Thursday, August 29, 2019

ASKARI WA USALAMA BARABARANI PWANI, WAPATA MAFUNZO KUTOKA ITDA.

Askari wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani wamepata Mafunzo kutoka kwa wataalam wa Chama cha Madereva Wasafirishaji wa Nchi za nje (ITDA).

Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakiibu wa Polisi (SP) Mosi B. Ndozero, alisema amefurahi kuona Mkoa wa Pwani umekuwa ni moja ya Mikoa ambayo imepatiwa Elimu hiyo ambayo itawasaidia Askari wa usalama Barabarani kuweza kumtambua Dereva anayeendesha gari husika na uelekeo wa gari hilo katika Nchi jirani.

Kwa upande wake afisa kutoka Chama cha Madereva Wasafirishaji wa Nchi za nje (ITDA), Solomon Kassa alisema mfumo huo utaongeza ufanisi katika kazi na uhakika katika kazi kwa ujumla kwa askari wa usalama barabarani ikiwemo kupunguza ajali za Barabarani zianazosababishwa na madereva (IN-TRANSIT VEHICLES) wasio na sifa Barabarani kwani kwa kutumia mfumo huu madereva wenye sifa ndio watakaoruhusiwa kuendesha magari ya IT.

Sambamba na hilo ameleeza kuwa Chama cha Madereva Wasafirishaji wa Nchi za nje (ITDA) kimedhamiria kuondoa vikwazo visivyo vya forodha ambavyo vipo Barabarani.

Aidha, askari wa usalama Barabarani Mkoa wa Pwani walishukuru maofisa kutoka Chama cha Madereva Wasafirishaji wa Nchi za nje (ITDA) kwa elimu waliyowapatia nakuahidi kwenda kuyafanyia kazi yale yote ambayo wameyapata toka kwa maofisa hao wa ITDA .

Jumla ya askari walioshiriki walikuwa 44, wawakilishi kutoka kila wilaya za Mkoa wa Pwani wakiwa ni watano, pamoja na ofisi ya RTO Pwani ambao wametakiwa kwenda kuwa mabalozi kwa wenzao kwa elimu waliyopata.

Mara baada ya askari hao kumaliza mafunzo hayo walienda Barabarani kufanya mazoezi kwa vitendo kwa kutumia mfumo wa kielectronic ambapo magari matano ya mfano yalibandikwa Bima ambayo namba ya gari kupitia taarifa ya Bima iliyobandikwa na Afisa wa ITDA inasomwa moja kwa moja kwenye system ya Google ( www.ITDA.co.tz//sticker_verification.php) kwa kumtambua dereva na maelezo yote ya gari anayoendesha na nchi anayokwenda.

Aidha, magari mengi ya IT yanayopita yaliweza kubainika yamebandikwa Bima feki toka Kariakoo kwa mawakala wa Clearing & Forwarding (C&F) kinyume cha utaratibu.

Elimu hiyo iliyotolewa kwa madereva itasaidia kubadilisha mfumo wa kimazoea wa magari ya IT kwenda mfumo wa teknolojia maridhawa kiasi ambacho dereva akifanya kosa/ajali nchini akielekea nchi yoyote ni rahisi kupatikana.

MUWEKEZAJI MTURUKI AMPIGA MFANYAKAZI WAKE KIBAHA.

Na Omary Mngindo, Kibaha.


Mkazi wa Kijiji cha Soga Kata ya Soga wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Kashinde Maonaje, amejeruhiwa eneo la shingo kufuatia kupigwa Kareti na muwekezaji Mturuki akiwa kazini kampuni ya yapiMarkezi.
 


Mkazi huyo amepigwa na Mturuki huyo ambaye ni bosi wame, akiwa kazini saa 4 usiku, baada ya kumkabili kiongozi huyo akimwelezea moja ya changamoto iliyopo, inayohusiana na utendaji wa kazi anayoifanya kitengo cha umeme.


Alisema kuwa akiwa katika eneo lake la kazi, kulijitokeza tatizo la kiufundi kuhusu umeme, ambapo alimfuata bosi huyo akamwelezea hali hiyo, lakini cha kushangaza alijikuta anapigwa kareti eneo la shingo, hali iliyomsababishia madhara makubwa.


"Ilikuwa usiku kulijitokeza tatizo linaohusiana na umeme kwenye kebo, nikamkabili bosi wangu, ghafla nikamuona amekunja uso, nikajikuta nimepigwa kareti shingoni, kama mnavyoniona hata kugeuka ni shida," alisema Maonaje.


Baada ya kujionea tukio hilo baya na la kusikitisha, MNEC Haji alisema kuwa hawezi kukubaliana na unyanyasaji huo na kueleza kwamba matukio ya aina hiyo yanazidi kushamiri katika maeneo ya kazi, huku akitaka hatua za kisheria lazima zichukuliwe.


"Hatuwezi kuvumilia unyanyasaji aina hii ukiendelea, tunawakaribisha nchini kwetu, tunawapatia ardhi, mwisho wa siku wanatunyanyasa kiasi hiki, haya ni manyanyaso yasiyovumilika, kuna maeneo mengine wa-Tanzania wenzetu wanabakwa," alisema Haji.


Mbali ya tukio hilo, Haji aliyeungana na MNEC mwenzake Bundalla Richard kutokea Shinyanga, alipokea malalamiko kuhusiana na kampuni ya Mohamed Dewj, kupitia shamba lake lijulikanalo kwa jina la A lave, linalohusiana na kilimo cha mkonge.


Diwani wa Kata hiyo Ramadhani Chezeni na wakazi wake walimweleza Haji kwamba, pamoja na kuwepo kwa usitishaji wa undelezwaji wa eneo hilo, bado kampuni hiyo inashughulika na upandaji wa mkonge, hali inayowapa sintofahamu kubwa.


"Hili suala limefika katika ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mkoa lakini mpaka sasa hatuoni kitu konachoendelea, tunakuomba MNEC lichukue ukamfikishie Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa Rais Dkt. John Magufuli," alisema Chezeni.


Baada ya taarifa hiyo alimpigia simu mbunge wa jimbo hilo Humoud Jumaa ambaye alimweleza kwamba suala hilo limefika kwa Waziri nwenye dhamana William Lukuvi, hivyo anaimani kuwa litakuwa katika hatua mbalimbali.


Kwa upande wake Haji alimuomba MNEC mwenzake amkumbushe watakapokuwa kwenye kikao chao mbele ya Mwenyekiti wao Dkt. Magufuli, ili amwelezee kilio hicho kinachodaiwa kudumu kwa zaidi ya miaka kumi sasa.


Haji aliyekuwa ziarani wilayani Kibaha, alianzia Kata za Gwata na Magindu, ambapo akiwa Gwata alikutana na mgogoro wa mifugo na mpaka wa vijiji vya Ndwati na Kigoda, ambapo aliwataka viongozi waumalize, kinyume chake ataufikisha wizarani ili vifutwe kiwe kimoja kama ilivyokuwa awali.

Monday, August 26, 2019

MGALU ATOA ONYO KWA MKANDARASI WA UMEME VIJIJINI KILIMANJARO

Image may contain: 1 person, crowd and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
...................................

Na Veronica Simba – Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering, ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti kwani njiti zimejaa na kitawaka.


Alitoa onyo hilo kwa nyakati tofauti Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.


Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.


Akielezea zaidi, Naibu Waziri alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.


“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake. Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”


“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,” alisema Naibu Waziri.


Kufuatia hali hiyo, alimwagiza Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”


Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 12.


Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.


Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.


Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai, pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha.
Image may contain: 2 people, people standing, hat and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
 Image may contain: one or more people and outdoor
Umati wa wananchi wakishuhudia tukio la uwashwaji rasmi wa umeme katika shule ya msingi Msamadi iliyopo wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro. Tukio hilo lilifanywa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.


AMUIBA MTOTO WA MIEZI 3 NA KUTOWEKA NAE.

Mtu asiyejulikana amemuiba mtoto wa miezi mitatu aitwae Swaum Saidi na kutoweka nae kusikojulikana.
Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, alisema tukio hilo limetokea Tarehe 25 agosti 2019 majira ya saa saba mchana maeneo ya Msongola wilaya ya kipolisi Mlandizi.


Alisema mama wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Mariam Shomari mwenye umri wa miaka 25 aligundua kuibiwa mtoto wake baada ya kurejea nyumbani kutoka kuomba kibiriti nyumba ya jirani.


Kamanda Nyigesa aliendelea kusema kuwa, mama wa mtoto huyo alienda kuomba Kibiriti kwa jirani yake umbali wa mita mia mbili na kwamba baada ya kurejea nyumbani hakumkuta mtoto wake ambae alimuacha chumbaani.


Alisema mwizi huyo wa mtoto alitumia mbinu ya kumdanganya mtoto mdogo wa miaka mitatu3, Fatma Saidi aliyebaki na mtoto huyo kwa kumwambia ametumwa kumchukua mtoto ili ampeleke kwa mama yake.


Mwizi huyo wa mtoto alifanikiwa kutekeleza kitendo hicho kiovu cha kuiba mtoto na kutokomea kusikojulikana.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mwizi huyo wa mtoto.


Kamanda wa Mkoa wa Pwani, anatoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata, wenyeviti wa vitongoji na vijiji na wananchi wote kwa ujumla, kutoa taarifa iwapo watamtilia mashaka mtu watakaemuona na mtoto ili akamatwe.