Wednesday, March 6, 2019

MTUMISHI WA SERIKALI APIMIWA VIWANJA BARABARANI BAGAMOYO.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Bagamoyo limetoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kumaliza mgogoro wa ardhi kata ya Kisutu pamoja na kutafuta eneo la kujenga shule kitongoji cha Sanzale kata ya Magomeni.


Maagizo hayo yametolewa jana Machi 05, 2019 katika kikao cha robo ya pili ambapo madiwani waliwasilisha taarifa za utekelezaji za kata zao.


Diwani wa kata ya Kisutu, Aweso Mwidini amesema kuna mgogoro wa muda mrefu kwenye kata yake ambapo idara ya ardhi imepima viwanja kwenye eneo la barabara na kusababisha mgogoro baina ya wananchi wengine na mmiliki wa viwanja hivyo.


Alisema amefanya juhudi za kukutana na mmiliki wa viwanja hivyo ambapo mmiliki huyo wa viwanja ambae ni mtumishi wa Serikali aliyekuwa Bagamoyo na sasa amehamishiwa Halmashauri ya Mkuranga, alisema aliuziwa mpaka eneo la barabara na kwamba hawezi kuachia barabara kwakuwa ni mali yake.


Diwani huyo alisema alifanya juhudi ya kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo ambapo Mkurugenzi alifika eneo la tukio lakini majibu ya kuridhisha hayajapatikana.


Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo kushughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo.


 Alisema barabara hiyo ndiyo inayotumika kufika shule ya Sekondari kingani pamoja na wananchi wengine wakazi eneo hilo hivyo Mkurugenzi atafute namna ya kutatua mgogoro huo ili barabara ibaki kama kawaida.


Katika hatua nyingine Diwani wa kata ya  Magomeni Mwanaharusi Jarufu, amesema kitongoji cha Sanzale kilichopo kata ya Magomeni kinakabiliwa na ukosefu wa shule ya msingi hali inayopelekea watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.


Aidha, ametaka hatua za makusudi zichukuliwe ili wananchi wa eneo la sanzale wapatiwe eneo la kujenga shule.


Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Ally Ally Issa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kutafuta eneo katika kitongoji cha Sanzale kwaajili ya ujenzi wa shule.


Mwenyekiti huyo alisema yapo maeneo makubwa katika kitongoji hicho ambayo mpaka sasa hayajaendelezwa hivyo ofisi ya Mkurugenzi ifanye haraka kupitia maeneo hayo na kujua wamiliki wake ili yule ambae hawezi kuendeleza eneo hilo lichukuliwe kwa maslahi ya wananchi.
 Diwani wa kata ya  Magomeni Mwanaharusi Jarufu, akiwasilisha taarifa za kata.

CHALINZE WAKABIDHI PIKIPIKI 15 ZA MIL. 37.5

Said Zikatimu akimkabidhi pikipiki Hashimu Ally Matonga ofisa Kata ya Kibindu baada ya halmashauri hiyo kununua pikipiki 15 zenye thamani ya sh. Mil. 37.5.

.................................

Na Omary Mngindo, Chalinze.

HALMASHAURI ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Jumanne ya Machi 5 imewakabidhi Maofisa Ugani wa Kata 15 kila mmoja pikipiki moja, zikiwa na thamani ya sh. Mil. 37.5.

Hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya halmashauri hiyo chini ya Mwenyekiti Said Zikatimu, Ofisa Kilmo Jovin Bararata aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi, alisema kuwa pikipiki hizo zinalenga kuboresha kilimo kwa wananchi.

Alisema kuwa shughuli za ugani zina changamoto nyingi lakini kubwa zaidi ni jinsi ya kuwafikia wakulima, na kwamba katika mwaka was 2018/2019 halmashauri ilitenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki hizo 15, na kwamba kwa mwaka wa 2019/2020 wanataraji knunua pikipiki nyingine 10.

"Kupitia mapato yetu ya ndani tumefanikiwa kununia pikipiki 15 zilizogjarimu kiasi cha sh. Milioni 37.5 lengo ni kuwapatia fursa watumishi hao kuwafikia kwa urahisi wakulima wetu katika kuleta tija kwenye sekta hiyo," alisema Bararata.

Kwa upande wake Zikatimu alisema kwamba hatua hiyo imetokana na baraza la Madiwani katika vikao vyake kutenga bajeti ya kununua pikipiki hizo, zinazolenga kuboresha kilimo, huku akiwataka wakazitumie kwa madhumuni yaliyolenga.

"Pikipiki hizi zimenunuliwa kwa mapato yetu ya ndani, chanzo kikubwa cha halmashauri ni kokoto, zikatumike pia katika kuendeleza zao pamba, korosho na ikiwa no mikakati ya kuongeza maoato sanjali kusaidia wananchi wetu katika sekta hiyo," alisema Zikatimu.

Mmoja wa ofisa ugani aliyezungumza kwa niaba ya wenzake, Joseph Kangambili alianza kwa kuishukuru halmashauri hiyo kwa kutenga fedha kisha kununua pikipiki hizo, zinazolenga kuboresha sekta hiyo.

MAGAZETI YA LEO MACHI 06, 2019.

Tuesday, March 5, 2019

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YAELEZA MVUA ZA MASIKA ZITAKAVYOKUWA


MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa utabiri wa mvua za masika ambazo tayari zimeanza kwa baadhi ya mikoa na zitaendelea kunyesha hadi mwaka huu. 
Taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyoitolewa leo jijini Dar es Salaam imesema utabiri wa mvua za masika (MAM) 2019 ni kwamba kuanzia wiki ya nne ya Februari katika mikoa ya Kagera mvua itanyesha na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga,Simiyu,Kigoma Kaskazini na Mara wiki ya pili ya Machi 2019. 
Mvua hizo kwa baadhi ya meeneo zitakuwa juu ya wastani hadi wastani na kwamba mvua za msimu 2018,2019 zinaendelea hadi Aprili mwaka huu.Kwa mujibu wa TMA ni kwamba mvua zitaisha wiki ya kwanza ya Mei mwaka huu. 
Pia kuanzia kati ya wiki ya nne ya Februari na wiki ya kwanza ya Machi 2019 mvua itanyesha katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ,Visiwa vya Unguja na Pemba na kusambaa maeneo ya mikoa ya Tanga na Morogoro Kaskazini ifikapo wiki ya kwanza ya Machi 2019 na itaisha wiki ya nne ya Aprili 2019.

KAMATI ZA BUNGE KUANZA JUMATATU JIJINI DODOMA

Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Jumatatu tarehe 11 hadi 31 Machi, 2019 Mjini Dodoma kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 02 Aprili, 2019.  Kwa mujibu wa Ratiba ya Shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wote wanapaswa kuwasili Mjini Dodoma Jumapili tarehe 10 Machi, 2019 tayari kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya Kamati. 


Shughuli zitakazotekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:


1.  KUPOKEA WASILISHO LA SERIKALI KUHUSU KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI.


Katika kipindi hicho cha vikao vya Kamati za Bunge, siku ya tarehe 12 Machi 2019, Wabunge watapokea Wasilisho la Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.


1.  KUFANYA ZIARA ZA UKAGUZI WA MIRADI
Kamati zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi ya Maendeleo iliyotengewa fedha katika Bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016. 


Kamati zitakagua miradi ya uwekezaji liyotekelezwa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma.  Aidha, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi mingine iliyotekelezwa na Serikali ili kulinganisha matokeo ya utekelezaji na thamani halisi ya fedha za Umma zilizotumika katika miradi hiyo.


1.  KUFANYA UCHAMBUZI WA BAJETI
Katika vikao hivyo pia Kamati zitafanya uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti za Wizara inazozisimamia kwa Mwaka wa Fedha unaoishia 2018/2019 kwa ajili ya kufanya ulinganisho kuhusu makadirio ya matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.


1.  KUFANYA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI


Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.


1.  UCHAMBUZI WA SHERIA NDOGO


Kamati ya Sheria Ndogo itafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Nne Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016


Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo Kamati hizo zitafanya ziara zinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz. mara baada ya Kamati hizo kuanza kazi.


Imetolewa na:     Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa.

  Ofisi ya Bunge
DODOMA
05 Machi, 2019