Tuesday, August 13, 2019

Mabalozi 42 Wanaoiwakilisha Tanzania Nchi ya Nje Warejeshwa Nyumbaniu Kushiriki Mkutano wa SADC



Mabalozi 42 wanaoiwakilisha  Tanzania  katika mataifa mbalimbali wamerejea Tanzania ili kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu na Serikali katika Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC) utakaofanyika Agosti 17 na 18, 2019, Dar es Salaam na  kesho Agosti 14 watatembelea mradi wa ufuaji umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) uliopo Rufiji Mkoani Pwani kujionea mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa fedha za ndani  ili kufanya diplomasia ya kiuchumi katika mataifa wanayotuwakilisha.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Agosti 12, 2019 Jijini Dar es Salaam, Dk Abbas amesema ziara ya kutembelea mradi huo ni kukusanya taarifa zitakazowasaidia kujenga uwezo wakushawishi mazingira ya uwekezaji Tanzania.

“Kesho pia Tanzania tutampokea Rais wa Afrika Kusini, Cyill Ramaphoza kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa ya siku tatu, itaanza kesho jioni hadi Agosti 16, pia atatembelea eneo la kihistoria Mazimbu, Morogoro lililotumika kusaidia ukombozi wa bara la Afrika.”

“Kwa hiyo viongozi wengi wa kusini mwa Afrika, si tu kwamba wanakuja katika mkutano ila wanarudi nyumbani na viongozi wote wamethibitisha kushiriki katika mkutano huo mkuu,” amesema Dk Abbas 


Aidha amesema kuwa Agosti 15 mwaka huu Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ataongoza mhadhara wa wazi ambapo ataeleza uzoefu wake juu ya jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza kuwa mhadhara huo ni wa wazi kabisa na kila mmoja anaweza kushiriki ili kuweza kupata uzoefu kutoka kwa mzee Mkapa.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi, viongozi wa serikali na wafalme unatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 17 na 18 mwaka huu.

Kabudi: Tuendelee Kushikamana Kujenga Jumuiya Imara Ya SADC Kwa Maslahi Ya Wananchi Wetu


MWENYEKITI Mpya wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Prof. Palamagamba Kabudi amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea kushikamana katika Umoja na Mshikamano baina yao ili kujenga Uchumi imara na kuleta Maendeleo ya wananchi wake.
 
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa nafasi hiyo leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, alisema wakati umefika kwa Nchi za SADC kuungana pamoja katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika taasisi mbalimbali za kikanda na kujenga msingi imara wa ushirikiano.
 
Prof. Kabudi alisema kwa miaka mingi Nchi za SADC zimekuwa na ushirikiano mkubwa baina yao hivyo wakati umefika kwa wananchi wa Mataifa hayo kushuhudia manufaa ya ushirikiano huo yakileta manufaa makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
 
Aliongeza kuwa Tanzania kwa upande wake imeendelea kuwa nchi rafiki na mshirika wa karibu kwa mataifa yote ya SADC kama inavyojidhihirisha katika historia ya mapambano ya uhuru wa Nchi nyingi za Kusini mwa Afrika, ambapo mataifa mbalimbali yaliweka kambi kwa ajili ya wapigania uhuru wake katika harakati zao za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni.
 
“Mwaka huu tunatimiza miaka 20 tangu kufariki wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi shupavu aliyejitoa pamoja na viongozi wengine wa SADC katika kupigania harakati za ukombozi wa Afrika, tunapaswa kumuenzi kwa kuhakikisha tunaimarisha umoja na ushirikiano uliopo kwa maslahi ya wananchi wetu” alisem Prof. Kabudi. 
 
Prof. Kabudi aliwataka Viongozi wa SADC kuimarisha Umoja kwa kuwa ndiyo silaha kubwa ya ushindi katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji na biashara ndani ya Nchi za SADC pamoja na kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuibua na kujenga fursa za uchumi jumuishi.
 
Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Tax alisema jumuiya hiyo imekuwa ikitekeleza programu na miradi mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda ndani ya jumuiya hiyo ambayo tayari imeleta mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo ambao umeweza kutumia rasilimali mbalimbali ikiwemo madini na nishati kwa ajili ya kujenga uchumi jumuishi.
 
Anaongeza kuwa katika Mkutano huo wa 39 unaotarajiwa kuhitimishwa na Mkutano Mkuu wa Marais wa Nchi za Jumuiya hiyo tarehe 17-18 Agosti mwaka huu, Sekretarieti ya Baraza hilo imeweza kuzindua Baraza la Biashara la SADC ambalo litakuwa chachu ya kuunganisha sekta binafsi na ile ya umma katika kujenga uchumi jumuishi kupitia ajenda ya viwanda pamoja na usimamizi wa rasilimali mbalimbali ndani ya jumuiya hiyo.
 
Akizungumzia kuhusu majanga ya kibinadamu ndani ya SADC. Dkt. Tax alisema kati ya Mwezi Machi-April Jumuiya hiyo ilipata majanga ya kibinadamu katika Nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, ambapo pamoja na changamoto hiyo Wakuu wa Jumuiya hiyo waliungana pamoja na kuweza kuzisadia nchi hizo kwa kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo madawa na vyakula.
 
Kwa upande Mwenyekiti wa Baraza hilo anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah alisema Umoja na mshikamano wa Jumuiya hiyo umeendelea kuimarika kwa kuwa nchi nyingi zimeendelea kuwa katika hali ya umoja, amani na utulivu.

Jeshi La Polisi Kutumia mbwa, farasi na helicopter Kulinda Wageni wa Mkutano wa SADC Jeshi La Polisi Kutumia mbwa, farasi na helicopter Kulinda Wageni wa Mkutano wa SADC

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam  limesema kuanzia kesho Jumatano litaimarisha ulinzi kwa kutumia vikosi vyote vya doria ikiwemo mbwa, farasi na helicopter ili kuhakikisha mkutano wa 39 Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), unamalizika salama.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 13, 2019 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema doria hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuwapokea wakuu wa nchi 16 ambao wote wamedhibitisha kuhudhuria mkutano huo.

"Tuliweka zuio la baadhi ya vyombo vya moto kutoingia katikati ya mji katika kipindi hiki cha mikutano ya SADC ,  kuna baadhi wamekiuka hasa pikipiki (bodaboda) ambazo zimekuwa hazifuati sheria, wanabeba mishikikaki, hawavai kofia ngumu na kupitia msako uliofanywa na jeshi la polisi vyombo vya moto 126 vimekamatwa na hivyo vikihusisha pikipiki 87, bajaji 13 na magari yenye ving'ora na taa sumbufu barabarani 26 na baadhi ya wahusika wanashikiliwa na watapelekwa mahakamani" amesema  Mambosasa. 

Aidha Mambosasa amesema baadhi ya barabara katikati ya jiji la Dar es Salaam zitafungwa na kwamba barabara hizi zitatangazwa baadaye.


Pia amewahakikishia wananchi na wageni usalama wa hali ya juu na bado wanaendelea na kazi ya kuhakikisha jiji hilo linaendelea kubaki salama salimini hata baada ya mkutano huo kumalizika

Uteuzi Mpya Uliofanywa na Rais Magufuli Leo


Jaji Mstaafu Mipawa anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu Januari Msofe ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Aliyemuua Mkewe kwa kumchoma Moto Atoa Vitisho Mahakamani...."Nitafanya Kitu Kibaya Hadi Mahakama Itashangaa"


Mshtakiwa anayekabiliwa na kesi ya kumuua na kumchoma moto mkewe Naomi Marijani, Hamis Said, ametoa tishio kwa waandishi wa habari wanaompiga picha anapowasili mahakamani ambapo amesema akimkamata mmoja wao atamfanya kitu kibaya ambacho mahakama haitakitarajia. 

Mfanyabiashara huyo ambaye yupo gerezani kwa siku 14 tangu alipofikishwa mahakamani hapo Julai 30, 2019 ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally.

“Mheshimwa Hakimu tangu nimefika hapa naona waandishi wa habari wamekazana kunipiga picha sana, yaani mpaka nimeingia humu ndani bado wananipiga picha tu bila kujua kwenye akili yangu nawaza nini, unajua mimi kwa sasa kichwa changu kimechanganyikiwa sana, hata hii kesi yenyewe sielewi itakuwaje.

“Nimekaa nitulize akili yangu halafu na wao wananisogelea sogelea kunipiga picha mwisho wanisababishe nifanye jambo ambalo si la kawaida, kwa sababu wanakuja hadi kunivua kofia jambo ambalo si japenda, wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya Mahakama, sasa nitakuja  kuwafanyia kitu kibaya hadi mahakama itashangaa,” amesema

 Baada ya maelezo  hayo Wakili wa serikali Wankyo Simon alisimama na kujibu kwamba Waandishi wanafanya kazi yao hivyo awape uhuru kwani wanazingatia sheria ya taaluma zao.

” Unajua Mahakama zote hapa nchini zinakuwa na waandishi wa habari wanapiga picha na kutekeleza majukumu yao, hivyo naomba uwape uhuru wao, lakini kwa hilo ulilosema kwamba wamekuja mpaka kukufunua kofia ili wakupige picha sio kweli tena siamini kama wanaweza wakafanya hivyo.

“Kwa sababu wakati wanakupiga picha nilikuwepo na niliona tukio zima hawajakufunua kofia ila walikuwa wanakusogelea Karibu ili wapate uso wako kwakuwa ulikuwa umejifunika na kofia,” alisema Wankyo. 

Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, 2019 kwa ajili ya kutajwa

Mshitakiwa anakabiliwa na kosa la mauaji ambapo adaiwa alilitenda Mei 15, 2019 katika oneo la Geza Ulole Kigamboni Dar es Salaam ambapo alimuua mtu anayeitwa Naomi Marajani.

Hamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya Mkaa ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake.

Monday, August 12, 2019

JWTZ laonya watakaovuruga amani

Editha Karlo,Kigoma
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema litawaadhibu wale wote watakaojaribu kuvuruga amani na usalama wa nchi.
Jeshi hilo, limetoa tahadhari kwa watu wanaotumia mapori ya akiba vibaya kuacha kufanya hivyo.
Kauli hiyo, imetolewa na Mkuu wa Brigedi ya Kanda ya Magharibi (202 Kikundi cha Vikosi), Brigedia Jenerali Julius Mkunda jana, wakati wakati akiahirisha zoezi la kijeshi la kujiweka tayari kwa wapiganaji kupambana na adui.
“Amani na usalama wa Watanzania, lazima upewe kiupaumbele, yeyote atakayejaribu kuchezea amani tutamshughulikia,”alisema.
Zoezi hilo ambalo lilifanyika kwenye mapori ya wilaya za Kibondo, Kasulu na Kakonko na kupewa jina la Opereshini KIKAKA, lilikuwa la mafanikio makubwa.
Brigedia Jenerali Mkunda alisema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mapori kutumika kwa shughuli za maficho ya ujambazi, uwindaji haramu na kilimo mambo ambayo yanafanywa na wageni kutoka nchi jirani.
“Tanzania sio shamba la bibi kwa kila anayetaka anakuja kufanya anachojisikia, hatutakubali tutawaadhibu wote wenye nia mbaya ya kutumia mapori yetu kwa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi yetu, vinatishia amani na usalama wa raia na mali zao na kuwafanya waishi kwa  woga,”alisema Brigedia Jenerali Mkunda.
 Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita kutoka Brigedi ya Kanda ya Magharibi, Kanali Wilbert Ibuge alisema mapori yote ambayo watu wanayaona nchini yana wenyewe na wenyewe ni jeshi hilo ambalo lina wajibu wa kuyatunza.
“Tuna wajibu wa kuyatunza mapori haya, hakuna mtu yeyote ambaye ataingia akaachwa ayatumie anavyotaka,”alisema.
Alisema mafunzo hayo, ni sehemu ya utimamu na utayari wa jeshi kujindaa kupambana pindi adui anapotokea na kwa sababu kwenye vita hakuna mahali pa kufanya majaribio.
Alisema kazi ya kuwasaka na kuwakamata wote ambao wataingia kwenye mapori hayo na kufanya vitendo vya uhalifu, itatumika kama sehemu ya mazoezi kwa vitendo kwa wapiganaji.
 Mkuu wa Kikosi cha 24, ambacho kimesimamia na kuratibu mafunzo hayo, Meja J.S.Luhonyva alisema  mazoezi hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wameonyesha tayari kukabiliana na adui.
Alisema lengo la mazoezi hayo kwa kiasi kikubwa limefikiwa medani zote za mapambano ya kivita. Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kigoma,Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga, Mkuu wa Wilaya Kasulu, Kanali Simon Hanange alisema mazoezi hayo yatasaidia mkoa kuendelea kuwa na aman muda wote.

10 wanusurika kifo, mmoja hajulikani alipo boti ikizama Tanga



Oscar Assenga, Tanga

Watu 10 wamenusufika kifo huku mmoja akiwa hajulikani alipo baada ya boti waliyopanda kuzama kwenye Bahari ya Hindi Jijini Tanga, walipokuwa wakienda kuangalia visiwa vilivyopo baharini humo.

Akizungumza leo na Mtanzania Digital leo Jumatatu Agosti 12,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema limetokea jana ambao walikuwa  watu hao walikuwa wamepanda boti waliyokodi kutoka eneo la Yatch Club.

“Baada ya watu hao kupanda boti hiyo, ambao walikuwa wakienda kutembelea visiwa mbalimbali vilivyopo kwenye bahari hiyo na ndipo upepo mkali uliwazuia kwenda mbele na walipotaka kugeuza kurudi walipotoka ndipo ilipopinduka na kuwamwaga.

“Kwenye boti hiyo kulikuwa na watu 11 ambapo 10 kati yao waliokolewa kutokana na kuvaa maboya wakati wakiwa baharini na mwingine mmoja ambaye inadaiwa hakuwa nayo hadi sasa hajulikani alipo,” amesema.

Aidha, Kamanda Bukombe ametoa wito kwa wananchi wanaotumia bahari kusafiria kuchukua tahadhari wanapokuwa baharini kwa kuhakikisha wanavaa maboya ya kujiokolea ili wakati yanapotokea majanga kama hayo waweze kuona namna ya kujiokoa.

Sheikh Dodoma ataka asilaumiwe mtu ajali Morogoro

Waumini wa dini ya Kiislamu wakiswali Ibada ya Eid El Hajj, katika Msaikiti wa Ghadaf jijini Dodoma.
Ramadhan Hassan, Dodoma
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amewaomba Watanzania kuwaombea waliofariki na majeruhi wa ajali ya moto ilivyotokea mkoani Morogoro juzi Jumamosi Agosti 10.
Aidha, amesema hakuna wa kulaumiwa kutokana na tukio hilo ambapo watu zaidi ya 65 na walifariki dunia.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 12, katika Ibada ya Iddi El Hajj iliyofanyika katika Msikiti wa Gaddaf Jijini hapa, Sheikh Rajabu amesema hakuna wa kumlaumu katika ajali hiyo kwani kila mmoja Mwenyezi Mungu amempanguia namna ambavyo atafariki.
“Kutokana na ile ajali nani wa kulaumiwa, hakuna wa kulaumiwa, hatupaswi kulalamika, Mwenyezi Mungu amepanga kila mmoja atakufa kwa namna ambayo atakuwa amepanga yeye.
“Kuna wengine watakufa kwa upanga,kuna wengine watakufa majini na kwenye ajali kwa hiyo hakuna wa kulaumiwa katika hili,” amesema.
Aidha aliipongeza Serikali kwa kuwasaidia majeruhi wa ajali hiyo pamoja na kuwahifadhi wale ambao wamefariki.

SADC YAMUUNGA MKONO RAIS DKT MAGUFULI UJENZI WA MRADI MKUBWA WA UMEME RUFIJI

 

Mkurugenzi wa Miundo mbinu katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC), Mapolao Makoena akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa habari za SADC katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC),kuhusu uboreshaji wa miundombinu hasa kwa nchi wanachama wa SADC,Makoena amempongeza Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuzindua ujenzi wa mradi mkubwa uzalishaji wa umeme mtoto Rufiji,amesema mradi huo ni wa kujivunia sana na kwamba ukikamilika utasaidia kuondoa changamoto ya nishati hiyo katika nchi wanachama wa SADC na nchi Wanachama wa Afrika Mashariki. Picha na Michuzi Jr.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Viwanda katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC), ,Calicious Tutalife akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa habari za SADC katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC),Kuhusu uwezeshaji wa biashara huria sambamba na uwepo wa upatikanaji wa ushindani na maendeleo ya Viwanda anuai,kuongezeka kwa uwekezaji wa viwanda na tija,kufuata ubora na viwango vilivyowekwa Kimataifa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC),
Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Viwanda katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC),Calicious Tutalife,Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano- SADC Barbara Lopi na Mkurugenzi wa Miundo mbinu katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC), Mapolao Makoena .
 
Wanahabari wakisikiliza yaliyokuwa yakijiri kwenye mkutano huo 

Ujenzi wa mradi wa umeme katika Mto Rufiji umetajwa kuwa wa mfano katika nchi za SADC na nchi wanachama wa Afrika Mashariki wa EAC, kutokana na namna Serikali ilivyoamua kuusimamia. 
Akizungumza katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar  leo na Wanahabari , Mkurugenzi wa Miundo mbinu katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika ( SADC), Mapolao Makoena  amesema mradi huo mkubwa unaojengwa nchini ni wa kipekee, ambao unasimamiwa moja kwa moja na Serikali na unagharamiwa na fedha za ndani. 
“Mradi huu mkubwa wa Rufiji ni jambo la kujivunia, sisi SADC tunajivunia na si kwa SADC tu, lakini pia kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema mradi huo ni wa kujivunia sana na kwamba ukikamilika utasaidia kuondoa changamoto ya nishati hiyo katika nchi wanachama wa SADC na nchi Wanachama wa Afrika Mashariki.
Mokoena amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu wake wa kutekeleza mradi huo mkubwa wa umeme, ambao utasaidia kupunguza tatizo la umeme katika nchi za SADC huku akisema SADC inamuunga mkono katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa umeme. 
Amesema mradi huo unaonesha unatoa funzo kwamba uongozi unahusika katika kuhakikisha miradi yenye tija inasimamiwa kwa nguvu zote ili kuzinasua nchi zetu katika matatizo ambayo yanaweza kutatuliwa kwa uwezo wa ndani. 
Mokoena amesema kutokana na uhaba wa nishati unaozikabili nchi nyingi wanachama wa SADC, juhudi za ziada zinahitajika kuboresha upatikanaji wa nishati, ambayo ni muhimu katika kutimiza malengo ya uwekzaji katika viwanda na uzalishaji wa bidhaa. 
Amesema miongoni mwa mikakati muhimu ya SADC kwa sasa ni kuhakikisha kuwa na uhakika wa nishati rahisi, yenye uhakika, gharama ya chini, kupitia mpango maalumu uliowekewa ukomo wa mwaka 2027.

MKUTANO WA SADC NGAZI ZA MAWAZIRI KUANZA KESHO


Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unatarajiwa kuanza kufanyika jumanne ya Agosti 12,2019 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi anatarajiwa kukabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa ngazi za Mawaziri.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa pikipiki mpya zinazotarajiwa kutumiwa katika mapokezi ya viongozi na wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa SADC unaoendelea Jijini Dar Es Salaam,waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema serikali imekuwa ikiendelea na maandalizi mbalimbali ya mapokezi ya viongozi hao ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri ikiwemo magari na pikipiki achilia mbali hotel watakazofikia viongozi hao.

Aidha Prof. Kabudi kwa niaba ya serikali,ameeleza kuridhishwa na kufurahishwa kwa namna vyombo vya habari Nchini vinavyoripoti kizalendo Mkutano unaoendelea wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) jambo ambalo limeongeza uelewa wa wananchi kuhusu SADC na kuvitaka kuendelea kufanya hivyo katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya nchi.

Katika tukio jingine Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Denmark Nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet.

Katika mazungumzo yao Prof. kabudi amemkaribisha Balozi huyo mteule nchini na kumhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini huku Balozi Mteule Mette Norgaard Dissing-Spandet akiipongeza serikali kwa mageuzi ya haraka inayoyafanya ili kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na kuongeza uwajibikaji serikalini.