Sunday, June 2, 2019

DC BAGAMOYO ATOA NASAHA KWA WANANCHI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa  amefuturisha ofisini kwake na kuwataka wananchi kudumisha amani iliyopo wilayani humo ili kila mmoja afanye shughuli zake za maendeleo kwa uhuru.


Alisema katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhani kila mmoja amejifunza subira, huruma na kusamehe na kusema kuwa hali hizo zinapaswa ziendlezwe katika miezi mingine iliyobaki.


Katika hutuba yake mara baada kufuturu aliwataka wananchi wa wilaya ya Bagamoyo kujitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mita unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ili kila mmoja ashiriki kwa nafasi yake kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ndani ya wilaya hiyo.


Alisema wale wote wenye sifa wajitokeze kugombea nafasi hizo huku wananchi wote wanapaswa kushiriki kwenye uchaguzi huo kwa kujitokeza kupiga kura.


Aidha, alisema takwimu inaonyesha Mkoa wa pwani unaongoza kwa ujenzi wa viwanda hapa nchini na kwamba wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zenye viwanda vingi mkoani Pwani.


Alitumia nafasi hiyo kuwataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia watoto waende shule ili hatimae wapate elimu itakayowasidia kupata ajira kwenye viwanda hivyo.


Mkuu huyo wa wilaya amemalizia kwa kuwataka wanachi wa Bagamoyo kujiandaa kuupokea mwenge wa uhuru ambao unatarajiwa kuingia katika wilaya hiyo Tarehe 24 Julai.


Alisema Bagamoyo imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka katika mapokezi ya Mwenge na kwamba kufanya vizuri huko kunatokana na umoja, mshikamano miongoni mwa wananchi na wataalamu kutoka idra mbalimbali za serikali na watu binafsi.


Aliwataka wananchi kuendelea na mshikamano huo ili kwa mara nyingine wilaya ya Bagamoyo ifanye vizuri katika miradi yake ambayo inatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge za mwaka 2019.


 Katibu wa ccm wilaya ya Bagamoyo, Salim Mtelela wa kwanza kushoto, akiwa na mzee maarufu mjini Bagamoyo Aliy bin Nasiri (katikati na Sheikh Ramiya Muhammad Ramiay, kulia.

 Waislamu an wanachi mbalimbali wakiwa katika mstari wa kupata futari ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alipokuwa anafuturisha katika viwanja vya ofisi yake.

 
Waislamu an wanachi mbalimbali wakiwa katika mstari wa kupata futari ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alipokuwa anafuturisha katika viwanja vya ofisi yake.



MADIWANI CHALINZE WAPEWA ELIMU

Diwani wa kata ya Mkange, Hussein Juma Hading'oka akichangia mada katika mafunzo hayo.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shaabani Millao, akitwasilisha mada mbele ya madiwani wa Halmashauri hiyo.
.............................................


Na Omary Mngindo, Lugoba


MADIWANI wa Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamepatiwa mafunzo maalumu ya namna ya kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.


Mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhusu usimamiaji wa miradi, kupitia sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2016 kuingiza utaratibu huo kwa kifungu 64 (5) cha sheria hiyo ya mwaka 2016.


Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti Said Zikatimu, Makamu Juma Mpwimbwi na Mkurugenzi Amina Kiwanuka, wakufunzi wa mafunzo Shaabani Millao ofisa mipango wa halmashauri na Dkt. Daud Paschal kutoka Chuo Kikuu Mzumbe idara ya Uhasibu na fedha wametoa mada mbalimbali.


Akisoma mada katika kikao hicho, Millao amewaambia madiwani hao kwamba, ofisi hiyo kupitia sekretariet za mikoa na Mamlaka za mitaa imetekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na shule za msingi na sekondari.


"Kifungu 64 (6) cha sheria hiyo kinatoa maana ya matumizi ya manunuzi ya umma ambayo ni utaratibu wa ushirikiano wa taasisi za umma kufanya ujenzi kwa kutumia wafanyajazi wake na mitambo yake yenyewe au kwa kushirikiana na taasisi za umma au nyingine binafsi," ilieleza sehemu ya taarifa ya Millao.


Imeongeza kwamba utaratibu huo umefafanuliwa katika sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011, kanuni ya 167 ya ununuzi ya mwaka 2013 na sheria ya (marekebisho) ya 2016 kanuni ya 64 za ununuzi wa umma ya mwaka huo.


Taarifa ya Dkt. Paschal imegusia masuala ya fedha ambayo imewataka wanaosimamia miradi katika maeneo ya wananchi kuwajulisha wananchi fedha zinazoingia katika miradi yao, hatua itayowaongezea hamasa ya kujitoa kwenye utekelezaji wake.


"Fedha lazima zipokelewe kwa kukiri mapokezi ha kiadi kilichopokelewa, jamii husika ijulishwe kupitia mikutano kiasi kilichopokelewa, pia kuhimizwa wahusika kuchangia nguvu ili wajisikie kuwa wao ni wamiliki wa miradi," ilieleza taarifa ya Dkt. Paschal.


Kwa upande wao madiwani Ramadhani Mwinyikondo na Malota Kwaga wametaka mwongozo wa namna zinavyopatikana kamati za kusimamia miradi, na kujulishwa tofauti ya Mkandarasi na utaratibu mpya.


Rehema Mwene amegusia changamoto ya kuchelewa malipo ambapo mara kadhaa wamekuwa wakiambiwa kikwazo ni epika, hivyo wameomba washirikishwe kikamilifu ili wajionee sababu zinazochangia hali hiyo ya ucheleweshwaji wa malipo mbalimbali.


Kwa upande wake Zikatimu alisema kuwa utaratibu wa sasa wa manunuzi umekuwa mkombozi katika utekelezaji wa miradi ukilinganidha na hapo awali, ambapo miradi mingi ilikuwa inasuasua kutokana na mlolongo wa kumpata mkandarasi.

WAKAZI PWANI WATAKIWA KUONGEZA UPENDO

Na Omary Mngindo, Kibaha.


WAKAZI Mkoa wa Pwani wametakiwa kuendeleza umoja, upendo na mshikamano, ambao hauna ubaguzi wa dini ya aina yeyote.


Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo, katika futari iliyoandaliwa na mmiliki wa shule ya KIPS iliyoko Kibaha Mailimoja mkoani hapa Alhaj Yusufu Mginanga ambae pia ni mmiliki wa hoteli Njuweni.


Alisema kwamba dini imeendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya haraka nchini, kutolana na viongozi wake kuwahimiza waumini wake katika kuzingatia upendo, umoja na mshikamano na kuondoa utofauti ambao zinaambatana na udini.


"Nawapongeza viongozi wa dini mkoani Pwani, baadhi yenu hivi karibuni tumesafiri kwenda kujionea mradi mkubwa wa umeme wa maji Mto Rufiji, unaotekelezwa na serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli, nawapongeza kwa kazi zenu za kuhimiza amani, umoja, upendo na mshikamano," alisema Mhandisi Ndikilo.


Aliongeza kwamba mradi huo unaotaraji kuinufaisha nchi yetu katika kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika, amewaomba viongozi wa dini wamuombee Rais aendelee kuwa na afya njema, pia kwa kazi kubwa ya kuuanzisha mradi huo ulioasisiwa na watangulizi wake.


"Wakoloni hawakuupenda mradi huu, sababu kubwa ni kwamba wamejua ungeleta maendeleo makubwa katika nchi yetu ya Tanzania, hivyo hatua ya Rais Magufuli kuuendeleza ni kitendo cha ujasili wa hali ya juu, tuanapaswa kuunga mkono kwa kazi hiyo," alisema Mhandisi huyo.


Kwa upande wake mkurugenzi wa Kampuni hiyo Alhaj Mfinanga amewataka wakazi mkoani hapa, pasipo kujali itikadi zao za dini, rangi wala siasa katika kuhakikisha kila mmoja anamsaidia Rais Magufuli katika utekelezaji wa ujenzi wa nchi, huku akisisitiza elimu.


Akizungumzia shule ya KIPS, Mfinaga alisema kwamba ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa ni shule ya awali na msingi, ambapo tangu kipindi hicho inaendelea na utoaji wa elimu na kwamba wanafunzi wanafanya vizuri katika mithihani yao ya kuingia kidato cha kwanza.


Baadhi ya waumini wa dini waliohudhulia futari wamemshukuru mmiliki wa shule hiyo, huku wakimhaidi Mkuu wa Mkoa kwamba wataendelea na utoaji wa elimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano.

JUMAA ASAIDIA PWANI POLISI VIFAA VYA UJENZI

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akimkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. Wankyo Nyigesa, risiti iliyonunuliwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 2.8.
.................................................... 

Na Omary Mmgindo, Kibaha.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amekabidhi Jipsam 100 na ndoo tano za rangi vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 2.8.


Katika hafla fupi iliyofanyika eneo linalojengwa nyumba 20 za jeshi hilo mkoani Kibaha mjini hapa, Jumaa amemkabidhi Kamanda wa jeshi hilo Wankyo Nyigesa Jipsam hizo, kwa ajili ya ujenzi huo unaolenga kuwaweka pamoja askari hao.


"Nilikuja nikakutana na Kamanda Nyigesa kanielezea mikakati ya ujenzi wa nyumba 20 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali chini ya Dkt. John Magufuli inayotazama sekta zote, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, leo nimekabidhi jipsam na ndoo za rangi za sh. Mil. 2.8,


"alisema Jumaa. Alisema kuwa anapongeza jeshi hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wilayani hapa na Mkoa kwa ujumla wanaishi kwa amani, upendo na mshikamano mkubwa ambao unachangiwa na uwepo wa askari Polisi.


"Nimpongeze Rais Dkt. John Magufuli kwa uongozi wake unaojali maendeleo ya watu wake, tunashuhudia inavyoboresha sekta zote zikiwemo elimu, afya, miundombinu, umeme na ulinzi na usalama tunatakiwa kumuunga mkono kwa vitendo," alisema Mbunge huyo.


Kwa upande wake Kamanda Nyigesa alisema kwamba kwa sasa ili kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi wa sita, wanahitaji kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 20 ili kukamilisha zoezi hilo, huku akiwaomba wadau zaidi wajitokeze katika kukamilisha mchakato huo.


"Niwaombe wabunge wengine na wadau mbalimbali wajitokeze katika kuunga mkono serikali yetu katika kuboresha masuala ya kimaendeleo kwenye nyanja zote," alisema Nyigesa. "


Tunapokea misaada kutoka kwa watu mbalimbali paaipokujali itikadi za kisiasa, polisi wananchi wote weti pasipokujali itikadi zao za kisiasa," alimalizia Kamanda Nyigesa.