Thursday, September 26, 2024

RAIS SAMIA AFUNGUA BARABARA YA MBINGA - MBAMBA BAY (KM 66) - RUVUMA




 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua barabara  ya Mbinga - Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Ruvuma, Septemba 25, 2024.


Ujenzi wa Barabara ya Mbinga - Mbamba Bay (km 66) umesimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara - TANROADS chini ya Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd kutoka China na Mhandisi Mshauri kutoka SMEC International Pty Ltd kutoka Australia kwa gharama ya Shilingi Bilioni 122.76.


Katika utekelezaji wa barabara hiyo, Kiasi cha shilingi Milioni 637.4 kilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi kwa mujibu wa sheria.


Barabara ya Mbinga - Mbamba Bay ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) yenye jumla ya urefu wa kilometa 826 inayoanzia Mtwara mpaka Mbamba Bay ambapo pia barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkoa wa Mbeya na nchi Jirani ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa.











Wednesday, September 25, 2024

JKCI YAENDELEA KUWA LULU UTALII TIBA AFRIKA

 

Madaktari wake waitwa Zambia kufanya upasuaji wa moyo


Na Mwandishi Wetu


 


Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya umeendelea kuipaisha Tanzania ambapo sasa madakati bingwa wanne wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI wako nchini Zambia wakiendelea  kufanya upasuaji wa moyo.


Timu hiyo ya madakari hao itashirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia na watafanyakazi upasuaji wa moyo kwa muda wa wiki moja .


Mkuu wa ujumbe huo, Dk Viviane Mlawi wa (JKCI),  ambaye ni daktari bingwa wa moyo kwa watoto, alisema  ujumbe huo pia umeambatana na mtaalam mbobezi wa chumba cha upasuaji na mtaalamu wa usingizi katika upasuaji Moyo.


Alisema wameambatana pia na mbobezi katika  kuhudumia wagonjwa wa nje wanaokuja kupata matibabu Tanzania,  Dk. Maiyer Msengi na wauguzi wawili ambao ni wabobezi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).


Dk Mlawi alisema malengo makubwa ya safari hiyo  ni matano ambayo ni kufanya upasuaji wa moyo kwa wahitaji ambao ni wengi nchini Zambia na kuwajengea uwezo madaktari wa Zambia mbinu za upasuaji ambazo bado hawajawa nazo na kubadilishana ujuzi.


Alitaja lengo lingine kuwa ni kukagua kwa pamoja na kubainisha maeneo ambayo Tanzania inaweza kushirikia na Zambia katika kuwasaidia wazambia matibabu ya kibingwa kwa wepesi na gharama nafuu.


Dk. Mlawi alisema madaktari hao watakagua na kubainisha vifaa tiba ambavyo vipo na vile ambavyo havipo ili kuweka mikakati ya jinsi gani wanaweza kushirikiana kuvipata ili kuboresha huduma zao.


Alitaja lengo lingine kuwa ni kuona maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika  tafiti, teknolojia na mambo ya msingi ambayo Tanzania iko  mbele sana katika eneo hilo kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.


Naye Dk. Maiyer ambaye ni mtaalam wa usimamizi wa wagonjwa kutoka nje ya nchi, alisema  yapo mambo mengi ambayo JKCI na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia wanaweza kuyafanya kwa kushirikiana kwaajili ya maendeleo ya nchi hizo mbili.


Alitaja masuala hayo kuwa ni kuhakikisha wanarahisisha utoaji wa vibali vya kuingia kwenye nchi hizo (visa), malazi kwa wanaotembelea nchi hizo na usajili wa mawasiliano ya namba za simu na vibali vya kwenda kupata matibabu.


Alisema kwa upande wa Tanzania watahakikisha kunakuwa na uhakika wa miadi ya kukutana na madaktari bingwa na kupata huduma kwa wakati ili kupunguza gharama za kuishi nchini kwa muda mrefu .


Alisema watahakikisha kunakuwa na huduma bora wakati na baada ya upasuaji wa wagonjwa wa moyo na kufanya JKCI iendelee kuwa kimbilio kwa mataifa mengi ya Afrika na kwingineko.


Alisema jambo lingine la msingi ambalo watahakikisha linazingatiwa ipasavyo ni uhakika wa gharama sahihi za vipimo na matibabu na usalama wa mgonjwa kwa kulinda haki zake zote akiwa anapata matibabu.


Alisema kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili katika utoaji wa taarifa  ubalozini hasa kwa kuzingatia kuwa kuna mahitaji makubwa ya watu kuja nchini kupata matibabu ya moyo.


Msemaji wa Hospitali ya Moyo ya Taifa ya Zambia, Dk. Chabwela Shumba alisema wamekutana na madaktari wa Tanzania na baada ya kufanya uchambuzi wa uwekezaji ambao serikali imefanya kwa JKCI wameona kwamba watanufaika kwa kiwango kikubwa kama watashirikiana na Tanzania.


“Tumeshangaa sana kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa  katika vifaa vya kisasa kama MRI, CT SCAN, rasilimali watu, teknolojia na kiwango kikubwa cha wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio makubwa,” alisema Shumba.


Alisema wamebaini kuwa JKCI inateklojia ile ile inayotumiwa na mataifa yaliyoendelea hivyo hakuna haja ya kuwapeleka wagonjwa wao kwenye nchi hizo kwani wanaweza kupata huduma kama hizo taasisi ya JKCI.






Tuesday, September 24, 2024

MAJID MWANGA AZINDUA SAMIA BODABODA DAY, MLELE.

 

Tarehe 23 September 2024 imekuwa ni siku ya neema na kukumbukwa kwa maafisa usafirishaji wa wilaya ya Mlele maarufu Kama bodaboda hii ni baada ya Ofisi ya mkuu wa wilaya ya mlele chini ya mkuu wa wilaya Mh Alhaj Majid mwanga kuandaa siku maalumu ya SAMIA BODABODA DAY iliyo fanyika halmashauri ya mlele shule ya msingi inyonga na kupambwa na kauli mbiu ya MIMI NI KIJANA WA SAMIA "nitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa November 27/ 2024



Siku hiyo maalumu ya boda boda Samia day imeyakutanisha makundi yote ya BODABODA kutoka pande zote za halmashauri ya mlele na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali Kama Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya mlele BI SIGILINDA MDEMU, Pia Wakuu mbalimbali wa taasisi, akiwemo mkuu wa kitengo cha usalama barabarani ambae alipata wasaa wa kutoa nasaha kwa madereva hawa wa bodaboda na kuwaasa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali mbazo zimekuwa zkijitokeza mara kwa mara kutokana na uzembe.


Akizungumza katika siku hiyo maalum ya SAMIA BODABODA DAY, Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga amewataka vijana wilayani humo kuweka kumbukumbu ya tarehe ya uchaguzi wa serikali za mitaa ili kila mmoja aweze kushiriki.



Alisema usoefu unaonyesha vijana wengi hawajitokezi kupiga kura jambo ambalo wanajinyima haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka ili wawaletee maendeleo.


Aliongeza kwa kusema kuwa vijana wa wilaya ya Mlele wanapaswa kutambua kuwa wana mambo matatu ya kufanya katika uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba.


Majid Mwanga, ameyataja mambo matatu hayo kuwa ni viajna waombe nafasi za kugombea nafasi za uongozi, wajiandikishe na kisha wakapige kura siku ya uchaguzi.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele Bi Sigilinda Mdemu, amesema ni matumaini yake kuwa vijana watajitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi wao 


Kwa upande wao vijana hao wa bodaboda wamesema wamefurahishwa sana na kitendo cha kuwakusanya pamoja na kufanya siku maalum kwao jambo lilioongeza upendo na mshikamano baina yao na serikali pia.


Aidha, wameomba ushirikiano huo uendelee kila siku na kujenga mahusiano mema baina ya waendesha bodaboda na mkuu wa usalama barabarani wilaya (DTO) ili vijana waweze kupata elimu ya usalama barabarani mara kwa mara.













SERIKALI YAIPONGEZA GREEN ACRES KWA KUENDELEA NA KUFANYA VIZURI KITAALUMA.

 

Na Mwandishi Wetu


SERIKALI imeipongeza shule ya msingi na sekondari, Green Acres ya jijini Dar es Salaam kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa kuanzia ngazi ya Wilaya hadi taifa.


Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu wa Wizara ya Elimu,  Sayansi na Teknolojia, Victor George, wakati wa mahafali ya 24 ya  shule hiyo  yaliyohusisha wanafunzi wa awali, msingi na sekondari.


“Nawapongeza sana kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma na nawashauri muendelee kuwekeza kwa wanafunzi hawa maana bila hivyo hatuwezi kuwa na taifa bora la kesho na mmeweka miundombonu mizuri ambayo inawawezesha kusoma kwa utulivu,” alisema.


Alisema serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele kwenye kuwekeza kwenye ngazi zote za  elimu kuanzia awali, msingi sekondari, vyuo vikuu vikuu vya kati ili watoto wanaopata fursa ya kwenda huko kupata elimu bora.


“Vijana huu ni mwanzo tu wa safari ndefu ya maisha, msione mmefika mwisho mnapaswa kuwekaa bidii sana katika masomo yenu kwa hiyo ili mpate mafanikio maishani lazima mhakikishe mnasoma kwa bidii sana,” alisema


Aliwataka wazazi waendelee kuwa karibu na wanafunzi hao kwa kuhakikisha wanasoma kwa bidii kufikia elimu ya vyuo vikuu ili waweze kufikia ndoto zao.


Alisema amefurahi kuona vipaji mbalimbali vilivyoonyeshwa na wanafunzi wa shule hiyo kwenye maonyesho ya kitaaluma hali inayoonyesha kwamba walimu wa shule hiyo wamefanyakazi kubwa kuwaandaa.


“Hata matokeo yenu ya kuanzia shule ya msingi na sekondari yamekuwa mazuri mwaka hadi mwaka nawapongeza sana mmekuwa mkifanya vizuri kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Kitaifa msibweteke endeeni kufanya vizuri zaidi,” alisema


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Green Acres,  John Pinda alisema wanafunzi wa shule hiyo kuanzia awali, msingi na sekondari wameandaliwa vizuri na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kitaifa.


Alisema wamefanikiwa kutengeneza chumba cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, maktaba kubwa ya kisasa, uwanja wa kisasa yote hiyo katika kuongeza mnyororo wa thamani wa elimu.


  “Wizara imeelekeza kila shule iwe na darasa la TEHAMA sisi tumeshakamilisha kwasababu tunataka wanafunzi wawe na uwezo wa kujua masuala mbalimbali ya teknolojia ya kisasa duniani kwa hiyo tunakwenda na wakati,” alisema






RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI MTYANGIMBOLE KWA NIABA YA MIRADI 30 YA MAJI MKOA WA RUVUMA.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt,Samia Suluhu Hassan leo September 24,2023 ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji Mtyangimbole Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma kwa niaba ya Miradi 30 ya Maji inayotekelezwa Mkoani humo.

Mradi wa tank la Maji Mtyangimbole una uwezo wa kupokea Lita milioni 1.9 na utahudumia Wananchi takribani 14,000.













NAIBU QADHI MKUU AMPONGEZA SHIRAZI KWA KUJENGA MSIKITI DAR ES SALAAM.

 

Na Mwandishi Wetu


Naibu Qadhi Mkuu, Ali Khamis Ali amempongeza mfanyabiashara Shiraz Rashid kwa kujitolea kujenga Msikiti wa Imam Ali Bin Abu Talib eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.


Alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa Msikiti huo hafla ambayo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali mbali wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao.


Alisema lengo la kujenga Msikiti huo ni kuhudumia waumini kwenye ibada ya swala tano na aliwashauri watanzania wengine kuiga mfano huo kwani hiyo ni kazi ya MwenyeziMungu.


“Tunatoa wito watu wengine waige mfano wa Shiraz ili tujenge nyumba za ibada kwani nyumba hizi zinasaidia kurejesha utulivu na amani kwa watu kufanya ibada, huu ni moyo wa upendo wa ndugu yetu aliouonyesha kwa hiyo natoa wito kwa wengine waige,” alisema


Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh, Walid Kawambwa, alisema ujenzi wa Msikiti huo ni jambo jema na kuwataka watu wengine kuanzisha ujenzi kama huo kwani hiyo ni kazi ya MwenyeziMungu.


“Mtume alipoingia Madina alijenga Msikiti kwanza kwa maana kwamba ile ni sehemu ya Waislamu kukutana na kujadiliana na washirikiane kufanya mambo yao pale kwa hiyo namshukuru Shiraz kwa kunialika kuja kwenye ufunguzi huu,” alisema Sheikh Walid







Picha mbalimbali za ufunguzi wa Msikiti wa Imam Ali Bin Abu Talib eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam, 

Sunday, September 22, 2024

WATOTO 1,500 WENYE MATATIZO YA MOYO WASUBIRI MSAADA.

 

Kikwete kuongoza harambee matibabu yao mwezi ujao

Na Mwandishi Wetu

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuongoza harambee ya kuchangia matibabu ya watoto 1,500 wanaougua magonjwa mbalimbali ya moyo ili wapate matibabu kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).


Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Naibu Spika wa Bunge, Musa Azzan Zungu, wakati akizungumzia harambee hiyo inayotarajiwa kufanyika tarehe 2, Novemba mwaka huu kwenye hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam.


Alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa, wawili wanakuwa na matatizo ya moyo na kwamba hadi sasa watoto 1,500 wameandikishwa kwaajili ya kupata matibabu hayo lakini hawana uwezo.


Naibu Spika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Heart Team Africa Foundation, alisema watoto hao wasipopata matibabu hayo kwa wakati wanaweza kupoteza maisha hivyo aliwaomba watanzania kujitokeza wakati wa harambee hiyo kuwachangia matibabu.


“Nawaomba watanzania tuungane kumuunga mkono rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuimarisha huduma za mama na mtoto. Serikali yake imekuwa ikichangia asilimia 70 ya gharama ya matibabu kwa watoto wanaozaliwa na mataizo ya moyo kwa hiyo ni wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais wetu,” alisema


Alisema watoto wengi wenye matatizo hayo wanatoka katika familia zisizo na uwezo hivyo aliomba taasisi na mashirika mbalimbali kujitokeza kusaidia juhudi za Rais Samia kuwagharamia matibabu watoto hao ili wakatibiwe (JKCI).


Alisema JKCI kwa kushirikiana na taasisi ya Heart Team Africa Foundation wameandaa harambee hiyo kwa ajili ya kukusanya asilimia 30 ya matibabu ya watoto hao ambayo ni sawa na shilingi milioni nne kwa kila mtoto atakayetibiwa.


“Nawaomba watanzania wote, wafanyabiashara, taasisi binafsi na za umma, vilabu vya michezo, wasanii, mabalozi wa nchi mbalimbali na vyombo vya habari tuunge mkono juhudi hizi za Rais Samia Suluhu Hassan katika harambee hii ya kuokoa maisha ya watoto wetu yenye kauli mbiu ya tia nuru, gusa moyo lete matumaini kwa watoto,” alisema


Naye Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dk Peter Kisenge alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya kwa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu kwa hospitali zote kubwa nchini pamoja na kusomesha wataalamu bobezi.


Alisema madaktari  bingwa wa JKCI wamejiandaa kutoa huduma bora za upasuaji kwa watoto na watu wazima watakaokwenda kupata matibabu ya moyo kwenye taasisi hiyo na kuhakikisha maarifa ambayo wataalamu wa taasisi hiyo wameyapata yanawasaidia watanzania na nchi jirani.


“Katika  ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati JKCI imeendelea kuwa ndiyo hosptali kubwa na ya kutegemewa yenye vifaa vya kutosha, yenye  madaktari bingwa wa kutosha na ambayo mafanikio ya wanaokuja kupata tiba kwetu ni kubwa sawa sawa na wanaopata matibabu nchi zilizoendelea ndiyo maana madaktari bingwa duniani wanapenda kuja hapa nchini kufanyakazi na JKCI,” alisema


Dk. Kisenge alisema uboreshaji wa huduma za afya nchini umewavutia wagonjwa wa nchi mbalimbali ambao wamekuwa wakija kwenye (JKCI) kupata matibabu ya kibingwa.


“Namshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa maono makubwa aliyonayo kwenye sekta ya afya kwani ameendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya ambapo mabadiliko makubwa sana yametokea kiasi kwamba vifaa vya kisasa ambavyo tulilazimika kuvifuata nje ya nchi sasa vinapatikana kwenye hospitali zetu nchini,” alisema


MACHIFU WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUENZI UTAMADUNI.

 

Wasema atasaidia kurejesha maadili yanayoendelea kuporomoka


Na Mwandishi Wetu


VIONGOZI wa Kimila kutoka mikoa mbalimbali nchini, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Tamasha la Utamaduni la Kitaifa pamoja na kuongeza thamani ya viongozi wa mila iliyoonekana kushuka kwa miaka mingi.


Wamesema hatua hiyo ya kuthamini, kufufua misingi na kuenzi tamaduni zilizokuwa zimeanza kuwekwa kando itasaidia kwa kiwango kikubwa kulinda maadili na tamaduni za Kitanzania.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Ruvuma linakofanyika kongamano hilo la tatu la utamaduni la kitaifa, viongozi hao wa kimila wamesema kwa miaka mingi mila na tamaduni za Kitanzania zilionekana kutokuthaminiwa lakini Rais Samia ametambua umuhimu wake na kufufua.


“Tunamshukuru Chifu Hangaya (Rais Samia), yeye kama kiongozi namba moja wa Machifu wote Tanzania, ameona umuhimu wa kuenzi mila na tamaduni zetu ambazo zilikuwa zimeachwa kupewa kipaumbele sana, kwa kifupi ni kwamba amezifufua na kuupa thamani kubwa utamaduni wa Mtanzania, na kwa kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu, tunaamini maadili ya nchi yetu yatalindwa zaidi,”amesema Chifu Nyamironda, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Machifu Tanzania.


“Leo hii viongozi wa kimila wanakaa pamoja, wanajadili mstakabali wa taifa lao, hili  ni jambo jema sana na tunaamini hili litazidi kulinda pia utulivu na amani kwenye nchi yetu kwa sababu viongozi wa kimila wana nafasi na nguvu kubwa kutoka kwenye jamii zao wanazoziongoza.”


Belinje Yasini, Mwenyekiti wa Machifu mkoa wa Dodoma, amesema kati ya tunu ya kujivunia ni kuwa Mtanzania na kwamba, umoja na mshikamano uliopo mpaka sasa, unapaswa kulindwa zaidi.


“Amani, umoja na mshikamano tulionao ni vya kulindwa sana kwa sababu kuna baadhi ya mataifa yanatamani kuwa kama sisi lakini hayawezi, sisi tunakaa pamoja, tunazungumza lugha moja, ni wakarimu, wenye upendo na utulivu licha ya kuwa tuna makabila mengi, lakini bado tunadumisha na kulinda umoja wetu tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine,”anasema Chifu Yasini.


“Yaani tungekuwa na ukabila, tukabaguana, tukatengana, tungeenda kuishi wapi, lakini taifa teule, lililobarikiwa kuliko mataifa yote, tunamshukuru Mungu bado tumezidi kuwa na mshikamano na amani, ni vema tukaendelea kulinda tunu hii ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu."


Chifu Yasini alisema kitendo cha Rais Samia kutambua mchango wa viongozi hao wa dini ni jambo jema na anapaswa kupongezwa na kuungwa mkono kutimiza azma yake ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kulinda tamaduni na maadili yake.


“Tumekuwa na viongozi wengi waliopita katika nafasi hiyo ya Rais, lakini hawakuzipa nguvu kubwa tamaduni zetu kama ilvyo kwa Rais Samia, kwa hiyo tunamsifu katika hili, tumuunge mkono ili kurejesha tamaduni zetu na kupambana na tamaduni potofu zisizo zetu ambazo zimeanza kuchangia mmonyoko wa maadili kwenye taifa letu,”alisema Chifu Yasini.


 “Tushirikiane na Rais Samia kupambana na vitendo vinavyochangia mmomonyoko wa maadili katika taifa letu, yeye ameonyesha njia na sisi tufuate.Tunapoona leo kuna unyanyasi, ukatili wa kijinsia na vitendo vingine vinavyotokea sasa, kazi ya kupambana navyo siyo ya serikali pekee, ni ya sisi sote jamii,” alisema


Alisema viongozi wa mila wana mchango wa kipekee katika kujenga taifa lenye mshikamano, amani, utulivu na kuchangia katika maendeleo endelevu yanayozingatia urithi wa kitamaduni na maadili ya kitaifa.


Chifu Yasini alisema viongozi hao wa kimila wamekuwa hawashirikishwi kwenye mambo mengi kwa kutokuthamini umuhimu wao.


“Unakuta mtu anatoka mbali huko anakuja anakusanya watu kupiga kampeni lakini kiongozi wa mila wa eneo husika hashirikishwi na ndio maana wakati mwingine baadae huwa mambo yanakuja kutugharimu au kuharibika, kwa hiyo thamani aliyoionyesha Rais Samia kwa sasa kwa viongozi hawa liwe funzo kwa wengine na naamini tutafika mbali,”alisema Chifu Ismail Hassan kutoka Nachingwea mkoani Lindi.


Saturday, September 21, 2024

TASSIM YAANDAA MAONYESHO YA VIWANDA VIDOGO DODOMA.

 




Na  Mwandishi Wetu

SERIKALI imewaalika wananchi na wadau mbalimbali kuhudhuria mkutano wa kukusanya maoni kuhusu Sera mpya ya biashara ndogo ndogo (SMEs) utakaofanyika mkoani Dodoma .

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. John  Simbachawene, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa siku ya viwanda vidogo vidogo (TAMISID).

Siku ya viwanda vidogo vidogo inayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu mkoani Dodoma inaratibiwa na Chama cha Wenye Viwanda Vidogo Tanzania Association of Small Scale Industries and Manufacturers (TASSIM).

Alisema serikali ilikusanya maoni ya watu mbalimbali kwenye awamu ya kwanza hivyo imeamua kuandaa mkutano wa awamu ya pili kuchukua maoni kwa wale ambao walikosa nafasi kwenye awamu ya kwanza.

Alisema mkutano huo utafanyika wiki hii mkoani Dodoma na kuwataka wananchi,  wajasiriamali, wafanyabiashara kushiriki kwenye mkutano huo ili watoe maoni ya kuchangia kuboresha sera hiyo.

“Wizara inaendelea kuifanyia kazi Sera mpya ya viwanda  na tumeitisha mkutano wa wadau mbalimbali mkoani Dodoma waje kutoa maoni yao kwa awamu ya pili kwa ambao hawakutoa maoni yao ili tukamilishe hiyo Sera na  iweze kutoa mchango wake kwenye taifa letu na tuweze kuizindua rasmi,” alisema Dk. Simbachawene

Alisema malengo makuu ya siku ya viwanda vidogo ni pamoja na kuongeza uelewa wa mchanago wa viwanda vidogo katika uchumi na kukuza ubunifu kwenye sekta.

”Kama tulivyoona wakati tunatembelea maonyesho zipo bidhaa ambazo zimetengenezwa na wajasiriamali wadogo ambazo ni bora na zinaweza kushindana kimataifa kwa hiyo nawasisitiza wajasiriamali waendelee kuwa wabunifu wa bidhaa,” alisema

Aidha, alisema kuanzishwa kwa taasisi hiyo kutakuwa ni jukwaaa la kuwaunganisha wadau wawekezaji na washirika wa maendeleo katika kuendeleza viwanda vidogo na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo.

Alisema TASIM inafanya maandalizi ya maonyesho ya viwanda vidogo Tanzania yatakayofanyika tarehe 28 Oktoba hadi Novemba Mosi kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma na kuwataka wajasiriamali kuitumia kama fusa kwao kuongeza ufanisi.

“Tunatarajia kufanya maonyesho rasmi Dodoma tutumie nafasi hii kama TASIM tujitangaze kwenye vyombo vya habari ili wafanyabiashara washiriki na kutangaza bidhaa zao na tutangaze kwenye balozi zilizopo hapa nchini ili zione namna ya kusaidia wajasiriamali,” alisema

Alisema viwanda vidogo vidogo vimekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania kwa kuchangia kutoa ajira nyingi na kupunguza kiwango cha umaskini.

Dk. Simbachawene alisema viwanda vidogo ni injini ya ukuaji wa uchumi kwa kuzalisha bidhaa na huduma muhimu na kukuza ujasiriamali wa ndani kwa watanzania walio wengi ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi.

Mwenyekiti wa TASSIM, Masoud Ali alisema lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kuinua viwanda vidogo vidogo ambavyo ndivyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kwenye sekta ya viwanda.

Alisema imekadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 99 ya viwanda vyote nchini viko kwenye makundi ya viwanda vidogo sana, viwanda vidogo sana na viwanda vya kati kwa maana ya small, micro and medium industries.

 “Kwa hiyo sisi wawakilishi wa haya makundi tuna mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya nchi yetu na kauli mbiu ya TAMISID 2024 ni kusherehekea nguvu ya viwanda vidogo,kujenga Tanzania imara na kuwekeza kwenye mustakabali wetu kwa kuwekezesha watu wetu,” alisema

Alisema kauli mbiu hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya chama hicho kuinua vianda vidogo vidogo na kuvitumia ipasavyo kama injini ya ukuaji wa uchumi na kuomba wadau kujitokeza kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.