Tuesday, August 6, 2019

NDEGE YAUNGUA MAFIA MKOANI PWANI.

NA MWAMVUA MWINYI,MAFIA

WATU sita wamenusurika kifo kufuatia ndege ndogo iliyokuwa ikitoka wilayani Mafia ,mkoani Pwani kuelekea Jijini Dar es Salaam kuanguka na kushika moto.

Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizotolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Rufiji ,Onesmo Lyanga zinasema hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa,zaidi ya watu sita kujeruhiwa.

Lyanga alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitoka Mafia kwenda uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere.

“Ndege hiyo ndogo ilianguka ilipokuwa ikitaka kuruka na kurudi chini na kudababisha majeruhi hao ambapo hadi sasa hakuna ripoti ya mtu yoyote aliyefariki dunia,” alifafanua Lyanga.

Alieleza bado jeshi la polisi wako eneo la tukio kukagua na kufuatilia ajali hiyo na taarifa zaidi zitatolewa.

RAS LINDI ATAKA UDHIBITI WA RISITI VITUO VYA MAFUTA.

Hadija Hassan, Lindi.

Kutokana na Mfumo wa Mashine za kielektroniki (EFD) zilizofungwa katika vituo vya Mafuta hapa Nchini kutoa Lisiti ambazo hazina majina ya wateja wanaopatiwa Huduma, Katibu tawala wa Mkoa wa Lindi , BI, Rehema Madenge amewashauri Wamiliki wa Vituo vya Mafuta kuhakikisha risiti wanazozalisha hazibaki hovyo ili kuwadhibiti watu wenye nia ovu wanaofanya udanganyifu.

Madenge alitoa ushauri huo jana alipotembelea katika Banda la Maonesho la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Lindi katika Maonesho ya 27 yanayofanyika Kanda ya Kusini katika Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi.

Alisema wapo baadhi ya Madereva wanaofanya ujanja ujanja wa hela za Mafuta wanazopewa na Ofisi zao ambao sio waaminifu wanatumia risiti wanazozikuta katika vituo vya mafuta kulinganisha na fedha walizopewa ofisini kwao.

Alisema ili kudhibiti hali hiyo ni vyema wamiliki hao wa vituo vya mafuta kufanya udhibiti wa risiti wanazozalisha pasipo kuwapa wateja wanaowahudumia pamoja na kuwataka wateja wote wanaokwenda kupata huduma katika vituo hivyo kuchukuwa risiti zao mara baada ya kuhudumiwa.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda ambae alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Pili ya Maonesho ya Nane nane kanda ya kusini 2019 alitoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwadhibiti pamoja na kuwasimamia mawakala wa mashine hizo za Kielektronik (EFD) kupeleka mashine hizo kwa wafanya biashara kwa wakati.

Mmanda alisema Mamlaka hiyo haina budi kukabiliana na upungufu wa mashine hizo huku akisisitiza usimamizi wa karibu ili kuondoa changamoto hiyo ya upungufu wa mashine.

TCRA LINDI YATAKA WANANCHI WAJITOKEZE KUSAJILI LAINI ZA SIMU.

Wananchi wa Lindi na viunga vyake wakipata huduma za usajili laini za simu kwa alama za vidole katika banda la TCRA ambapo NIDA na watoa huduma walikuwepo.
...............................


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wananchi wa Kanda ya Kusini watumie maonesho ya Nane Nane kupata elimu ya Mawasiliano pamoja na usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Hayo ameyasema Afisa wa TCRA Abdulrahaman Millas katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini mkoani Lindi.

Alisema maonesho ya Nane Nane yatumike kwa wananchi kusajili laini za simu kwa alama za vidole na  kwamba huduma zote za kufanya usajili zipo ndani za maonesho hayo.

Millas aliongeza kuwa, ni vyema kutumia muda uliokuwepo wananchi kusajili laini za simu kwa alama za vidole kwani mwisho wa usajili huo ni Desemba 31 mwaka huu.

Alisema kuwa muda uliopangwa lazima utumike kikamilifu kupunguza kujazana kwa watoa huduma katika tarehe za mwisho za Desemba.

“Muda uliowekwa ni mkubwa kwa wananchi kupata kitambulisho cha Taifa na kusajili laini zao za simu na walio na vitambulisho vya Taifa wasajili laini zao za simu kuondokana na usumbufu wa kufungiwa mawasiliano simu hizo.

Aidha alisema kuwa TCRA ipo bega kwa bega katika kutoa elimu kwa wananchi kwa huduma mbalimbali za mawasiliano ili wasitumie mawasiliano kinyume cha sheria.

MAGAZETI YA LEO AGOSTI 06, 2019.

Monday, August 5, 2019

MALIPO YA KOROSHO YAWATESA WAKULIMA BAGAMOYO.

Na Omary Mngindo.

Wakazi wa Kijiji cha Yombo Kata ya Yombo jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatamani kubadilishana kopo la korosho na kilo ya unga, ili kujikimu kimaisha.


Hatua hiyo inatokana na kukabiliwa na hali mbaya kiuchumi, kutokana na kutegemea kilimo cha korosho na mahindi, huku sekta hiyo ikikabiliwa na changamoto luluki, iliwemo kuchelewa malipo ya korosho na mifugo mashambani.


Mkazi Mwajuma Kilakala akiwakilisha wenzake katika mkutano ulioitishwa na Mbunge Dkt. Shukuru Kawambwa, Kilaka alisema kuwa, kucheleweshwa malipo ya korosho wanaishi maisha magumu, huku wakitamani kubadilishana korosho na kilo ya unga.


"Mbunge, tunaomba utupatie ridhaa sisi wakulima kuuza korosho kwa wanunuzi wa binafsi, msimu wa kuhudumia mikorosho umefika, malipo yetu bado, tunahitaji kununua dawa za kupulizia, hela hatuna, pia mtu mwenye kilo mbili za korosho lazima apeleke kwenye gurio?," alihoji Kilakala.


Kwa upande wake Juma Hemed amelalamikia ardhi ya shule ya secondari ya Miembesaba ambapo eneo lake linachukuliwa kiholela, huku Sijali Hemed akilalamikia mifugo katika mashamba.


Akitolea majibu ya malalamiko hayo, Dkt. Kawambwa alianza kujibu lililohusiana na korosho ambapo alisema uuzwaji wa korosho hawezi kulitolea taarifa kwani ni agizo kutoka serikali kuu linalowataka wakulima kupeleka katika maghara ili zinunuliwe na serikali.


"Kuhusu mifugo kuchungwa kwenye mashamba amekemea tabia hiyo, huku akiwataka watu wanaojihusisha na ufugaji kuheshimu mashamba, huku alisema ataliwasilisha kwa Mkuu wa wilaya ili hatua zichukuliwe," alisema Dkt. Kawambwa.