Tuesday, January 15, 2019

TFDA YAIMARISHA UDHIBITI WA BIDHAA KATIKA VITUO VYA FORODHA.

Mkaguzi wa dawa wa TFDA kituo cha Namanga akiendelea na ukaguzi.
......................................

NA WAMJW-ARUSHA

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kaskazini imeeleza kuwa, itaendelea kulinda soko la ndani la bidhaa za vyakula ,dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuimarisha huduma kwenye mipaka yote nchini ikiwemo mpaka wa Namanga, Mkoani Arusha.

Udhibiti katika mipaka hiyo ni unalenga kuhakikisha kuwa bidhaa bora, salama na zenye ufanisi pekee ndiyo zinaingia nchini ili kulinda afya ya wananchi.

Hayo yamebainishwa katika kituo cha TFDA kilichopo Mpaka wa Namanga mkoani hapa wakati wa Maafisa Uhusiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo walipotembelea Kituo hicho cha ukaguzi ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni ya ‘ Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Maafisa ukaguzi wa Mpaka wa Namanga ambao unatenganisha nchi za Tanzania na Kenya walieleza mikakati ya utoaji wa huduma za ukaguzi kutokana na Serikali kuwekeza rasimali watu pamoja vitendea kazi katika kurahisisha utoaji wa huduma katika Mpaka huo.

Kaimu Meneja TFDA Kanda ya Kaskazini, Benny John amesema ofisi ya Kanda imeendelea kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa vipodozi, vifaa Tiba na vitendanishi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata kanuni na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanalinda maslahi mapana ya kulinda afya ya wananchi.

“Udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini umeongezeka kwa wafanyabiashara kulipa ada na tozo za Serikali na hivyo kuongeza pato la Taifa” alisema Kaimu Meneja huyo.

Nae Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Mpaka wa Namanga, Bw. Elia Nyeura amesema takwimu za uingizaji wa mizigo katika kituo cha Namanga zimeongezeka kutoka shehena 724 mwaka 2015/16 hadi kufikia 1,223 kwa mwaka 2016/2018.

“Kwa sera ya awamu ya tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda, bidhaa zinazodhibitiwa na TFDA na kuruhusiwa kwenda nje ya nchi hususani zilizosindikwa kwa kipindi cha miaka mitatu zimeongezeka kutoka shehena 429 hadi kufikia 640 kwa 2017/18 ” amesema Nyeura na kuongeza kuwa, mamlaka imepunguza upotevu wa mapato kutokana na bidhaa zisizofaa kwa kuimarisha ukaguzi”. Alisema.

Hata hivyo amebainisha kuwa thamani ya bidhaa zilizokamatwa kwa kuingizwa nchini bila kufuata utaratibu zimepungua kutoka Milioni 630.3 hadi kufikia Milioni 24.7 kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018.

Aidha, maafisa Uhusiano hao wameweza kutembelea maeneo mbalimbali ya kituo hicho ikiwemo chumba maalum cha Maabara na kujionea namna bidhaa za dawa zinavyochunguzwa katika kuangalia ubora wake kabla hazijaingizwa Nchini.

Mpaka wa Namanga ni moja ya mipaka ambayo tayari imeanza kufanya kazi kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa kwa upande mmoja tu wa Nchi (One Stop Boder Post-OSBP) ambapo bidhaa inaingia na kukaguliwa kwa pamoja na wakaguzi wa nchi mbili (Tanzania na Kenya) ili kupunguza muda wa wadau kukaa mpakani kwa muda mrefu kwa ukaguzi.

MGALU ACHANGIA MIL. 43 KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII NA KIMAENDELEO PWANI

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

MBUNGE wa viti maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu, amechangia shughuli za maendeleo katika wilaya mbalimbali mkoani hapo, iliyogharimu sh. milioni 43 kwa kipindi cha mwaka mmoja.


Aidha amekabidhi vifaa vya ofisi vyenye thamani ya milioni 5, kwa ofisi za jumuiya ya UWT katika kata zote 133 kimkoa ili kurahisisha utendaji kazi na kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.


Akitolea ufafanuzi juu ya utekelezaji wa shughuli zake za kibunge wakati wa baraza la UWT mkoa, Subira alisema moja ya majukumu yake ni kuunga mkono juhudi za serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kushiriki shughuli za kijamii.


Alisema kati ya mambo alitoshiriki kuweka mkono wake ni pamoja na kujitolea mifuko ya saruji kwenye ujenzi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.


Hata hivyo Subira alieleza, katika kutekeleza ilani kwenye sekta ya nishati alianzisha kampeni ya zima vibatari ,washa taa kwa kuchangia taa za solar akiambatana na uongozi wa UWT Mkoa wa Pwani .


“Taa hizo nilizigawa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu hususan katika mashule kwa lengo la kuboresha elimu bora kwa wanafunzi na zahanati kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa huduma za kiafya ikiwemo wadi za kujifungulia, uboreshaji wa afya za mama wajawazito ,watoto na kurahisisha huduma za afya kwa makundi maalum”. 


“Pia niliambatana na mrs. Barbara Wentworth wa Wentworth Foundation na kutembelea shule ya sekondari Mandela na kukabidhi vitaulo yaani PADS kwaajili ya wanafunzi wa kike;”alifafanua Subira.


Subira alibainisha, taulo hizo ni za mwaka mzima kwa kila msichana, kwa wasichana 500, huo ni msaada mkubwa na utasaidia kuboresha mahudhurio yao darasani ,amekabidhi maboksi ya vitabu na kuahidi kujenga maktaba.


Mbunge huyo, ambae pia ni naibu waziri wa nishati alisema kwamba, licha ya majukumu hayo amefanya ziara wilaya mbalimbali kukagua miradi ya ujenzi wa nishati ya umeme na kuwasha umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa .


Anaipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais dkt.John Magufuli kwa jitihada za kuondoa changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya maeneo.

Thursday, January 10, 2019

RC MAKONDA AWAHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA KUIPOKEA NDEGE YA SITA YA SERIKALI AIRBUS A220-300.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda anawaalika Wananchi wote Wapenda maendeleo kujiunga na Mtekelezaji namba moja wa Ahadi Rais Dkt. John Magufuli kwenye mapokezi ya Ndege ya Sita ya Serikali (Airbus A220-300) itakayowasili Nchini Kesho January 11 Saa sita Mchana ikitokea Nchini Canada.
 
Hafla ya mapokezi itafanyika kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere.

Rais Magufuli aliahidi na sasa anatekeleza
WANANCHI WOTE MNAKARIBISHWA

MAGAZETI YA LEO JANUARI 10, 2019.

Wednesday, January 9, 2019

WAZIRI KALEMANI ARIDHISHWA NA KASI YA UBORESHAJI WA KITUO CHA UMEME CHA ZUZU.

Image may contain: 10 people, people smiling, people standing and outdoor
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya kampuni ya KEC ya nchini India ambayo imepewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Dodoma ambacho kinaongezewa uwezo wa megawati 400, mbali ya megawati 48 za sasa.


Dkt. Kalemani ameyasema hayo leo jijini Dodoma baada ya kufanya ziara ya kukagua vituo mbalimbali vya kupoza umeme ikiwemo cha Msalato, Mnadani na Zuzu ambapo aliambatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati.


Hata hivyo, Dkt Kalemani ameeleza kuwa, mkandarasi huyo anapaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi januari mwakani ili kuweza kuboresha zaidi hali ya upatikanaji umeme jijini Dodoma ambapo kazi ya uunganishaji umeme kwa wananchi inaendelea na hivyo kuongeza matumizi ya nishati hiyo muhimu.


Dkt. Kalemani amesema kuwa, mkandarasi huyo anafanya kazi tatu ambazo ni kushusha umeme kwa kV 400 katika kituo hicho, kujenga kituo cha kupoza umeme cha uwezo wa megawati 400 na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.


Ameongeza kuwa, mkandarasi huyo alianza kazi hiyo mwezi Machi mwaka 2018 ambapo gharama ya mradi huo ni Dola za Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).


Aidha, baada ya kukagua vituo hivyo vya kupoza umeme, Dkt Kalemani amewaagiza TANESCO kuhakikisha kuwa kila kituo kinakuwa na fundi sanifu atakayekuwa kituoni kwa masaa 24 ili inapotokea hitilafu ya umeme, iweze kutatuliwa kwa haraka.


Vilevile, Dkt Kalemani ameagiza kuwa, kila kituo kiwe na vifaa vya ziada vya umeme badala ya kusubiri kuagiza vifaa hivyo mara linapotokea tatizo hali inayopelekea wananchi kukosa umeme na kueleza kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu atakagua utekelezaji wa agizo hilo na Meneja ambaye hatatekeleza, atachukuliwa hatua.


Aidha ametoa agizo kwa TANESCO kuweka walinzi katika miundombinu ya umeme kwani kumekuwa na matukio ya baadhi ya wananchi kuhujumu miundombinu hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kukata nguzo za umeme na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiusika.


Katika ziara hiyo pia Waziri wa Nishati alizungumza na wafanyakazi wa TANESCO katika kituo cha kupoza umeme kilichopo mjini Dodoma ambapo pamoja na kuwapongeza kwa kazi wanazofanya, alionya kuwa, katika mwaka 2019, mfanyakazi atakayeonekana amefanya uzembe utakaopeleka kukosekana kwa umeme, atachukuliwa hatua.