Friday, October 18, 2019

TANESCO ELEZENI WANANCHI HATUA ZILIZOFIKIWA KATIKA KUTEKELEZA MIRADI

 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua na kuwasha umeme katika moja ya nyumba  za Kijiji cha Mpiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Jumaa, na wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama.
 .......................................


Na Zuena Msuya , Pwani


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kutoa taarifa za utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini kwa viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wa maeneo husika ili wafahamu hatua zaidi za utekelezaji wa miradi hiyo.


Mgalu alisema hayo kwa nyakati tofauti, Oktoba 16, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuzindua na kuwasha Umeme katika Kijiji cha Mpiji, Kata Boko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani na kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji Umeme katika vijiji vya Kiluvya, Misugusugu, Mkombozi pamoja na katika Mtaa wa Mwambisi wilayani humo.


Aidha Mgalu alisema, kuwa TANESCO wakiweka utaratibu wa kuzungumza na Viongozi wa Vijiji pamoja na wananchi mara kwa mara juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi husika, kutaondoa maswali mengi pamoja na  wasiwasi walionao wananchi dhidi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa usambazaji wa umeme.


“Unajua watanzania ni waelewa sana, unapompa mtu taarifa ya kile kinachofanyika katika eneo lake kwa wakati sahihi inamfanya awe na amani na wale waliopewa dhamana ya kutekeleza jambo husika, pia kuendelea kuiamini serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake, na hii itawaondolea hofu na maswali mengi  wananchi, sasa msipofanya hivyo, wao watajuaje kinachoendelea katika maeneo yao!? Tanesco waelezeni wananchi kila hatua inayofikiwa katika kutekeleza miradi ya umeme”, alisisitiza Mgalu.


Vilevile alitumia ziara hiyo kuwaeleza watanzania ambao bado hawajafikiwa na miradi ya usambazaji wa umeme  kuwa na subira wakati serikali inaendelea kutekeleza kazi hiyo kwa awamu, kwa kuwa si jambo jepesi kuwafikia wananchi wote kwa siku moja.


Aliweka wazi kuwa lengo la serikali ni kufikisha huduma ya umeme kwa kila mtanzania, na kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Vijiji 2018 tu, ndiyo vilivyokuwa na umeme, sasa hivi idadi imeongezeka na kufikia zaidi ya vijiji 8100 na tayari zaidi ya vijiji 6000 vimeunganishwa, lengo ni kuvifikia vijiji vyote 12,319 nchi nzima ikifikapo  mwezi Juni ,2021.


“ Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mingi na muhimu katika kila sekta, kuna miradi ya Afya, Elimu, Barabara, Maji na kadhalika, hii yote inahitaji fedha nyingi na iwafikie wananchi wote na kwa wakati, serikali yetu ni sikivu na inatekeleza haya yote kwa wananchi wake, hivyo fedha inayopatikana inagawanywa katika kila sekta ili kutekeleza huduma zote muhimu kwa awamu kadri fedha inavyopatikana, hivyo wale ambao bado hamjafikiwa kuweni na subira, lengo ni kuwapatia wananchi wote huduma bora”, alisema Mgalu.


Mgalu alieleza kuwa, mkandarasi wa kampuni ya Sengerema amefikia 90% ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme katika vijijini vyote vya Wilaya ya Kibaha, kazi kubwa aliyonayo sasa ni kuwasha vijiji hivyo hadi mwezi Desemba 2019, kisha kuangalia mapungufu yalipo na kuyafanyia kazi, ili ifikapo mwezi Juni 2020 awe amemaliza mradi huo na kuukamilisha kwa wakati.


Aliendelea kumsihi mkandarasi huyo kuongeza kasi ya kuwaunganisha wateja ambao tayari wamelipia huduma hiyo, sambamba na hilo aliwahimiza wananchi kulipia haraka gharama za kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu.


Serikali ilitenga zaidi ya shilingi Bilioni 17, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini  katika Mkoa wa Pwani, pia iliongeza shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme katika Vijiji vilivyopo Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban) katika Wilaya ya Kibaha pekee, vilevile kupitia mapato ya ndani ya TANESCO, miradi ya usambazaji umeme 11 itatekelezwa katika wilaya hiyo  kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya umeme katika wilaya hiyo yanayosababishwa na uwepo wa viwanda.


Aidha katika mazungumzo yake na wakazi wa Kijiji cha Misugusugu, aliitaka TANESCO kuwafungia Transfoma inayokidhi mahitaji ya umeme katika kijiji hicho na maeneo yanayowazunguka ili kuondoa adha ya kukatika umeme katika eneo hilo mara kwa mara ambayo inasababishwa na kuelemewa kwa transfoma iliyopo.


Hata hivyo aliwaagiza watendaji wa TANESCO kufanya uchunguzi upya kubaini kaya za maeneo ya kijiji cha Misugusugu  zilizoachwa katika awamu zilizotangulia ili na wao wapate umeme katika awamu zijazo kwa kuwa zoezi la kusambaza umeme vijijini na kuwaunganisha wateja ni endelevu kwa kuwa kila siku mahitaji ya umeme yanaongezeka nchini.

DC. JOKATE AWATAKA WANANCHI BAGAMOYO KUCHAGUA VIONGOZI WANAOENDANA NA KASI YA RAIS MAGUFULI

 
Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akizungumza na wananchi wa kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo wakati alipotembelea halmashauri hiyo kuangalia hali halisi ya uandishaji wapiga kura ulivyofanyika.
.........................................
Na Shushu Joel.

Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, Jokate Mwegelo amewataka wananchi wilayani Bagamoyo kuwachagua viongozi wenye Utayari na Uwezo wa kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Wito huo ameutoa alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze kwenye viwanja vya kituo cha mabasi Cha Barabara ya Morogoro.

Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha na kuwasisitiza wananchi hao kutambua dhamana kubwa waliyonayo ya kuchagua kiongozi atakayekuwa ni kiungo kikubwa kwa viongozi wa juu na anayeweza kuendana na utendaji wa Rais Dkt. Magufuli.

"Jambo hili nimewatahadharisha mapema kabla ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwezi wa kumi na moja" Alisema DC Jokate.

Mbali na kuwahimiza Wananchi kujitokeza katika zoezi hilo Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, amempongeza Mbunge wa jimbo la Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete kwa utekelezaji na ufanikishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo lake na juu ya yote alivyojitokeza yeye akishirikiana na wananchi kuhamasisha uandikishaji wapiga kura.

Hivyo amewataka wananchi hao kuwa na viongozi watakaochaguliwa katika vitongoji na vijiji wawe wachapakazi kama Mh. Mbunge na Mh. Rais wanavyoshirikiana kufanya kazi nzuri ya kuleta Maendeleo.

"Ninyi wenyewe Mashuhuda na Mbunge ameeleza jinsi Miradi mikubwa kama ya maji, afya, madarasa, miundombinu na umeme ilivyotekelezwa kwa asilimia kubwa sana, nakupongeza Mh. Mbunge kwa utekelezaji Mzuri wa majukumu yako, Alisema DC Jokate.

Naye mzee Zaidi Lufunga (78) akizungumza kwa niaba ya Wana Chalinze amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kujionea mafanikio makubwa yalifanywa na serikali ya awamu ya tano katika jimbo la chalinze.

"Miaka yetu changamoto zilikuwa nyingi sana lakini kipindi hiki cha Rais Magufuli kwa kushirikiana na mbunge wetu Ridhiwani Kikwete mafanikio tunayapata na kazi nzuri inaonekana, Alisema Mzee Lufunga.

Aidha amemuhakikishia Jokate kuwa, kwa hali hii ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na iliyokuwa ndio ndoto zao watachagua viongozi wenye hofu ya Mungu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa maslahi ya wananchi wote.


Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa ujio wake wa kujionea jinsi wana Chalinze walivyojitokeza katika zoezi la kujiandikisha kwaajili ya kupiga kura za viongozi wa serikali za mitaa na vijiji.


Aidha, amewapongeza wakazi wa kata ya Bwilingu kwa kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza mkuu huyo wa wilaya.

Mpaka kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura hapo jana Oktoba 17, Halmashauri ya Chalinze imefanikiwa kuandikisha  Asilimia 74 ya wananchi waliotarajiwa kujiandikisha.
  
Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, alipofika kwenye moja ya vituo vya kuandikisha wapiga kura Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, pembeni yake mwenye kiremba ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni na mwenye fulana nyeupe ni Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao. 
Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya Jokate Mwegelo.
 
Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (katikati) akimueleza Kaimu Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Jokate Mwegelo (kushoto) hali ya uandikishaji wapiga kura ilivyokuwa katika Halmashauri hiyo, katikati ya Mbunge na Mkuu wa wilaya ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni na kulia ni Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao.

MAHAKAMA KUU KANDA YA BUKOBA IMEENDELEA KUSIKILIZA KESI YA MBUNGE WA BUKOBA VIJIJINI.

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Mahakama kuu Kanda ya Bukoba Mkoani Kagera imeendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mdaiwa katika kesi ya madai namba 12 ya mwaka 2016 ya shilingi 1 bilioni moja na milioni 216 fidia ya udhalilishaji iliyofunguliwa na mbunge wa Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza dhidi ya mdaiwa Novatus Rwechungura Nkwama mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha mapinduzi ( CCM ) Mkoa wa Kagera.

Shahidi wa mtuhumiwa Raurent Buteni (59) akitoa ushahidi wake mahakamani akiongozwa na wakili Dastan Mujaki ameeleza mahakama kuu mbele ya Jaji Dk. Ntemi Kilekamajenga wa mahakama hiyo kuwa julai tano mwaka 2016 ulikuwepo mkutano wa kitongoji cha Buryankuro na yeye alikuwa katibu wa mkutano huo ambao ulikuwa na ajenda tatu ambazo ni kufungua, kujadili wizi wa ndizi na ndizi kali uliokuwa katika kitongoji hicho na ajenda ya kufunga.

Baada ya wakiri Dastan Mujack kumuhoji shahidi juu ya kashifa zinazotajwa dhidi ya mshitakiwa kuwa alimkashifu Jasson Rweikiza kuwa ni mwizi na alishirikiana na Novatus Nkwama kuchakachua kura za mwaka 2015 wakati amepata ubunge, Shahidi Buteni ameeleza mahakama kuwa, hakuna maneno ya kashfa yaliyoongelewa kwenye mkutano huo kwani yangeongelewa muhusika angetolewa katika mkutano huo.

Naye wakili wa upande wa Mdai Alli Chamani akimuhoji shahidi wa upande wa mdaiwa amemuuliza kwamba, katika eneo la mkutano waliweka bango la kuonyesha kuwa ni mkutano wa kitongoji? na katika eneo la mkutano ilikuwepo barabara iliyokuwa inakatiza? na je mwanakitongoji jirani alikuwa anaruhusiwa kuhudhuria mkutano huo?.

Akijibu maswali hayo, shahidi Buteni amesema kuwa, katika eneo la mkutano liliwekwa bango la kuonyesha kuna mkutano na hivyo hakuna mwananchi wa kitongoji jirani aliyeruhusiwa kuhudhuria mkutano huo na ilikuwepo barabara inayokatisha kutoka kitwe kwenda Amugenge.

Aidha katika kesi hiyo upande wa mdai ambaye ni Mbunge Jasson Rweikiza mashahidi wanane tayari wametoa ushahidi wao na upande wa mdaiwa Novatus Nkwama mashahidi watatu tayari wametoa ushahidi wao mahakamani na bado shahidi mmoja ambaye atatoa ushahidi wake octoba 18 mwaka huu kesi itakapotajwa tena