Thursday, July 11, 2024

KITUO CHA UTAFITI RUANGWA KAMPASI YA UDSM KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI 18

 






NA HADIJA OMARY 





Naibu makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dar es salaam ambae ni mratibu wa Mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi (HEET) Profesa Benadeta Kiliani amesema watahakikisha  ujenzi wa kituo cha utafiti wa sayansi ya Kilimo  na chakula  cha chuo kikuu cha Dar es salaam unaofanyika katika kijiji cha Likunja  wilayani Ruangwa unakamilika ndani ya miezi 18




Profesa kiliani Ameyasema hayo katika kikao kazi cha uzinduzi wa kamati ya "kasema" ambayo ni sehemu ya ulinzi na usalama wa mradi huo na  yenye jukumu la kuweka kumbukumbu za kile kinachoendelea katika mradi



Profesa kilian ametoa wito kwa kamati na  wananchi wa Ruangwa kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo



Kamati hiyo ya " kasema " Ina wajumbe watano na inalengo la kukusanya na kushughulikia maoni au malalamiko ya wananchi katika eneo la mradi  husika 



Jukumu lingine la kamati hiyo ni kuweka kumbukumbu za kile kinachoendelea na kufanyika katika mradi huku ikiwa sehemu ya ulinzi na usalama katika utekelezaji wa mradi




Kwa upande wake Naibu mratibu wa Mradi  huo wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi ( HEET)  Liberato Haule amesema mradi huo  unaotekelezwa  na chuo kikuu cha Dar es salaam umedhaminiwa na serikali kupitia fedha ya mkopo kutoka benk ya dunia ukilenga kuboresha huduma za Elimu ya juu nchini ili iweze kuchangia maendeleo ya uchumi.



Amesema mradi huo unatekelezwa katika maeneo mapya 14 ambapo mpaka sasa maeneo mapya matatu tayari yameshafikiwa ambayo ni pamoja na Ngongo (Manispaa ya Lindi), Likunja Wilayani Ruangwa pamoja na Halmashauri ya Bukoba mkoani  Kagera 





Mwenyekiti wa Halmashari hiyo Andrew  Chikongwe anatumia fursa hiyo kuitaka kamati hiyo kutimiza wajibu wao kwa maslah ya halmashauri hiyo





Baadhi ya viongozi na watendaji walioshiriki katika uzinduzi wa kamati hiyo wamepokea kwa shauku na matumaini makubwa na kwamba kituo hicho kitakuwa msaada  kwa wakulima na kuongeza fursa za kiuchumi



Wednesday, July 10, 2024

WAFUNGWA/MAHABUSU ZAIDI YA 7,000 WANUFAIKA NA KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID.

 

Na Mwandishi Wetu


 


KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid imeanza kuzunguka kwenye magereza mbalimbali hapa nchini kuwapa msaada wa kisheria wafungwa na mahabusu na mpaka sasa imeshawahudumia zaidi ya  7,000.


 


Hayo yamesemwa julai 09, na Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi wakati akizungumza kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama (DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.


Alisema wameamua kwenda magerezani kwani wanaamini kwamba kuna watu wanaweza kujikuta kwenye mazingira hayo kwa kukosa tu wakili au watu wa kuwaongoza kwenye mashauri yanayowakabili.


“Kuna watu wako mahabusu kwasababu tu wamekosa mwongozo wa kisheria na wakipata mwongozo wanaweza kutoka kwa dhamana au suala linalomkabili likazungumzwa na pande zote mbili na likafikia mwisho,” alisema


Kuhusu wafungwa, alisema kuna watu wanaweza kuwa wamefungwa kifungo cha ndani lakini kupitia kampeni hiyo wanaweza kumsaidia akapata kifungo cha nje kwa kufanyakazi za kijamii au kukata rufaa mahakama za juu.


“Kwa hiyo huduma ya msaada wa kisheria kwa watu walioko kizuizini ni muhimu sana na huwa tunaenda kwenye vituo vya polisi na kwenye magereza na tunapokwenda magerezani tunatoa elimu ya haki jinai kwa watu walioko gerezani,” alisema


Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu ukamataji upelelezi uendeshaji wa mashauri, haki na wajibu wa mahabusu na wafungwa wanapokutwa na hatia kwenye kesi mbalimbali za jinai na kupewa kifungo cha ndani.


Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu namna ya kupata dhamana na kukata rufaa kwa wale ambao wamehukumiwa lakini hawajaridhishwa na hukumu walizopewa kwenye Mahakama mbalimbali nchini.


“Kupitia kampeni hii tunatoa ushauri kwa mfungwa au mahabusu mmoja mmoja tunakwenda na wanasheria wanaitwa mmoja moja wanashauriwa wanachotakiwa kufanya na wanaandaliwa nyaraka kwasababu wengine wamekaa mahabusu muda mrefu inabidi waandaliwe kila kitu,” alisema


Alisema timu ya wanasheria imekuwa ikiambatana na watu kutoka Ofisi ya Raifa ya Mashtaka, Wizara ya Katiba na Sheria, Jeshi la Polisi Makao Mkuu, Jeshi la Magereza Makao Makuu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.


“Kwa mfano tukikuta mtu amekaa ndani muda mrefu shauri lake linapigwa dana dana, ushahidi haukamiliki kwa wakati anayehusika hapo atakuwa anayetoka ofisi ya mashitaka kwa hiyo atawajibika kufuatilia kujua kesi imekwamia wapi na kisha ataikwamua na itaanza kusikilizwa na kwenda haraka ili mtu apate haki,” alisema.


Alisema timu hiyo pia imekuwa ikimshirikisha Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Mkoa na vyombo vingine vya utoaji wa haki ngazi ya mkoa wakati wa kusikiliza mashauri hayo ya wafungwa na mahabusu.


“Kuna wafungwa na mahabusu wanapewa msaada wa kisheria na  wanatoka kabisa mahabusu au jela na kuna wengine tunawapa elimu tu ya namna ya kudai haki zao wanapoona zinakiukwa  kwa hiyo wengi wameshanufaika na kampeni hii ambayo imefika mikoa saba,” alisema



Alisema Mama Samia Legal Aid Campaign pia imekuwa  ikiwapa msaada wa kisheria wahamiaji haramu ambao kesi zao zimeshasikilizwa na kutolewa maamuzi warejeshwe nchini kwao lakini wanakosa namna ya kuondoka.


Alisema wamekuwa wakiwasaidia kuhakikisha wanakwenda nchini mwao kwani baadhi ya wahamiaji hao wamekuwa wakishindwa kurudi kwao kutokana na kukosa fedha za kuwafikisha kwenye nchi zao.






Thursday, June 27, 2024

ETDCO YAENDELEA KUJENGA MIUNDO MBINU YA KUSAFIRISHA UMEME MRADI WA TABORA - KATAVI 132kV

 

Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya ETDCO CPA Sadock Mugendi, Amesema Wanaendelea kujenga miundo mbinu ya Umeme Nchini ikiwemo Njia ya kusafirisha umeme kutoka  Tabora  hadi Katavi ambao ni mradi wa kusafirisha  Umeme na tayari  Mradi Umefkia Asilimia 67.


Mugendi amesema ETDCO ni kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania na ni suluhisho la miundo mbinu ya umeme kwani ipo kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundo mbinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.


Kaimu Meneja Mkuu CPA Sadock Amesema Mradi wa Kutoka Tabora kwenda Katavi wenye Urefu wa kilometa 383 wa msongo wa 132kV ambao Unatarajiwa kumalizika Mwaka huu kupelekea    Mkoa wa Katavi kupata  Umeme wa Uhakika pia Kuipunguzia Gharama Tanesco za Kununua Mafuta ya Dizeli kwajili ya Jenereta ili kuzalisha Umeme kwenye Mkoa Wa Katavi.


CPA Sadock Ameipongeza Serikali kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati ili Kuhudumia Wananchi wake vizuri, Amesema Hayo Wakati Akitembelea Mradi wa Kimkakati wa Tabora kwenda Katavi wenye msongo wa 132kV.



Wednesday, June 26, 2024

KIKWETE MWENYEKITI WA BARAZA LA WAZEE WA SADC YUKO LESOTHO

 


NA MWANDISHI WETU, LESOTHO


Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo tarehe 26 Juni, 2024, yuko katika Ufalme wa Lesotho kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Jopo hili la Wazee wa SADC ambalo Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Paramasivum Pillay B. Vyapoory, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mauritius, limekutana na Serikali na wadau mbalimbali ndani ya Ufalme wa Lesotho, kama mwendelezo wa juhudi ya kusaidia upatikanaji wa utulivu wa kisiasa katika Ufalme huo. 


Jopo limekutana na Mhe. Ntsokoane Samuel Matekane, Waziri Mkuu wa Ufalme wa Lesotho; Mhe. Nthomeng Justina Majara, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Sheria na Masuala ya Bunge; Mhe. Mamonaheng Mokitimi, Mwenyekiti wa Seneti; Viongozi wa Vyama vya Upinzani; Mhe. Constance Seoposengwe, Balozi wa Afrika Kusini nchini Lesotho na wadau mbalimbali.






WAZIRI MKUU AZINDUA VITABU VYA HISTORIA YA BUNGE

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vitabu vya historia ya Bunge ambavyo vitasaidia kuhamasisha tafiti na kujua zaidi kuhusu mchango wa Bunge katika maendeleo ya jamii nchini.


Amesema kuwa vitabu hivyo pia vitakuwa kielelezo cha mafanikio na changamoto ilizopitia Bunge la Tanzania katika kudumisha demokrasia na utawala wa sheria. “Historia yetu ni sehemu ya mchango wetu kwa jumuiya ya kimataifa katika kukuza amani, utulivu na maendeleo.”


Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 26, 2024) wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya historia ya bunge katika ukumbi wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma.Vitabu vilivyozinduliwa ni Kitabu cha Historia ya Bunge kutoka 1926-2024 na Wabunge wa Tanzania na nafasi zao kuanzia mwaka 1965-2023


“Kumbukumbu za historia ya Bunge zinaweza kuchochea utafiti wa kitaaluma na maendeleo ya nadharia za kisiasa na utawala. Watafiti wanaweza kutumia taarifa hizi kujenga ufahamu mpya na kupendekeza mifumo bora ya kisiasa.”


Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amepongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sehemu ya maono ya bunge ikiwemo kuridhia kulikabidhi bunge maeneo yote yanayozunguka jengo la bunge.


“Tunatarajia kujenga makumbusho ya bunge ambayo yatakuwa ni makubwa kwa nchi nzima ili mtu anapokuja bungeni apate historia ambayo tumeipitia kama nchi lakini pia historia ya bunge letu”




TANESCO, WAWEKEZAJI BINAFSI LUDEWA WAFIKIA MAKUBALIANO

 

TANESCO, WAWEKEZAJI BINAFSI LUDEWA WAFIKIA MAKUBALIANO


Ni kuhusu TANESCO kukabidhiwa  miundombinu ya kusambaza umeme*


Ludewa kujengwa kituo cha Kupokea na Kupoza umeme


Kapinga asema Vijiji 70  kati ya  76 Mbulu vimepatiwa umeme


Imeelezwa kuwa, Serikali na Wawekezaji wanaowauzia umeme wananchi katika baadhi ya kata za Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wamefikia makubaliano ya kisheria ili miundombinu ya usambazaji umeme katika Kata hizo ikabidhiwe kwa Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO).


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga leo Juni 26, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mbunge wa Ludewa, Mhe. Zacharius Kamonga aliyetaka kufahamu Serikali itamaliza lini changamoto za bei na mgao wa umeme katika Kata hizo.


Kapinga ameongeza kuwa, hatua zote za makabidhiano zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai, 2024 na baada ya kukamilika, TANESCO watabadilisha mita za umeme ili ziendane na mifumo ya TANESCO na kuwawezesha wananchi wa Kata hizo kutumia umeme wa Gridi ya Taifa.


Alitaja Kata hizo kuwa ni Mawengi, Lubonde, Lugarawa, Lupanga, Mlangali, Madilu, Milo na Mawengi ambazo  zimekuwa zikipata umeme kutoka kwa Wawekezaji binafsi (JUWUMA na MADOPE HCL.


Kuhusu ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme kujengwa katika Wilaya ya Ludewa,  amesema Serikali inaangalia namna bora ya kutekeleza ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kutumia Mpango wa Gridi Imara.


Amesisitiza kuwa, Wananchi wa Ludewa wanahitaji umeme mwingi na wa uhakika kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao vikiwemo viwanda vidogo na vikubwa. 


Vilevile amesema kuwa, Serikali kupitia Mkandarasi  Ok Electrical inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na tayari mkandarasi  ameshafanya upimaji na usanifu wa kina na mwanzoni mwa mwezi Julai 2024 anatarajiwa kuanza kusimika nguzo  ili kuziunganisha Kata hizo na Gridi ya Taifa.


Katika hatua nyingine, Serikali imemtaka  mkandarasi anayetekeleza mradi wa Usambazaji wa umeme katika  Vijiji vilivyopo  mwambao wa Ziwa Nyasa, kukamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati.


Naibu Waziri Kapinga amesema  kuwa iwapo mkandarasi huyo atashindwa kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa, atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo wakandarasi wengine wazembe.


Pia, Kapinga amesema Serikali inaendelea 

 na usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Mbulu   ambapo vijiji 70 kati ya 76 vimeshapatiwa umeme kupitia REA.


Aidha, kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji  6 vilivyosalia inaendelea ambapo mkandarasi anafanya  kazi ya kuvuta waya na kuweka Mashineumba katika vijiji hivyo.


Pia Mradi wa Ujazilizi utapeleka umeme  katika Vitongoji vyote nchini kwa awamu tofauti.

Friday, June 21, 2024

CTI YALIA NA UTITIRI WA TOZO MIKOANI

 

Na Mwandishi Wetu


 


SHIRIKISHO la Wenye Viwanda (CTI), limeseme kuwepo kwa utitiri wa tozo katika kila mkoa na halmashauri kumekuwa kikwazo katika ustawi wa biashara na uwekezaji nchini.


 


Hayo yalisemwa  jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga katika warsha maalumu ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya viwanda vya chakula na vinywaji kupitia utafiti uliofanywa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo ya Wajasiriamali, Dk. Donath Olomi.


 


Utafiti huo ulioangazia namna tozo hizo zilivyo kikwazo kwa wafanyabiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini.


 


Tenga alisema Dk Olomi ni mtafiti msomi na ameainisha vitu vingi ikiwemo mapendekezo ya kufuata kuondoa vikwazo hivyo, akisisitiza kuwa lengo ni kuwapa nafasi nzuri wafanyabiashara wakubwa wanaotamani kuja kuwekeza nchini.


 


Tenga alisema athari ya utofauti wa tozo unaathari kibiashara ikiwamo kuongezeka kwa bei za bidhaa, na hivyo kusababisha  mlaji kununua bidhaa ya bei ndogo kwa gharama kubwa.


 


“Kwa mfano mtu amevuna mazao yake Mbeya sasa ili aje kuuza Dar es Salaam kwenye soko kubwa atalazimika kusafirisha, sasa anatozwa huko  akifika Iringa anatozwa tena, njiani pia hivyohivyo anakutana na tozo nyingine akifika Dar es Salaam nako anakutana na tozo nyingine,” alisema.


 


“Tunataka huyu mfanyabiashara akishatozwa Mbeya asitozwe tena sehemu nyingine, tunapaswa tuwe na utaratibu ambao utatambua kama ameshatozwa, hatujafanikiwa kuondoa vikwazo. Tusipofanya hivyo tunawakwamisha hawa wafanyabiashara au watafanya ujanja wa kutoa rushwa njiani ili kupunguza hizo tozo,” alisema Tenga


 


Naye Dk. Olomi alisema kutokana na utafiti alioufanya alipendekeza kuwe na uwazi kuhusu  tozo hizo akifafanua kwamba katika halmashauri karibu zote tozo hizo hazijatangazwa mahali popote hivyo mwekezaji anayataka kuwekeza hawezi kujua viwango vya tozo na kama ziko kwa mujibu wa sheria au siyo.


 


Pia alipendekeza serikali iangalie namna ya kuondoa tozo zinazokinzana na kujirudia rudia kwenye mikoa na halmashauri nchini akitolea mfano kwamba mtu akiingiza lori mjini (kariakoo) kwaajili ya kupakia au kuondoa bidhaa atakutana na tozo ya maegesho.


 


Alisema pia lori hilo litatozwa malipo ya kuingia katikati ya Jiji na wakati mwingine haijulikani wapi ni mwisho wa kulipia kwa hiyo kuna maeneo kama hayo yanahitaji marekebisho.


 


Alisema mkanganyiko mwingine ni zile tozo zinazotozwa na halmashauri na nyingine serikali kuu. “kwa mfano tozo ya kupima afya kwenye viwanda unatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (OSHA) lakini pia serikali za mitaaa kiutaratibu zinatofautiana kama unapima  magonjwa yanayoambukizwa unapimwa na halmashauri na yale yasiyoambukiza unapimwa na OSHA na tozo wanayotoza kwa mtu mmoja ni sh 70,000 sasa ukiangalia hii haijakaa sawa,”


 


“Hizi tozo zisiwepo kama zinania ya kukomoa wenye viwanda bali zitumike kuweka mazingira mazuri kwahiyo kuna changamoto za aina hiyo,” alisema Dk Olomi


 


Mhandisi wa Viwanda Mkuu Kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Karoline Varelian alisema serikali itachukua  mapendekezo ya wadau hao, kuchambua na kuyafanyia kazi ili kuweka mazingira rafiki.


 


Alisema tayari Wizara imeshaanza kuzifanyia marekebisho baadhi ya sera na sheria ila kwa sasa watakwenda kuyafanyia kazi kwa haraka mapendekezo yaliyotolewa na wadau ili kuondoa mlalamiko ya wenye viwanda.


 


Alisema tozo zimekuwa nyingi  na kuahidi kuwa  watapitia ushauri uliotolewa kwenye utafiti uliofanywa na Dk Olomi ili kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara hususani wenye viwanda vya chakula na vinywaji.






Tuesday, June 18, 2024

CTI YASEMA BAJETI ITASISIMUA UKUAJI WA VIWANDA


 Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini (CTI), limepongeza bajeti kuu ya serikali kwa kuweka mambo muhimu ambayo yatachochea ukuaji wa viwanda nchini.


 


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari.


 


Amesema serikali imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na kila wanapokuwa na jambo wamekuwa wakifunguliwa milango ya majadiliano na kwamba hakuna jambo la wenye viwanda ambalo linakwama.


 


Amesema wenye viwanda wamefurahia sana bajeti ya serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa SGR ambayo alisema itasiadia kwa kiwango kikubwa kukuza viwanda vya  ndani kuzalisha kwa wingi bidhaa.


 


Amesema miradi kama SGR inasaidia kukuza uchumi kwani viwanda vitazalisha kwa wingi na bidhaa kusafirishwa kwa urahisi tofauti na sasa ambapo usafirishaji umekuwa ukisababisha bei kupanda.


 


“Nchi ambayo iko makini inaendeleza miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli, barabara, miradi ya maji kama kuendeleza miradi ya kimkakati barabara maji, bandari kwasabbau huwezi kuendeleza viwanda kama huna umeme au unamatatizo ya usafirishaji,” alisema tenga


“Mfano bei ya mfuko wa saruji hapa Dar inaweza kuwa shilingi 16, 000 au 17,000 lakini bei ya kuubeba mpaka Mwanza ni kati y ash 10,000 hadi 12,000 kwa hiyo mtu ananunua mfuko wa saruji hapa kwa 16, 000 lakini mpaka kuufikisha Mwanza unauzwa shilingi 28,000,” alisema


“SGR itapunguza gharama ya usafirishaji na bei ya bidhaa itapungua sana na itasaidia sana viwanda vya ndani kukua na kuongeza mapato na ni vizuri serikali inapofanya vizuri sekta binafsi tuseme kwamba inafanya vizuri,” alisema.


Tenga alisema bajeti ya mwaka huu inakusudia kuhamasisha mapato ya ndani zaidi ikilinganishwa na bajeti ya 2023/24.


Amesema jambo muhimu katika bajeti ya mwaka huu ni Serikali kufanya mageuzi mbalimbali ya muundo wa kodi, ada, tozo na marekebisho ya sheria na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara.


 


Amesema marekebisho ambayo yamependekezwa kuhusiana na sekta ya viwanda ni katika ongezeko la thamani VAT, ushuru wa bidhaa, ada na tozo za wakala pamoja na ushuru wa forodha.


 


Tenga amesema baadhi ya hatua chanya ni pamoja na kuanzishwa kwa tozo ya maendeleo ya viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje yenye lengo la kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji na kuongeza mauzo ya nje; kupunguza ada na tozo zinazotolewa na vyombo vya udhibiti ili kupunguza gharama za uzalishaji.


 


Amesema pia wamefurahishwa na kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kwenye malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji ili kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kutozwa ushuru wa VAT kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa hapa nchini ili kuchochea uwekezaji katika viwanda vya nguo vya ndani.


 


Amesema hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya vifaa vya ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi.




 

DKT. MPANGO AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA TAASISI YA KIMATAIFA YA UWEKEZAJI YA UINGEREZA.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji ya Uingereza (BII) Nick O’Donohoe na ujumbe wake, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dodoma.

 

Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea kuwekeza nchini tangu mwaka 1949 katika sekta muhimu na za kipaumbele kwa uchumi wa Taifa ikiwemo Nishati, Kilimo na Chakula, Misitu, Huduma za Fedha, Huduma za Mawasiliano pamoja na kushirikiana na Benki za Tanzania ikiwemo Benki ya NMB.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo katika kuendelea kufungua uchumi kwa kufanya mageuzi muhimu yanayochochea na kuvutia biashara na uwekezaji. Ameongeza kwamba Serikali imeendelea kufanya mageuzi ya kisera kwa kuhakikisha sera na sheria zinazotabirika. Aidha, Serikali inaendelea kufanya mageuzi ya kitaasisi ili kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa salama.

 

Amesema Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali zinazoikumba dunia kwa sasa.

 

Vilevile, amewakaribisha kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda misitu na mazingira kwa ujumla.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji ya Uingereza (BII) Bw. Nick O’Donohoe amesema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Nishati hususani nishati ya jua na upepo. Pia kuunga mkono uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji umeme, Kilimo pamoja na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya mbogamboga na maua.

 

Bwana O’Donohoe amesema nchi ya Tanzania imekua moja ya nchi zenye uchumi imara na unaokuwa kwa kwa kasi na hivyo kuvutia wawekezaji. Ameishukuru Serikali kwa mazingira wezeshi kwa Taaasisi hiyo katika kutekeleza miradi mbalimbali.

 

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Taasisi ya BII Afrika Bw. Chris Chijuitomi na Mkuu wa Mipango Bw. John Trees. Ujumbe wa Tanzania ni pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Mbelwa Kairuki pamoja na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomaisa ya Kiuchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga.



Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

18 Juni 2024

Dodoma.





Monday, June 17, 2024

RC LINDI AZIAGIZA HALMASHAURI KUANZISHA NA KUHUWISHA MADAWATI YA ULINZI MASHULENI

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.



Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinafufua au kuunda madawati ya ulinzi ya watoto  sambamba na kuunda klabu za watoto mashuleni zitakazowasaidia kuelezea na kutatua changamoto zao


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa huko katika kijiji cha chienjele halmashauri ya Ruangwa Jana Juny 16/2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi , Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawale  amesema vyombo hivyo ni  muhimu  kwa ajili ya kutetea maslahi yao pindi watoto wanapokuwa wamefanyiwa ukatili. 



Amesema ili Taifa liweze kuendelea kupiga hatua ni muhimu kutilia maanani mahitaji  ya watoto  ikiwa pamoja na watoto  masikini , walemavu na walio na mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za Halmashauri.



hata hivyo ameendelea  kuikumbusha Jamii kuwa inawajibu wa  kutoa taarifa na ushahidi kuhusu mtoto ambae haki zake zinakiukwa na wazazi na walezi au ndugu yoyote kwenye  serikali za mitaa na kwenye vyombo vya dola kwa vitendo vya ulawiti, ubakaji na ukatili  wanaofanyiwa  watoto  ili serikali ichukue hatua na adhabu zitolewe.



Akitoa salamu za Wilaya ya Ruangwa Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Ngoma amesema siku hiyo ya Mtoto wa Afrika ni muhimu kwa Nchi za Afrika kutathimini na kueleza Dunia mabadiliko Makubwa yaliyofanywa na Nchi hizo Katika kuwapambania watoto hao Katika kuondoa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi unyanyapaa Elimu na kadhalika


 


Awali afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Lindi ndugu Charles Kigahe alieleza changamoto kadhaa zinazowakabili watoto wa Mkoa huo wa Lindi 


Miongoni changamoto hizo ni pamoja na Watoto kutotimiziwa haki ya kupata elimu, hii imetokana na wazazi kutoona umuhimu wa kuwafuatilia watoto pindi wakiwa shuleni ambapo imesababisha watoto kuacha shule.



Watoto kukosa malezi ya wazazi, hii imetokana na wazazi kutengana ambapo mtoto anaendelea kulelewa na mzazi mmoja au bibi. Watoto kukosa mahitaji ya msingi kwa sababu ya kutoelewana kwa wazazi,

Watoto kufanyiwa ukatili wa kingono.



Changamoto nyingine ni Migogoro ya ndoa kwa wazazi,  ambapo wazazi wanaachana inapelekea mtoto kuendelea kuhangaika na hatimaye kuacha shule.

Wazazi na walezi hawatimizi wajibu wao wa kuwalea watoto ambapo inasababisha kuongezeka kwa watoto wa mtaani.


Kauli mbiu ya siku ya Mtoto wa Afrika 2024 ni Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maadili, maarifa na stadi za kazi