Saturday, January 19, 2019

HALMASHAURI 33 ZAVUKA MALENGO YA UKUSANYAJI WA MAPATO

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya siku 68 kwa  halmsahauri  nne kurejesha fedha za mradi wa elimu(Equip)zilizotumika kinyume na utaratibu.
........................


Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.

Halmashauri 33  kati ya halmashauri 185 zimeweza kukusanya mapato ya ndani kwa kiwango cha asilimia 50 na zaidi ya makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 huku  halmashauri 21 zikiwa zimefanya vibaya kwa kusanya chini ya asilimi 20 ya makisio yake kwa mwaka.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo alipokuwa  akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa robo ya pili ya mwaka.


Alisema katika Halmashauri 33 zilizokusanya asilimia 50 na zaidi zimo Halmashauri za  Majiji tatu zikiongozwa na Jiji la Dodoma, Manispaa ni mbili zikiongozwa na manispaa ya Iringa, Halmashauri za Miji nane zikizongozwa na Mji wa Geita na Halmashauri za Wilaya ni ishirini zikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.


“Uchambuzi unaonyesha kuwa Katika Majiji 6, Jiji la Dodoma linaongoza kwa kukusanya asilimia 59 ya makisio na Jiji la Tanga limekuwa la mwisho kwa kukusanya asilimia 33 ya makisio” alisema.


Aidha Manispaa ya Iringa imeongoza katika kundi la Manispaa kwa kukusanya asilimia 64 ya makisio ambapo Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 20 ya makisio.


Jafo aliongeza kuwa kwa upande wa Halmashauri za Miji, Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 84 ya makisio na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 9 tu ya makisio,


Alisema Katika kundi la Halmashauri za Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 78 ya makisio ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 6 tu ya makisio.


Kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ya mapato ya  Halmashauri Jafo alibainisha Halmashauri iliyoongoza kwa kuwa ni Jiji la Dodoma ambalo limekusanya Shilingi Bilioni 40.12 na halmashauri iliyokusanya kiasi kidogo cha fedha ni halmashauri ya Wilaya ya Momba ambayo imekusanya shilingi milioni 105.04.


Waziri Jafo pia alibainisha Mkoa ambao Halmashauri zake zimekusanya mapato kwa kuzingatia wingi wa mapato kuwa ni Mkoa wa Dar es salaam ambao kwa jumla halmashauri zake zimekusanya shilingi bilioni 77.4 na Mkoa wa Mwisho ni Katavi ambao halmashauri zake zimekusanya shilingi bilioni 2.4 tu.


Alisema katika Mkoa uliokusanya vizuri kwa kuzingatia asilimia ya makusanyo ni  Mkoa wa Geita Halmashauri zake zimekusanya asilimia 56.4 ya makisio ya mwaka ukifuatiwa kwa karibu na Mkoa wa Dodoma uliokusanya asilimia 55.9 ya makisio yake na Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Mtwara ambao umekusanya asilimia 15 ya makisio yake ya mwaka.


Wakati huo huo Waziri Jafo amewataka wakurugenzi wote ambao Halmashauri zao hazikufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya chini ya asilimia kumi ya makisio yake kwa kipindi cha nusu mwaka kujieleza na kujitathimini na kuhakikisha wanaongeza bidii katika suala la ukusanyaji wa mapato.


“Halmashauri 9 kati ya 10 zilizofanya vibaya katika mwaka wa fedha uliopita zimefanikiwa kufanya vizuri katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2018/19 kwa kukusanya zaidi ya asilimia 20 ya makisio yake” alisema .


Waziri Jafo pia aliwaagiza Wakurugenzi wote kuhakikisha takwimu zote za mapato katika mfumo wa LGRCIS zinafanyiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa IFMS(Epicor)  kwani taarifa zote za mapato na matumizi ya fedha zinatakiwa kutolewa kupitia mfumo huo.


Ulinganifu huu wa taarifa za mapato umelenga kuonesha jinsi kazi za ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa inavyoendelea kusimamiwa vyema na takwimu hizi zinazotolewa ni kwa mujibu wa taarifa zilizofanywiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa IFMS(Epicor).


Katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashaurti zilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na hadi kufikia Disemba 31,2018 Halmashauri zimekusanya shilingi bilioni 300 sawa na asilimia 41 ya makisio.


Kwa kipindi cha kwa mwaka 2017/18 halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 687.3 na hadi  kufikia Disemba,2017 halmashauri hizo zilikuwa zimekusanya sh bilioni 281.3 sawa na asilimia 41 ya makisio.


Takwimu hizi zinabainisha kuwa kuna ongezeko la Shilingi bilioni 18.7 kwa mwaka wa fedha 2018/19 ikilinganishwa na makusanyo kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Friday, January 18, 2019

SEKTA YA AFYA YAENDELEA KUPAA – SERIKALI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akielezea jambo mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu hali ya Huduma za Afya mwaka 2018, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya jijini Dodoma.Waziri wa Afya,
..................................

Na WAMJW – DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Sekta ya Afya nchini yaendelea kukua kwa kasi, kutokana na Serikali kuendelea kuboresha Huduma kwa Wananchi zikiwemo upatikanaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, huduma za chanjo, huduma za afya ya uzazi na mtoto na Huduma za Dharura.



Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akitoa tamko mbele ya Waandishi wa Habari na baadhi ya viongozi wa Wizara, kuhusu hali ya Huduma za Afya mwaka 2018, katika ukumbi wa Wizara ya Afya jijini Dodoma.


Waziri Ummy amesema kuwa Katika mwaka 2018, jumla ya wajawazito 2,086, 930 walihudhuria na kuandikishwa Kliniki, ikilinganishwa na wajawazito 2,009,879 Mwaka 2017, huku mwongozo wa utoaji huduma za afya ya uzazi na mtoto unaelekeza wajawazito kuanza huduma mapema kabla ya majuma 12 ya ujauzito na kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito.


Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa, Katika kipindi cha mwaka 2018 jumla ya watoto 1,568,832 walizaliwa ikilinganishwa na Watoto 1,498,488 mwaka 2017, huku wakipatiwa huduma mbalimbali za chanjo ili kuzuia magonjwa yanayowaathiri Watoto ikiwemo ugonjwa Kupooza, Kuharisha, Pepopunda, Pneumonia, homa ya ini na Surua.


“Katika kipindi cha mwaka 2018 hali ya chanjo kwa Watoto nchini imeendelea kuwa katika kiwango cha juu zaidi ya asilimia 85 ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kama inavyoonyeshaa katik hapa chini” Alisema Waziri Ummy.


Hata hivyo nWaziri Ummy amesema mwaka 2018 kumetokea jumla ya vifo 20,087 ikilinganishwa na vifo 19,693 mwaka 2017, huku Katika kipindi cha miaka yote miwili 2017 na 2018, homa ya mapafu imeongoza kwa kusababisha vifo, ambapo kwa mwaka 2017, imechangia asilimia 18.2 ya vifo vyote na mwaka 2018 imechangia kwa asilimia 12.9 ya vifo vyote.


Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Mwaka 2018, ugonjwa usio wa kuambukiza (shinikizo la damu) umejitokeza katika magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo ambapo umechangia vifo kwa asilimia 1.9 ya vifo vyote.


Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amesema kuwa Hali ya upatikanaji wa Dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuimarika, hii ni kutokana na Serikali kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Milioni 31 mwaka 2015/16 hadi kufikia Shilingi milioni 251 mwaka 2016/17 na Shilingi 270 mwaka 2018/19.


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa hali ya upatikanaji wa Damu Salama ambapo katika kipindi cha mwaka 2018, huku jumla ya chupa za damu salama 307,835 sawa na asilimia 85.5 ya lengo zilikusanywa ikilinganishwa na chupa 233,933 mwaka 2017, huku akiwahasa Wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuendelea kuokoa maisha ya wahitaji.


“Chupa zote 307,835 zilizokusanywa zilipimwa makundi ya damu pamoja na magonjwa makuu manne ambayo ni Ukimwi (HIV,) Homa ya Ini B na C (HBV, HCV) na Kaswende (Syphilis). Jumla ya chupa 262,283 sawa na asilimia 85.3 zilikuwa salama na kusambazwa katika hospitali kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.” Alisema Waziri Ummy.


Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa, katika mwaka 2018 jumla watu 47,967 waligundulika kuwa na vijidudu vya Kifua kikuu ikilinganishwa na wagonjwa 44,714 waliogunduliwa mwaka 2017., huku akisisitiza kuwa tatizo la ugonjwa wa Kifua Kikuu limeendelea kuwepo takribani mikoa yote nchini.


kwa upande mwingine, Waziri Ummya amesema kuwa, hadi kufikia Desemba 2018, jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya vilifikia 7,768 kutoka vituo 7,435 mwaka 2017 sawa na ongezeko la vituo 333 kwa mwaka, amedai kuwa Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 71 ya vituo vya kutolea huduma; Mashirika ya dini asilimia 12, Taasisi za Serikali asilimia 3 na vituo binafisi asilimia 15.


Sambamba na hilo, waziri Ummy amesema kuwa, hadi kufikia Desemba mwaka 2018, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa na jumla ya wanachama 899,654 na ikihudumia jumla ya wanufaika 4,219,192 sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote.

CHALINZE WAKUSANYA MIL. 700 MWEZI DESEMBA

Na Omary Mngindo, Chalinze

HALMASHAURI ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kwa mwezi wa 12 mwaka 2018 imeweza kukusanya mapato kiasi cha sh. Mil. 700 kupitia makusanyo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Zikatimu ameyasema hayo juzi alipozungumza na wakazi wa Kitongoji cha Pingo, kikao alichokiandaa kuzungunzia mikakati ya elimu kwa wanafunzi waliokosa nafasi ya kuanza Kidato cha kwanza mwaka 2019.

Alisema kuwa mapato hayo yamegawanywa katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo elimu, afya, mifugo na nyinginezo, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

"Tunawaomba viongozi endeleeni kuwahamasisha vijana kuunda vikundi vya Ujasiriamali kisha kuvisajili ili viweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri yao, ambayo haina riba unalipa kulingana na unachokikopa," alisema Zikatimu.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kulipa na kusimamia malipo ya tozo mbalimbali zinazotakuwa kulipwa kulingana na sheria na taratibu kwani mwisho wa siku zinarudi katika shughuli za kimaendeleo kwenye maeneo yao.

"Katika nakusanyo yanayoendelea kukusanywa, sehemu yake ndio hizi sh. Mil. 132 ambazo tumeziingiza kwenye ujenzi wetu wa sekondari ya Kata ya Pera ambayo imeshaanza kujengwa hapa Pingo," alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Pingo Miraji Dibwe aliishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kusaidia juhudi zilizoanzishwa na wananchi wa Kitongoji hicho.

Nae Shabani Kiwamba akielezea kilimo cha kutokamilika kwa zahanati yao ambayo inataraji kuwa Kituo cha afya cha Kata, ambapo alisema ni cha miaka mingi pasipokuwepo dalili za kukamilika.