Monday, September 30, 2019

OMARI MGUMBA AKEMEA KILIMO KUFANYWA ADHABU SHULENI.

NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba akizungumza na watumishi wa Halamashauri ya wilaya ya Pangani wakati wa ziara yake kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah
.....................................



NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amewataka walimu wa shule za Msingi na Sekondari waache kutumia kilimo kama adhabu ya kuwapa wanafunzi wakati wanapokosea kwani inawajengea tafsiri mbaya kwa jamii na baadae wanapokuwa, wanachukia kilimo.

Mgumba alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake wilayani Pangani ambapo alisema kwamba kuna tabia ambayo imejengeka kwa walimu hao kwamba mtoto anapokosea anaambiwa leo utakwenda kulima siku nzima, utakwenda kumwagilia hali ambayo inapelekea baadae wakikua wanakuwa hawahitaji kilimo kwa sababu awali waliona kama adhabu.


Alisema hapana, suala hilo sio jema na ndio maana wao wanasema kilimo ni uti wa mgongo lakini watafungamanisha kilimo na elimu ili watoto tokea anakuwa ajue kwamba nchi hii uchumi wake unategemea kilimo.


“Hivyo ninapoambiwa niwe na tuta la mchicha sio adhabu bali ni sehemu ya kuniandaa kielimu nije kujitegemea au nije kuajiri wengine kwenye mashamba yao kwani bila kufanya hivyo tutakuwa tunaimba kitu kingine wakati uchumi wetu unategemea kilimo”Alisema Naibu Waziri huyo.


Naibu Waziri huyo alisema kwamba mkakati wa serikali ni kuimarisha kilimo hivyo wataendelea kufungamanisha elimu na kilimo chao.


Akizungumzia Kilimo cha Minazi wilayani humo Naibu Waziri huyo alisema kwamba kilimo cha minazi ni kweli hawajapata ufumbuzi wa magonjwa yake kwa miaka zaidi ya 30 sasa, ambayo yanasababsihwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.


Alisema pia hilo linatokana na kukubali kuletewe mbegu ya kisasa ambayo haiendani na mazingira ya nchi hivyo kama Taifa  wameendelea kuimarisha vituo vyao vya utafiti hasa cha utafiti wa minazi mikocheni lengo ni kuanza kurudi kwenye kuzalisha miche kutumia minazi ya asili inayokabiliana na hali ya hewa na ikolojia ya ya nchi yetu .


“Na sasa tumeanza kuzalisha kitalu cha miche asili Bagamoyo na itasambazwa nchi nzima kwa lengo la kupanda na hatimaye kuweza kurejesha minazi hiyo ”Alisema.



Akizungumzia udogo wa bei ya nazi nchini Naibu Waziri huyo alisema kwamba nazi zinauzwa bei ndogo na imeendelea kuwa ndogo ni kutokana na ushindani uliopo kwenye soko la ndani, kanda na kimataifa kwa sababu ya bidhaa mbadala.


“Hivyo kila nazi ikipanda bei, watu wanakwenda kutumia mafuta lakini kila tunapoacha kutumia nazi na kutumia mafuta na kwenda kwenye chukuchuku wanapunguza mahitaji ya nazi ”Alisema.


Hata hivyo alisema kwamba wanakuja na mkakati wa kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza thamani bidhaa hiyo ili kupanua soko la nazi hapa nchini na mbegu za nazi ambazo zinaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi huku akieleza kwamba wakienda kuongeza thamai tatizo hilo litakwisha.


Katika hatua nyengine Naibu Waziri huyo aliwataka watanzania kuendelea kutumia nazi kwani wanapoendelea kuitumia zaidi wanaongeza mahitaji na soko la nazi litakuwa kubwa huku akisistiza kwamba watakaendelea kutumia mafuta bei ya nazi itashuka.


Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso alisema kwamba zao la nazi limeathiriwa na maradhi kwa muda mrefu na bado tiba yake haijapatikana miaka 30 sasa.

Alimwambia Naibu Waziri Mgumba kwamba ugonjwa huo umekuwa haupati ufumbuzi kama lilivyokuwa gonjwa la ukimwi hivyo walimuomba watafiti na watalamu wafanye utafiti ambao utafika mwisho na wenye manufaa na kuweza kurudisha uchumi wake.

Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji kulia akimueleza jambo Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba wakati wa ziara yake wialayani humo.

MKUU wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani, Mwalimu Hassani Nyange.

AHUKUMIWA JELA MAISHA, KWA KULAWITI, KUBAKA MTOTO WA MIAKA 10.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Lindi, Mkoani hapa, imemuhukumu kifungo cha maisha Gerezani, Emmanuel Thomasi Msemakweli (29), mkazi wa Mtaa wa Kariakoo, Kata ya Rasbura, Manispaa ya Lindi, baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 27 Septemba 2019 na Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga, baada ya mshtakiwa kukutwa na makosa mawili likiwemo kubaka na kulawiti Mtoto wa kike na mwanafunzi mwenye umri wa miaka 10, (jina limehifadhiwa).

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Kiswaga alimuuliza mshtakiwa kwa nini Mahakama isimpe adhabu kali kutokana na makosa aliyoyafanya dhidi ya mlalamikaji, ambapo aliomba imuonee huruma kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza na alifanya kosa hilo baada ya kupitiwa na Ibirisi.

Baada ya utetezi huo, Mwanasheria wa Serikali Yahaya Gumbo akisaidiana na Godfrey Mramba waliiomba Mahakama kumpa mshitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, alisema anakubaliana na maombi yao, lakini kutokana na Sheria kumfunga mikono, huku akitumia vifungu 130 (1), (2) (a) na 131 (1) kanuni ya adhabu sura ya 16/2002 kutoa adhabu, alimuhukumu kutumikia kifungo cha miaka (30) kwa kosa la kubaka.

Pia, Hakimu Kiswaga akitumia kifungu namba 154 (1) (a) kanuni hiyo ya adhabu sura ya 16/2002 katika kesi hiyo namba 37/2019, alimuhukumu kifungo cha Maisha, na kwa kuwa adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, Emmanuel Thomas Msemakweli atalazimika kuishi Gerezani maisha yake yote hapa duniani.

Awali ilidaiwa Mahakamani hapo na wanasheria wa Serikali, Yahaya Gumbo na Godfrey Mramba, kuwa mshitakiwa kwa muda, siku na nyakati tofauti, huku akifahamu anacho kifanya ni kosa, alimbaka Mtoto wa kike na mwanafunzi mwenye umri wa miaka kumi (majina likiwemo la Shule anayosoma yamehifadhiwa).

Wanasheria hao waliiambia Mahakama kuwa hali hiyo ilifahamika baada ya walimu wake na mama yake kuona mabadiliko, yakiwemo utembeaji wake na kushuka kwa maendeleo yake Shuleni.

Aidha, walieleza kwamba kufuatia hali hiyo, walimu na mzazi wake, walimuhoji na kuelezea kile kinachomsibu, kisha kuchukuwa hatua ya kumpeleka Hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kubainika kuingiliwa sanjari na kinyume na maumbile.

Wanasheria hao walieleza kuwa baada ya kubaini hilo, walimu wakishirikiana na mama wa mwanafunzi huyo walitoa taaifa kwa vyombo husika vya Serikali, ndipo mshitakiwa alipokamatwa.