Monday, October 14, 2019

APIGWA NA WAFUGAJI, APATA ULEMAVU NA MKE KADAI TALAKA.

Na Omary Mngindo, Kibiti.


JUMA Mwinyilaka (31) mkazi wa Kibiti Mkoa wa Pwani, amepatwa na ulemavu wa kudumu kufuati kupigwa mkuki mkononi na mgongoni na mfugaji aliyemtaja kwa jina la Ndingwa Nune Ndaki.


Mwinyilaka ambaye kwa sasa ana ulemavu unaosababisha kutoweza kufanya jambo lolote, umetokana na Ndaki aliyeingiza mifugo shambani kwake, ambapo wakati yeye na wenzake wakiiswaga kwenda ofisi ya Kijiji, mfugaji huyo akaanza kuwashambulia na mkuki.


Alisema kuwa wakiwa njiani kuelekea katika ofisi ya Kijiji umbali wa kilometa moja kutoka shamba, Ndakia akaanza kuwashambulia Nassoro na Fadhili Mchoro, alipotaka kuingilia ndipo akamchoma kwa mkuki mkononi na kiunoni.


"Baada ya tukio hilo nilipoteza fahamu, nikazindukia hospitali ya Mchukwi nikitibiwa, lakini kutokana na hali yangu kuwa mbaya nikahamishiwa Hospitali ya Muhimbili ambako nilikaa kwa miezi miwili," alisema Mwinyilaka.


Aliongeza kwamba kutokana na hali yake kuwa mbaya, mke wake alipoona hana uwezo wowote wa kufanyakazi za kilimo na za kujiingizia kipato, aliomba ampatie talaka ili akaolewe mbele.


"Nikawa sina budi nikaandika talaka nimkabidhi na hivi sasa ameshaolewa, lakini nimezaa nae, kwa sasa naomba msaada niweze kwenda nchini India nikatibiwe, nimeambiwa naweza kurudi katika hali yangu," alisema Mwinyilaka.


Mama yake Mwinyilaka Mauwa Mrisho alisema kuwa baada ya tukio hilo, alipigiwa simu na watu wakimweleza kuwa mtoto wake amepoteza maisha kutokana na kupigwa na wafugaji walioingiza mifugo katika shamba lake.


Aliongeza kuwa baadae akaambiwa kwamba hajafa, isipokuwa hali yake ni mbaya na kuwa amekimbizwa hospitali ya Mchukwi, kabla ya kupelekwa Muhimbili, kwa ajili ya matibabu zaidi.



Mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulam Husein Shaabani Kifu alikiri kutokea kwa tatizo hilo, huku akisema kwamba sheria imechukua mkondo wake, ikiwa ni pamoja na mtuhumiwa kukaamatwa kisha kufikishwa Mahakamani na hukumu kutolewa.


"Mahakama imehukumu kutokana na sheria zinavyoongoza, hukumu imetolewa lakini mlalamikaji kama hajaridhishwa na hukumu hiyo ana haki ya kukata rufaa ngazi za juu," alisema Kifu.


Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibiti Ally Ungando alielezea kusikitishwa kwake kufuatia tukio hilo na mengine yanayojitokeza, huku akiwataka wana-Kibiti kutokubali kuwapokea wafugaji wavamizi ambao ndio chanzo cha matukio hayo.

MAGAZETI YA LEO OKTOBA 14, 2019.

HOSPITALI YA KILWA YAPATA CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Hatimae changamoto ya ufinyu wa jengo la kuhifadhia maiti iliyokuwa ikiikabili Hospitari ya Wilaya ya Kilwa Kinyonga, Mkoani Lindi imepatiwa ufumbuzi baada ya kampumi ya PAN AFRICA ENERGY kufadhili ujenzi wa jengo hilo.

Ujenzi wa chumba hicho cha kuhifadhia maiti kinaenda sambamba na ujenzi wa Duka kubwa la dawa litakalokuwa linamilikiwa na Hospital hiyo ya Wilaya ambavyo vyote kwa ujumla wake vitagharimu zaidi ya shilingi milioni 361 kwa makubaliano ya kampuni hiyo ya Gesi na Halmashauri hiyo.



Akisoma taarifa ya mradi huo katibu wa Afya wa Hospital hiyo Zabibu Uledi mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema kuwa makubaliano ya jengo hilo yalikuja baada ya Hospital hiyo kutumia chumba kidogo cha muchwari ambacho kilikuwa hakikidhi mahitaji kutokana na ongezeko la watu wanaohitaji huduma katika Maeneo hayo.

Akizungumza katika ghafla hiyo ya uwekwaji wa jiwe la msingi baada ya kutembelea, kukagua na kuridhishwa na taarifa za ujenzi huo kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally amemtaka mkandarasi anaetekeleza mradi huo Kuhakikisha majengo hayo yanajengwa kwa ubora na kwamba vifaa vyote vitakavyotumika katika ujenzi huo viwe vinapitia maabara ya Serikali ili kujihakikishia ubora wake.

Kwa upande wake Meneja uwajibikaji wa Shughuli za kijamii wa kampuni ya Pan African Energy Andrew Kashangaki alisema kuwa kampuni yao licha ya ujenzi wanaofadhili katika Hospital hiyo ya Wilaya lakini pia kampuni yao kwa kuthamini afya za Wananchi wa Wilaya hiyo pia wanafadhili ujenzi wa kituo cha Afya cha somanga katika kata ya somanga

SIKU TATU ZAONGEZWA KUJIANDIKISHA WAPIGA KURA.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akijiandikisha kwenye Orodha ya Daftari la Mpiga kura kwenye Kitongoji cha Kimani Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani leo Tarehe 13.10.2019.
................................................

Na Oscar Job, Kisarawe.

WAZIRI wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameongeza siku tatu kwa wananchi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 Mwaka huu.

Akizungumza kabla ya kujiandikisha Kijijini kwake Kimani, Kisarawe mkoani Pwani jana, Waziri Jafo alisema kuongezwa kwa siku tatu hizo kumetokana na sababu mbalimbali ambazo kimsingi zimesababisha wananchi kuikosa fursa hiyo.

Alisema kimsingi siku za uandikishaji huo zilizoongezwa kutoka leo hadi Oktoba 17, kumesabishwa na tatizo la mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali na hivyo kuleta shida kwa wananchi wengi kujiandikisha.

Aliitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na uwepo wa zoezi la wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, hali iliyoleta dhana kwa baadhi ya wananchi kuwa kitambulisho cha mpiga kura kitawawezesha kupiga kura katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.

“Kutokana na sababu hizo na kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 na matangazo ya Serikali Na 371,372,373 na 374 ya Mwaka 2019 Waziri mwenye dhamana na Serikali za mitaa ana mamlaka ya kutoa miongozo mbalimbali kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa” alisema Jafo.

Alisema kutokana na kanuni hizo na changamoto zilizojitokeza Wizara yake imeona vyema kuongeza siku hizo tatu ili kuwapa nafasi wananchi kujiandikisha na hivyo kutumia fursa yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.

Aidha alisema tangu kuanza kwa Oktoba 8 hadi Octoba 12 Mwaka huu wananchi zaidi ya Milioni 11 walikuwa tayari wamejiandikisha nchi nzima kushiriki uchaguzi huo huku akilitaja zoezi hilo kuwa lenye mafanikio makubwa ikilinganishwa na kipindi kingine chote.

Alisema kufuatia mabadiliko, ratiba ya uandikishaji wa orodha ya wapiga kura na matukio yanayohusu uandikishanji yatakuwa na mabadiliko fulani fulani ikiwemo kubandikwa kwa orodha ya wapiga kura litakalofanyika kuanzia Oktoba 18, utoaji wa pingamizi kuhusu uandikishaji wapiga kura litakalofanyika Oktoba 14 hadi 24.

Mabadiliko mengine ni pamoja na uamuzi kuhusu pingamizi litalofanyika kuanzia Oktoba 24 hadi 25,marekebisho ya orodha ya wapiga kura kuanziaa Oktoba 25 hadi 25 pamoja na ukataji wa rufaa dhidi ya uamuzi wa pingamizi utakaofanyika Oktoba 24 hadi 26 sambamba na ukataji wa rufaa utakaofanyika Oktoba 24 hadi 29 Mwaka huu.

Aidha alisema matukio mengine yote zikiwemo kampeni za wagombea zitaendelea kubaki kama kawaida huku akiwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuwa na sifa ya kupiga kura katika uchaguzi huo.