Wednesday, July 31, 2019

NDALICHAKO ASAIDIA SHULE YA NYAMPAKU, RUFIJI.

Na Omary Mngindo, Muhoro

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Profesa Joyce Ndalichako, kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA, ameipatia shule ya Msingi ya Kijiji cha Nyampaku sh. Mil. 60, kujenga vyumba vitatu vya madarasa shuleni hapo.


Shule hiyo iliyoko ndani ya Kata ya Muhoro wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, awali ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, hali iliyowalazimu wanafunzi kuingia darasani kwa zamu.


Akizungumza na Majira shuleni hapo, Mwalimu Mkuu Abdallah Simba alisema kuwa, mafanikio hayo yametokana na yeye kumwelezea Waziri Ndalichako, kuhusiana na changamoto hiyo, ambapo alimuunganisha na Mkurugenzi wa TEA ambaye ameiwezesha shule kupata kiasi hicho cha fedha.


"Waziri Ndalichako alifika nikamwelezea changamoto ya vyumba vya madarasa, akaniunganisha na Mkurugenzi wa TEA aliyetusaidia shilingi milioni 60 tulizojenga vyumba vitatu, tumekarabati darasa moja, tumechimba vyoo sanjali na kisima cha maji," alisema Mwalimu Simba.


Aliongeza kuwa awali shuleni hapo hali ilikuwa mbaya kutokana na kukabiliwa na changaamoto hiyo, ambayo baada ya kumwelezea Waziri huyo na kupatiwa fedha hizo walizojenga vyumba vitatu, kukarabati darasa moja, kujenga vyoo vya walimu sanjali na kuchimba kisima cha maji.


Mwalimu Mkuu Msaidizi Ziada Salumu alisema kuwa kwa sasa shule yao imeboreshwa, wanafunzi wanafurahia masomo ukilinganisha na hapo awali ambapo walikuwa wanaingia darasani kwa zamu kutokana na upungufu wa vyumba.


"Tunaiahukiru sana serikali yetu ya awamu ya tano kwa kutupatia fedha hizo ambazo zinetumika kikamilifu katika uboreshaji wa shule yetu, sasa hivi wanafunzi hawaji shule na maji, tunayo ya kutosha," aliasema Ziada.


Nae Selemani Omary alielezea furaha yake iliyotokana na mazingira yaliyopo hivi sasa shuleni hapo ikilinganishwa na hapo awali, huku akimshukuri Waziri Ndalichako.

WANANCHI WA UDINDIVU, MAPINGA BAGAMOYO WATENGENEZA BARABARA KWA NGUVU ZAO.

Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi wa Barabara vijijini na mijjini (TARURA) kuwajengea makaravati katika ujenzi wa Barabara unaoendelea kwa nguvu zao wenyewe.


Wananchi hao wametoa ombi hilo baada ya kutengeneza barabara kwa kuchangishana wenyewe ambapo wamekwama sehemu zinazohitaji madaraja.


Wakiongea na BAGAMOYO KWANZA BLOG katika eneo hilo, wananchi hao wamesema kwa muda mrefu barabara hiyo imekuwa haipitiki kutokana na ubovu wake hali iliyopelekea wananchi kujikusanya kutengeneza wenyewe barabara hiyo.


Walisema barabara hiyo ilikuwa imejaa mashimo, na kipindi cha mvua hujaa maji na kupelekea wananchi kushindwa kabisa kuitumia barabara hiyo.


Waliongeza kuwa, hapo awali gari zilikiwa haziwezi kupita hivyo hata kusafirisha wagonjwa kuwafikisha zahanati ilikuwa ni shida kutokana na hali ya barabara hiyo.


Barabara hiyo ni kiunganishi kati ya kata ya Mbweni jijini Dar es Salaam na kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo ambayo husaidia wananchi katika shughuli zao za kila siku.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Udindivu, Chandika Dismas alisema ujenzi huo wa barabara unagharimu shilingi milioni saba ikiwa ni michango ya wananchi.


Alisema wananchi wenyewe waliamua kuunda umoja wao ili kutengeneza barabara hiyo ambapo bajeti yake ni shilingi milioni saba na kwamba kazi inaendelea vizuri kutokana na wananchi wote wamekubaliana kwa kauli moja kuitengeneza kwa manufaa yao.


Aliongeza kuwa, pamoja na kazi hiyo kubwa iliyofanywa na wananchi, bado kunahitajika madaraja ambayo yapo nje ya uwezo wa wananchi na kwamba tayari wamewasiliana na Halmashauri ya Bagamoyo li waweze kuwasaidia sehemu zinazohitaji madaraja.

 
Kaimu meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa Barabara vijijini na mijjini (TARURA) wilaya ya Bagamoyo,Mhandisi Christopher Philip alisema wanatarajia kuiweka kwenye bajeti ijayo ili kuwaondolea adha wananchi wa Kitongoji hicho.

Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo, wakiendelea na kazi ya kutengeneza barabara katika kitongoji hicho.
Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo, wakiendelea na kazi ya kutengeneza barabara katika kitongoji hicho.

Monday, July 29, 2019

WAZIRI MKUU APOKEA VIFAATIBA KUTOKA SHIRIKA LA HHRD.

Na Hadija Hassan, Lindi.

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa amepokea msaada wa vifaa Tiba kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Helping Hand for Relief and Development (HHRD) inayojihusisha na utoaji huduma na Misaada kwa Maendeleo ya wananchi.


Vifaa vilivyotolewa ni vitanda vya kujifungulia akina mama wajawazito, Magodoro, Mashine za Matibabu na vingine mbali mbali kwa ajili ya kutolea huduma kwa wananchi wanao kwenda vituo vya kutolea tiba katika Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi.


Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo thamani yake inafikia Dola za Kimarekani 100,007 sawa na fedha za Kitanzania Sh,milioni 250. kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mbunge wa Ruangwa, Mwenyekiti wa wa Bodi ya taasisi hiyo, Yassir Salim Awadhi alisema ni moja ya kazi ya taasisi yao kuunga mkono juhudi za Serikali.


“HHRD ni wadau wa Maendeleo na ni mashuhuda kwa Serikali ilivyo na mikakati ya kuibadilisha Taifa hili liweze kusonga mbele katika Sekta zote, viwanda, Afya na Elimu ”Alisema Awdhi.


Mwenyekiti huyo alisema msaada huo utakuwa unasaidia katika kuboresha Afya kwa wananchi wa Wilaya ya Ruangwa na Tanzania kwa ujumla bila ya kujali itikadi walizonazo,huku akisisitiza kuendelea kushirikiana na Serikali katika masuala ya Maendeleo.


Awadhi alisema Shirika hilo,lisilo la kiserikali lenye makao makuu yake nchini Marekani, na Afrika hufanya kazi katika nchi (16), Ofisi ndogo ipo Nairobi nchini Kenya na kwamba hujishughulisha zaidi na changamoto za kijamii, wakiwemo yatima katika Sekta mbalimbali zikiwemo Afya, Elimu na matukio ya dharura.


Pia, alisema kwa Tanzania Shirika hilo la (HHRD) limejikita katika miradi mbalimbali, ikiwemo msimu wa ugawaji Nyama na Chakula kwa Jamii kipindi cha Mafuriko na kile kpindi cha maujaji wanaoenda Hijja.


Aidha alisema Shirika hilo kwa sasa linahudumia watoto yatima (250) Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani kwa kulipiwa mahitaji ya Shule, vikiwemo vifaa, Sare, Vitabu, Makazi, Chakula na Nguo za Sikukuu, upimaji Afya, Mafunzo na Malezi kwa wazazi na walimu.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mbunge wa Ruangwa amelishukuru Shirika la (HHRD) kwa msaada uliotolewa, huku akiendelea kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhudumia watanznia.


Majaliwa alisema msaada huo utakaogaiwa kwa vituo vyote vya Afya na Zahanati, utapunguza usumbufu kwa wananchi wenye matatizo kufuata huduma za matibabu mbali na maeneo wanayoishi.


Waziri Mkuu Majaliwa yupo Wilayani Ruangwa kwa mapumziko ya muda mfupi.

MHANDISI KILUMBI AMSHUKURU DKT. MAGUFULI

Na Omary Mngindo, Kibuta.

DIWANI wa Kata ya Kibuta wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Mhandisi Juma Kilumbi, ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli, kwa kuipatia Kata yake sh. Mil. 93,200 zilizotumika kujenga madarasa katani humo.


Sanjali na hilo pia amemshukuru Waziri Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo ambaye ni mbunge wa jimbo hilo kupitia mfuko wa jimbo kwa kuipatia Kata sh. Mil. 2, kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.


Aidha vijiji vya Mlegele na Mloo ndani ya Kata hiyo vimepatiwa fedha za ujenzi wa vyumna vya madarasa na matundu ya vyoo kwenye shule hizo, hatua inayolenga kuboresha sekta hiyo wilayani Kisarawe.


Kilumbi alisema kuwa Mlegele imepatiwa sh. Mil. 40.6 sanjali na shule ya Kijiji cha Mloo, ambazo zote zimepelekewa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule katika vijiji hivyo, ambavyo vyumba vyao vilikuwa katika hali mbaya ya kuendelea na utoaji wa elimu.


"Pia tumepokea sh. Mil. 294 kwa ajili ya uwekaji wa miundombinu wezeshi shule ya sekondari ya Kata, ambayo mwakani itakuwa ya kidato cha tano na sita, zitajenga majengo mapya ya madarasa, mabweni, bwalo na vyoo, sanjali na ujenzi wa Maabara ambapo tumepatiwa sh. Mil. 12," alisema Mhandisi Kilumbi.


Aliongeza kuwa kupitia mradi mkubwa wa ujenzia reli ya Mwendokasi inayojengwa na Kampuni ya Yapi Markez, wamenufaika kwa uboreshaji wa elimu katani humo, huku akimshukuru Mkuu wa wilaya hiyo Joketi Mwegelo, kwa kasi yake inayolenga kutokomeza ziro wilayani humo.


"Katika wilaya yetu kuna ushirikiano mkubwa kuanzia viongozi wa vijiji, halmashauri ya wilaya pamoja na viongozi wa ngazi zote, umoja huu unaounganishwa na mbunge wetu Jafo ndio unaoleta maendeleo katika nyanja zote," alisema Kilumbi.


"Katika mpango wa serikali kusukuma juhudi za sekta ya elimu katani kwangu vijiji vya Kauzeni, Mlegele, Mtamba na Mloo vimenufaika na fedha kutoka serikali Kuu na mfuko wa jimbo, kwaniaba ya wana- Kibuta tunashukuru sana" alimalizia Kilumbi.