Friday, September 13, 2019

WALIOZEMBEA AJALI YA MOTO WACHUKULIWE HATUA-MAJALIWA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo kufuatia tukio la ajali ya moto iliyotokea Agosti 11, 2019 mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 104, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe 3, Novemba mwaka huu.

“Baada ya tukio hilo la kusikitisha tarehe 12 Agosti 2019niliunda Kamati Maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.”

“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nawadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.

“Nawasihi Watanzania wenzangu tujifunze kutokana na ajali hiyo iliyotokea Morogoro na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika maeneo ya ajali. Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada kwa waathirika wa ajali badala ya kutumia kama fursa za kujinufaisha isivyo halali.” 

SERIKALI YATOA ONYO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau watakaoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa amani kwani Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika.

Waziri Mkuu amesema wadau hao mbalimbali kutoka katika Vyama vya Siasa, Taasisi za Serikali na Zisizo za Serikali na wananchi ni vyema wakahakikisha wanasoma na kuelewa kanuni na miongozo ya uchaguzi huo ili waweze kushiriki ipasavyo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu amewataka Watanzania wote wenye sifa washiriki uchaguzi huo kwani ni haki yao ya msingi.

“Natoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika orodha ya wapiga kura, wachukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki kupiga kura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.”

Mbali na wadau hao, pia, Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi kwenye mazingira ya amani na utulivu bila kubugudhiwa.

Waziri Mkuu amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo wahakikishe wanazielewa kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya waratibu vizuri shughuli za uchaguzi kwenye maeneo yao na wahakikishe uwepo wa ulinzi na usalama wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha kampeni na wakati wa kupiga kura.

Waziri Mkuu amewasihi wabunge na madiwani wawahamasishe wananchi ili watumie haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa. “Natoa rai kwenu mhakikishe mnashiriki kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo.”

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019. Uchaguzi huo unafanyika kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi.

Kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Waziri Mkuu amesema tarehe 18 Julai 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro na kuongeza kuwa uboreshaji huo, unahusisha wapiga kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

“Makundi mengine yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo jingine la uchaguzi, waliopoteza kadi au kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao; mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa pamoja na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki dunia.”

Amesema kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba). Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe

RC. PWANI AWEKA JIWE LA MSINGI KIWANDA CHA VIFUNGASHIO.

Image may contain: 2 people, people smiling, people standing and suit
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ametembelea na kuweka Jiwe la Msingi Kiwanda cha Wande Printing and Packaging Company Ltd kilichopo Pangani Wilayani Kibaha kitakacho tengeneza Vifungashio vya Plastiki kwa ajili ya bidhaa za viwandani, kilimo, chakula, na sekta ya Afya.


Kiwanda hicho kitagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 6.6 na kitatengeneze ajira 350 kitakapo kamilika
Akiweka jiwe la Msingi leo Septemba 13, 2019, Mhandisi Evarist Ndikilo amesisitiza kuwa ataendelea kutembelea miradi kama hiyo ya viwanda katika Mkoa wa Pwani kwa kuwa wenye viwanda hao wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuipeleka Tanzania katika Uchumi wa Kati ifikapo 2025.


Aidha, alisema Wanatengeneza Ajira, wanalipa Kodi na Ushuru kwa Serikali na wanasaidia Jamii inayowazunguka na kama Serikali anao wajibu wa kusikiliza na kutatua changamoto zinazo wakabili.


Ameitaka kampuni hiyo kupanua wigo wa uzalishaji wa vifungashio na kuwa suluhisho la changamoto za upatikanaji wa vifungashio nchini kwa kutengeneza vifungashio mbalimbali vitakavyotumiwa na wajasiriamali wadogo na wa kati.


Aidha, Mhandisi Ndikilo amewataka wawekezaji wote Mkoani Pwani kuwa na mahusiano mazuri na Wafanyakazi wao, na kuhakikisha wanaangalia maslahi yao.
Image may contain: 2 people, people standing

NG'OMBE 12 WAKATWA NA MAPANGA BWAWANI

Pichani ni Suriani Sosopi, akiwaonesha waandishi wa habari jeraha mmoja wa Ng'ombe  3 waliokatwa miguu kwa mapanga, PICHA NA OMARY MNGINDO.
......................................

Na Omary Mngindo, Bwawani

Ng'ombe 12 wanaomilikiwa na Seif Lukake mkazi wa Kijiji cha Visakazi Kata ya Ubena Chalinze, wilayani Bagamoyo Pwani, wameshambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao, ikiwemo watatu kuvunjwa miguu.

Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumanne ya Sept 10 kijijini hapo, ambapo inadaiwa kwamba mifugo hiyo iliingizwa kwenye shamba la mkazi aliyetajwa kwa jina moja tu la Daud, mtoto wa mzee Maarufu kijijini hapo aitwaye Mzee Selemani.


Wakizungumza na Waandishi wa habari eneo la tukio, Surian Sosopi Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji (CCWT) Kata ya Ubena, alisema kuwa alipewa taarifa ya kuwepo kwa tukio hilo, lililofanyika mbele ya Seif ambaye ndio mwenye ng'ombe hao.

"Hili tukio nilijulishwa jana usiku, kutokana na muda huo kutokuwa rafiki sikuweza kuja, leo asubuhi nimefika hapa na kama nilivyowaonesha, ng'ombe wapo 12 kati ya hao watatu wamevunjwa kabisa miguu," alisema Sosopi.

Mtendaji wa Kijiji hicho Ramadhani Tiku alisema kuwa alipigiwa simu usiku kujulishwa tukio hilo, akawajulisha askari Mgambo ambao walifika eneo husika ambapo waliweka ulinzi wa kuwadhibiti ng'ombe hao mpaka asubuhi.

"Daud ndio mwenye shamba alinijuza kuwa kuna kundi la ng'ombe limeingia shambani kwake, niliwapigia askari wa Mgambo, walifika hapa kwa ajili ya kulinda ng'ombe hawa ambao hawawezi hata kusimama," alisema Tiku.

Aliongeza kuwa wakati akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya usuluhishi na kufanyika kwa tathimi, mtuhumiwa akachukua panga na kuanza kuwakatakata ng'ombe mbele ya mmiliki huyo aliyekuwa tayari kufanya mazungumzo na kulipa gharama husika.


Sada Mdeka Mjumbe Kamati ya usuluhishi kati ya wafugaji na wakulima alisema kuwa, Daud amekuwa na tabia ya ubabe, na kwamba hata panapofanyika mazungu ya kusuluhisha migongano, yeye hufika na kuwashawishi wakulima wawafukuze wafugaji.

Akizungumzia tukio hilo, Seif mmiliki wa ng'ombe hao aliwashukuru wafugaji wenzake waliomsikiliza, baada ya kuwaomba wasifanye fujo kwani hali ingekuwa mbaya zaidi.