Wednesday, March 6, 2019

MWALIMU AHUKUMIWA KUNYONGWA BAADA YA KUKUTWA NA HATIA YA KUMPIGA MWANAFUNZI HADI KUFA.

 Mwalimu Respicius Mutazangira ambae amehukumiwa kunyongwa akiongozwa na polisi.
............................. 

Mahakama kuu kanda ya Bukoba imemuhuku kumnyonga hadi kufa Mwalimu Respicius Mutazangira baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga hadi kumuua Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Kibeta, Sperius Eradius mwishoni mwa mwaka 2008.


Aidha, mshtakiwa mwenzake Mwalimu Heriet Gerald ameachiwa huru.


Katika kesi hiyo walimu hao walishitakiwa kwa kosa la kumuadhibu kwa kipigo Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Kibeta, Sperius Eradius.

Hukumu hiyo imetolewa leo na jaji Lameck Ml
acha ambae alisikiliza kesi hiyo kwa muda wa mwezi mmoja.
  

TUKIO LILIVYOTOKEA KWA UFUPI.

Mwanafunzi huyo alipata adhabu ya kupigwa na kumsababishia kifo chake.



Mwanafunzi huyo inadaiwa alikwenda kumpokea mizigo mwalimu wake (Heriet Gerald) aliyefika shuleni hapo kwa usafiri wa bodaboda, lakini baada ya kuingia ofisini alianza kulalamika kutoiona pochi yake.


Kwa mujibu wa Wanafunzi wenzake, walidai mwanafunzi mwenzao (Sperius Eradius) aliitwa na kuanza kuhojiwa kuhusu kupotea kwa pochi hiyo na akakana kuichukua, hali iliyosababisha kuanza kupigwa akitakiwa kuirejesha.


Walisema kuwa baadaye walitakiwa kuitafuta pochi hiyo mpaka chooni, lakini hawakuiona huku mwanafunzi huyo akiendelea kuadhibiwa.


Hata hivyo, ilielezwa na wanafunzi hao kuwa wakati mwanafunzi mwenzao akiendelea kupigwa, dereva bodaboda alifika shuleni hapo akimtafuta mwalimu aliyepoteza pochi na kumkabidhi pochi aliyokuwa ameisahau kwenye pikipiki yake.


Mashuhuda hao walisema kuwa baada ya pochi hiyo kupatikana, mmoja wa walimu aliagiza mwanafunzi huyo apatiwe juisi na bagia, chakula ambacho hakuweza kukila kutokana na maumivu.
 
Mwalimu Heriet Gerald ambae ameachiwa huru na mahakama.


UWT PWANI WAUKARABATI MNARA WA BIBI TITI

Na Omary Mngindo, Rufiji

JUMUIA ya Wanawake Mkoa wa Pwani, mwishoni mwa wiki imetembelea na kuukarabati mnara wa kumbukumbu ya Mwanasiasa mkongwe hapa nchini Bibi Titi Mohamed.

Mnara huo wa kumbukumbu uliojengwa katika Kijiji cha Mkongo, Kata ya Mkongo Tarafa ya Mkongo jimbo la Rufiji mkoani hapa, unataraji kuboreshwa kisha kutangazwa kuwa utalii, ikiwa ni kumtangaza mwanasiasa huyo mkongwe, aliyepigania Uhuru wa nchi na Afrika Mashariki ambapo mnara wake umejengwa kijijini hapo.

Hayo yamebainika katika kuelekea siku ya Wanawake Duniani inayotaraji kufanyika Machi 8 mwaka huu, ambako Mkoa umekuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea mnara huo ukitanguliwa na zoezi la kutembelea vituo vya watoto waishio kwenye mazingira hatarishi pamoja na wagonjwa.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Ramadhani Maneno Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwapongeza wana-UWT hao kwa kuona umuhimu wa kutembelea mnara huo, wa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kupigania Uhuru, pia Naibu Waziri wa kwanza kutokea mkoani Pwani wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza.

"Nimeridhishwa na maamuzi yenu ya  kunipatia heshima ya kuwa mgeni rasmi, kwani mlikuwa na maamuzi ya kumteuwa mwengine yeyote kuja katika hafla hii, niwaombe mtafute jambo lingine litalotujumuisha kama hivi likiwa ni la ngazi ya Mkoa badala ya Kitaifa pekee," alisema Maneno.

Sherehe hiyo ambayo Maneno aliongozwa na Mwenyekiti wa Jumuia husika Farida Mgomi, pia imehudhuliwa na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, wakiwemo wabunge Mohamed Mchengerwa wa Rufiji na Ally Ungando wa Kibiti, pia kulikuwa na kongamano maalumu likijumuisha mada mbalimbali.

Mgomi alisema kuwa chanzo cha kuwepo kwa siku hiyo imetokana na wanawake waliokuwa wanafanyakazi viwandani kukosa muda wa kupumzika, kufungiwa ndani wakati mwingine kulikuwa na joto, pia ujira mdogo.

"Kutokana na hali hiyo ndipo wakaamua kuandamana wakidai haki yao, katika tukio hilo ikatumika nguvu hali iliyosababisha kuuawa kwa wanawake, nchini Marekani, nasi Pwani kwa makusudi kutoka katika nafsi zetu tuneamua kuja katika mnara wa Bibi Titi Mohamed ikiwa ni sehemu ha kuelekea maadhimisho hayo," alisema Mgomi.

Ramadhani Maneno Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani akitoa neno kwa wanaJumuia wa Wanawake mkoani hapa walipokuwa katika Mnara wa Bibi Titi Mohamed uliopo Kijiji cha Mkongo wilayani Rufiji. Picha zote na Omary Mngindo.

LUGOLA KUANZA ZIARA MKOANI MOROGORO KESHO, KUFUATILIA MAAGIZO YAKE, KUZUNGUMZA NA WANANCHI WILAYA ZOTE MKOANI HUMO

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili mjini Morogoro leo, kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kikazi kwa kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo, akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.


Waziri Lugola anatarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Machi 7, 2019 mjini Morogoro kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kupokea taarifa ya Kamati hiyo, pia atakutana na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa na Wilaya, na baadaye atazungumza na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Wizara yake, na baada ya hapo atafanya kikao na Baraza la Askari na Watumishi raia wote wa Wizara hiyo waliopo mjini humo.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, leo, Lugola amesema atafanya mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi utakaofanyika mjini humo ili aweze kusikiliza na kuzitatua kero mbalimbali zitakazosemwa na wananchi katika mkutano huo.


“Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Wilaya zake, wahakikishe wanakuja kwa wingi katika mikutano yangu kuanzia mkoani hapa na Wilaya zote nitakazozitembelea, ili tuweze kubadilishana mawazo, kusikiliza  kero zao na pia kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, wananchi nileteeni kero zenu ili tuzitatue na tuijenge nchi yetu,” alisema Lugola.


Lugola aliongeza kuwa, mkutano huo utafanyika saa 10:00 hadi 12:00 jioni utaanza mjini humo na pia atatoa muda wa wananchi kujitokeza mbele kuja kuuliza maswali na yeye aweze kuyajibu.


Waziri Lugola ambaye alisema atafanya mikutano katika Wilaya zote atakazozitembelea pamoja na kufuatilia maagizo yake mbalimbali ambayo aliyatoa mwaka jana 2018 katika mikutano yake, kama yalifanyiwa kazi na viongozi wa Taasisi anazoziongoza au yalipuuzwa.


Maagizo hayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote nchini zilizopo vituoni ziondolewe ambazo hazina kesi mahakamani.


Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma, na mwaka huu Mkoa wa Kagera na Arusha, aligundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kukaa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo baadhi yao wakiwalalamikia Polisi wakiwaonea.


 “Wananchi wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Dokta Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola.


Lugola alisema Taasisi zilizopo ndani ya Wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii, wajipange ili waweze kumpa taarifa za utendaji kazi wao kuanzia ofisi za Mkoa hadi Wilaya zilizopo mkoani humo.

TAWA YASITISHA KIBALI CHA KUWINDA KAMPUNI YA GREEN MILES SAFARIS

Mwandishi wetu,Arusha

Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori nchini(TAWA),imejipanga kuendelea kuboresha sekta ya uwindaji wa kitalii na imesitisha kibali cha uwindaji wa kitalii cha kampuni ya Green Miles Safaris Ltd, kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya umiliki wa vitalu vya uwindaji.

Naibu Kamishna wa Utalii na Biashara wa TAWA, Imani Nkuwi alisema kampuni hiyo, imeshindwa kulipa ada za kutotumia zaidi ya asilimia 40 ya mgao wa kuwinda katika vitalu.

“kampuni hii tumeinyia huduma za kuwinda katika vitalu vyake vyote wakati suala lao likifanyiwa kazi”alisema.

Kampuni hiyo, inamiliki vitalu wilayani Longido na katika pori la akiba la Selous na katika siku za karibuni, imekuwa na migogoro na vijiji ilipowekeza wilayani Longido.

Hata hivyo, Nkuwi alisema bado wamiliki wengi wa vitalu wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na serikali, ikiwepo kutunza vitalu vyao, kuzuia matukio ya ujangili na kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ametoa agizo , kukamatwa mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Green Miles Salim Abdalah Awadhi, kutokana na kushindwa kulipa deni hilo la vijiji na halmashauri ya Longido mkoa wa Arusha.

Mwaisumbe alisema vijiji 23 vya wilaya hiyo, vinaidai kampuni hiyo, kiasi cha sh 329 milioni kutokana na makubaliano walioingia tangu mwaka 2017/18 na jitihada za malipo zimekwama kwa njia ya mazungumzo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido, Wakili Jumaa Mhina, alisema ofisini yake imekuwa ikiitaka kampuni hiyo kuwa na mahusiano na vijiji na kulipa fedha za vijiji na halmashauri bila ya mafanikio.

Hata hivyo,Mkurugenzi wa Green Miles Safari Ltd, Salim Abdalah Awadhi ambaye yupo nje ya nchi , amekuwa akikanusha tuhuma mbali mbali dhidi ya kampuni yake,ikiwepo kudaiwa na vijiji fedha .