Thursday, October 10, 2019

HALMASHAURI YA BUKOBA YAANZISHA KLABU ZA LISHE KATIKA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI.

Na Alodia Dominick, Bukoba

Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa lishe wameweka mkakati wa kuanzisha klabu za lishe katika shule za msingi na sekondari ili kutoa elimu kwa kundi la vijana barehe kutokana na kundi hilo kuwa na mahitaji makubwa ya ki lishe.

Hayo yamebainshwa na Afisa lishe wa wilaya hiyo Desdery Karugaba kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa masuala ya lishe katika kikao cha kamati ya lishe cha wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/20 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.


Karugaba kwa kushirikiana na wadau wa kikao hicho ikiwemo Idara ya Elimu wamepanga mikakati kuanzisha klabu za lishe katika shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kutoa elimu hasa kwa kundi la vijana barehe kutokana na kundi hilo kuwa na mahitaji makubwa ya ki lishe.

Ameongeza kuwa, halmashauri hiyo imefanikiwa katika mpango wa lishe kwa makundi ya watoto wachanga, wajawazito isipokuwa kundi ambalo limesahaulika ni vijana barehe ambalo ni eneo muhimu kwa kizazi kijacho.



Akitaja kundi hilo amesema Vijana barehe ni kundi lenye miaka 9 hadi 20 ni kundi ambalo lina mahitaji makubwa ya ki lishe ambayo katika ukuaji kuna hatua mbili ambazo binadamu anajiita.

Alisema kundi hili ni kundi muhimu sana kwa kuwa ukuaji wake huenda kwa kasi na kusababisha mahitaji ya ki lishe kuongezeka hivyo kundi hili lazima lipate elimu ya kutosha ya lishe ili kujua ni vyakula gani vinahitajika.

Aliongeza kwa kusema kuwa, katika ukuaji kuna hatua mbili ambazo binadamu anakua kwa haraka sana ambapo kwa upande wa watoto wa kike ni kipindi ambacho mtoto anaanza kuingi kwenye hedhi hivyo hupoteza damu na kuwa watendaji wa vijiji wanapaswa kuweka nguvu kubwa kuhakikisha wanajadili na kufanikisha suala la lishe katika maeneo yao kwa kuitisha mikutano ya hadhara.

Naye Sr. Margareth Ishengoma amesema ushirikiano wa kina unatakiwa ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa mara moja.

UWT PWANI WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI.

Image may contain: 5 people, including Subira Mgalu, people smiling, people standing
Na Shushu Joel

Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani umempongeza Rais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyojali wanawake katika teuzi mbalimbali pia katika utekelezaji wa miradi mikubwa kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo Afya inayolenga kumsaidia Mwanamke moja kwa moja.


Akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya wiki ya UWT iliyohitimishwa wilayani Kibiti Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Pwani Bi Farida Mgomi amesema kuwa Rais Magufuli amekuwa kiongozi mwenye kuwaamini na kuwapatia nafasi mbalimbali wanawake katika serikali ili waweze kumsaidia kusimamia shughuli za maendeleo kwa ajili ya wananchi.


Alisema mkoa wa Pwani umekuwa na wanawake shupavu na wenye kujitoa katika kuwahudumia wanyonge na ndio maana wengi wamepata nafasi Serikalini na Chama pia.


"Umoja wa wanawake mkoa wa Pwani tunampongeza sana Mhe Rais na Mkiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwapatia wanawake nchini nafasi, na kiukweli tunaona wanavyochapakazi na hawajamuangusha Mhe Rais na tunaahidi kumuunga mkono katika uongozi wake "Alisema Mgomi.


Aidha Mwenyekiti huyo amewataka wanawake kuendelea kuwa kinara wa upigaji kura kukichagua Chama Cha Mapinduzi  (CCM), Kujiandikisha kwa wingi katika daftari la Ukaazi na la wapiga kura na kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali.


Kwa upande wake, Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani ambae pia ni Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu amewapongeza wanawake wa mkoa wa Pwani na nchi nzima, kwa uchapakazi wao na kupelekea kuonekana katika ngazi za juu ya serikali na hata kupata uteuzi.


Mbali na hilo Mgalu amewahakikishia kinamama hao kuwa serikali ya awamu ya tano ipo makini katika utekelezaji wa ilani kwenye Sekta zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi wa kawaida hususan Kina Mama mfano wa Afya , Maji , Kilimo , Nishati , Ardhi nk.


Aidha Mgalu ametoa doti za kanga 800 katika kila wilaya za mkoa wa Pwani ili kuuzwa kwa wanachama wenye kipato cha chini ili nao waweze kupata sare hizo kwa bei nafuu na waweze kuendelea kukitangaza Chama na UWT, pia uwe ni mradi rasmi wa Jumuiya hiyo ili iweze kujiendesha.


Nae Mbunge mwingine wa Viti maalum Mkoa wa Pwani,  Mhe Zainabu Vulu, alisema kuwa wanawake ni jeshi kubwa lenye mshikamano mkubwa na lenye uwezo wa kufanya maamuzi.


Vulu aliongeza kuwa kuelekea uchaguzi wa serikali za vijiji na mtaa amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi ili kukipigia kura za ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wapinzani waendelee kuisoma namba.


Aidha, alisema kuwa kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, CCM itashinda kwa kishindo na hii ni kutokana na utekelezaji wake wa ilani ya Mwaka 2015 ambayo imelenga kuletea maendeleo kwa wananchi .


Katika hatua nyingine Waheshimiwa Zainabu Vulu Ma Subira Mgalu walitoa Seti moja ya Kompyuta na (Printer) ikiwa ni hatua ya mwisho kumalizia utoaji wa Kompyuta na Printer ambapo umefanyika kwa UWT wilaya zote nane za Mkoa wa Pwani lengo likiwa ni kuimarisha utendaji wa jumuiya hizo.

WATANZANIA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA.

 
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Ally Mkongea akizungumza katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu wilayani humo, Oktoba 9, 2019, kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa.

.....................................

Na Hdija Hassan, Lindi.


Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Mzee Mkongea Ally amewataka Watanzania waliokuwa na sifa ya kupiga Kura kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye dafutari la kupiga kura ili waweza kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa.


Mkongea ametoa wito huo alipokuwa akitoa ujumbe wa Mwenge wa uhuru kitaifa katika kijiji cha Nangumbu Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi kwa wananchi wa Wilaya hiyo.


Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika November 24 utahusisha wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji, wajumbe wa Halmashauri kuu na wajumbe wa Viti maalumu.


Mzee alisema swala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni suala la kikatiba na kisheria kwamba ni haki ya kila mwananchi aliekuwa na sifa kushiriki katika Uchaguzi huo.


"Serikali za mitaa zinatambulika kutokana na Katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 , Serikali za mitaa zimekuwa zikifanya Kazi muhimu Sana katika maeneo yetu ikiwemo kushajihisha shughuli za maendeleo, kuhamasisha Wananchi kutunza mazingira, pamoja na kuhakikisha Wananchi wanaishi katika hali ya usalama na amani" Alisema Mkongea.


Awali akiwasalimia wananchi, Mbunge wa Jimbo hilo la Ruangwa ambae pia ni Waziri Mkuu wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Alitumia fursa hiyo kutoa taarifa ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika dafutari la kupigia kura katika Wilaya hiyo ya Ruangwa Ambapo alisema kuwa kwa siku ya Tarehe 8 Pekee jumla ya wananchi 28 elfu waliojitokeza kujiandikisha.


Pamoja na mambo mengine Majaliwa pia, aliwataka wananchi ambao wanasifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitokeza kugombea pamoja na kuwataka kuwaasa wapiga Kura kuchagua viongozi Bora, wachapa Kazi na waadilifu.
 

Wednesday, October 9, 2019

TMA YATOA TAHADHARI YA MVUA.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini kwenye mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba.


Tahadhari hiyo imetolewa leo na TMA, ikionesha uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mvua kubwa sambamba na mawimbi makubwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Oktoba 9 hadi Oktoba 12, 2019.


Angalizo hilo la mawimbi Mmakubwa limetolewa pia kwa baadhi ya maeneo Pwani ya Bahari ya Hindi na kusini mwa mikoa ya Mtwara na Lindi.


Mamlaka hiyo imewataka watumiaji wa bahari na maeneo yaliyotajwa kuchukua tahadhari.


“Tahadhari ya upepo mkali na mawimbi makubwa imetolewa kwa maeneo ya ukanda wa pwani yote, katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,”  imeeleza sehemu ya taarifa hiyo fupi.


Katika taarifa hiyo ya  kifurushi cha siku nne cha tahadhari za hali ya hewa, TMA imeeleza athari kuwa kiwango kikubwa cha athari kinaweza kujitokeza.


TMA pia imeeleza athari zinazoweza kutokea ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, kutawanyishwa na ucheleweshwaji wa usafiri baharini na nchi kavu na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.