Friday, January 25, 2019

MAGEREZA KUMI(10) YA KIMKAKATI KUZALISHA CHAKULA CHA WAFUNGWA, LIKIWEMO GEREZA SONGWE

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akiangalia zao la mahindi ambalo linakaribia kukauka katika eneo la mradi wa Kilimo cha umwagiliaji cha Gereza Songwe.
 

 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akisalimiana na Mkuu wa Gereza Songwe, SSP. Peter Anatory alipowasili katika Gereza la Kilimo Songwe leo Januari 25, 2019 kwa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Jeshi hilo pamoja na kukagua mashamba ya kimkakati katika kuelekea kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.

..................................

Na ASP Lucas Mboje, Mbeya

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Jeshi la Magereza limeanza utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa kuelekea kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani katika magereza kumi (10) ya kimkakati likiwemo Gereza Songwe, lililopo Mkoani Mbeya ambalo limelima hekari 750 za zao la mahindi.

Akizungumza na wanahabari leo mara baada ya kukagua mashamba ya mahindi katika Gereza la Kilimo Songwe, Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike amesema kuwa lengo la ziara yake ni kujionea hali halisi ya ufanikishaji wa jukumu walilopewa na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanazalisha chakula kwa wingi cha wafungwa waliopo magerezani.

Amesema kuwa Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imeingizwa katika utekelezaji wa mpango huo wa uzalishaji chakula cha wafungwa ambapo kila Gereza la kimkakati limepangiwa malengo ya kulima mazao mbalimbali ya chakula cha wafungwa ikiwemo mahindi, maharage na mpunga.

“Mpango huu ni lazima tuufanikishe, hivyo tayari tumekwishajipanga na nguvu kazi ya wafungwa inatumika ipasavyo katika kufanya kazi katika magereza hayo kama mlivyojionea leo hapa Gereza Songwe, pia tunajitahidi kusimamia rasilimali nyinginezo tulizonazo katika maeneo yetu ya magereza ili tuweze kutekeleza ipasavyo maelekezo ya Serikali”. Alisisitiza Jenerali Kasike.

Aidha, Jenerali Kasike ameongeza kuwa kwa sasa Jeshi hilo linakusanya rasilimali zilizopo na kutoa kipaumbele katika magereza yakimkakati, ambapo katika kukidhi mahitaji ya nguvu kazi ya wafungwa, tayari wafungwa kutoka sehemu mbalimbali nchini wamehamishiwa katika magereza yenye mkakakati ili kuongeza nguvu kazi yakutosha katika maeneo hayo yenye uzalishaji.

Akisoma taarifa ya Magereza Mkoa kwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Mkuu wa Magereza Mkoani Mbeya, SACP. Luhende Makwaia amesema kuwa Mkoa huo una jumla ya magereza matano ambayo yanatekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya kilimo, likiwemo Gereza Songwe.

Kuhusu msongamano wa wahalifu, SACP. Luhende Makwaia amesema kuwa magereza yote ya mkoa wa mbeya yanakabiliwa na tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kutokana na ongezeko la uhalifu unaotokana na kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na kukosekana kwa gereza moja la wilaya katika mkoa huo.

Mkoa wa Mbeya una jumla ya wilaya sita(6) ambazo ni Mbeya mjini, Mbeya Vijijini, Chunya, Rungwe, Mbarali, na Kyela. Katika wilaya hizo ni wilaya tano(5) tu zina magereza, wilaya moja(1) ya chunya hakuna gereza hali inayochangia uwepo wa msongamano wa wahalifu katika mkoa. Aidha, katika magereza matano yaliyopo hupokea na kuhifadhi wafungwa na mahabusu katika mkoa huo.
Muonekano wa mashamba ya mahindi katika Gereza la Kilimo yakiwa yamestawi kama inavyoonekana katika picha.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akikagua moja ya mashamba ya mahindi ya Gereza Songwe alipofanya ziara ya kikazi katika Gereza hilo kabla ya kuendelea na ziara yake Mkoani Rukwa leo Januari 25, 2019.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitoa maelekezo kwa Maafisa Waandamizi wa Magereza Mkoani Mbeya alipotembelea na kukagua mashamba ya mahindi ya Gereza Songwe.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Jeremia Minja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na  Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya.(Picha zote na Jeshi la Magereza).

TIDO MHANDO AACHIWA HURU NA MAHAKAMA YA KISUTU

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake.


Tido alipanda kizimbani jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi MKuu Huruma Shaidi, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya kusomewa hukumu.


Mshitakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na mashitaka manne ya kutumia madaraka vibaya likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya sh. milioni 887.1.


Akisoma hukumu hiyo jana na Hakimu Shaidi, alisema upande wa mashitaka wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo ulipeleka mashahidi watano ambao walishindwa kuthibitisha shitaka hilo.


Hakimu Shahidi alisema kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka hivyo anamwachia huru.


Awali, akichambua ushahidi huo, alisema Tido kipindi akiwa Mkurugenzi wa TBC aliingia mkataba wa makubaliano na Channel 2 kwa kuibadilisha TBC kutoka analogi kwenda digital.


Alisema mshitakiwa huyo alisaini mkataba huo yeye peke yake bila ya uongozi wa shirika hilo wala wakili.


Aliendelea kuchambua ushahidi huo alisema mkataba huo inadaiwa ulikuwa sio wa halali kwani yalikuwa ni makubaliano ya awali.


Pia mkataba huo ulikuwa hauna ligo ya TBC na haukuwa na nguvu kisheria.


Upande wa mashitaka unadai mkataba huo haukufuata utaratibu wa kisheria.


” Kwali mkataba kuitwa mkataba lazima ukamilike lazima kuwepo na watu ambao wanahusika na lazima kuwepo na mwanasheria hivyo mkataba huo sio halali bali ni makubaliano ya awali, ” alisema.


Baada ya uchambuzi huo, Hakimu Huruma alisema mshitakiwa huyo hakuna sehemu ilithibitisha kwamba ulikuwa ni mkataba hivyo anamwachia huru.


Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TUKUKURU), Leonard Swai, baada ya uamuzi huo, aliambia mahakama kwamba ana nia ya kukata rufaa.


Mshitakiwa alikuwa anatetewa na wakili Dk. Ramadhani Maleta.
Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashitaka waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni pamoja na Afisa uchunguzi wa TAKUKURU, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.


Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16, mwaka 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.


Katika shitaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, mwaka 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.


Katika shitaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, mwaka 2008 na Septemba mwaka 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.


Katika shitaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, mwaka 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.


Katika shitaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, mwaka 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya sh.887,122,219.19.

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU

1.   Ofisi ya Waziri Mkuu inapenda kuujulisha UMMA wa Watanzania kuwa kumekuwepo na taarifa zilizozua taharuki baina ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo “Whatsapp” kuhusu Ukaguzi Maalumu utakaohusisha Maafisa kazi kupita nyumba kwa nyumba na kukagua Mikataba ya Kazi, Mshahara kima cha chini cha Mshahara, Mazingira ya Kazi, malipo ya Hifadhi ya Jamii na fidia kwa Wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa majumbani. Aidha, tangazo hilo liliainisha faini ya mil 50 kwa kutojisajili kwenye mfumo wa fidia kwa wafanyakazi (WCF).

2.   Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa zoezi hilo litaanzia Mkoani Mbeya.

3.   Ofisi inakanusha taarifa hizo na kuueleza UMMA kuwa wapuuze taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli wowote na wala hazijatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambayo ndio yenye dhamana ya kusimamia Sheria za Kazi

4.   Ofisi inawataka watu wanaoeneza taarifa hizo za uongo kuacha upotoshaji huo mara moja. Aidha, Serikali kupitia vyombo mbalimbali inafuatilia taarifa hizi ili kubaini chanzo chake na wahusika, ili kuchukua hatua za Kisheria na haki ionekane inatendeka dhidi yao.

5.   Aidha, Ofisi inatoa wito kwa Waajiri wote kuendelea kutekeleza Sheria za Kazi kwa kuwapatia Wafanyakazi wao mikataba na kuwalipa stahiki zao kwa mujibu wa Sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza katika kaguzi mbalimbali.


Thursday, January 24, 2019

WENYE DALADALA WAKARIBISHWA KIBUTA. KIARAWE.

Na Omary Mngindo, Kibuta

WAMILIKI wa magari ya kusafirisha abiria katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, wametakiwa kwenda kuwapatia huduma wakazi kwenye Kata ya Kibuta na maeneo mengine.

Diwani wa Kata hiyo Mhandisi Juma Kilumbi ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika stendi mpya ya Kilumbi Basi stendi, ambapo alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Vyombo Vya Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetangaza njia.

Mhandisi Kilumbi alisema kwamba njia zilizotangazwa na SUMATRA ni Kibuta, Masaki mpaka Chanika yenye urefu wa kilometa 32, Kibuta, Mpuyani, Kiluvya kuishia Mbezi urefu wa kilometa 55.

Njia nyingine ni Kibuta, Kisarawe na Pugu Station kilometa 55, pia Chanika, Mwanzo Mgumu kuelekea Bwana yenye urefu wa kilometa 45, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuboresha urahisishaji wa huduma ya usafiri na usafirishaji.

"Kwanza niwashukuru wana-Kibuta kwa kunichagua kuwa diwani wao, pili kuungana na viongozi wenzangu katika kujitokeza kwenye mikutano na kujadili maendeleo, tumepata soko la kila Alhamisi ya wiki, pamoja na stendi tuliyoizindua hivi karibuni," alisema Mhandisi Kilumbi.

Alisema kuwa Maofisa wa SUMATRA walifika katani humo kukagua stendi ya Kilumbi Basi Stendi ya Kibuta na kwamba wamejirishisha kulingana na ubora wake, kisha kutangaza njia hizo ambapo Maofisa hao wamewaomba wamiliko wa magari kuwasiliana nao tayari kuanza kutoka huduma.

"Nawashukuru Maofisa wa SUMATRA kwa kuja katani kwangu, wamekagua njia kutoka hapa kuelekea maeneo mbalimbali, lengo kubwa ni kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma kama ilivyo katika maeneo mengine," alisema Kilumbi.

Kwa upande wao wakazi wa Kijiji cha Kibuta katani hapo Asha Tingo na Jumanne Magomba walisema kwamba baada ya kuwepo kwa solo la kila wiki na usafiri wa Kibuta kuelekea Chanika kumeongeza mzunguko wa pesa katika eneo hilo.

"Hili la kuwepo usafiri kutoka hapa kuelekea maeneo mbalinbali haswa Kiluvya na Mbezi no hatua kubwa ya kimaendeleo kwani itaturahisishia usafiri na usafirishaji wa biashara zetu," alisema Tingo.