Monday, June 24, 2019

DC. BAGAMOYO AZINDUA SOKO LA WANAWAKE WAJASIRIAMALI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa, (katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa soko la pamoja la wanawake wajasiriamali wilayani humo, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, wilaya ya Bagamoyo, Teddy Davis.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, wilaya ya Bagamoyo, Teddy Davis, (wa pili kulia) akipunga mkono mara baada ya Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bi Zainabu Kawawa (kushoto) kukata utepe kama ishara ya kuzinduliwa rasmi kwa soko la pamoja la wanawake wajasiriamali Bagamoyo.
.........................................

 Na Selestian James

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa  amezindua soko la Pamoja la wanawake wajasiriamali wilayani humo, ikiwa kama hatua ya kuwakwamua katika shughuli zao za kiuchumi.


Shuguli hiyo ya uzinduzi iliyofanyika hivi karibuni katika mgahawa wa smoke house uliopo kata ya Dunda wilayani Bagamoyo ilikutanisha wanawake wajasiriamali kutoka kata mbalimbali wilayani humo ikiwemo kata ya Dunda, Magomeni, Zinga, Kiromo na Nianjema.


Wanawake hao walifika wakiwa na bidhaa mbalimbali za ubunifu na mazao mbalimbali ya kilimo zikiwa kama shughuli kuu za kujiingizia kipato.


Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewapongeza wanawake hao kwa hatua ya kuanzisha soko hilo kwa kutumia eneo lao binafsi badala ya kuisubiri serikali.


Alisema amefarijika na hatua hiyo na kwambaametoa ahadi ya kushirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanapata  eneo kubwa zaidi kwa ajili ya ujenzi wa soko.


Alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi  wilayani humo kushirikiana nae na kumuonesha ni sehemu gani inayofaa kulingana na shughuli zao, ili nae kama kama kiongozi wa serikali afuate taratibu atimae wafanikishe.


"Hatuwezi kuwa na bidhaa nzuri kama hizi halafu tukakosa soko la kuuzia, bihaa nzuri kama hizi ndio alama ya Bagamoyo" Alisema Zainabu.


lakini pia kiongozi huyo amewakaribisha ofisini kwake kinamama hao ambapo kila siku za jumanne huwa anasikliza kero mbalimbali za wananchi na kuona ni namna gani anaweza kuzitatua akiwa na wataalam mbalimbali wakiwemo wanasheria.


Naye mweyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanaweke Kiuchumi wilaya ya Bagamoyo, Teddy Devis alimshukuru mkuu wa wilaya huyo kwa kuweza kufika eneo hilo  kuwatia moyo  na kuwaunga mkono.


Alisema kwa muda mrefu wamekosa sehemu ya kuwaunganisha  kama wanawake wajasiriamali, ambapo sasa kupitia soko  hilo litakalokua linafanyika kila siku ya jumamosi litawafungulia fursa kuweza kuuza na kutangaza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.


kwa upande wa wanawake waliokuwepo katika eneo hilo wameonesha furaha zao kwa hatua hiyo iliyochukuliwa na kiongozi huyo.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa, akiwa anaangalia bidhaa za wajasiriamali katika uzinduzi wa soko la pamoja la wanawake Bagamoyo.
 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa, pamoja na Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, wilaya ya Bagamoyo, Teddy Davis, wakifurahia jambo wakati akitembelea bidhaa za wajasiriamali kwenye uzinduzi wa soko la pamoja la wanawake Bagamoyo.
 
Viongozi mbalimbali wa chama na serikali waliofika kushuhudia uzinduzi wa soko la pamoja la wanawake Bagamoyo.

PICHA ZOTE NA SELESTIAN JAMES. 
    

ZAIDI YA TANI 5,000 ZA UFUTA ZAUZWA MKOANI LINDI.

Sehemu ya magunia ya zao la ufuta kama yanavyoonekana pichani wakati wa mnada uliofanyioka mkoani Lindi.
....................................................

 NA HADIJA HASSAN, LINDI.


Jumla ya Tani 5405 na kilo 791 za ufuta wa wakulima wa Chama kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Lindi, Kilwa na Manispaa ya Lindi Mkoani humo zimeuzwa Katika Mnada wa Tatu wa zao hilo kwa Bei ya Juu ya Tsh. 2802 na Bei ya chini 2738.


Mnada huo wa Tatu umefanyika Katika ghara la chama cha Msingi Mnazi mmoja AMCOS kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo ambapo Jumla ya Makampuni 14 yaliomba kununua ufuta huo.


Akizungumza Mara baada ya kufanyika mnada huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Jomari Satura pamoja na mambo Mengine aliwaasa wananchi wa Lindi kwa ujumla kutumia fedha wanazozipata Katika mauzo ya ufuta kuwekeza Katika mambo ya kimaendele.


Alisema ili kilimo hicho kiweze kuonekana kimeleta tija Katika Mkoa huo ni vyama, wakulima baada ya kupata fedha zao wakafanya mambo yanayoweza kuwainua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba mzuri ambayo itaonyesha utofauti wa kabla ya Msimu na baada ya msimu


 Aliongeza kwa kusema kuwa, ni ajabu kuona mpaka Msimu wa mauzo unaisha Huku mabilioni ya fedha yakiwa yamewafikia wananchi lakini maendeleo ya Moja kwa Moja yasionekane.


Nae Mstahiki meya wa Manispaa Lindi Lidume Liumbo Akifunga mkutano huo wa Mnada wa ufuta Alitumia fulsa hiyo kuwaasa wananchi wa Manispaa hiyo kuongeza Tija ya uzalishaji wa zao hilo Ili kuweza kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, Mkoa na nchi kwa ujumla.

Wananchi wakiwa katika mnada wa Ufuta mkoani Lindi.

DIWANI WA TENGELEA, MKURANGA ATATUA TATIZO LA MAJI.

DIWANI wa kata ya Tengelea wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Shabani Manda amefanikiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu.


Akizungumza na wananchi wa eneo kata hiyo, Manda alisema walikuwa wakisubiri huduma hiyo kwa muda mrefu na kwamba sasa imefanikiwa kwa wananchi hao kupata huduma ya maji.


"Maji ni uhai maji ni maisha ya kila siku kwa mahitaji ya viumbe hai hivyo kupatikana kwa mradi huu mkubwa wa kisima utasaidia wananchi wa kata yangu kuondokana na changamoto hiyo. Alisema Manda.


Alisema Awali wananchi hao walikuwa wakipata tabu kubwa sana kutokana na kutumia visima vya kienyeji.


Aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo kudumu kwa muda mrefu aliweza kupambana kutafuta wadau na kufanikiwa kuwapata wafadhili waliojitolea kujengea kisima kirefu katika msikiti wa Sunguni.


Aidha alisema kuwa Al Fridaus Charitable Foundation ndio taasisi iliyojitolea kuwajengea wananchi wa kata yangu kisima Chenye uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi wasiopungua 500.


Aliongeza kuwa maji hayo ni ya wananchi wote bila ubaguzi wa dini wala kabila hivyo kila mmoja yuko huru kutumia maji hayo.


Kwa upande wake kiongozi wa msikiti huo Hamisi Mohamed amempongeza diwani huyo kwa jinsi anavyojituma katika kutafuta wafadhili mbalimbali kwa lengo la kuendeleza kata ya Tengelea.


Aidha ameipongeza taasisi ya Al Firdaus Charitable Foundation kwa msaada wa kisima walichokitoa kwa wakazi wa eneo hilo kwani walikuwa na changamoto kubwa ya maandalizi kwa ajili ya kupata huduma ya kutawadha wakati wa kuswali.


Naye mwakilishi wa taasisi hiyo hapa nchini Buddy Amour amesema kuwa Taasisi yao imejikita katika kutatua changamoto mbalimbali kwa lengo la kuisaidia serikali kwani peke yake ni vigumu kumaliza changamoto za wananchi wake.


"Tumejipanga kama taasisi ili kuhakikisha tunawasaidia wananchi wa maeneo tofauti tofauti ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wake popote pale walipo " Alisema Amour.


Aidha amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa jinsi walivyokuwa wakijitolea kwa lengo la ufanikishaji wa mradi bila ya malipo ya aina yeyote.


Aliongeza kuwa kwa wilaya ya Mkuranga wamekabidhi visima 10 katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutokomeza uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali na hivyo takribani ya wananchi wote watakuwa na huduma ya maji.

DED-BAGAMOYO ATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA.

Image may contain: 3 people, people sitting
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Fatuma Latu amewaasa watumishi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) za utumishi wa Umma ili kuleta matokeo chanya kwenye utumishi.


Bi. Fatuma Latu, ameyasema hayo mapema wakati alipokuwa akifungua mkutano maalum wa watumishi takribani 200 wa Halmashauri hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, katika kilele cha maadhimisho ya juma la utumishi wa Umma.


“Kila mtumishi ahakikishe anafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa Umma, hizi ziwe dira wakati tukitimiza majukumu yetu ya kila siku ili kuleta matokeo chanya ya utekelezaji wa shughuli za Serikali katika Halmashauri yetu” Alisema Bi. Fatuma Latu.


Bi. Fatuma Latu pia ametumia fursa hiyo kuwaasa Watumishi kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa, matumizi ya lugha chafu, na kuhimiza ushirikiano baina ya watumishi katika ngazi zote, huku akitanabaisha kwamba hatamvumilia mtumishi yeyote ambaye atapatikana na makosa ya kuomba ama kupokea rushwa.


Akaongeza, Suala la kutunza siri pia ni muhimu sana wakati wa utekelezaji wa Shughuli za Serikali kila mmoja katika nafasi yake, utunzaji wa Siri unatufanya kufanya kazi kwa kuaminiana na kwa usalama wakati wote hivyo kuongeza ari ya kutumikia Wananchi.


Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Fatuma Latu, amewakumbusha watumishi kuhakikisha wanapata chakula bora na kujipa muda wa kupumzika baada ya kumaliza kutimiza majukumu yao ya kila siku ili mwili uwe na Afya wakati wote na kuongeza uwezo wa kufanya kazi.


Nae, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Ndg. George Mwalukasa akizungumza na watumishi katika Mkutano huo amewahimiza watumishi kuwa makini pale wanapotakiwa kuhuisha taarifa zao za kiutumishi, kwani wengi wao wamekuwa na hulka ya kupuuzia maagizo ya usafishaji taarifa za kiutumishi yanapotolewa, kwani kupuuzia usafishaji wa taarifa za mtumishi kunaweza kupelekea mtumishi kuondolewa katika orodha ya malipo ya mshahara.


Aliongeza kwa kusema  “Mtumishi ambaye hatajaza fomu za OPRAS kuaniza tarehe 01 Julai, 2019, ambapo OPRAS zitaanza kujazwa kwa njia ya kielektroniki, hatapata mshahara hadi hapo atakapokuwa amejaza fomu hiyo ya upimaji wa utendaji kazi wa Mtumishi, yaani OPRAS”.


Wakati huo huo, watumishi wamepata darasa maalum la madhara ya kujihususha na vitendo vya rushwa ambapo Afisa TAKUKURU – Elimu kwa Umma, Bi. Jane Mgaya amezungumzia mada maalum ya madhara ya vitendo vya Rushwa katika utendaji kazi wa kila mtumishi anapokuwa akitekeleza majukumu yake ya kila siku.


“Tuepuke mambo yanayopelekea uwepo wa mazingira ya vitendo vya rushwa kutengenezwa, tunapokuwa tukitekeleza majukumu yetu ya kila siku, mambo hayo ni pamoja na ukosekanaji wa uwazi katika uwajibikaji, urasimu katika utoaji huduma na tamaa ya kujipatia mafanikio kwa haraka” Alisema Bi. Jane Mgaya


Aliongeza, athari za rushwa ni kubwa kwani rushwa huondoa utu na thamani ya mtu, hudhoofisha utoaji huduma bora, kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma na hupelekea mtumishi kufanya maamuzi yenye upendeleo, hivyo akasisitiza kila mmoja kushiriki katika vita dhidi ya rushwa ili kuiletea jamii yetu maendeleo kwani vita dhidi ya rushwa si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya jamii nzima ili kuiletea jamii yetu maendeleo.


Wiki ya utumishi wa umma huadhimishwa mara moja kila Mwaka kila ifikapo Mwezi Juni, ambapo shughuli mbalimbali za kiutumishi huambatana na maadhimisho hayo, ikiwa na pamoja kusikiliza kero na malalamiko toka kwa Watumishi na kuzipatia ufumbuzi,


Aidha, katika maadhimisho hayo kunakuwa na semina mbalimbali zinazohamasisha weledi na utawala bora katika utumishi wa umma, pamoja na mkutano maalum wa watumishi ambao hufanyika siku ya kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma ambao huhudhuriwa pia na wadau mbali mbali toka sekta binafsi zikiwemo taasisi za kifedha na mashirika binafsi Wilayani hapa.
Image may contain: 2 people, people sitting, table and indoor