.

Akipokea taarifa hizo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Mohemed Usinga aliwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Madiwani wa Kata zote kwa kazi nzuri walizozifanya katika kipindi hiki cha robo ya kwanza.

Aidha Mwenyekiti huyo aliagiza Madiwani pamoja na watendaji wa kata zote kutoanzisha miradi mipya ya maendeleo mpaka miradi iliyopo ikamilike, "Waheshimiwa Madiwani pamoja na Watendaji wa Kata hakikisheni mnamaliza miradi yote iliyokuwa haijakamilika kabla ya kuanzisha miradi mingine, tuhakikishe kwenye kata zetu tunamaliza viporo vyote vya miradi inayoendelea" alisema Mhe Usinga

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Majid Mhina alipokea maelekezo ya Baraza hilo na kwenda kuifanyia kazi. "Tumepokea maelekezo ya Baraza kwa ushirikiano wa Idara zetu na wataalamu tulio nao tunaenda kuyafanyia kazi" amesema Bw. Mhina 






ZAIDI YA WANAFUNZI 2,000 WANUFAIKA NA MRADI WA CAMFED CHALINZE.

 

Zaidi ya wanafunzi 2,000 wasichana wamenufaika na Mradi wa Kampeni ya Elimu kwa mtoto wa kike (CAMFED) Halmashauri ya Chalinze kuanzia mwaka 2016 hadi sasa.


Mkuu wa Kitengo cha Shule ya Sekondari, Madam Salama Ndyetabura akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Timu na Watoto wa Kampeni ya Elimu kwa Wanawake (CAMFED), katika mada iliyowasilishwa leo Tarehe 08 Novemba 2023, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Chalinze.


Madam Ndyetabura wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa CAMFED, alifafanua historia ya CAMFED katika Halmashauri ya Chalinze, Wanafunzi wakisaidiwa na CAMFED, CAMA network, miradi ya CAMFED katika Halmashauri ya Chalinze, Serikali na Ushirikiano wa CAMFED kusaidia elimu ya wasichana Chalinze.


Madam Ndyetabura aliendelea kueleza kuwa CAMFED Tanzania ilitekeleza miradi mingi ya kusaidia elimu ya mtoto wa kike na wanawake vijana kama msaada wa elimu ya Msichana, mradi ambao ulianza 2016 hadi sasa na kusaidia jumla ya wanafunzi 2,347, Vijana wa kike, mradi huu ulianza 2019 ambapo 72 wanawake waliopata mafunzo,14 walifanikiwa kukamilisha makubaliano yao ya miezi 12, na  4 waliacha shule.


Hata hivyo serikali kwa kushirikiana na CAMFED ilisaidiana katika harakati za kumlinda na kumsaidia mtoto wa kike kupata elimu na kumaliza masomo yake.


Halmashauri imeanzisha na kuimarisha sheria mbalimbali kwa mfano kusisitiza sheria ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya kijiji na kutumia mamlaka kwa maofisa watendaji wa vijiji (VEO) na maofisa watendaji wa kata (WEO) kushughulikia masuala yote yaliyoripotiwa yanayohusu ukatili dhidi ya watoto.





DC OKASH AIPONGEZA HALMASHAURI YA CHALINZE KWA UKUSANYAJI MAPATO

 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Mheshimiwa Halima Okash ametoa pongezi kwa Madiwani na wataalam wa halmashauri ya Chalinze kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika suala zima la ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri na kuvuka asilimia 27 ya malengo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.


Mheshimiwa Okash ametoa Pongezi hizo leo Tarehe 08 Novemba 2023 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.


Katika hotuba yake ya kutoa Salaam za Serikali amewataka madiwani na watendaji wa Halmashauri kuendelea na jitihada za ukusanyaji mapato ya ndani na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kufikia malengo ya ukusanyaji mapato ili kutoa huduma stahiki kwa Wananchi.


Okash Pia ametoa Pongezi kwa Halmashauri ya Chalinze katika suala zima la usimamizi wa mkataba wa lishe ulioiwezesha Halmashauri kushika nafasi nzuri kimkoa na kuwataka uongozi wa halmashauri kuifanya lishe kuwa ajenda ya kudumu kuanzia ngazi ya kitongoji mpaka wilaya.


Mkuu wa wilaya amewataka viongozi wa halmashauri kuzingatia utawala bora kwa kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa wakati kuanzia Kitongoji,kijiji na Kata ili kuweza kubaini changamoto na kero mbalimbali zinazoweza kutokea katika jamii na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati pasipo kuchelewa.


Aidha Okash ametoa rai kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze kuchukua tahadhali kutokana na mvua za Elinino zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Pwani hususan Chalinze, kwa kuondoka katika mabonde na kukaa maeneo yenye miinuko ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo.


Mkuu wa wilaya alimalizia hotuba yake kwa kuwataka viongozi wote katika Mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea kuisemea Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya katika kuboresha maisha ya watanzania kwa kujenga miundombinu mbalimbali katika sekta za afya,elimu,barabara na Maji ili watanzania wapate kufahamu yanayoendelea.


“Namshukuru Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuimarisha maisha ya watanzania,hususan wanachalinze kwa kuwaletea fedha zaidi ya Bilioni 2 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024 Mungu azidi kumtunza.” Okash alisema.









SERIKALI YAWATAKA WAWEKEZAJI KUJENGA VIWANDA VYA KUONGEZA THAMANI MADINI MKAKATI

 

Mahenge kunufaika na mradi wa madini ya Kinywe

Kuboresha sekta ya Maji, Afya na Miundombinu

Korea Kusini yaridhishwa na miundombinu ya Reli nchini

Na.Samwel Mtuwa- Dodoma.

Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa nchi ya Korea ya Kusini ikiwemo kuendeleza ushirikiano wa kikazi katika kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030:MadinI Maisha na Utajiri.

Hayo yamesemwa leo Novemba 8, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati wa mazungumzo ya ushirikiano wa kisekta baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini yaliyofanyika jijini Dodoma.

Wakati akizungumza na ujumbe huo kuhusu uwepo wa madini , Waziri Mavunde amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini mkakati kama vile madini ya kinywe, lithium , Nibioum na Makaa ya mawe ambayo kwasasa mataifa mengi yanatafuta kuwekeza huko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Waziri Mavunde amezikaribisha kampuni mbalimbali kutoka Korea ya Kusini kuja kuwekeza Tanzani na kuwaeleza kuwa kwasasa sekta ya madini nchini Tanzania ipo na vision2030 ambayo lengo lake ni kupata taarifa za utafiti ambazo zitatoa dira ya uwekezaji na uendelezaji kwa kufungamanisha sekta za kiuchumi.

Akielezea kuhusu kufungua kiwanda cha uchakataji madini ya kinywe na uongezaji thamani madini nchini Tanzania , Mkurugenzi wa Kampuni ya POSCO ya nchini Korea Ji Ki Chun amesema , baada ya kukamilisha uchimbaji wa madini ya kinywe wilayani Mahenge watafungua kiwanda cha kuchakata madini ghafi ya Kinywe na uingezaji thamani kabla ya kusafirisha nje ya nchi.

Chun amefafanua kuwa menejimenti ya POSCO imeridhika na hali ya miundombinu nchini ikiwemo reli ya kati pamoja ujenzi wa SGR.

Naye , Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Kim Sumpyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha uhusiano mzuri wa kiuchumi na serikali ya Korea Kusini amebainisha kuwa Korea Kusini ina mkataba wa hiyari katika ushirikiano wa kikazi ndani ya sekta ya madini hivyo itaendelea kutoa ushirikiano katika uwekezaji.

Balozi Sumpyo ameongeza kuwa mazingira salama na Sera nzuri zinavutia wawekezaji wetu na kuahidi kuendelea kuwaleta wawekezaji wengi kutoka nchini korea kusini kuja kuwekeza Tanzania.

Awali , akifungua mazungumzo hayo ya ushirikiano Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameimshukuru Balozi wa Korea kusini nchini Tanzania kwa uwekezaji mzuri katika sekta ya madini akitolea mfano uwekezaji katika madini ya Kinywe wilayani Mahenge.

Mahimbali amemuomba Balozi Sumpyo kuendeleza ushirikiana na kubadilishana uzoefu wa kisekta baina ya wataalam wa Korea kusini na wataalam wa sekta ya madini Tanzania.

VISION2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI










EWURA ZINGATIENI MASLAHI YA NCHI KATIKA SHUGHULI ZA UDHIBITI WA MAFUTA NA MAJI -DKT. BITEKO

 

Awapongeza kwa kushusha gharama za uagizaji mafuta.


Asisitiza EWURA kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji na Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuzingatia maslahi ya Watanzania na maslahi ya nchi katika kazi zao za Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ili Watanzania wapate huduma bora na kwa unafuu mkubwa.


Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika tarehe 8 Novemba, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.


“Tambueni kuwa Taifa lina mategemeno makubwa na ninyi, hivyo fanyeni kazi zenu kwa weledi na ubunifu mkubwa unaoendana na kasi ya teknolojia na maendeleo ya dunia; kanuni na miongozo yenu mnayotumia katika utekelezaji wa majukumu iundwe katika mifumo rafiki kulingana na hali iliyopo ili ilenge kuleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa na hivyo Watanzania waendelee kupata huduma bora na kwa gharama stahiki.” Amesema Dkt. Biteko.


Pia amewataka Watumishi wa EWURA kuweka mkazo kwenye kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi, kutoangalia maslahi binafsi wakati wa kutenda kazi ili kuepusha kuwaumiza Watanzania walio wengi, na ametoa wito kwa wafanyakazi hao kumkemea mtu yeyote anayeonekana kuwa na vitendo vya rushwa na ubinafsi katika eneo la kazi.


Vilevile, amewasisitiza Wafanyakazi wa EWURA kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa Watoa Huduma wanafanya ushindani wenye tija na ufanisi wa kiuchumi, kulinda maslahi ya Walaji na mitaji ya kifedha ya Watoa Huduma pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo ya watu wanaoishi vijijini.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu ameipongeza EWURA kwa kupitia upya gharama za uagizaji wa mafuta ambazo amesema kuwa, awali zilikuwa kubwa na zilikuwa zikipelekea athari mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa gharama katika Sekta ya Usafirishaji na Uzalishaji.


“Gharama hizi za uagizaji mafuta zilikuwa kubwa mno huku kukiwa hakuna sababu ya kuwa kubwa kwa kiasi hicho, niliwapa maelekezo mkazitazame upya, nashukuru mmeziangalia na ninafurahi kwamba zimeshuka na hivyo kupunguza makali kwa watumiaji." Amesema Dkt. Biteko.


Vilevile Naibu Waziri Mkuu ameiagiza TUGHE- Taifa kueleza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu masuala ya Wafanyakazi akitolea mfano upandishwaji madaraja wa mseleleko kwa watumishi ambao hawajapanda madaraja kwa muda mrefu. Amewataka pia kuwashirikisha wanachama wao ili kuisaidia Serikali katika kupeleka maendeleo kwa wananchi na pia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake kwa Wafanyakazi.


Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa, Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi lengo likiwa ni kuhakikisha Huduma za Nishati na Maji zinapatikana kwa uhakika, kwa kutosha, kwa uendelevu na kwa gharama ambazo wananchi wanazidumu.


Alimshukuru, Dkt. Biteko kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi hiyo na miongozo anayotoa ambayo inafanya EWURA iendelee kuboresha utendaji wake katika kuhudumia Watanzania.


Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA kinachoendelea jijini Dodoma kimelenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Bajeti ya EWURA kwa mwaka 2022/2023 na Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za EWURA za mwaka 2022/23.