Thursday, November 14, 2019

TRA YAHIMIZA WANANCHI KUCHUKUA RISITI WANAPOHUDUMIWA.

Na Shushu Joel

MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) imewataka wananchi kujenga utamaduni wa kuchukua risiti kwa kila manunuzi wanayofanya kwa kuwa kutokuchukua risiti ni kosa kisheria.

Akizungumza na baadhi ya wateja katika moja ya vituo vya mafuta vilivyoko wilaya ya Kibiti mkoani Pwani Mkurugenzi wa huduma ya elimu kwa walipa Kodi Richard Kayombo alisema kuwa wananchi walio wengi hawachukui risti zao mara baada ya kuhudumiwa.

Alisema kuwa kitendo wanachokifanya ni hasara kwao kwani inaweza ikatokea kitu kibaya katika biashara hiyo huku risiti uliacha kwenye kituo cha mafuta hivyo msaada wako utakuwa ni mdogo sana ukilinganisha na ukiwa na risti.

"Nasikitika sana kuona kuna ndoo iliyojaa risti zilizoachwa na watu ambao wamehudumiwa mafuta, jamani risiti ni muhimu sana pia ni kosa kisheria kutokuchukua risiti yako"Alisema Kayombo.

Kayombo amesema kuwa Sheria ya usimamizi wa Kodi inatanabaisha kuwa mtu yoyote asiyechukua risiti anafanya kosa kisheria na anaweza kutozwa faini kuanzia shilingi 30,000 hadi 1.5ml au kwenda jela kifungo kisichozidi mwaka mmoja.

"Sheria iko wazi kabisa lakini TRA tunawasisitiza wateja wote kudai na kuchukua risiti kila wanaponunua bidhaa au kupata huduma", alisema.

Aidha aliongeza kuwa mamlaka ya mapatoTanzania imeanzisha mfumo wa utoaji wa elimu kwa mikoa miwili miwili ingawa kwa sasa tumeanza na mkoa wa Morogoro na Pwani kisha baada ya hapo tutaenda mikoa mingine miwili kwa lengo la kuwaelimisha wananchi.

Mbali na hilo Kayombo amewasisitiza wananchi wote kulipa kodi ya majengo mapema ili kuondoa usumbufu wa mwisho wa mwaka kama walivyozoea.

"Wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kuelewa ni kwanini wanasisitizwa kulipa kodi, jamani Kodi ndio zinaleta maendeleo nchini hivyo mkilipa kwa uaminifu maendeleo makubwa mtayaona "Alisema.

Pia amempongeza Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kupeleka maendeleo makubwa sehemu mbalimbali kwa kusudi la wananchi kutambua thamani ya Kodi zao wanazolipa.

Naye Juma Ally mkazi wa kibiti amewapongeza TRA kwa kujitoa kwa wananchi katika kuwaelisha juu ya masuala ya kulipa kodi.

Aliongeza kuwa wananchi mnapaswa mjitokeze kwa wingi ili muweze kuvuna elimu hii maana ni ya muhimu sana kutambua kiwango chako cha ulipaji Kodi.

Kwa upande wake Fatma Hamadi ni mmoja wa wafanyabiashara wa duka katika wilaya ya Kibiti ameipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli kwa usimamizi wake wa miradi kwa kuonyesha wananchi kile wanachokitoa kupitia TRA kukiona katika uhalisia.  

Aidha amiopongeza mamlaka ya mapato nchini TRA kwa elimu wanayoitoa kwa jamii.

NG'OMBE ZAIDI YA 9,000 WILAYANI LINDI KUOGESHWA KWENYE MAJOSHO NA KUPATIWA CHANJO YA MAGONJWA.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Jumla ya Ng'ombe 9774 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi (Mtama) Mkoani Lindi wanatarajia kupitishwa na Kuogeshwa katika majosho mbali mbali ya Wilaya hiyo kwa lengo la kupatiwa chanjo dhidi ya Magonjwa yaenezwayo na kupe (Ndigana kali).

Hayo yameelezwa na Daktari wa mifugo wa Halmashauri hiyo Dokta Joseph Sijapenda wakati wa uzinduzi wa zoezi la kuogesha Ng'ombe katika Josho la Gereza la kingurungundwa lililopo kata ya kitomanga Wilayani humo.

Katika uzinduzi huo jumla ya Ng'ombe 400 kutoka kata ya kitomanga na maeneo jirani ya wilaya hiyo walipatiwa chanjo dhidi ya Magonjwa yaenezwayo na kupe.

Akizungumza katika uzinduzi huo Sijapenda lisema kuwa Halmashauri yao imepokea jumla ya lita 54 za dawa kwa ajili ya kuwapatia Ng'ombe 9774 waliopo katika Wilaya hiyo ambapo lita 42 ni dawa aina ya mitraz na lita 12 aina ya palanents Huku akifafanua kuwa lengo kubwa la Serikali kuanzisha zoezi hilo ni kuhamasisha wafugaji kuogesha Mifugo yao ili kuwa na ufugaji wenye tija.

Hata hivyo Sijapenda aliongeza kuwa baada ya uzinduzi huo wafungaji watalazimika kuwapeleka Ng'ombe wao kila siku za juma mosi katika majosho yaliyo karibu nao kwa ajili ya kuogeshwa na kupatiwa kinga hiyo.

Nae mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na uvuvi kutoka kituo cha huduma na mifugo kanda ya kusini jostinian lutatina alisema kuwa Magonjwa ya yaenezwayo na kupe hususani Ndigana kali ni miongoni mwa changamoto kubwa katika maendeleo ya sekta ya Mifugo kwa kuwa yanasababisha vifo vingi vya mifugo hapa Nchini.

"hapo mwanzo uogeshwaji wa mifugo ulikuwa unagharamiwa na Serikali ambapo wafugaji walikuwa wanaogeshwa bure, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti na mabadiliko ya Sera gharama za uogeshwaji zilibaki kwa wafugaji wenyewe na matokeo yake wafugaji wengi walikosa mwamko wa kuogesha mifugo yao" alisema.

Hata hiyo lutatina alisema kuwa Viuwatilifu hivyo vilivyotolewa na Serikali vitatumika kama ruzuku ambapo wafugaji watalazimika kulipa shilingi mia sita 600 kwa ng'ombe mmoja kila anapokwenda kumpatia chanjo hiyo kwa kipindi cha miezi sita ili kiasi kitakachopatikana kiweze kununua dawa zingine.

Nae Mwenyekiti wa wafugaji kata ya kitomanga Ntima Ngusa aliishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku hiyo ya viuwatilifu kwani itapunguza gharama ya uendeshaji katika kuhudumia mifugo yao.

Ngusa alisema kuwa hapo awali walikuwa wanalazimika kutumia zaidi ya shilingi elfu mbili kwa ajili ya kununua dawa ya kuogesha Ng'ombe mmoja kwa siku.

Nae mkuu wa Wilaya ya Lindi ambae ndie aliekuwa Mgeni rasm katika uzinduzi huo aliwataka wafugaji kujitokeza kwa wingi siku zitakazopangwa kwa ajili ya kuwapatia chanjo mifugo yao Ili waweze kunusuru mifugo yao na magonjwa.

KIKWETE ATAKA WAZEE WAHUSISHWE KUTATUA MIGOGORO YA MIPAKA.

Na Shushu Joel

MBUNGE wa Jimbo la chalinze Mh Ridhiwani Kikwete ameitaka serikali kuwatumia wazee wa maeneo husika  ili kuondoa migogoro ya mipaka baina ya Kijiji na Kijiji au ile ya kata kwakuwa wao wameishi maeneo hayo kwa kipindi kirefu.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo la chalinze ambapo mbunge huyo alisisitiza kuwa endapo wazee wakipewa nafasi ya kutatua migogoro hiyo itabaki kuwa ni historia.

Aliongeza kuwa katika jimbo lake kuna changamoto ya uwepo kwa baadhi ya maeneo kuwa na matatizo hayo hivyo amewashauri wataalamu wa idara ya ardhi kuwatumia wazee wa maeneo husika ili wawape mwelekeo wa kujua jinsi ya kumaliza changamoto hizo.

"Nimefanya mikutano katika jimbo langu kwenye vijiji takribani vyote hivyo mimi kama mbunge nimeshauri kutumiwa kwa wazee ili kutatua changamoto hiyo"Alisema Kikwete.

Aidha aliongeza kuwa kitu kingine ambacho kimekuwa kikiwachanganya wananchi ni maamuzi yanayofanywa na wataalam katika utatuzi wa migogoro hiyo kwa wao kwenda kwenye maeneo na kuwahusisha watu ambao si sahihi.

Kwa upande wake mzee Said Lufunga (79) amempongeza mbunge huyo kwa kutambua changamoto za mipaka ambazo zimekuwa ni kero kubwa katika jamii.

"Ukimuona nyani kazeeka amekwepa mishale mingi hivyo aminini wazee ni kimbilio la matatizo yote" Alisema Lufunga.

Naye Bi, Amina Ramadhani(76) amesema kuwa migogoro inatengenezwa na wataalam kutokana na kutotaka kusikiliza wazawa kwani wao wamekuwa wakitumia vifaa vya kisasa tu.

Hivyo amemuomba mbunge Kikwete kuendelea kulipigia kelele Jambo hilo huenda mwafaka ukapatikana.

"Wazee kwa kushirikiana na viongozi wa dini wanaweza wakawa suluhiaho la hili Jambo katika halmashauri yetu ya chalinze " Alisema.

MASHUJAA FM LINDI WAKABIDHI VIFAA VYA KUHIFADHIA TAKA KWA DC WA LINDI.

 
Meneja wa Mashujaa FM Mkoa wa Lindi zakia Mdemu (kulia) akimkabidhi Mkuu wa wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga vifaa vya kuhifadhia taka katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za usafi wa mazingira.
.............................................

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kampuni ya mashujaa group kupitia kituo chao cha radio cha mashujaa FM mkoa wa Lindi imekabidhi vifaa vya kuwekea taka vyenye thamani ya Shilingi milioni 1.2 kwa Manispaa ya Lindi Mkoani humo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo meneja wa Mashujaa FM Mkoa wa Lindi zakia Mdemu alisema kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni kutaka kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Mkoa huo za kufanya mji huo kuwa msafi.

Zakia alisema wao kama Mashujaa FM moja ya matamanio yao ni kuona Manispaa ya Lindi kuwa ni miongoni mwa Manispaa na Wilaya zinazoongoza kwa usafi hapa nchini.

Alisema ili kutimiza azma hiyo Kampuni yao pamoja na kutoa vifaa hivyo vya kuhifadhia taka imejikita katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usafi wa mazingira katika maeneo yao.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga aliushukuru uongozi wa Mashujaa FM kwa kukubali ombi lao la kusaidia vifaa hivyo ambavyo vitakuwa chachu ya kuendeleza usafi wa Manispaa hiyo.

Alisema moja ya changamoto kubwa inayoikabili Manispaa hiyo ni kukosa vifaa maalumu vya kuhifadhia taka kwenye barabara za mitaa ambapo kwa kiasi kikubwa inachangia taka zinazozalishwa na watembea kwa miguu kuzagaa katika mitaa jambo ambalo licha ya kuwa ni hatari kwa afya za wananchi, lakini pia halileti taswira nzuri ya mji.

Hata hivyo Ndemanga alisema kuwa vifaa hivyo vitawekwa katika maeneo ya wazi hasa maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi na Hospitali ambapo kunamsongamano mkubwa wa watu ili taka watakazokuwa wanazizalisha waweze kuziweka katika vifaa hivyo.

Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Jomary Satura alisema kuwa vifaa hivyo vitaenda kupunguza changamoto ya uwepo wa vifaa vya kuhifadhia taka kwenye mitaa ambapo kwa sasa mahitaji ni 200 na zilizopo ni 38.

Hata hivyo Stura alitoa wito kwa Taasisi zingine zilizopo katika Manispaa hiyo kuunga mkono jitihada za kuweka mji safi zinazofanywa na Manispaa pamoja na Mkoa kwa ujumla kwa kununua vifaa mbali mbali vifaa vya kuhifadhia taka na vifaa vingine vya usafi wa mazingira.
 
Sehemu ya vifaa hivyo vya kuhifadhia taka vilivyotolewa na Kampuni ya mashujaa group kupitia kituo chao cha radio cha mashujaa FM mkoa wa Lindi kama vinavyoonekana katika picha.

PICHA ZOTE NA HADIJA HASSAN. 

KAMISHNA WA UHAMIAJI AWAONYA WAHAMIANJI HARAMU.

 
Kamishna wa uhamiaji Taifa Dr Anna Makakala, akizungumza na waandishi wa habari, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
........................................

Na Alodia Dominick.

Kamishna wa uhamiaji Taifa Dr Anna Makakala amesema kwa yeyote atakayekamatwa amemficha mhamiaji haramu atakumbwa na Kifungo cha miaka ishirini jela na kutozwa faini ya shilingi milioni 20.


Kauli hiyo ameitoa Novemba 13, mwaka huu wa 2019 akiwa mkoani Kagera katika ziara ya siku tatu inayolenga kuhakikisha vitendo vya wahamiaji haramu vinakomeshwa hasa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika nov 24 mwaka huu.


Alisema idara hiyo itahakikisha wahamiaji haramu hawavurugi uchaguzi huo na kuwa hawana nafasi kuingia nchini kiholela kwani tayari sheria kali zipo kwa ajiri ya kuwabana wahamiaji ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watu watakao vunja sheria za nchi kwa kuwaingiza watu ambao sio raia wa hapa nchini.


Dr Makakala amesema, wananchi wafahamu kuwa, wahamiaji haramu hawana nafasi ya kuingia na kupiga kura katika nchi ya Tanzania hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini nao kwa kutowakaribisha vinginevyo wafuate kanuni na sheria za kuingia nchini.


Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti amesema kwamba, mwaka jana wamezindua nyumba kumi za usalama lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kutokaribisha wageni wanaoingia nchini kihorela.


Brigedia Gaguti ametoa wito kwa wananchi kutowakumbatia wahamiaji haramu na badala yake waende kutoa taarifa pale wanapobaini wageni wasio halali kwenye maeneo yake.