Sunday, June 30, 2019

WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA MWAKITOLYO SHINYANGA.

Image may contain: 6 people, people smiling, people standing
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (aliyeinua mkono), akifurahi na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kukata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Kijiji cha Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, Juni 29, 2019.
Image may contain: 7 people, people standing

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, Juni 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
.......................................


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametimiza ahadi yake aliyoitoa mwanzoni mwa mwezi huu (Juni) 2019 kwa wananchi wa Kijiji cha Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, kuwa umeme utawashwa katika eneo lao kabla ya Julai, 2019.


Dkt. Kalemani alitimiza ahadi hiyo jana, Juni 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi mkoani Shinyanga, ambapo aliwasha rasmi umeme katika jengo la Ofisi ya Serikali, Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano.


Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara kijijini Mwakitolyo, Waziri Kalemani alisema Serikali inatambua umuhimu na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo wa madini katika uchumi wa nchi.


Alisema, ndiyo maana aliagiza mchakato wa kupeleka umeme eneo hilo uharakishwe; baada ya kufanya ziara katika eneo hilo awali na kushuhudia wachimbaji wadogo wa madini wakifanya kazi zao bila umeme.


Kuhusu Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA) katika eneo hilo, Kampuni ya Angelique International Limited ya India, ambaye katika ziara yake ya awali, Waziri aliagiza kushikiliwa kwa Hati za kusafiria za Wakurugenzi wa Kampuni husika, kutokana na kusuasua kwa kazi, ambapo sasa aliruhusu mmoja kati yao arejeshewe hati hiyo baada ya kuridhishwa na maendeleo ya kazi.


“Maendeleo ya kazi yao kwa sasa yanaridhisha. Naagiza Kiongozi wao mkuu, arejeshewe Hati yake lakini wenzake watatu wataendelea kuwepo hapa hadi watakapokamilisha kazi ya kuunganisha vitongoji vyote vya Mwakitolyo,” alielekeza Waziri.


Aidha, Dkt. Kalemani alitoa maagizo kwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Fedgrace Shuma pamoja na Mkandarasi husika, kukamilisha kazi ya kusambaza nguzo za umeme katika eneo hilo ndani ya Wiki mbili tu ili eneo lote liwashwe umeme katika kipindi hicho.


Waziri alitoa rai kwa wananchi wa Mwakitolyo kujitokeza kwa wingi na kuendelea kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000/- tu.


Aidha, aliwataka viongozi wanaosimamia Taasisi mbalimbali za Umma na Miradi ya kijamii, kutenga fedha katika bajeti zao na kulipia gharama hiyo ndogo ili Taasisi na Miradi husika iunganishiwe umeme.


Awali, akikagua maendeleo ya kazi ya kuunganisha umeme katika Kijiji cha Mahembe, Waziri Kalemani aliuagiza uongozi wa TANESCO Shinyanga, kufunga Transfoma kubwa yenye uwezo wa kilovoti 200, kwenye Kituo cha Afya katika eneo hilo, ndani ya siku Tano, ili kuboresha huduma kwa wananchi.


Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwapelekea wananchi maendeleo, hususani umeme vijijini.


Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Donald Magesa, alisema uongozi na wanachama wa CCM mkoani humo, wanafurahi kuona Ilani ya Chama Tawala ikitekelezwa kwa vitendo.


“Ilani ya Chama inasema umeme uende kila nyumba. Tunatekeleza. Nawaombeni wananchi tujitokeze kwa wingi kulipia shilingi 27,000 ili kila mmoja apate umeme na tupate maendeleo kama Serikali inavyokusudia,” alisema Katibu.


Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwakitolyo, Nuhi Shomi na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano, Benedict Robert, kwa nyakati tofauti, walimpongeza Waziri Kalemani, kutimiza ahadi aliyoitoa kwa wananchi wa eneo hilo kwa kuwashiwa umeme ndani ya muda mfupi.


Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alifuatana na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Tawala na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, REA na TANESCO.
Image may contain: 3 people, people standing, sky and outdoor
 Fundi kutoka Kampuni ya Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Kampuni ya Angelique International Limited ya India, akikamilisha zoezi la kuunganisha umeme katika Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano, Shinyanga Vijijini wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) Juni 29, 2019. Wanaoshuhudia ni wananchi wa eneo hilo.
Image may contain: 14 people, people standing, crowd and outdoor

 Sehemu ya umati wa wananchi wa Kata ya Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, Juni 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.


TRUMP AKUTANA NA KIM NA KUFANYA MAZUNGUMZO.

Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na kiongozi wa Korea Kaskazini katika eneo lisilo la kijeshi la mpaka wa Korea mbili ambapo viongozi hao wawili walipeana mikono kuonesha ishara ya matumaini ya amani.


Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, wamekubaliana kuanzisha tena mazungumzo ya nyuklia yaliyokwama hapo awali.


Katika wiki zijazo, vikosi kazi vitaanzishwa kutoka pande zote mbili ili kuanza ukurasa mpya wa kuendeleza amani.


Upande wa Marekani utaongozwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo.


Trump hakutoa maelezo zaidi kuhusu yale yatakayojadiliwa lakini ameeleza wazi kwamba vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini vitaendelea kubaki kwa muda mpaka hapo itakapofikiri vinginevyo.


Marekani imeitaka Korea Kaskazini isimamishe kabisa mpango wake wa nyuklia.


Korea Kusini na Marekani pia wanahimiza upatikane mkataba rasmi wa amani kati ya Korea Kusini na Kaskazini.

CCM WILAYA YA MKURANGA YAANZA ZIARA.

Na Omary Mngindo, Mkuranga.

SEKRETARIET ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, ipo katika ziara ya kikazi kwenye Kata 25, lengo likiwa ni kujenga mahusiano zaidi na yenye tija, ndani ya chama hicho.


Katibu wa Sekretariet hiyo Hanzuruni Mtebwa ameiambia BAGAMOYO KWANZA BLOG kwa njia ya simu kwamba, ziara hiyo chini ya Katibu wa chama hicho wilaya Rukia Mbasha aliyehamia wilayani humo hivi karibuni akitokea mkoani Lindi, inalenga kujenga mahusiano ya wana-CCM hao.


Ametanabaisha kuwa, tayari wameshazitembelea Kata saba kati 25, ambazo ni Tengelea, Vianzi, Vikindu, Mwandege, Mkuranga, Mtambani na Mipeko ambapo pia ziara hiyo imetumika kumtambulisha Katibu huyo mpya.


Aidha katika kufikia malengo hayo, Sekretariet hiyo imekabidhi REJA za wanachama kwa Mabalozi wote wenye jukumu la balozi, ili kuhakiksha wanaweka taarifa sahihi za wanachama wanaoishi ndani ya eneo lao la uongozi.


"Sanjali na hayo, pia tumewahimiza kuwa na vikao ikiwemo kuanza maandalizi ya uchaguzi ujao kuanzia serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kama unavyofahamu mwishoni kwa mwaka huu tutaanza kuchagua Wenyeviti," alisema Mtebwa.


Sanjali na hayo, Sekretariet hiyo imempongeza Mbunge wao Abdallah Ulega, ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwa namna anavyojitoa katika kukitumikia chama na wananchi, ambapo ameboresha jengo la sanjali na kuweka fremu za biadhara ikiwa ni mradi wa chama hicho.


"Katika ziara hiyo tumepokea ushuhuda kutoka kwa viongozi, waasisi na wanachama wa CCM, juu ya jitihada za kukisaidia Chama kwa kuchangia Ujenzi wa majengo ya Chama ambapo Mbunge Abdallah Ulega amejitoa katika hilo," alisema Mtebwa.


Akizungumzia usajili wa wanachama kwa mfumo wa Kielekrtonic, Katibu huyo alisema kuwa katika uzinduzi uliofanyika kila Kata, wanachama zaidi ya 100 wamasajiliwa, huku akigusia changamoto ya uchache wa simu ambapo kila eneo kuna simu moja tu.


Kutokana na hali hiyo, Sektretariet imeanzisha harambee iliyokusanya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni tano, ikiwemo ahadi pamoja na pesa taslim zitakazotumika kwa ununuzi wa simu ili kuboresha usajili kwa wana-CCM hao.

MTAMBO WA MEGAWATI 300 KUTENGENEZWA MTWARA.

Image may contain: 9 people, people standing and outdoor
Na Omary Mngindo, Mkuranga.

SERIKALI imeeleza kuwa ina mpango wa kutengeneza mtambo mkubwa utakaozalisha Megawati 300 za umeme, kisha kuusafirishwa kutoka mkoani Mtwara kwenda Kinyerezi jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu ameyasema hayo alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Njopeka, Kata ya Mjawa wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, akiwa kijijini hapo mwishoni mwa wiki, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuboresha huduma ya umeme.


Aidha alisema kuwa serikali imefanya tathmini ya fidia kwa wananchi wa maeneo ya Rufiji, Mkuranga na Dar es Salaam ambao wamepitiwa na bomba la gesi na nguzo za umeme, huku akiomba radhi kuchelewa kulipwa fidia, na kwamba zoezi hilo linataraji kuanza Julai mwaka huu.


"Malipo yataanza mwezi Julai kwa wakazi waishio Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya hapo zoezi litaendelea tena kuanzia mwezi wa nane mpaka wa kumi na mbili mwaka huu kwa wakazi wa maeneo ya Mkuranga, niwaombe radhi kwa kuchelewa fidia hizo" alisema Mgalu.


Aidha Mgalu amewataka mafundi wa shirika la umeme Kanda ya Rufiji kuweka kambi katika eneo la Njopeka, ili kuhakikisha wanasambaza umeme katika nyumba za wananchi sanjali na kwenye kisima cha maji, lengo likiwa ni kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi kijijini hapo.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo Alhaj Abdallah Ulega, ameelezea shukrani zake kwa serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ya usambazaji umeme jimboni mwake.


"Nikuondoe hofu dada yangu Mgalu, Serikali kupitia wizara yenu ya Nishati mmefanyakazi kubwa sana ya kusambaza umeme katika vijiji jimboni kwangu, nitumie fursa hii kuishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa namna inavyosimamia usambazaji wa nishati hii," alisema Ulega.


Nae Mwenyekiti wa Kijijini cha Njopeka Muharami Mketo alisema kuwa tangu kijiji hicho kianzishwe pamoja na kupitiwa na umeme mkubwa ndio kwanza wanaonja ladha ya umeme.

WAZIRI KAIRUKI AIPONGEZA MKURANGA.

Image may contain: 3 people, people standing and stripes
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angela Kairuki, (katikati) akikagua kiwanda cha kinachotengeneza marumaru wilayani Mkuranga.

Image may contain: 4 people, people sitting, table and indoor

 Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angela Kairuki amewapongeza viongozi na wataalam wa Halmashauri ya wilaya ya mkuranga Mkoa Pwani kwa mikakati yao ya kuwavutia wawekezaji.


Akizungumza kwenye kijiji cha Mwanambaya baada ya kukagua ujenzi wa kiwanda cha “Fiber Solution” waziri Kairuki aliwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itawashika mkono ili kufanikisha azma yao.


Aidha Kairuki aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa asilimia (100) na watanzania wazawa kufungua bohari Makao makuu ya serikali Dodoma sambamba na kusambaza mikoani.


Awali mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho cha kutengeneza nyaya za mkongo Raddy Fiber Solution Ramadhani Hassan Mlanzi alisema pamoja na uzoefu na ukomavu katika teknolojia ya mawasiliano hasa mfumo wa Fiber wanakabiliwa na changamoto zikiwemo uagizaji wa bidhaa za waya na viunganishi toka nje ya nchi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mhandisi Mshamu Munde alisema wamevutia wawekezaji kuwekeza katika viwanda vya kilimo, uvuvi, na mifugo ambapo hadi kufikia June 2019 wana viwanda (71) vilivyoajiri watanzania 5424 kati ya hivyo viwanda vikubwa 12.


Munde alimhakikishia Waziri kairuki kuwa mkakati wao ni kufanya uwekezaji kuwa endelevu hatimaye kufanikisha kufikia uchumi wa kati kufikia (2025)
Akiwa wilayani mkuranga Kairuki alitembelea kiwanda cha marumaru MKIU kilichozinduliwa na Raisi Magufuli April 2017.