Saturday, February 23, 2019

WAZIRI MBARAWA AAGIZA TAASISI ZA SERIKALI ZIFUNGIWE MITA ZA LUKU

 WAZIRI wa Maji Proffesa Makame Mbarawa
akizungumza baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake leo.
...........................

WAZIRI wa Maji Proffesa Makame Mbarawa ameagiza taasisi zote za serikali zifungiwe mita za luku ili ziweze kwenda na matumizi mazuri ya maji ili kupunguza changamoto za kutokulipa kwa wakati bili za majina kujikuta zikiingia kwenye madeni makubwa.


Proffesa Mbarawa aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake mkoani Tanga ambapo alisema mita za luku litasaidia kuweza kuondokana na kasumba za
watu kumwaga maji hivyo na hivyo kuweza kusimamia matumizi ya maji kwenye maeneo yao.



“Ndugu zangu mita za luku msiwapelee wateja sugu bali wapelekeeni hata wale watu wengine ambao wapo kwenye maeneo mbalimbali lakini pia Jeshi la Polisi sio wabaya wanalipa bili lakini wawekeeni mita za luko isipokuwa ndani ya kituo cha Polisi msiweke”Alisema Waziri Mbarawa.


“Lakini hatupelekei wateja sugu tunakosea kwa sababu hii inaweza kupelekwa kukote kwa sababu inaweza kusimamia matumizi ya maji ndani
ya mwezi husika…..nirudir Jeshi la Polisi sio wabaya wanalipa bili zao lakini wawekeni mita sio mwanzo maeneo mengi Mtwara,,Iringa nao
wanatumia kwenye kota zao wawekeeni mita hizo ”Alisema Waziri Mbarawa.



Aidha pia mita hizo la luku zitaweza kusaidia kuweka matumizi mazuri ya maji na mambo ya kuanza kulalamika hawalipi tuwafungie traasisi zio
nyingi mita moja laki mbili ukchukua wateja 20 karibuni milioni nne na mapato yatakayopatikana ni makubwa.



Hata hivyo alsema serikali imejipanga kuhakikisha changamoto ya huduma ya maji hapa nchini inatatuliwa ili wananweza waweze kunufaika na
huduma hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo.
 

Katika ziara hiyo Waziri Mbarawa alitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo
kwenye chanzo cha Maji cha Mabayani,Mtambo wa kusafirishia maji eneo la Mowe na eneo la Horohoro wilayani Mkinga.
WAZIRI wa Maji Proffesa Makame Mbarawa kushoto akimsikiliza kwa Katibu Tawala wa
Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Saidi wakati akielezea hali ya upatikanaji wa maji kwa mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake.

WAZIRI wa Maji Proffesa Makame Mbarawa
kulia akisaini kitabu cha wageni wakati alipofika Ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) kushoto ni
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Mhandisi Geofrey Hilly


WAZIRI MKUU ATOA SIKU 16 KWA MKURUGENZI ROMBO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John awe amepeleka asilimia 20 sawa na sh milioni 114 ya kijiji cha Holili kabla ya Machi 10 mwaka huu, fedha hizo zinatokana na mauzo ya madini ya pozolana.


Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 23, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili pamoja na wananchi wa kijiji cha Holili, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro. 

Kituo hicho kipo katika mpaka wa Tanzania na Kenya.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Holili kuwasilisha malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili Halmashauri hiyo iweze kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo ya madini hayo yanayochimbwa kijijini kwao.


 “Mkuu wa wilaya (Agness Hokororo) simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dkt. Anna Mgwira) nataka nipate taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi kutenga muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.


Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema hali ulinzi na usalama katika mpaka huo si nzuri, Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo, hivyo ni muhimu kwa wananchi washirikiane katika kuulinda mpaka huo.


Hivyo, Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaokamatwa wakipita au kuingiza mizigo kupitia njia zisizo rasmi kwa sababu hao ndio wanaopitisha silaha.


Waziri Mkuu amesema wananchi wa Tanzania na Kenya hawajazuiwa kufanya biashara upande wowote bali wanatakiwa wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika nchi husika ikiwa ni pamoja na kutumia njia rasmi.


Amewataka viongozi na watendaji waliopo maeneo ya mipaka huo wa Holili wawe makini kwa sababu mpaka huo hauko salama na kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yapo kinyume cha sheria.

DKT. MWANJELWA AMUONYA AFISA UTUMISHI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA KWA KUMTOLEA LUGHA CHAFU MSTAAFU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la  kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hizo mkoani Pwani.
............................


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amempa onyo kali Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Ruth Mwelo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu  wa Halmashauri hiyo kwa kumtolea lugha chafu mstaafu aliyekuwa akidai haki yake na kumtaka afisa huyo ajirekebishe haraka iwezekanavyo.


Onyo hilo amelitoa wilayani Kibaha, wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika wilaya hizo ili kujiridhisha na utekelezaji wake.


Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, haiwezekani afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu za kiutumishi ndio awe kikwazo cha utendaji kazi katika Halmashauri hiyo kwa kutoa lugha chafu dhidi ya wanaofuta huduma ofisini kwake, na kuongeza kuwa, afisa huyo ndiye anayestahili kuwa kwenye Kamati ya Maadili ili kutoa miongozo ya uadilifu na kusimamia maadili ya watumishi kwa ujumla katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

 
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka afisa huyo kutotumia cheo chake vibaya na badala yake asimamie vema nidhamu na masilahi ya watumishi wa umma.


Sanjari na hilo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka afisa huyo kuacha tabia ya kutoa siri za ofisi na kutokuwa mchonganishi miongoni mwa watumishi wenzie kwani matendo hayo hayapaswi kufanywa na mtumishi yeyote nchini.


Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema ameamua kuweka bayana  mapungufu ya afisa huyo mbele ya watumishi wenzie ili ajifunze kutokana na matendo yake yasiyoridhisha na aweze kubadili mwenendo wake mbaya wa kimaadili.


Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameendelea kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini, kwa kutoa onyo kwa watumishi wote wanaobainika  kukiuka Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi. Theresia Mbando akitoa neno la utangulizi kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao  chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hizo mkoani Pwani.
Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha  wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi cha watumishi hao na Naibu Waziri huyo chenye  lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hizo mkoani Pwani.