Friday, March 1, 2019

MWILI WA RUGE WAWASILI DAR ES SALAAM.

Mwili wa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group, Ndugu Ruge Mutahaba umewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukitokea Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Aliyeongoza mapokezi ya Mwili wa Ruge Mutahaba ni Waziri January Makamba akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es aalaam Paul Makonda pamoja na Mkurugenzi wa Clouds Media Group Bw. Joseph Kusaga.

LOWASA AREJEA CCM RASMI

Image may contain: 9 people, people smiling, people standing
Waziri Mkuu mstaafu Edwardi Lowasa leo tarehe 1 Machi amerejea CCM rasmi na kupkelewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Dkt. John Magufuli katika ofisi ndog za chama hicho zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.


Akizungumza wakati wa kumpokea Dkt. Magufuli alisema CCM imepokea mawazo ya Lowasa ya kurejea CCM kwakuwa ndio nyumbani.


Alisema Lowasa ni mkongwe kwenye CCM na anajua mambo na kwamba alijamia CHADEMA kutokana na mambo ambayo hayakuweza kuzuilika.


Katika hafla hiyo fupi ya kumpkea Lowasa ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. John Magufuli, Makamo Mwenyekiti CCM Mzee Philipo Mangula, Katibu Mkuu Dkt. Bashiru Ally Katibu Mwenezi na uenezi Hamphrey Polepole na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa.

Vodacom, TPB kuwawezesha wanachama wa Vicoba kutunza fedha kidijitali


  • Wamezindua huduma ya  mtandaoni ya M-Koba iliyounganishwa na M-Pesa inayotoa fursa ya kuhifadhi fedha kwa usalama na uwazi.
  • Inatarajia kuondoa changamoto za upotevu wa fedha na kuimarisha mitaji ya vikundi hivyo.
Dar es Salaam. Wanachama wa vikundi vya kifedha vya kijamii (Vicoba), vikundi rasmi na visivyo rasmi maarufu kama ‘upatu’ sasa wamepata suluhu ya kuhifadhi fedha zao baada ya kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom kwa kushirikiana na benki ya Posta Tanzania (TPB) kuzindua huduma ya mtandaoni inalotoa suluhisho la utunzaji fedha kidijitali.
Huduma hiyo, iliyopewa jina la M-Koba, iko chini mfumo wa huduma za kifedha kwa njia ya simu wa M-Pesa, itawezesha vikundi hivyo kutunza fedha kidijitali kwa usalama na uwazi zaidi.
Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi huo leo (Februari 28, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema huduma hiyo itakuwa endelevu na kukidhi mahitaji ya vikundi vya kifedha kupata eneo salama la kutunza fedha na kuimarisha mitaji yao.
"Huduma hii ya kidijitali inalenga kutoa huduma endelevu ambayo itatumiwa na kufikia vikundi vilivyopo maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya mtandao mkubwa wa Vodacom, "amesema Hendi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vodacom, inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya watanzania (zaidi ya watu milioni 4.4) wengi wao wakiwa wanawake, ni wanachama wa vikundi zaidi ya 50,000 vya kuweka akiba na mikopo (Vicoba) ambao huhifadhi akiba zaidi ya Sh100 bilioni kwa mwaka.
Pia kuna vikundi visivyo rasmi zaidi ya 50,000 visivyo rasmi vya wahitimu wa vyuo, wafanyakazi na wanafamilia ambao wanatumia mitandao ya kijamii kuweka akiba na kukopa.  
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi wa kwanza kulia akishirikiana na viongozi wengine kuonesha jarida la M-Koba wakati wa hafla ya kuzindua huduma ya M-Koba, huduma ya kwanza na ya kipekee nchini kwa ajili ya vikundi vya kuweka akiba nchini Tanzania.Picha|Vodacom.
Afisa Mtendaji mkuu wa TPB,  Sabasaba Moshingi amesema huduma hiyo inalenga kuongeza theluthi moja ya idadi ya watu waliosajiliwa katika mifumo rasmi ya kifedha na zaidi kuwafikia wanawake wa vijijini ambao wanajihusisha na shughuli hizo. 
“Kama taasisi ya kifedha, tunatambua umuhimu wa vikundi hivi na ndiyo sababu tumeshirikiana na vinara hawa wa sekta ya simu kuleta suluhisho hili la kidijitali ambalo litarahisisha kutunza akiba na kuwezesha watu kufikia malengo yao," amesema Moshingi


Naye Mwenyekiti wa mojawapo wa Vicoba aliyehudhuria uzinduzi huo, Abdallah Mkenga amesema huduma hiyo limekuja wakati mwafaka kwa sababu itawasaidia kutatua changamoto za utunzaji fedha. 
“Sasa tuna mfumo salama zaidi wa vikundi vyetu na tunachanga kwa uwazi kwani mfumo huu unaruhusu kuonekana kwa shughuli za kikundi," amesema Mkenga.
Kutokana na umuhimu wake katika jamii, Vicoba vimejumuishwa katika Sheria mpya ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 ambapo sheria hiyo imeweka utaratibu wa kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma ndogo za fedha hususan vikundi vya kijamii kwa lengo la kunufaika na fursa zilizopo.
Vicoba,wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii vinaingia katika daraja la nne la sheria hiyo ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati wa kupitisha sheria hiyo bungeni mwaka jana alisema vikundi hivyo viitaandaliwa kanuni na miongozo mahsusi kwa ajili ya kusimamia daraja hilo.

IGP SIRRO APANGUA PANGUA MAKAMANDA WA POLISI...RPC SHINYANGA ASUKUMWA MAKAO




Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amefanya mabadiliko ya kiuongozi kwa maofisa wa jeshi hilo baada ya Rais John Magufuli kufanya uteuzi wa makamishna wapya.


Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi Mosi, IGP Sirro amewataja makamishna walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa ni Charles Mkumbo ambaye anakwenda kuongoza kamisheni ya intelijensia na Liberatus Sabas ambaye anakuwa mkuu wa operesheni na mafunzo.
Wengine ni Leonard Lwabuzala ambaye ataongoza kamisheni ya fedha na logistics na Benedicto Wakulyamba ambaye anakuwa mkuu wa kamisheni ya utawala na menejimenti ya utumishi na Shaaban Mlai ambaye ataongoza kamisheni ya maabara ya uchunguzi wa kisayansi.
Mbali na makamishna hao, Sirro amefanya mabadiliko ya kiutawala kwa maofisa wa jeshi hilo; James Mushi ambaye alikuwa kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma anakuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi (CCP) Moshi wakati RPC wa Njombe, Renata Mzinga akirudishwa Makao Makuu.
Sirro amewataja makamanda wapya wa mikoa kuwa ni Amon Kakwale (RPC wa Temeke), Jonathan Shana (RPC Arusha), Marwa Mahiga (RPC Ruvuma), Salum Hamduni (RPC Njombe) na Zuberi Chembela (RPC Ilala).
Viongozi wengine waliohamishwa vituo vya kazi ni Mihayo Nsekela (ofisi ya operesheni na mafunzo), Simon Haule ambaye alikuwa RPC wa Shinyanga anarudishwa Makao Makuu na Yusuph Sarungi ambaye alikuwa RPC Songwe anakuwa mkuu wa kitengo cha kushughulikia wizi wa mifugo (SPU).
Benedict Mapugila ameteuliwa kuongoza kikosi cha bandari wakati Michael Marwa anapelekwa makao makuu Zanzibar. Sirro amesema Albert Nyamhanga na Nsato Marijani wanakwenda Idara ya Wakimbizi ambayo iko chini ya Idara ya Uhamiaji.

MIPANGO YA SERIKALI KUHUSU GESI YA KUSINI IKO PALEPALE – MGALU

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27, 2019.

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye akizungumza, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba cha njano – meza kuu) kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, Februari 27, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme kijijini hapo.
...................................


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watanzania kuondoa shaka kuhusu mipango ya serikali kufuatia gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini, kwani haijabadilika na inaendelea kutekelezwa.


Aliyasema hayo jana Februari 27, 2019 kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Lindi ambapo alikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme katika vijiji mbalimbali na kuzungumza na wananchi.


“Nataka niwaaminishe wana-kusini, yale ambayo serikali iliahidi baada ya kugundua gesi, mipango yake iko palepale na inafanyiwa kazi,” alisema.


Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Mgalu alisema moja ya mambo ambayo serikali iliahidi ni umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji.


Alisema hadi sasa, taratibu za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi Mtwara wenye megawati 300 na Somanga Fungu wenye megawati 330 ziko katika hatua za mwisho.


“Mradi utaanza ndani ya mwaka huu wa fedha ambao utawezesha mikoa hii kuzalisha umeme wa kutosha kuweza kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.”


Aidha, aliongeza kuwa, jambo jingine kubwa ni kuviwezesha viwanda vya maeneo husika kupata umeme wa gesi ambapo alisema tayari kiwanda cha saruji cha Dangote kimeshaunganishiwa.


Pia, alisema, serikali inaendelea kuzungumza na viwanda vya mbolea ili vizalishe mbolea inayotokana na gesi ili pamoja na mambo mengine viongeze ajira kwa wananchi.


Vilevile, alisema kwa Mkoa wa Lindi, eneo la Likongo, serikali inatarajia kujenga kiwanda cha kusindika gesi iwe katika hali ya kimiminika ambapo Rais John Magufuli ametoa mwongozo wa kufanya mazungumzo na mbia mmoja mmoja. Alisema mazungumzo yanaendelea vizuri.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alizungumzia tathmini ya ziara yake mkoani Lindi, ambapo alisema imekuwa yenye mafanikio.


Alisema, kazi ya kuwaunganishia wananchi umeme vijijini inaendelea na ametoa wito kwa mkandarasi husika kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha anafikia malengo ya kukamilisha kazi yote kwa mujibu wa mkataba ifikapo Juni 30, mwaka huu ambapo ndipo mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza utakuwa unahitimishwa.


Naibu Waziri alisema yeyé pamoja na viongozi wengine wa Lindi akiwemo Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge wamekubaliana kumsimamia mkandarasi husika katika kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, ambaye alifuatana na Waziri wakati akihitimisha ziara yake, aliwahakikishia wananchi wa eneo husika kuwa yeyé pamoja na viongozi wenzake watamsimamia mkandarasi husika ili kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ufanisi.


“Tumekabidhiwa hawa tuwasimamie, kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwathibitishia kwamba tutawasimamia kwelikweli ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika vizuri sana,” alisisitiza.


Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wa nishati ambapo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri sana.


“Tunawashukuru sana Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama kuna Wizara inafanya vizuri, basi Wizara hii inafanya vizuri.”


Hata hivyo, Nnape alisema anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kuwasihi kuwa wastahimilivu maana zoezi la kuunganisha umeme ni hatua kwa hatua, awamu kwa awamu. Alisema anayo imani kubwa kwamba vijiji vyote vitafikiwa na huduma hiyo kabla ya mradi kuisha.


Mkurugenzi wa kampuni ya State Grid, ambayo ndiyo inatekeleza uunganishaji wa umeme mkoani Lindi, Charles Mlawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.


Katika ziara hiyo, viongozi wa ngazi mbalimbali walipongeza utendaji kazi wa Wizara pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuomba jitihada zinazofanyika ziendelee.


Katika Miradi ya Umeme Vijijini, Mzunguko wa Kwanza (REA III – 1), jumla ya vijiji takribani 133 vitaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 31.9. Matarajio ni kuwaunganishia wananchi takribani 5,337.


Akiwa Lindi vijijini, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Ntauna, Mvuleni na Tulieni.