Thursday, November 14, 2019

BRELA yataja mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli




Kaimu Afisa Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA Bw.Emmanuel Kakwezi akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa miaka minne iliyopita, katika kipindi ambacho Rais John pombe Magufuli amekuwa madarakani

Bw.Emmanuel Kakwezi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, Mkutano huo ulifanyika habari maelezo.

By Mwandishi wetu,

Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) imesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano  chini ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli wameweza kupata mafanikio mengi ikiwamo kutoa leseni na huduma zote za Brela kwa njia ya mtandao.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, Kaimu afisa Mtendaji Mkuu wa Brela Bw. Emamnuel Kakwezi amesema mbali na kufanikiwa kutoa huduma za Brela kwa njia ya mtandao pia, wa kushirikiana na COSTECH pamoja na shirika la miliki ubunifu duniani (WIPO) wameweza kutekeleza mradi wa upatikanaji wa taarifa za teknolojia zilizopo kwenye kanzidata za hataza (TISCs) kwa ajili ya kutumiwa na watafiti na watumiaji wengine, jumla ya hataza milioni sabini na sita (76,00,000) zinapatikana kwenye kanzidata husika.

Pia katika kipindi hicho, brela imeweza kuanzisha utoaji wa leseni za kundi A na kundi B kwa njia ya mtandao. Mfumo huo umeunganishwa na mifumo ya malipo ya serikali yaani Government electronic payment gateway (GEPG) na mfumo wa taarifa ya mapato wa mamlaka za serikali za mitaa yaani Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS).

Itakumbukwa kuwa majaribio ya mfumo huo ulianza rasmi October 1, 2019 na mpaka sasa leseni za Biashara Kundi A zilizotolewa na Brela na Leseni za Biashara kundi B katika Manispaa ya Bukoba, Chalinze,Wilaya ya Karagwe, Mji wa Mafinga, Manispaa za Ilala na halimashauri za Jiji la Mwanza zinatolewa kwa njia ya mtandao.

Akizungumzia takwimu katika utoaji leseni kwa mfumo wa mtandao toka Octoba 1, 2019, jumla ya leseni za biashara 1206 zimetolewa, kati ya hizo Brela imetoa leseni 470, Jiji la Mwanza leseni 199, na Manispaa ya Ilala leseni 537.

Pia brela imeweza kuanzisha dirisha la mfumo wa utoaji wa taarifa za kibiashara za Kimataifa, dirisha hilo linamuwezesha mtumiaji au muombaji kufahamu taarifa mbalimbali za upatikanaji wa leseni na vibali kwa bidhaa zinazouzwa nje na zinazoingizwa ndani ya nchi.

Dirisha hilo linatoa fursa kwa mwomabji kutembelea tovuti ya www.trade.business.go.tz na kupata taarifa zote za kibiashara zinazohusiana na uuzaji wa biashara nje ya nchi na ndani kwa ujumla wake (export and import process)

Kupitia dirisha hilo mtumiaji atafahamu sharia, kanuni, taratibu, muda utakaotumika pamoja na gharama za kila aina ya huduma (administrative procedures) atakaohitaji na wapi apite ili kufanikisha upatikanaji wa huduma anayohitaji.

Wednesday, November 13, 2019

NMB LIWALE YAWATAHADHARISHA WAKULIMA WA KOROSHO.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Bank ya NMB wilayani Liwale imewatahadharisha wakulima wa zao la Korosho wanaotumia benk hiyo kutotoa taarifa za kibenk kwa mtu yeyote kupitia njia ya simu.

Wito huo umetolewa na meneja wa Benk hiyo wilaya ya Liwale Mkoani lindi Shamsi Kashoro wakati wa mnada wa pili wa zao hilo wa chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kinachojumuisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale Mkoani Lindi uliofanyika katika kata ya likongowele wilayani humo.

Kashoro alisema wakati huu wa msimu matapeli wengi wanatumia mwanya huo kujifanya wao kuwa ni maofisa wa benki ili kuchukuwa taarifa za Wakulima na baadae kupata mpenyo wa kuwaibia wakulima hao.

Kashoro alieleza kuwa benk yao haitajihusisha na mawasiliano ya aina yoyote ya moja kwa moja kwa njia ya simu na wakulima bali taarifa zote zinazohusiana na benk wakulima watapata taarifa kutoka kwa viongozi wa vyama vyao vya Msingi AMCOS.

Hata hivyo aliwasisitiza wakulima kuhakikisha wanaandika majina yao kwa usahihi wakati wa kuandikisha korosho zao kwenye chama cha msingi AMCOS yakiwa yanafanana na jina la akount anayotakiwa kulipiwa fedha zake ili kuondoa usumbufu unaoweza kumcheleweshea Mkulima fedha yake.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Liwale Sara Chiwamba alitumia nafasi hiyo kuwaaasa wakulima kuwa na nidhamu na fedha zao pamoja na kutumia fedha hizo kwa shughuli za kimaendeleo.

Kwa upande wake mkulima wa korosho wa Wilaya ya Liwale Malima Evalist aliipongeza Serikali kwa kuanzisha mfumo wa wazi wa ununuzi wa Zao hilo ambao unaweka uwazi kwa wakulima na wanunuzi wa Zao hilo.

DHAMIRA YA RAIS LAZIMA ITIMIZWE -MGALU

Image may contain: 2 people, including Subira Mgalu, people smiling, people sitting
Na Omary Mngindo, Mkuranga
VIJIJI takribani 12,319 vinataraji kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2021, ikiwa ni dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuhakikisha vijiji hivyo vinakuwa na Nishati hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu aliyasema hayo wilayani Mkuranga, katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliozungumzia utekelezaji wa Ilani, huku Katibu wa NEC (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga alikuwa mgeni rasmi.

Alisema kuwa dhamira ya Rais John Magufuli ya kutaka vijiji vyote vinakuwa na umeme ifikapo Juni 2021, Wizara yake chini ya Waziri Dkt. Medard Kalemani wanaitekeleza kikamilifu, na kwamba wana matumaini mpaka ifikapo 2020 watakuwa wametimiza adhima hiyo.

Aliongeza kuwa kazi ya uunganishaji umeme vijijini inaendelea vizuri, na kwamba kwa Wilaya ya Mkuranga tayari vijiji vipya 36 vimeunganishiwa Nishati hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, iliyoingia madarakani Oktoba 2015.

"Oktoba 2015 wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani, kulikuwa na vijiji 20 tu vilivyokuwa vimeunganishwa na umeme hapa Mkuranga, kutokana na kasi iliyopo, sasa tumeongeza vijiji vingine 36 na kazi inaendelea," alisema Mgalu.

Aidha Mgalu amempongeza Mbunge wa Mkuranga (Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi) Alhaj Abdallah Ulega kwa kazi anayondelea kuifanya, huku akisema kwamba kupitia ziara zake za kuwasha umeme, akiwa na Ulega wananchi takribani 1,200 wameunganishwa.

Akizungumzia sekta ya gesi, Naibu Waziri huyo alisema kuwa kwa kipindi hiki cha 2019 viwanda takribani 50 vimeshaunganishiwa Nishari hiyo, huku akieleza kuwa ni hatua nzuri na ya kujivunia katika kipindi cha miaka minne ya Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Mbunge Ulega ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika ya kuhakikisha wa-Tanzania wote wanafikiwa na umeme pasipo kubagua.

WATOA HUDUMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

  Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Heavenlight Majule akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa
rushwa mahala pa kazi.
............................................


Watoa huduma wa afya wameaswa kuzingatia uadilifu na uaminifu mahala pa kazi kwa kutokuomba wala kupokea rushwa wakati wa kutoa huduma.

Hayo yamezungumzwa na Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa kufunga mafunzo elekezi kwa
wataalam tarajali 80 walioko kwenye mafunzo ya mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa njia ya vitendo yanayolenga kuwawezesha kutoa huduma bora za afya kwa jamii.


“Kupokea zawadi au pesa kabla na baada ya kutoa huduma ni kosa kisheria na pindi utakapogundulika umefanya hivyo basi utachukuliwa hatua kulingana na

vifungu 24 vya makosa ya rushwa vilivyoainishwa katika sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kuzuia na kupambana na rushwa,” Amesema Bi. Majule.

Amesisitiza kila mmoja ana wajibu wakushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa huduma bora za afya bila malipo yoyote kwani rushwa humnyima haki anayepatiwa huduma na kupunguza ufanisi katika kazi.


Kwa upande wake Muuguzi katika Hospitali ya Mloganzila, Bw. Mosama John ametoa wito kwa wataalam hao kuwa na kauli nzuri wakati wa kuwahudumia wateja wanaokuja hospitalini hapa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.


Mada ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na elimu elekezi juu ya udhibiti wa rushwa mahala pa kazi, elimu ya maambukizi ya ukimwi na jinsi ya kujikinga, kanuni za maadili ya utendaji kwa watumishi wa Umma, matumizi bora ya vifaa tiba na dawa, huduma za kliniki, mahusiano kwa Umma na huduma kwa wateja.