Saturday, May 18, 2019

ROOM TO READ YAWEZESHA WASICHANA KUJIFUNZA UJASIRIAMALI.

Afisa mradi wa elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, Bi Rehema Juakali, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelea kiwanda cha mjasiriamali mwanamke wa Bagamoyo Teddy Davis.
 
Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Bagamoyo, Teddy davis, akizungumza na waandishi wa habari kiwandani kwake Nianjema Bagamoyo alipotembelewa na wanafunzi wa shule ya sekondari Matimbwa ambao walifika hapo kujifunza ujasiriamali.
................................



Shirika lisilo la kiserikali la  Room to read nchini Tanzania limeendelea kumuwezsha msichana kielimu ambapo kupitia mradi wa elimu ya fedha, wasichana wengi wameweza kunufaika kwa kupata elimu ya utunzaji wa fedha, kukuza mitaji na hatimae kuweza kujiajiri kupitia elimu hiyo ya fedha chini ya mradi wa elimu kwa msichana.


Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Afisa mradi wa
elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, Bi Rehema Juakali walipokuwa kwenye ziara ya kimasomo na wasichana wa shule ya Sekondari Matimbwa ambapo walitembelea kiwanda cha Mjasiriamali wa Bagamoyo Tedy Davis ili kuona namna mwanamke anavyoweza kujitegemea kwa kutumia ujasiriamali wa vitu mbalimbali.


Alisema shirika hilo limeandaa mitaala maalum ya kufundishia ujasiriamali ikiwa ni pamoja na misingi mikuu ya ujasiriamali huku wanafunzi wakipata nafasi ya kwenda kwenye ziara za kimasomo nje ya shule ili kujifunza mambo mbalimbali kwa uhalisia wake.


Juakali, alisema mradi wa elimu ya fedha ni mradi ulionzishwa rasmi mwaka 2018 kwa shule zinazofadhiliwa na shirika la Room to Read ili kuwajengea uwezo wasichana katika maswala ya kifedha na uchumi kwa ujumla.


Aliongeza kuwa, mpaka sasa shule kumi zimepata fursa ya kupata mradi huo ambazo Halmashauri ya Bagamoyo ni shule nne Chalinze shule mbili huku Kibaha kukiwa na shule nne.


Alisema shule hizo kumi ni wanufaika wakubwa wa mradi wa elimu ya fedha ambapo wanafunzi wake wameweza kuwa na mabadiliko ya kitabia na kiuchumi hasa katika kujiwekea akiba ya fedha na hatimae kuweza kujifanyia mambo mbalimbali ya maendeleo katika familia zao.


Aliendela kusema kuwa, kwa wasichana wa ngazi ya sekondari tayari wamekuwa na uwezo wa kuandaa mpango wa biashara (Business plan) na kufahamu mbinu za kukuza mitaji na kuvutia wateja katika biashara husika.


Nae Mwalimu muwakilishi wa mradi wa elimu ya fedha, Jamila Kaniki, amesema mradi huo umewasaidia wasichana kujitambua na kuwa na uwezo wa kufikiri mambo ya maendeleo.


Alisema  elimu hiyo inamfanya msichana aweze kufikia malengo yake jambo ambalo kwenye mitaala ya kawaida halipo.


Aliongeza kwa kusema kuwa, inamfanya msichana kuwa na uwezo wa kujiamini hali iliyopelekea kupungua kwa mimba za utotoni.


Mwalimu Jamila, aliongeza kwa kusema kuwa, vijana wengi baada ya kumaliza masomo na kukosa nafasi za kazi huingia mitaani na kujiunga na makundi yanayokwenda kinyume na maadili lakini kwa msichana aliyepata elimu ya fedha chini ya mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read ni rahisi kwake kujiajiri na kuendesha maisha yake.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Bagamoyo, Teddy davis ambae ndie mjasiliamali aliyetembelewa na wanafunzi hao alisema wasichana wanapaswa kuwa na ndoto ya mafanikio na kwamba haifai kukata tamaa na kujiona kama hawawezi.


Teddy ambae alishinda tunzo ya Malkia wa nguvu 2018 kutoka Bagamoyo alisema yeye alithubutu akaweza hivyo anaamini kila mwanamke anaweza kufikia malengo yake.


Alisema wasichana wanapokosa alama za kuendelea kimasomo wasikate tamaa na badala yake watumie fursa ya kujifunza ujasiriamali ili waweze kutimiza ndoto zao za maisha.


Aliongeza kuwa, kufeli masomo sio kufeli maisha, hivyo mwanafunzi anaweza kufeli masomo lakini akafaulu maisha kupitia ujasiriamali.


Teddy alisema anafikiria kuomba fursa ya kufundisha elimu ya ujasiriamali katika shule mbalimbali ili kuwajengea uwezo wasichana waweze kujiamini na kuwa na elimu ya kuendesha maisha yao mara tu wanapomaliza masomo yao.


Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa wamefurahia ziara hiyo ya kimasomo na kusema kuwa wamejifunza vitu vingi kupitia mjasiriamali Teddy.


Aidha, wakizungumzia elimu ya fedha wanayopata kupitia mpango wa elimu kwa msichana kutoka shirika la Room to Read, wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa iliyopo wilayani Bagamoyo, wamesema wamenufaika sana na kwamba nao wanaweza kuiendeleza elimu hiyo kwa jamii.
  
Mwalimu muwakilishi wa mradi wa elimu ya fedha, Jamila Kaniki akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelea kiwanda cha mjasiriamali mwanamke wa Bagamoyo Teddy Davis.
 
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Matimbwa wakisikilza elimu ya ujasiriamali walipotembelea katika kiwanda cha mjasiriamali Teddy Davis mjini Bagamoyo.
    
Mkurugenzi wa kiwanda cha Smoke Hause StoreTeddy Davis Teddy Davis akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Matimbwa Bagamoyo ambao walifika kujifunza kiwandani hapo.


ULEGA AKABIDHI MIL. 2.5 KUKARABATI ZAHANATI.

Na Omary Mngindo, Mkuranga

MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani Alhaj Abdallah Ulega, amemkabidhi fundi atayekarabati zahanati ya Kijiji cha Mpafu, Kata ya Dondo Tarafa ya Kisiju kiasi cha sh. Mil 2,560,000 kufuatia kuezuliwa kwa paa lake.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Katibu wa mbunge huyo Zuwena Mtuliya alisema kuwa, hatua hiyo inalenga kuirejesha zahanati hiyo katika hali yake ya kawaida, kutokana na kuezuliwa paa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, iliyoambatana na upepo mkali. 


Akiambatana na diwani wa Kata hiyo Maulid Ubuguyu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata Nassoro Mgalu na Katibu wake Hassani Kiumbo, Mtuliya alimkabidhi fundi Omary Adui kiasi hicho kwa ajili ya ukarabati huo.


"Katika kuhakikisha huduma zinarejea katika hali yake ya kawaida, Mbunge wetu Abdallah Ulega amejitolea kumlipa fundi kiasi cha shilingi milioni 2,560,000 kwa ajili ya ukarabati huo, nimemkabidhi fundi atayefanya kazi hiyo Omary Adui" alisema Mtuliya.


Alisema kuwa kulikuwa na upungufu wa kiasi hicho cha pesa ambazo ni gharama za fundi zilizokwamisha ujenzi huo, ambapo kijiji kilinunua bati za kupaua jengo lote, halmashauri ya wilaya ilinunua mbao, saruji, gypsum, rangi pamoja na misumari.


"Ukarabati unaoendelea kufanyika kwenye zahanati ya Mpafu ni pamoja na kuvunja paa lote, kupandisha ukuta, kupaua, kuvunja sakafu ya awali na kuweka upya, kisha kumalizia kwa kupaka rangi," alisema Mtuliya.


Diwani Ubuguyu alianza kwa kuishukuru halmashauri, mbunge na wananchi kwa juhudi zao ambazo zinaonesha kupatikana kwa mwanga wa kurejesha huduma za matibabu katika zahanati hiyo.

DC KAWAWA AWATAKA. WAWEKEZAJI CHALINZE KULIPA KODI KWA MUJIBU WA SHERIA

Image may contain: 3 people, people sitting and indoor
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa amefanya warsha na wadau wa madini ujenzi, wa halmashauri ya Chalinze katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Lugoba na kuwataka kuzingatia sheria taratibu na kanuni za ulipaji ushuru na mapato mbalimbali ya halmashauri na kukemea utoaji rushwa ili kukwepa ulipaji mapato na shuru mbalimbali ambazo zimeainishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria ndogo za halmashauri.


Mkuu wa Wilaya katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyojumuisha wamiliki wa migodi ya madini ujenzi, kamati ya ulinzi na Usalama na wakuu wa idara wa halmashauri ya Chalinze aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuwa waadilifu kwa kuzingatia sheria ya kupambana na kuzuia rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na sheria zingine za nchi zinazohusu mapambano dhidi ya rushwa.


Naye Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo Bwana Raymond Katima alitoa mada ya mapambano dhidi ya rushwa kwa washiriki wa warsha na kuwataka kuzingatia sheria za nchi, pia aliweza kutoa taarifa fupi ya uchunguzi wa namna ya ukusanyaji mapato katika halmashauri ya Chalinze kwa upande wa madini ujenzi na kueleza kuwa mapato yanayotokana na madini kokoto hayakusanywi inavyotakiwa kwani kuna ukwepaji kwa namna moja au nyingine kwa wamiliki wa migodi.


Katima alieleza madhara ya rushwa kwa maendeleo ya nchi na kuwaagiza washiriki katika makampuni yao kuendelea kutoa Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa mara kwa mara kwani rushwa ni suala mtambuka ambalo linatakiwa kuzungumziwa kila wakati mahali pa kazi.


Kamanda wa TAKUKURU aliwasilisha changamoto za kiutendaji katika ukusanyaji wa Mapato na mapendekezo ya utatuzi wa changamoto hizo ili ukusanyaji wa Mapato ya serikali uweze kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kwa ufanisi zaidi.


Mapendekezo yaliyotolewa katika warsha hiyo ni pamoja na kuweka waangalizi watakaokuwa wanashuhudia namna kokoto zinavyotoka kutoka eneo la uzalishaji kwenda kwa watumiaji, waangalizi hao watakuwa kila sehemu patakapokuwa na uzalishaji wa kokoto ili kudhibiti upotevu wa mapato ya halmashauri. Sanjari na hilo washiriki katika warsha hiyo walikiagiza kitengo cha Tehama kuzikagua mara kwa mara mashine za kukusanyia mapato ili zisihujumiwe na kutumika vibaya na watu wasio waadilifu.

 
Mheshimiwa Kawawa alimalizia hotuba yake kwa kuwataka wamiliki wa makampuni kuwa wazalendo kwa kulipa kodi na shuru mbalimbali kwa wakati pasipo shuruti na kuendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa kutoa huduma bora kwa wananchi katika halmashauri ya Chalinze.

Monday, May 13, 2019

UNGANDO AKABIDHI KOMPYUTA ZA MIL. 9.2

Na Omary Mngindo, Kibiti


MBUNGE wa Jimbo la Kibiti Mkoa wa Pwani Ally Ungando ameikabidhi shule ya sekondari ya Zimbwini kompyuta 5 zenye thamani ya shilingi milioni 9.250,000.


Katibu wa mbunge huyo Rajabu Mtwiku ameyasema hayo katika kikao cha Wazazi wa wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo, iliyoko Kata ya Kibiti kilichojadili maendeleo ambapo wazazi na walezi walijitokeza kwa wingi kwa ajili ya uboreshaji wa elimu shuleni hapo.


Kikao hicho kilichohudhuliwa na diwani wa Kata hiyo Hamidu Ungando, mwishoni kulifanyika harambee iliyokusanya shilingi laki 418,000, hatua inayounga mkono serikali ya awamu ya tano iliyoipatia shule hiyo shilingi milioni 138 kwa ajili ya kuboresha vyumba vya madarasa. 


Mtwiku aliwaambia wazazi hao kwamba, mbunge wao Ungando ambaye alikabidhi kompyuta 5 za milioni 9,250,000, kaa sasa yupo katika majukumu ya bunge mjini Dodoma, na kwamba amewaahidi kuendelea kuungana na wanajimbo hilo katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. 


"Mbunge anawasalimia, amesema yupo pamoja nasi katika shughuli za kimaemdeleo, ikiwemo kugawa chakula na vitendea kazi wakati wa mitihani ya kidato cha nne 2019 katika shule zote 12 kama anavyo fanya toka aingie madarakani 2015," alisema Katibu huyo.


Kwa upande wake diwani Ungando alisema kuwa harambee hiyo ya upatikanaji wa fedha hizo kiasi cha shilingi 418,000 ni kuunga mkono jitihada za wazazi hao waliojenga vyumba viwili kwa nguvu zao, hivyo kutimia vyumba 8 vipya vinavyo endelea kujengwa. Katika mkutano huo diwani Hamidu ameunga mkono juhudi za wazazi hao kwa kuchangia rimu 10, zenye thamani ya shilingi 120,000 kwa ajili ya matumizi ya shule, huku akiahidi kuendelea kuchangia kila wakati ikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu stahiki. 


Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Said Mng'ombe amewataka wakazi wa Kibiti wabadilike na kutambua umuhimu wa elimu, huku akisema kwamba wapo nyuma katika sekta hiyo, hivyo waungane kuhakikisha shule infanya vizuri kitaaluma.