Monday, October 2, 2023

JAJI MKUU: MAJAJI WAPYA MTAPIMWA KWA KUSHUGHULIKIA MAJALADA YA MASHAURI

 

NA MWANDISHI WETU, LUSHOTO.


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaambia Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa ufanisi wao na utendaji wao wa kazi utapimwa kwa jinsi watakavyokuwa wanashughulikia majalada ya mashauri Mahakamani mara baada ya kuanza kazi hiyo mpya ya Ujaji.


Mhe. Prof. Juma amesema hayo leo tarehe 02/10/2023 wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wanne wa Mahakama ya Rufani na 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayofayika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wilayani Lushoto mkoani Tanga.


Mafunzo hayo ambayo kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yatachukua wiki moja na kwa Majaji wa Mahakama Kuu wiki tatu, yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA.


“Uwezo wako katika utoaji wa huduma utapimwa kila siku utakapoingia Mahakamani, na kwa kila jalada utakalolisimamia na kila utakalofanya na kusema litapimwa…viongozi wako watakupima, wananchi na wadau watakaofika mbele yako watakupima na kutoa tathmini juu ya utendaji wako,” amesema Jaji Mkuu.


Aidha Mhe. Prof. Juma amewataka Majaji hao kuishi maisha ya kawaida na kutotumia nafasi zao kwa ajili ya manufaa binafsi na amewakumbusha kujitayarisha kutoa huduma kwa njia ya kidigitali akisema kuwa kwa sasa mhimili wa Mahakama hautarudi nyuma kwenye matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).


Washiriki wa mafunzo hayo watapitishwa katika mada mbalimbali ambazo zitawasilishwa na wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania, Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi.


Nae Jaji Kiongozi Mhe. Mustapher Siyani akitoa neno la shukrani amewaambia Majaji hao kuwa Mahakama na wananchi wana matarajio makubwa kwao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi na kasi kubwa mara baada ya kumaliza mafunzo yao.


 “Tuna matarajio makubwa kuwa mara baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtashuka kwenye vituo mlivyopangiwa mkiwa mnakimbia kama askari mpya, mfahamu sisi sote na watanzania kwa ujumla tunawasubiri kwa hamu kubwa utendaji kazi wenu,” amesema Mhe. Jaji Siyani.


Awali akitoa neno la ukaribisho, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul F. Kihwelo amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajenga Majaji hao katika kazi yao mpya ya Ujaji na kwamba mada zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki.


“Mada za mafunzo hayo zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki na kutimiza malengo ya Mahakama na taifa kwa ujumla ,” na kuongeza,


“Mafunzo haya yatawajenga Majaji kwa ajili ya leo na kwa ajili ya Mahakama ya kesho kwenye kazi yao hiyo mpya ya Ujaji.”


Majaji hao wapya waliteuliwa na Rais wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo tarehe 03/09/2023 na kuapishwa tarehe 14/09/2023 Ikulu jijini Dar es Salaam. 


Kuteuliwa na kuapishwa kwa Majaji hao wapya kunaongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kufikia 30 na wa Mahakama Kuu kuwa jumla ya 105.


Ufunguzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wasajili wa ngazi mbalimbali za Mahakama ya Tanzania, na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma.


Aidha, mafunzo hayo elekezi ya awali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha IJA wa mwaka 2023/24-2027/28.

 








WAZIRI MKUU ATOA MIEZI MITATU KWA WAKUU WA MIKOA.

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.


Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Viongozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi waimarishe huduma za uwezeshaji ili waweze kuyafikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.


Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Oktoba 2, 2023) wakati akifunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. “Suala la kuanzisha vituo vya uwezeshaji ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 katika Ibara ya 26 (k) na hili ni jukumu letu viongozi kuhakiksha ilani inatekelezwa.”


Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe wanaimarisha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ambazo zitawaongezea kipato.


“Katika hili ninawapongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuwezesha Jukwaa la Mkoa kuanzisha SACCOs 76 za wanawake zenye wanachama 322 pamoja na Halmashauri ya Ushetu ambayo imeanzisha Jukwaa linaloendesha Mradi wa Kampuni ya Usafi wa Mazingira na usindikaji wa mboga za majani maarufu kwa jina la Nsansa.”


Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa alisema kongamano hilo linalenga kuongeza ufahamu wa wadau mbalimbali kuhusu dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuwakumbusha majukumu waliyonayo katika kuwawezesha Watanzania.


Alisema malengo mengine ni pamoja na wadau kupeana uzoefu katika kutekeleza shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuzindua taarifa ya mwaka 2022/2023 ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo pia imejumuisha masuala ya ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.


Katibu Mtendaji huyo alitaja kaulimbiu ya kongamano hilo kuwa ni “Uwezeshaji kwa Uchumi Endelevu”. “Kaulimbiu hii inaendana na azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watanzania wanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi ili kuweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.”


Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023, mifuko na programu za uwezeshaji ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 743.7 kwa wanufaika wapatao 6,064,957 ambapo miongoni mwao wanaume ni asilimia 46 na wanawake asilimia 54. 






DKT MSAMBICHAKA AWAFUNDA WAZAZI MORO

 

Na Mwandishi wetu- Morogoro.


KATIBU Mkuu wa taasisi ya Tawheed Development Network ya jijini Dar es Salaam Dkt Badria Msambichaka ameitaka jamii kuwasaidia watoto kuchunga maadili wanayofundishwa shuleni hasa wakati huu wanaposubiri matokeo ya mitihani ya kumaliza darasa la saba.


Wito huo ameutoa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Morogoro wakati alipozungumza na wazazi katika hafla ya mahafali ya sita ya shule ya msingi Eastern Arc.


Mbali na hilo Dkt Msambichaka ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa juhudi kubwa wanayoichukua ya kuwafundisha watoto masomo ya sayansi, lugha na maadili katika kiwango asichokitarajia.


Aidha Dkt Msambichaka amewakumbusha wanaume jukumu lao kuu la kuisimamia familia kwenye eneo la malezi ili kupata jamii bora iliyojengeka vema kimaadili.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo iliyopata usajili wake mwaka 2017 Bwana Khalid Mfinanga amemshukuru Dkt Msambichaka kwa kuitikia ombi lao la kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo pamoja na kuwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kujitoa kwao licha ya malipo madogo wanayopata.


Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa Easten Arc Pre and Primary School bwana Idd Jengo alitaja nyezo tano ambazo zinatumika katika kujenga na kuimarisha tabia ya mtoto.


Jengo ambaye ni Afisa Mitihani Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, alitaja nyezo hizo kuwa ni Malezi, Mazingira, Teknolojia, Ujasiri na Umahiri, huku akiwataka wazazi wenzake na jamii kwa ujumla kuwa makini katika kuwajenga watoto kitabia.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya wazazi wa shule hiyo Bwana Nuru Said Mohamed alimuomba Dkt Msambichaka kuzichukua changamoto za shule hiyo kama fursa kwake ya kujijengea pepo ya Mwenyezimungu kwa kuzifanyia kazi yeye binafsi na hata kwa rafiki zake.


Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo Mwalimu Ismail Said Ahmad, katika kipindi chote cha miaka mitano tokea watoe wanafunzi wa darasa la saba, hakujawahi kufeli hata mwanafunzi mmoja.


Easten Arc Pre and Primary School ilifaulisha wanafunzi wote 12 mwaka 2018, wanafuzi wote 18 wa mwaka 2019, tulifaulisha wanafunzi wote 24 mwaka 2020, wanafunzi wote 26 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2021, wanafunzi 31 pia walifaulu wote katika mwaka 2022 na mwaka huu tunatarajia wanafunzi wote 38 watafaulu, alisema Mwalimu Ahmad. 


RAIS SAMIA AMTEUA MATINYI KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI.

 



Sunday, October 1, 2023

TAWA KUJA NA MKAKATI MPYA WA KUONGEZA MAPATO

 



Na Beatus Maganja, ARUSHA.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaandaa mkakati mpya wa ukusanyaji mapato utakaolenga kuongeza mapato ya Taasisi hiyo mara dufu ya makisio yake ya Mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yamesemwa Leo Oktoba 1, 2023 na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda, katika kikao kazi na wakuu wa Kanda na wakuu wa mapori wa TAWA chenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika nyanja za kuongeza mapato na Uhifadhi kwa ujumla, kilichofanyika ukumbi wa NCAA Jijini Arusha

Kamishna Mabula amesema suala la kuongeza Kasi ya ukusanyaji mapato ni maelekezo mahsusi kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki na hivyo utekelezaji wake unapaswa kuanza haraka iwezekanavyo

"Hili suala la ukusanyaji mapato lisisubiri huo mkakati unaoandaliwa lianze Kuanzia Sasa hivi, Kila kitu unachokiona kwenye eneo lako ni rasilimali hakikisha unakitumia kuingiza mapato" amesisitiza Kamishna Mabula

Kamishna Mabula pia ametoa msisitizo katika suala zima la udhibiti wa Wanyamapori wakali na waharibifu na kuwataka maofisa hao kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha Wanyamapori hao hawaendelei kuleta madhara kwa maisha na mali za binadamu.

Aidha, amewataka maofisa hao kuzingatia maelekezo aliyoyatoa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili Kamishna Benedict Wakulyamba wakati wa semina elekezi kuhusiana na Wanyama Wakali na Waharibifu

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange amesema mtaji namba moja wa TAWA ni ulinzi wa maeneo yote waliyopewa kuyasimamia kwani maeneo yanapokuwa salama ndipo uzalishaji mapato unaongezeka ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya TAWA yanatokana na shughuli za Uwindaji wa Kitalii

Sanjari na hilo, amesisitiza kuongeza Kasi ya utekelezaji wa zoezi la kuweka alama za mipaka katika maeneo yote yaliyo chini ya Usimamizi wa Taasisi huku wakifuata miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali 













MADIWANI LINDI WAKANUSHA KUMKATAA MEYA.


Na Mwandishi wetu.

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi wameshangazwa na waraka uliotumwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ukidai hauna imani na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Frank Magali wakisema hawautambui na saini zinazoonekana humo hazikuwekwa kwa malengo hayo.


Wakizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hizi, baadhi ya madiwani hao wameonesha
kushangazwa kwao na madai hayo waliyoyaita ni ya uzushi unaosukumwa na
tamaa ya madaraka zaidi kuliko wanachokidai.

Waraka huo wa Septemba 26/2023 ambao  nakala yake tunayo ulikuwa na kichwa kisomekacho “Kutokuwa na imani na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mh.Frank R. Magali”.


Juma Lunda diwani wa Makonde Manispaa ya Lindi alisema licha ya jina lake kuorodheshwa kwenye waraka huo wa kumkataa Meya, lakini hana taarifa zozote za kina juu ya sababu za kufikia hatua hiyo.


“Sikiliza mwandishi, ninachokiona mimi ni kwamba, kuna badhi ya
madiwani walitumia fedha nyingi katika uchaguzi uliopita wakiwinda
nafasi ya U-Meya na wakaikosa, sasa wanachofanya ni kutapatapa tu,
maana kama huo mkopo waliousema, hakuna diwani asiyejua maana sisi
kamati ya Fedha tulihusika kwaniaba ya Madiwani” alisema Lunda ambaye
pia ni mjumbe wa kamati ya Fedha ya Manispaa ya Lindi.

Naye diwani wa Kata ya Rasibula bwana Abdallah Kikwei akizungumza na
Mwandishi wa habari hizi alisema Naibu Meya wa Manispaa hiyo Salum Ng’ondo ndiye kinara wa harakati hizo akidaiwa kumsaidia kigogo mmoja kuusaka Ubunge
jimbo la Lindi mjini.

Ng’ondo amekiri kuongoza kikosi cha madiwani na kuandika barua hiyo
wakimtaka Meya huyo kujiuzulu kwa madai ya kukiuka  kanuni mbalimbali
za uendeshaji wa Manispaa ya Lindi.

Kwa upande wake Meya Magali alisema madai hayo si ya kweli bali
yanachochewa na baadhi ya madiwani wanaotumika na wanasiasa wasio na
huruma na wanachi wa Lindi.

“Madiwani wetu wanahitaji ziara ya mafunzo (Tour), na katika vikao vyetu tulikubaliana bajeti ya shilingi Milioni 16, lakini madiwani wakaja na pendekezo la kwenda Dodoma, Bwawa la Mwalimu Nyerere na Ngorongoro ambako bajeti yake ni zaidi ya sh. Milioni 90.


“Nikawauliza pesa hizi zote haziwezi kutumika kutatua baadhi ya changamoto za wanachi kwenye kata zetu? Na je, Mkuu wa mkoa anaweza kuidhinisha matumizi haya makubwa ya fedha kwa ajili ya kutembea
tu”,alisema Magali.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Juma Mnwele licha
ya kukiri kupokea barua hiyo ambayo haikusainiwa, alisema ameshaijibu na kuwakabidhi wahusika na kuwataka wazingatie kanuni za kudumu za Halmashauri katika mchakato wa kumuondoa Meya na wala si kwa utaratibu huo waliofanya.

“Kuhusu Mkopo, Halmashauri ilipata Mkopo wa Mzunguko kwa Halmashauri
zote nchini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
tarehe 10.6.2023 pamoja na Halmashauri zingine za Kigamboni Chamwino
Kishapu na Maswa, hafla ilifanyika Dodoma chini ya Tamisemi na Ardhi”,alisema Mnwele na kuongeza.

“.Madai ya  bei ya viwanja vimewekwa na kuridhiwa na baraza la Madiwani, Kuhusu vikao, vikao vya Halmashauri huendeshwa kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Halmashauri za mwaka 2014 kifungu 42(1) cha sheria za serikali za mitaa (mamlaka za miji) sura 288. Hakuna ukiukwaji wa kanuni uliotajwa wowote uliofanyika kwenye eneo hilo.


“Kikao cha Mkutano wa Mwaka kinatekelezwa ipasavyo kwa vile mambo na
hadidurejea zote zilizoainishwa kwenye kanuni hiyo vinatekelezwa bila
dosari yoyote”.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lindi bwana Bakari Bwatamu alisema
haamini kama walioandika barua hiyo kwa Mkurugenzi ni madiwani wa
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wanaotokana na CCM.

“Awali barua yenye saini kama hizo waliileta kwetu chama wakidai wanahitaji kukutana na Mkurugenzi. Sasa tena tunaona barua ileile yenye saini za watu walewale inaelekezwa kwa Mkurugenzi wakidai hawana imani na Meya”


Kwa muda mrefu madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi yenye majimbo ya Lindi na Mchinga wamekuwa katika misuguano na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo kwa upande mmoja na Mkurugenzi wake kwa upande
mwingine wakidai kupunjwa posho na marupurupu mengine.

VIONGOZI WA DINI WAHAMASISHENI VIJANA KUFANYA KAZI KWA WELEDI-MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa staha, weledi na uadilifu ili kuzitumia rasilimali zilizopo nchini kujiletea maendeleo.

 

“Nchi yetu imebarikiwa fursa nyingi za kiuchumi, ili jamii ione matunda ya uwepo wa fursa hizo tunategemea sana nguvu kazi ya vijana katika kuzitumia rasilimali zilizopo”

 

Ametoa wito huo leo Jumapili (Oktoba 01, 2023) wakati wa Jubilei ya miaka 125 ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, kwenye kilima cha Peramiho, Songea mkoani Ruvuma.

 

Aidha, amezisihi Taasisi za dini kuweka mipango mahsusi na shirikishi ya malezi ya vijana. “Tumieni nafasi zenu kuongeza msukumo wa malezi kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwafuatilia kwa karibu na kuhimiza ushiriki wao kwenye vyama vya kitume”

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa masuala ya kipaumbele yanayohusu ustawi wa Taifa. 

 

“Niwasihi sana mtuunge mkono kuhamasisha uhifadhi wa mzingira na matumizi ya nishati safi, kampeni za kupanda miti na usafi wa mazingira, kukemea vikali vitendo vya mmomonyoko wa maadili, matumizi ya madawa ya kulevya na kukemea vitendo vya rushwa”

 

Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyapongeza madhehebu ya dini kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye sekta za elimu, afya, maji na huduma nyingine za kijamii hasa katika maeneo ya pembezoni.

 

“Kazi hiyo mnayoifanya ya kutoa huduma kwa jamii ni kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kusogeza huduma zote muhimu karibu na wananchi”

 

Katika Jubilei hiyo, Rais Dkt. Samia ametoa shilingi milioni kumi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 125 ya jubilei ya Uinjilishaji katika jimbo kuu Katoliki la Songea.

 

Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Damian Dallu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli mbalimbali za huduma za jamii na uinjilishaji zinazofanywa na kanisa katoliki nchini. 

SERIKALI YAANZA KUFANYIA KAZI MAPENDEKEZO 25 YA WAFANYABIASHARA - MAJALIWA

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeanza kufanyia kazi mapendekezo 25 ya Kamati Maalum ya Serikali na Wafanyabiashara iliyoundwa kufuatia mgomo wa wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Kariakoo.


 


Amesema kuwa Serikali imeyagawa mapendekezo hayo katika makundi ya utatuzi wa haraka makundi ya utatuzi wa kisera na makundi ambayo utatuzi wake unahitaji sheria.


 


Amesema hayo Jumamosi Septemba 30, 2023 wakati wa kilele cha Maonesho ya Juma la Utalii na Uchumi wa Bluu (Mafia Island Festival), yaliyofanyika Mafia mkoani Pwani.


 


“Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya haya ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara”


 


Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya kupitia kamati za mapato za wilaya wakutane na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wa Idara ya Mapato kwenye Halmashauri ili kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya biashara na kuhakikisha risiti za EFD zinazotumika ni zile zinazotokana mashine zilizothibitishwa na kusajiliwa.


 


“Ni muhimu kila kiongozi anayehusika ashiriki katika kuhamasisha matumizi ya mashine za EFD na kufuatilia hali ya utoaji wa risiti kwa nidhamu kubwa bila kusababisha usumbufu na kero kwa wafanya biashara."

WAZIRI MKUU, MAJALIWA AMPA RUNGU RC PWANI KUNYANG'ANYA VIWANJA VILIVYOMILIKIWA NA WAWEKEZAJI KWA MUDA MREFU BILA KUENDELEZWA.

 

Na Scolastica Msewa, Mafia.


Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassimu Majaliwa amempa rungu Mkuu wa mkoa wa Pwani Mheshimiwa Abubakari Kunenge kunyang'anya Visiwa na viwanja uwekezaji wa Utalii Wilayani Mafia vilivyong'ang'aniwa na wawekezaji miaka mingi bila kuendelezwa kwa kutofanya chochote ili vigawiwe kwa wawekezaji wengine.


Amesema hayo wakati akifunga siku tatu za maonyesho ya uwekezaji wa katika uchumi wa buluu na kutangaza Utalii mazao ya bahari katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua hizo zifanyike kwa kuzingatia taratibu na Sheria za nchi kwani muda wa mwekezaji kumiliki eneo la uwekezaji bila kuendeleza ni miezi 36. "Kweli nyinyi mnawaacha tu? Sheria sizipo? Watu wa ardhi simpo?"


Amesema "Mkuu wa mkoa uwekezaji katika viwanja ni miezi 36 hujaendeleza nyang'anya chukua tunampa mtu mwingine".


"Na nyinyi Wakuu wa Wilaya wengine mwende mkaainishe maeneo ya fulsa za uwekezaji wa Utalii mliyonayo yaliyoshikiriwa na wawekezaji kwa miaka mingi hayana kazi yoyote wala bila kuendelezwa kwani sisi tunatangaza fulsa za uwekezaji wa Utalii miaka kumi bila uendelezwaji wowote nyang"anya kwa mujibu wa sheria maana Sheria tunazo ili tukabidhi kwa wawekezaji wengine wawekeze"

 

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa ukiona kuna mwekezaji anamiliki kisiwa bila kuendeleza nyang'anya Sheria tunazo, watu wa ardhi mpo, hujaendeleza tunachukua tunampa mwekezaji mwingine.


"Tunatangaza fulsa, tunaita Watalii, tunaita wawekezaji halafu Kuna mtu anamiliki bila kuendeleza nyang'anya tukabidhi wengine wawekeze hayo ndio maelekezo yangu" 





MAGAZETI YA LEO TAREHE 01 OKTOBA 2023.