Rais mstaafu
wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza waandaaji wa Tamasha
la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni kwa
kuweka utaratibu wa kuwatembeza wageni kwenye vivutio mbalimbali ikiwemo historia ya mji wa Bagamoyo.
Dkt. Jakaya
alitoa pongezi hizo wakati wa kufunga Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na
utamaduni Tarehe 30 Oktoba 2021, katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambapo alisema historia ya Bagamoyo ni kubwa sana
na wananchi wa ndani na nje ya Bagamoyo, na wageni kutoka nje ya nchi wanapaswa kuijua
historia hiyo.
Alisema
kutokana na umuhimu wa historia ya Bagamoyo, imempelekea Rais Samia Suluhu
Hassan kufika Bagamoyo wakati wa maandalizi ya filamu ya Royal tour na kwamba
hiyo ni heshima kubwa kwa Bagamoyo ambapo wizara husika inapaswa kuendelea
kuielezea historia ya Bagamoyo kwa wageni.
Aliongeza kwa
kusema kuwa, ili wageni waweze kuvutiwa kusikiliza na kuelewa historia hiyo, ni
vyema wakapatikana watembeza watalii wenye uwezo wa kuelezea historia halisi ya
Bagamoyo yenye kueleweka kwakuwa maelezo mazuri yanamvutia msikilizaji na
kupata hamu kutaka kujua zaidi.
Aidha,
alipongeza maandalizi yaliyofanyika katika Tamasha hilo la 40 kwa namna
lilivyofana kwa kuwakusanya wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
ambapo kila mmoja alionyesha uwezo wake jukwaani huku wahudhuriaji wakiwa na
furaha kutokana na burudani zilizokuwa zikitolewa.
Alisema
katika nchi yetu swala la utamaduni ni muhimu sana kwakuwa linawarudisha
watanzania kwenye burudani zao za asili na kwamba siku zote anaekataa asili
yake ni mtumwa.
Aliendelea
kusema kuwa, kutokana na umuhimu huo ndiomana seikali ya Tanzania kuanzia awamu
ya kwanza hadi sasa wizara ya utamaduni ilikuwepo na bado ipo ili watanzania
waone umuhimu wa kutunza utamaduni wao.
Alisema
utamaduni ni kielelezo cha utashi na uhai wa Tanzania hivyo kila panapofanyika
Tamasha watanzania wanaendelea kukumbushana na kusisitiza umuhimu wa utamaduni
katika jamii yetu na Taifa kwa ujumla.
Alisema Rais
Samia ameendelea kutambua na kusisitiza umuhimu wa utamaduni kwakuwa utamaduni
unabeba ujumbe halisi wa jamii husika kwa kipindi hicho.
Rais mstaafu
wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, (katikati) Naibu waziri wa
Utamaduni , Sanaa na Michezo, Pauline Philipo Gekul,
(kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge (kulia) wakiangalia
vikundi vya sanaa wakati wa kufunga Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na
utamaduni lilifanyika katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo
(TaSUBa) Tarehe 30 Oktoba 2021.