Sunday, October 13, 2019

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ARIDHISHWA NA MRADI WA MACHINJIO LINDI.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally aridhishwa na kasi ya Mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Manispaa ya Lindi Mkoani humo.


Mkongea ameyasema hayo  alipotembelea na kukagua katika mradi huo na kuona maendeleo yake Pamoja na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo pia mkongea ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwa kuanzisha mradi mkubwa ambao utakuwa chanzo kizuri cha mapato katika Halmashauri yao.


Awali akisoma taarifa ya mradi huo Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Lindi Dkt. Iddi Nizar alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia mpango wa uendelezaji Miji na Manispaa Nchini (ULGSP) ambao kwa awamu ya kwanza unatekelezwa na mkandarasi M/S KINASHA BULDING CONSTRUCTION AND GENERAL SUPPLIES JV JECE LTD ya jijini Dar Es Salaam na kwamba utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.45.


Alisema Machinjio hayo kwa awamu ya kwanza yatahusisha Jengo la Machinjio, Nyumba ya mkaguzi wa nyama na kibanda cha mlinzi, ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha changalawe, milango mikuu na uzio wa kuzunguka machinjio na Sehemu ya kupumzikia mifugo huku awamu ya pili ikihusisha uwekaji wa vifaa kwa ajili ya kuchinja na kuchakata nyama.


Nae fundi mchundo wa kampuni hiyo Jafety Malima alisema kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza huku akitaja kazi zilizofanyika kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la machinjio kwa asilimia 95%, ujenzi wa nyumba ya mkaguzi na kibanda cha mlinzi kwa asilimia 95% na kwamba wanatarajia kuukabidhi kwa Halmashauri oktoba 28 mwaka huu.


Alizitaja kazi zingine kuwa ni Milango mikuu (mageti) na uzio 100%, sehemu ya kupumzikia wanyama asilimia 95% pamoja na miundombinu ya maji safi na salama kwa asilimia 95%.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema kuwa mradi huo utakapokamilika utasaidia upatikanaji wa Nyama bora na salama kwa walaji wa ndani na nje ya mji wa Lindi, kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia tozo za uchinjaji na uchakataji wa nyama, kuongezeka kwa Fursa katika sekta ya mifugo hususani ufugaji, pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Manspaa ya Lindi .

MVUA YALETA MADHARA KAGERA.

Migomba ikionekana kuanguka baadaa ya mvua iliyoambatana na upepo kunyesha katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera hapo jana Oktoba 12, 2019.
........................................

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Mvua za kimbunga zilizonyesha zikiwa zimembatana na upepo mkali zimeezua nyumba sita na mashamba ambayo idadi yake haijafahamika mara moja katika kitongoji cha Misha kata ya Rugu wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.


Diwani wa Kata ya Rugu Adirian Kobushoke amethibitisha kutokea kwa kimbunga hicho na kusema kuwa kimetokea jana Oktoba 12, 2019 majira ya saa tisa alasiri iliponyesha mvua kubwa ikiwa imeambatana na upepo mkali na kusababisha migomba na mikahawa kuanguka chini na nyumba sita kuezuliwa na upepo.


Kobushoke amesema, bwana shamba wa Kata ya Rugu akishirikiana na afisa mtendaji wa Kata hiyo wanafanya tathimini ya migomba na mikahawa iliyoanguka ili kubaini thamani halisi ya hasara iliyowakumba wananchi wa kitongoji cha Misha ni pamoja na thamani ya nyumba zilizoezuliwa na upepo.


"Kimbunga hicho licha ya kuangusha migomba na mikahawa pamoja na kuezua nyumba hakuna madhara mengine yaliyotokea kwa wananchi". Alisema Kobushoke.


Mmoja wapo ambaye nyumba yake imeezuliwa na upepo Vumilia Endrew amesema yeye ana familia ya watu nane, yeye na mkewe naa watoto sita, baada ya nyumba yake kubomoka jana ametoa taarifa katika uongozi wa kitongoji na kijiji pamoja na kata na kupewa turubai ambayo imemsaidia kwa ajili ya makazi tangu jana wakati jitihada nyingine zikiendelea kufanyika.
 
Baadhi ya nyumbazilizo ezuliwa mapaa yake katika kitongoji cha Misha kata ya Rugu wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

MWENGE WA UHURU WAMALIZA MBIO ZAKE KILWA NA KUINGIA HALMASHAURI YA MANISPAA YA LINDI.

Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa 2019 mzee Mkongea Ally akiwasalimia wananchi wa mtaa wa mto mkavu kata ya Mbanja wakatai makabidhiano ya Mwenge huo kati ya Halmashauri ya wilaya ya Kilwa na Halmashauri ya manispaa ya Lindi Mkoani humo.
 ..............................................


 NA HDIJA HASSAN, LINDI.


Mwenge wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa wilayani Kilwa Mkoni Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo.


Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ally amesema miradi mitano ya maendeleo iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.


Akizungumza na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (jumapili, Oktoba 13, 2019) kwenye mtaa wa mto Mkavu kata ya Mbanja halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mkongea aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa kuwa na miradi mizuri sambamba na kuwataka viongozi wa Manispaa ya Lindi kuhakikisha wanakuwa na Taarifa zote muhimu kwenye kila mradi utakaopitiwa na mwenge huo wa Uhuru sambamba na kuwataka wataalamu kuwa katika maeneo yao ya Miradi.


Mkongea pia aliwataka Viongozi kusimamia maadili pamoja na itifaki za mbio za mwenge wa Uhuru zinazotolewa na wakufunzi husika kwani Mwenge huo wa Uhuru sio wa mkimbiza Mwenge bali ni uwakulishi wa Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na tunu ya muasisi wa Taifa Mwalimu Julias kambalage Nyerere hivyo ni wajibu wa kila mtu kukiheshimu chombo hicho muhimu.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya kilwa Christopha Ngubiagai aliitaja miradi iliyopitiwa na Mwenge huo wa Uhuru ni pamoja na kutembelea na Kukabidhi mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali katika kijiji cha Njinjo, kuweka jiwe la msingi Duka la Dawa na Chumba cha kuhifadhia maiti, kuzindua Mradi wa maji katika kijiji cha Mpara, kutembelea Mradi wa Barabara Masoko pamoja na kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa ukarabati na ujenzi wa Madarasa na Bwalo la chakula katika Chuo cha wananchi Kilwa Masoko ambayo inathamani ya shilingi bilioni 1 na milioni 900.


Mapema akipokea Mwenge huo wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shihibu Ndemanga alisema kuwa Mwenge huo wa Uhuru katika Manispaa ya Lindi utakimbizwa kwa urefu wa km 200 na utakagua miradi 6 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.23.


Kesho (jumatatu, Oktoba 14) mbio hizo za mwenge wa uhuru zinatarajiwa kufikia tamati kwa kuzimwa ambapo katika sherehe hizo za kuitimisha zitafanyika katika viwanja vya Ilulu Manispaa ya Lindi Mkoani humo ambayo itaenda sambamba na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambalage Nyerere.