Monday, October 23, 2023

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA BALOZI WA QATAR HAPA NCHINI.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo terehe 23 Oktoba 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

 

Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Qatar na imedhamiria kuimarisha na kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya mataifa yote mawili. Makamu wa Rais ametaja maeneo yanayoweza kuongezwa ushirikiano baina ya Tanzania na Qatar ikiwemo sekta ya Afya, utafiti wa mafuta na gesi pamoja na biashara ikiwemo bidhaa zinazotokana na mafuta.

 

Halikadhalika Makamu wa Rais ameikaribisha Qatar kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji dawa na vifaa tiba pamoja na kushirikiana katika teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala. Pia amesema Qatar na Tanzania zinaweza kushirikiana kwenye utalii pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu ikiwemo wataalamu wa afya.

 

Kwa upande wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi amesema Tanzania na Qatar zinapaswa kuongeza ushirikiano wake ili kuweza kutumia vema fursa zilizopo katika mataifa hayo. Balozi muraikhi ameahidi kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania ili kuongeza ushirikiano katika masuala ya kibiashara.

 

Kwa pamoja viongozi hao wamejadili namna ya kufanyika kwa ziara za wafanyabiashara na wawekezaji baina ya mataifa hayo mawili ambazo zitaweza kusaidia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo za afya, michezo na utamaduni.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

23 Oktoba 2023

Chamwino – Dodoma.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 23 Oktoba 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 23 Oktoba 2023.


 

KILA SHULE BAGAMOYO, IWE NA SHAMBA LA MBOGAMBOGA NA MATUNDA-DED

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo Bwana Shauri Selenda leo tarehe 23 Oktoba 2023 ameiagiza Kamati ya Lishe Halmashauri ya Bagamoyo kusimamia na kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa na bustani ya mbogamboga pamoja na matunda Ili kujenga afya Kwa wanafunzi na jamii Kwa ujumla.



Akifungua Kikao cha Kamati ya Lishe na kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Kamati hiyo Selenda alisisitiza kuwa, Kwa Sasa suala la Lishe lazima kupewa kipaumbele kwani jamii yetu kwa sasa inashindwa kulitilia uzito.



" Niseme tuu kuwa tuwasaidie wananchi wetu katika masuala  ya Lishe ni jukumu letu na tuhakikishe kuwa kila shule inakuwa na eneo kwaajili ya bustani ya mboga na matunda hakikisheni mntekeleza hilo na nitapita kila shule kufanya ufuatiliaji wa suala hili".  Alisema Bwana Selenda. 


Kamati ya Lishe Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo imekutana kujadili taarifa mbalimbali za masuala ya Lishe robo ya kwanza Mwaka wa fedha 2023/2024.


MAGAZETI YA LEO TAREHE 23 OKTOBA 2023.

 KURASA ZA MBELE







KURASA ZA NYUMA









Sunday, October 22, 2023

SOPHIA MJEMA ATEULIWA KUWA MSHAURI WA RAIS MASUALA YA WANAWAKE

 



WAZAZI WAACHE TABIA YA KUELEWANA NA WABAKAJI, KUMALIZA KESI.

 

Anayezungumza akiwa amesimama ni diwani wa kata ya Bakoba Shaaban Said kulia kwake ni afisa elimu kata hiyo Anitha Mashulano katika mkutano na wananchi. Picha na Alodia Babara.
.............................

Na Alodia Babara

Bukoba. 

Diwani wa kata ya Bakoba manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Rashid Said amekemea wazazi ambao watoto wao wanafanyiwa vitendo vya ulawiti na ubakaji na wazazi hao wanachukua jukumu la kuelewana na watuhumiwa wa vitendo hivyo badala ya kuwachukulia hatua za sheria.


Diwani huyo akizungumza na wananchi wa kata hiyo kupitia mkutano uliofanyika hivi karibuni katika mtaa wa Forodhani alisema kuwa juhudi wanazochukua viongozi za kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa vitendo vya ulawiti na ubakaji zinakwamishwa na baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakielewana na watuhumiwa na kuyamaliza baada ya kutenda vitendo hivyo.


Amesema kata yake inazo shule mbili za msingi na moja ya sekondari, shule ya msingi Buyekera na Bunena na shule ya sekondari Bakoba, wanafunzi watatu wamebainika kulawitiwa na watuhumiwa wameshaanza kuchukuliwa hatua za kisheria na wengine kufikishwa mahakamani.


Amesema wanafunzi hao walibainika baada ya kikao cha maendeleo ya kata kuwaagiza afisa elimu kata na polisi kata kupita katika shule hizo na kutoa elimu mashuleni kuhusu madhara ya vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto ndipo baada ya elimu hiyo walienda kutoa taarifa kwa viongozi hao.


Amesema wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao kuwapa elimu na kuwauliza maswali bila kuwaonea aibu kwani wakishindwa kufanya hivyo watajikuta wamechelewa na watoto wao wataharibikiwa.


Aidha alipowahoji wananchi kama kuna mtu anakubali ushoga hakuna mwananchi hata mmoja aliyekubaliana na hilo hivyo amewasisitiza kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuendelea kukataa vitendo vya ushoga ambavyo vimeshamili katika nchi za Magharibi.


Shaaban amesema, bahati mbaya kuna matukio yanatokea katika jamii polisi kata na afisa elimu wanafanya wajibu wao lakini ajabu mzazi anakwenda kuelewana na mtuhumiwa ambaye anatuhumiwa kumfanyia mtoto wake kitendo cha ulawiti/ubakaji inasikitisha na kuumiza na inakatisha tamaa pia inarudisha nyuma mapambano ambayo tayari viongozi wameyaanza.


"Haiwezekani tuishi na watu katika mitaa yetu wanaofanya vitendo vya namna hiyo alafu tuendelee kukubali kuishi nao, tutambue vitendo vipo tuwabaini na kuwanyoshea vidole watu wanaohusika na mkiona viongozi wanashughulika nayo wapeni ushirikiano" amesema Shaaban.


Ameongeza kuwa wenyeviti wa mitaa wasikubali watu wazoee mitaa yao kwa kuishi tu bila wao kuwafahamu walikotoka kwani watu kama hao ndiyo wanafanya vitendo hivyo kwa watoto."Msikubali kuishi na watu wasiojulikana wametoka wapi na wanashughuli gani, yawezekana ndiyo wanatuharibia watoto wetu na vijiwe vinavyoonekana ni hatarishi futeni wakileta ubabe waleteni kwangu kwenye kata hii mimi ndiyo kiongozi mkuu" amesema Shaaban.


Kwa upande wake afisa elimu kata Bakoba Anitha Mashulano ameeleza kuwa wazazi wawatolee taarifa wanaume ambao hawana wanawake kwani hao ndiyo wanahusika katika kuwaharibu watoto.


"Tuna watoto wamebakwa shuleni wameishapata ukimwi wanaendelea na dozi unajiuliza mtoto yuko darasa la nne ameanza kumeza dawa za kufubaza virus vya ukimwi hadi afike utu uzima si shida kubwa! Lakini kwa sababu ya matamanio ya mtu katoka huko anabaka tu! Anamaliza haja zake" amezungumza kwa masikitiko Mashulano.


Amewasihi wazazi kutowaficha watoto wao kuwaeleza uwazi na ukweli juu ya madhara ya vitendo vya urawiti na ubakaji na kuwaeleza kuwa eneo hili matumizi yake ni haya, wasikubali kufanya katika umri wao mdogo na wakifanya hivyo wambie madhara yake.


"Kuna mambo au mazingira watoto wanaona kama hawajapata elimu ya hayo mambo lazima wajaribu kwa hiyo wazazi elimisheni watoto wetu tuondoe aibu hata katika vikundi vyenu vya ujasiriamali elimishaneni jamani na acheni tabia ya kuacha watoto peke yao ndani eti kwa kisingizio cha kufanya biashara mnatuma fedha kwenye simu za majirani zenu watoto wanatumika sana acheni" amesema Mashulano.


Aidha ameeleza kwamba, wanapokuwa wanaandika taarifa wanaelezwa mambo mengi na watoto hadi wanajikuta wanatoa machozi, na kuwa wazazi wawe karibu na watoto wao maana wanahangaika na kupambana kwa ajili yao hivyo wasiwaache wakaharibikiwa.


Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima akizindua program ya kupinga unyanyasaji na ukatiri wa kijinsia katika taasisi ya Tanzania Youth Development Organization (Tydo) iliyopo katika manispaa hiyo alisema kuwa wale wazazi wanaoelewana na watu wanaowafanyia vitendo vya ukatiri watoto wao kwa kuwapa chochote bila kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ipo siku watoto wakiwa watu wazima na wakajua mama au baba alikaa meza moja akakubaliana na mharifu kwa kumpa chochote, mtoto huyo hataweza kuelewana na wazazi wake.


Polisi kata, katika kata ya Bakoba Rashid Mminga amewatahadharisha wazazi wenye watoto sekondariya Bakoba na wamekuwa wakiwapatia simu wanapokuwa shuleni kuwa mtoto atakayebainika mzazi atatozwa faini na mtoto wake atafukuzwa shule.

Amewata kuwa wamoja katika swala la ulinzi na usalama na wanapobaini uvunjifu wa amani katika maeneo yao kutoa taarifa na wote wanaofungua vilabu (grosaries) na kuuza pombe muda wa kazi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

SERIKALI YA DKT SAMIA INAWAJALI NA KUWAPENDA WALIMU-DKT JAFO

 

Kisarawe Pwani


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira (Mb) Mhe Dkt Selemani Saidi Jafo amewataka Walimu wote nchini hasa wanawake kuendelea kulea Watoto katika maadili mema zaidi hasa wanapokua shuleni,


Akizungumza Leo 21.10.2023 Mkoa wa Pwani Wilaya Kisarawe katika mafunzo ya walimu wanawake ambapo alisisitiza walimu hao kuendelea malezi Bora ya kuwalea vijana katika Maadili mema,


*"Ndugu zangu katika Utumishi wa Umma ukitaka kuona utukufu wa mwenyezi Mungu basi kuwa Mwalimu maana katika ualimu unafundisha utukufu na ufalme wa Mwenyezi Mungu kwa vijana*" alisisitiza Mhe Dkt Jafo,


Nae kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Kisarawe Mhe FATMA NYANGASA akizungumza katika mafunzo hayo aliwatoa hofu na mashaka walimu kwa kuwaambia Kuwa serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt Samia ni sikivu,


*"Ndugu Walimu tumeyasikia yote yaliosomwa katika Risala na Katibu wenu mengi serikali inayafanyia kazi na mengine yameshafanyiwa kazi hivyo tumuombe Dua Rais wetu apate afya njema na nguvu katika kutatua Changamoto za Watumishi wakiwemo Walimu alisisitiza Mhe Nyangasa,*"


Mafunzo haya kwa Walimu wanawake wote wa Kisarawe yameratibiwa na Chama Cha Walimu Kisarawe kwa Ufadhili wa taasisi mbalimbali za Kisarawe ambapo wameweza kutoa mafunzo katika afya ya akili,ujasiriamali Nk kwa walimua hao zaidi ya mia Tano. 


Wednesday, October 18, 2023

BUKOBA: MTU MMOJA AFARIKI NA NYUMBA 100 ZAEZULIWA MAPAA KWA UPEPO.

 

NA Alodia Babara, Bukoba. 


Mvua kubwa iliyonyesha ikiwa imeambatana na upepo mkali katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera imesababisha kifo cha mtu mmoja huku nyumba zaidi ya 100 zikiezuliwa na upepo kutokana na mvua na upepo mkali.


Maafa hayo yametokea Oktoba 18,mwaka huu saa 11 alfajiri, na kata ambazo zimekumbwa na maafa hayo ni Kashai, Rwamishenye na Hamugembe.


Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima amesema mtu mmoja ambaye amepoteza maisha hajafahamika majina yake na mwili wake ulionekana kuwa ulikuwa umesombwa na maji na ulikuwa haujatambuliwa.

 

"Maafa yamesababisha kifo cha mtu mmoja ambaye mwili wake ulipokutwa ulikuwa umeletwa na maji na katika paji la uso wake alikuwa na jeraha kama alipigwa na mti au kitu, jeshi la polisi linafanya uchunguzi juu ya kifo hicho" amesema Sima.


Siima amesema miongoni mwa nyumba zaidi ya 100 zilizokumbwa na maafa zimo taasisi za serikali kama shule na kituo cha afya pamoja na kanisa na nguzo za umeme na miti pia vimeathirika.


Aidha amewataka wananchi mkoani Kagera kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ili kuepukana na madhara.


Diwani wa kata ya Rwamishenyi Sued Kagasheki amesema, akiwa anajiandaa kwenda mazoezini asubuhi ametoka nje na kuona mvua kubwa inataka kuanza kunyesha alirudi ndani na muda mfupi mvua ilianza kunyesha ulipopita muda mfupi kama dakika 20 ameanza kupokea simu kutoka kwa wananchi wakimweleza juu ya majanga yaliyotokea.


Ametaja mitaa iliyoathirika kuwa ni mitatu kati ya minne ambayo ni Kamizilente, National housing na Rwamishenye.


Aidha mmoja wa mashuhuda padre Egidius Rweyemamu wa parokia Rwamishenyi kanisa katoliki amesema kuwa majira ya asubuhi akiwa kanisani anasali alishuhudia kanisa la Rwamishenyi likiezuliwa na upepo na waaumini watatu wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini. 



Tuesday, October 17, 2023

SERIKALI YAHIMIZA UCHUMI WA KIDIGITALI KWA WANAWAKE NA VIJANA.

Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele (katikati) akifuatilia mada mbalimbali   katika siku ya kwanza ya Kongamano la Tehama iliyogusa zaidi wanawake na vijana. Anayefuatia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Tehama, Profesa Leonard Mselle na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dkt. NKUNDWE MWASAGA jana kwenye Ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam. Kongamano hilo linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, NAPE NNAUYE


Dkt. NKUNDWE MWASAGA, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA


.........................................

 Na Mwandishi Wetu


Serikali imehimiza kuongeza nguvu katika uchumi wa kidigitali kwa wanawake na vijana ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.

Hiyo ni kutokana kuwa wanawake na vijana ni msingi na chachu ya mabadiliko wa masuala yote ya kiuchumi na kijamii, hivyo serikali imetaka wadau wote kushirikiana kuwezesha makundi hayo kuchangamkia fursa zinazoambatana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). 

Aidha imesisitizwa kwamba kundi hilo lenye nafasi ya kipekee katika kuelimisha umma juu ya teknolojia mpya za kidijitali, matumizi salama na yenye tija ya TEHAMA ili kuwesha uchumi wa kidijitali ulio shirikishi, yaani “inclusive digital economy” ni lazima liandaliwe kuwa na kasi ya matumizi ya Teknolojia za kidijitali. 

Kauli hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Selestine Kakele akifungua Mkutano wa wanawake kwenye Kongamano la Saba la Tehama Tanzania jana lililoandaliwa na Tume ya Tehama chini ya uongozi wa Dkt Nkundwe Mwasaga.

“Serikali, kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inapenda kuwashukuru wadau wote wa maendeleo ya TEHAMA katika kulitambua kundi hili muhimu na kuendelea kuwezesha wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazoambatana na TEHAMA. “ alisema.

Alisema serikali imeweka mazingira rafiki ya kukuza na kuibua ubunifu, kuchochea uwekezaji na uendelezaji wa Teknolojia za kisasa na TEHEMA kwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.:
Aidha alisema nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali, inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide). Aidha, nguzo hii inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mtu pasipokujali hali yake au sehemu anayotoka anashiriki na kufaidika na uchumi wa kidigitali.

“Mtakubaliana nami kwamba ili maendeleo yaweze kuwa na maana hayana budi kufangamanishwa moja kwa moja na watu. Aidha, kigezo muhimu cha watu, ni kufikiwa kwa makundi yote katika jamii pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Katika muktadha huu, ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu, matumizi ya TEHAMA kama nyenzo wezeshi hayana budi kufikia makundi yote katika jamii.” alisema.

Naibu Katibu mkuu huyo alitoa rai kwa wanawake kutumia jukwaa hili na fursa hii, kupaza sauti zao na kupitia sauti hizo kama taifa tuweze kujadiliana kuhusu vikwazo vinavyowakabili wanawake na kufanya washindwe kuchangamkia matumizi ya Teknolojia na TEHAMA kwa ujumla katika shughuli zao za kila siku. Aidha katika matumizi hayo alisema kwamba wanawake na vijana wana nafasi maalumu ya kuongoza harakati za kupinga matumizi mabaya ya TEHAMA. 

“Sisi kama Wizara yenye dhamana ya TEHEMA hapa nchini, tungependa kusikia sauti zenu, mkielezea fursa zilizopo na changamoto za matumizi ya TEHEMA. Aidha, tutafurahi kusikia kuhusu mawazo yenu, maoni yenu na matarajio yenu kwa serikali juu ya nini kifanyike ili kuendelea kujenga mazingira mazuri na rafiki kwa wanawake kufikia na kutumia teknolojia zinazoibukia,” alisema.

Nguzo ya uchumi jumuishi wa kidigitali, inakusudia kupunguza na hatimae kuondoa kabisa pengo baina ya watu wanaofikia na kutumia huduma za kidigitali na wasiopata fursa hiyo (digital divide). Aidha, nguzo hii inaweka msingi wa kushughulikia vikwazo vya kupata fursa ya kupata elimu na mafunzo ya TEHAMA kwa jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mtu pasipokujali hali yake au sehemu anayotoka anashiriki na kufaidika na uchumi wa kidigitali.

“Wakati tukiendelea kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa TEHAMA nchini, ni vema tukashirikiana pamoja kutatua changamoto zinajitokeza kwa wakati. Tuhakikishe tunatoa elimu kwa umma juu ya matumizi salama ya TEHAMA pamoja na kujikinga na matumizi mabaya ya TEHAMA ili kujipatia maendeleo. “ alisema. 


Saturday, October 14, 2023

SERIKALI PWANI YATOA SIKU 14 KUKAMATWA VIGOGO WA UTAPELI.

 

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

SERIKALI mkoani Pwani, imetoa wiki mbili kukamatwa viongozi 24 ambao ni vinara wa utapeli ikiwemo mabalozi, wenyeviti wa Mitaa, na watendaji walioshirikiana kuuza maeneo katika shamba namba 34 ambalo ni mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mitamba kata ya Pangani,Kibaha Mjini mkoani Pwani.


Aidha amewaagiza wataalamu wa Halmashauri ya Kibaha Mjini kupima na kuweka alama eneo hilo ndani ya siku 60.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa shamba la Mitamba Kibaha ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) .


Akitoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo alimuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani pamoja na Kamanda wa TAKUKURU Pwani kuwahoji watu hao na endapo watabainika kuhusika kuwa sehemu ya kutapeli wananchi sheria ichukue mkondo wake.


‘”Ninayo majina 24 ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia wananchi eneo hilo la shamba namba 34 kinyemela, wahojiwe na sheria ichukue mkondo wake,” Na nyie wananchi wenzangu mliouziwa viwanja katika eneo hili fungueni kesi dhidi ya waliowauzia na serikali itatoa ushirikiano” alifafanua Kunenge.

"Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha nakupa siku 60 anzeni kutekeleza maagizo kwa kupanga mji , baada ya hapo ambao watakuwa nje ya eneo la makazi watatakiwa kupisha ” aliongeza Kunenge.

Kunenge pia aliwataka wananchi walioendeleza maeneo yao katika kiwanja namba 34 kuondoa maendelezo yao ndani ya siku 14.


Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, alieleza kiwanja hicho kimepimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.

Awali Mwenyekiti Mtaa wa Lumumba, Gideon Tairo, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati wataalam watakapofika kupima eneo hilo.


Maagizo mengine ni Mkurugenzi na Wataalamu wa Mji ,kuhakikisha wanafanyia kazi upimaji wa awali ili kuonyesha maeneo ya kiwanja namba 34, maeneo ya Taasisi kazi ambayo inatakiwa kufanyika kabla ya kuwaondosha waliovamia.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa shamba la hekta 4,000 na Wizara ilikubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kiasi cha hekta 2,963 bila malipo yeyote na Wizara ikabaki na hetka 1,037. Pamoja na kugawa eneo hilo bado kuna watu wamevamia kile kipande kidogo kilichobaki.