Tuesday, March 12, 2019

KILIMO CHA MUHOGO KUKOMBOA WAKULIMA BAGAMOYO

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa (kushoto) Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Saidi Ngatipula (katikati) na kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Dar Canton Investment Company Limited,John Vedasto Rwehumbiza.
 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Dar Canton Investment Company Limited,John Vedasto Rwehumbiza, akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani Halmashauri ya Bagamoyo.
.................................... 

 
Wakulima Wilayani Bagamoyo wamehimizwa kuongeza uzalishaji wa zao la Muhogo, kwani zao hilo kwa sasa, ni zao maalumu la kibiashara.





Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Ally Ally Issa katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.



Mwenyekiti Ally Ally Issa ambaye pia ni diwani wa Kata ya Fukayosi ameeleza kupitia mkutano huo wa baraza la madiwani kuwa, zao la Muhogo ndani ya Halmashauri ya Bagamoyo sasa ni zao la biashara na ukombozi kwa Wakulima wa Bagamoyo.



Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ameyasema hayo baada ya kuikaribisha kampuni ya Dar Canton Investment Limited ambayo ni kampuni ya Uwekezaji katika zao la muhogo inayotarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya Halmashauri ikijikita katika ununuzi na uchakataji wa muhogo.


“Waheshimiwa Madiwani wenzangu twende tukawahimize Wananchi kujikita katika uzalishaji wa zao la muhogo bora, Wataalamu mtusaidie kufika Vijijini kuwaelimisha Wananchi juu ya kutumia mbegu bora za muhogo na kulima kilimo kinachozingatia kanuni bora za kilimo.



Alisema kulima kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo kutapelekea wakulima wapate tija katika mazao yao, na kunufaika na ujio wa mwekezaji huyo aliye tayari kununua muhogo kwa Wananchi kuanzia sasa.



Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa kampuni ya Dar Canton Investment Limited, John Vedasto Rwehumbiza, alisema kampuni imepata eneo lililopo Kata ya Makurunge, katika Kitongoji cha Kifude ambapo imeshaanza kufanya upembuzi yakinifu ili kuanza ujenzi wa kiwanda cha uchakataji wa muhogo.



Alisema kwa sasa kampuni inaendelea kununua muhogo mkavu katika maeneo mbali mbali ndani ya Halmashauri na kiwanda kitakua na uwezo wa kununua tani 120 za muhogo kwa siku mara kitakapoanza uzalishaji wake, na kuongeza kuwa kwa sasa tayari wameanza ununuzi wa muhogo kwa wakulima mbalimbali ndani na nje ya Halmashauri hiyo.



Rwehumbiza, alisema wananchi wa wilaya ya Bagamoyo wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha muhogo kwani soko la uhakika lipo kupitia kampuni yao.


JAFO AKONGA NYOYO ZA WAFANYABIASHARA MLANDIZI ,WASEMA JPM HAKUKOSEA KUMTEUA

NA MWAMVUA MWINYI, MLANDIZI

MSAFARA wa Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo umezuiliwa na watumiaji wa Stendi ,wafanyabishara wa soko na wauza  mitumba (WARUMBA)  eneo la Mtongani Mlandizi  ,wilayani Kibaha kupinga kuhamia kwenye eneo jipya la Mama Salmini ambako wanadai hakuna maslahi kwao.


Kufuatia hali hiyo ametoa maelekezo kuwa kutokana na soko hilo kutokuwa mali ya serikali ni ya mtu binafsi kwa maslahi mapana ya wananchi soko la mama salmini wawe huru na wale wanaotegemea Mlandizi waendelee huku wakisubiri ukamilishaji wa soko jipya.


Kuhusu stendi ,Jafo amesema medereva daladala wanapata shida na stendi wawe na uhuru chini ya usimamizi wa wilaya waendelee kutumia stendi ya mlandizi hadi hapo stendi itakapokmilika.


Akizingumza na wafanyabiashara hao, alieleza wafanyabiashara hao waachiwe wafenye biashara kwa utaratibu na kufuata sheria bila kubughudhiwa. 
“Nimeangalia idadi ya watu na eneo hilo la mama Salmini wenye hiari ya kufanya biashara wafanye biashara kwenye eneo hilo,lakini na wanaotegemea biashara Mlandizi waendelee “alisisitiza Jafo.


“Mnajengewa soko la kisasa na serikali ipo kwenye mchakato wa kujengwa stendi mpya,hivyo taratibu nyingine zitafuata. “


Hata hivyo, Jafo alifafanua, Watu wadogo wasinyanyasike ofisi ya mkuu wa wilaya na halmashauri iangalie utaratibu wa kuwasogeza kwenye eneo lisilo hatarishi na wafanya biashara wafuate utaratibu, sheria na utaratibu hadi hapo soko maalum litakapokamilika.


“Wafanyabiashara toeni ushirikiano na serikali ya chama cha mapinduzi kwa maslahi ya wilaya na mkoa. “alisema Jafo.


Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa,aliwataka wawe watulivu na kutoa ushirikiano kwa serikali.


Jumaa alisema agizo la Jafo lipo sawa kwa maslahi ya wafanyabiashara hao wanyonge.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Warumba ,Nasoro Soma alisema kuwa wao hawako tayari kwenda kufanyabiashara kwenye soko jipya kutokana na mazingira yake hayako vizuri kibiashara .


Alisema Rais Dk John Magufuli hakukosea kumteua Jafo kwakuwa yupo makini kutekeleza kazi zake na kufuatilia mambo.

MAGAZETI YA LEO MACHI 12, 2019.

Monday, March 11, 2019

MAKAMU WA RAIS ANAONDOKA NCHINI LEO KUHUDHURIA MKUTANO WA AFRICA NOW SUMMIT 2019 UTAKAOFANYIKA KAMPALA – UGANDA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kuelekea Kampala, Uganda kushiriki kwenye Mkutano wa mwaka 2019 wa ‘Africa Now Summit’unaotarajiwa kufanyika tarehe12 na 13 Machi.Mhe. Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huu. Mkutano utakuwa na mada mbalimbali ikiwemo ya Uongozi unaohitajika kuchochea mabadiliko ya Kijamii na Uchumi Afrika, mada hii itatolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Viongozi wengine watakaotoa mada ni Rais wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA) Mhe. Abdel Fattah el Sisi; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Makamu wa Rais wa Kenya Mhe. William Ruto; na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Ahmed Abiy. Mada zote hizi zitajikita kwenye kuonesha chachu ya Uongozi katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika. 


Mkutano utamalizika tarehe 13 Machi 2019 utaanza na hotuba kutoka kwa Rais wa Somalia Mhe. Mohamed Abdullahi na baadae kufungwa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.


Makamu wa Rais ataambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.

MAGAZETI YA LEO MACI 11, 2019.

HAKUNA MTANZANIA ALIYEPOTEZA MAISHA KWENYE AJALI YA NDEGE ILIYOTOKEA ETHIOPIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa kuhusu ajali ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia, iliyotokea tarehe 10 Machi 2019 nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.


Ndege hiyo ya abiria, aina ya  Boeing 737 yenye namba za usajili ET 302 iliyokuwa inafanya safari zake za kawaida kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea mjini Nairobi, Kenya, ilikuwa imebeba abiria 149 kutoka mataifa mbalimbali na wafanyakazi wa kwenye ndege wapatao 8.


Kwa mujibu wa taarifa kuhusu ajali hiyo, iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia, ikiwemo orodha ya abiria na mataifa wanayotoka, hakuna Mtanzania aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.


Orodha ya nchi na idadi ya raia (kwenye mabano) waliokuwa kwenye ndege hiyo  ni kama ifuatavyo: Kenya (32), Canada (18), Ethiopia (9), China (8), Italia (8), Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7), Misri (6), Ujerumani (5), India (4), Slovakia (4), Austria (3), Urusi (3), Sweden (3), Hispania (2), Israel (2), Morocco (2) na Poland (2).


Nchi zingine ni Ubelgiji (1), Djibouti (1), Indonesia (1), Ireland (1), Msumbiji (1), Norway (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan (1), Somalia (1), Serbia (1), Togo (1), Uganda (1), Yemen (1), Nepal (1), Nigeria (1) na raia aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Umoja wa Mataifa (1).
Mamlaka husika zimeanza uchunguzi ili kujua  chanzo cha ajali hiyo.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na wote walioguswa na msiba huu mzito kutoa pole kwa mataifa yote yaliyopoteza raia wake kwenye ajali hiyo.