Wednesday, January 9, 2019

MBUNGE WA KIBAHA VIJIJINI AKABIDHI VIFAA VYA AFYA VYA MIL. 400

Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Mkoani Pwani, Hamoud Abuu Juma (kushoto) akikamkabidhi vifaa tiba Mganga Mkuu wa wilaya ya Kibaha Dkt. Ibrahim Isack.
 ....................................... 


Na Omary Mngindo, Mlandizi.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amenunua kontena la fut 40 lenye vifaa vya afya sanjali na vya shule, vyote vikiwa na thamani ya sh. Mil. 400.

Hayo yamebainika kwenye hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Ibrahimu Isack, iliyofanyika kwenye Hospitali ya Mlandizi mkoani Pwani, alivyovinunua kutoka nchini Uingereza.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Jumaa alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, ili kukabiliana na changamoto za hapa na pale katika sekta hiyo.

Alisema kwamba katika kontena hiyo mbali ya vifaa tiba, pia kuna vifaa vya shule ambavyo hivyo vitakabidhiwa kwa wahusika wa shule kwenye Kata mbalimbali jimboni humo, ambapo vifaa hivyo vitaongeza utendaji kazi kwa walimu na wanafunzi kupokea masomo.

"Hili Kontena nimelinunua kutoka nchini Uingereza, kuna vifaa vya Hospitali pamoja na vya shule, vyote vina thamani ya milioni 400, lengo kuu la vifaa ni kuboresha sekta ya afya na elimu," alisema Jumaa.

Akizungunzia changamoto kwenye sekta ya afya, Jumaa alianza kwa kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa dhamira yake njema ya kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa nchi kote, kwa kutenga fedha na kukabidhi katika Wilaya na mikoa kuboresha Vituo vya afya pamoja na Hospitali.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Dkt. Isack alianza kwa kumshukuru Mbunge Jumaa kwa msaada huo uliowafikia kwa wakati mwafaka, huku akisema kwamba vitasaidia kupunguza kama si kumaliza changamoto kwenye sekta hiyo.

"Hatua ya Mbunge inaunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli ambaye tangu aingie madarakani ameonesha dhamira ya kuboreshwa kwa sekta mbalimbali, huku kipaumbele kikubwa kikiwa kwenye sekta ya afya," alisema Dkt. Isack.
  Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Mkoani Pwani, Hamoud Abuu Juma akishusha vifaa tiba kwaajili ya kusambaza kwenye Zahanati na Vituo vya Afya katika jimbo lake.
 Sehemu ya vifaa hivyo vilivyotelwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Mkoani Pwani, Hamoud Abuu Juma kwaajili ya Zahanati na vituo vya Afya katika Jimbo lake.

MAGAZETI YA LEO JANUARI 09, 2019.

NAIBU WAZIRI DK MABULA AKERWA MAKUSANYO MADOGO YA KODI YA ARDHI KATIKA HALMASHAURI

Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza alipowasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita alipofanya ziara katika mkoa huo jana kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake kuhusiana na sekta ya ardhi katika halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita.
........................................

Na Munir Shemweta, WANMM Geita.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekerwa na makusanyo madogo ya mapato katika halmashauri mbalimbali nchini kupitia kodi ya ardhi.


Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita jana mkoani Geita alipofanya ziara ya kushtukiza kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika halmashauri hizo, Dk Mabula alisema, mapato ya sekta ya ardhi katika halmashauri nyingi hayaridhishi na kueleza kuwa halmashauri nyingi mapato yake yako chini ya asilimia 30.


Alisema pamoja na halmashauri hizo kuwa na mapato kidogo kupitia sekta ya ardhi lakini watendaji wake hawaoneshi jitihada zozote kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha kupitia sekta hiyo na hivyo aliwataka  watendaji hao kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwa kuwa msisitizo wa serikali ya awamu ya tano ni kukusanya kodi.


‘’Kwa staili hii tutafika kweli? Mna bahati mbaya sasa watendaji wa sekta ya ardhi katika halmshauri mtakuwa chini ya wizara moja kwa moja na rais amepiga kelele kuhuisiana na kodi ninyi mnarelax’’ alisema Dk mabula.


Hata hivyo, Dk Mabula aliisifu halmashauri ya Mji wa Geita kwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia sitini. Kwa Mujibu wa taarifa ya Halmshauri ya Mji wa Geita, kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba 2018, halmashauri hiyo imekusanya jumla ya shilingi 389,699,937.28 kati ya milioni 600,000,000 ilizopanga kukusanya.


Kwa upande wake Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia, Afisa Ardhi wake Faraja Kaluwa pamoja na halmashauri hiyo kupewa malengo ya kukusanya milioni 150 lakini kufikia desemba 2018 imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 12,480,500 tu. 


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka wakuu wa idara za ardhi katika halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita kutoa ahadi ya utekelezaji maagizo aliyoyatoa na hatua gani zichukuliwe kwao iwapo maagizo hayatatekelezwa kwa wakati.


Maagizo aliyoyatoa Dk Mabula ni kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi ya ardhi, uingizaji viwanja na mashamba katika mfumo wa kielektronik, utoaji hati za ardhi pamoja na utoaji hati za Madai (demand notes) kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.


Aidha, Dk Mabula ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaingiza viwanja na mashamba kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya kielektronik na kutaka kasi ya utoaji hati kuongezeka ili kuwawezesha wananchi kiuchumi na wakati huo kuiingizia serikali mapato kupitia kodi ya ardhi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinatoa leseni za makazi katika maeneo yenye nyumba zilizojengwa nje ya urasimishaji na mipango Miji na kueleza kuwa zoezi hizo linatakiwa kukamilika mwezi machi mwaka huu.


Dk Mabula amezitaka Halmashauri kuanisha maeneo yote ya nyumba hizo na kupatiwa leseni za makazi kwa gharama ya shilingi 5000 sambamba na kuziingiza katika kumbukumbu za halmashauri na kubainisha kuwa leseni hizo ni hatua za kuelekea wamiliki wake kupatiwa hati.

UFAFANUZI WA TANGAZO KUHUSU USIMAMIZI KWA WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania imetoa tangazo kwa umma kupitia tovuti yake (www.bot.go.tz) likiwataka watu na taasisi zote zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha zilizoko Tanzania Bara (isipokuwa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo – SACCOS) kutoa taarifa zitakazotumika katika utayarishaji wa Kanuni za Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha. Taarifa hizo zinatakiwa kutumwa Benki Kuu ya Tanzania hadi tarehe 31 Januari 2019.


Benki Kuu inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tangazo hilo:


1.   Lengo la tangazo hilo siyo kuvifunga au kuvibana vikundi vya kijamii kama VICOBA, watu binafsi na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kama ambavyo inapotoshwa na baadhi ya watu na mitandao mbalimbali ya kijamii, bali ni kukusanya taarifa za awali kuhusu huduma hizo. 


Kama ilivyoainishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, lengo la sheria hiyo  ni kuwalinda wadau wote wanaohusika na huduma hizi (watoaji na watumiaji) kwa kuziwekea utaratibu mzuri zaidi wa uwekaji kumbukumbu, uendeshaji na uongozi kwa ujumla. Pia kuwalinda wamiliki na watumiaji wa huduma hizi dhidi ya vitendo vinavyoweza kupelekea kupoteza fedha na mali zao, pamoja na kuzuia watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutumika kufanya uhalifu ikiwemo utakasishaji fedha haramu.
  

2.   Benki Kuu inafahamu kuwa baadhi ya watu binafsi, taasisi na vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VICOBA, havina usajili rasmi na hivyo havitambuliki kisheria. Kwa kutambua hilo, Sheria imeweka kipindi cha mpito cha mwaka mmoja (kuanzia sheria itakapoanza kutumika rasmi) kwa wote wanaojihusisha na utoaji huduma ndogo za fedha, kujipanga ili wawe tayari kusimamiwa pale kanuni zitakapokuwa zimetolewa rasmi. Hivyo, katika kipindi hiki cha mpito, siyo kosa kwa watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutokuwa na usajili rasmi.  


Aidha, Wadau wote watashirikishwa kikamilifu katika utayarishaji wa Kanuni hizo, na mara zitakapokuwa tayari na kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania, maelezo zaidi kuhusu usajili yatatolewa.


Benki Kuu inawasihi wananchi wote kutokuwa na taharuki na inasisitiza kwamba uamuzi wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha umechukuliwa kwa nia njema na  kwa faida ya watumiaji na watoaji wa huduma hizi.


Aidha, Benki Kuu  inautahadharisha umma kujiepusha na taarifa na miongozo inayotolewa kiholela na watu, kampuni na mashirika ambayo yanajitangaza kufanya shughuli za uandikishaji wa watoa huduma ndogo za fedha kwa wananchi kwa niaba ya Serikali au Benki Kuu. 


Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, kampuni au shirika lolote litakalojihusisha na vitendo vya kuwakanganya wananchi kwa lengo la kupotosha au/na kujipatia mapato haramu.


Tunawahamasisha wananchi kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tangazo hili zinazoendelea kutolewa na Benki Kuu katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania Bara.


Kwa ufafanuzi/maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu   022-2235585/0767503145 au barua pepe: 



au tembelea Benki Kuu Makao Makuu Mtaa wa 2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha.