Wednesday, December 12, 2018

MIKATABA YA WAKANDARASI WA UMEME VIJIJINI KUPITIWA NA WANASHERIA WA SERIKALI.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Haji Janabi wakati wa kikao kazi na watendaji wa REA na TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA, TANESCO na Wizara ya Nishati.
..................................

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameeleza kuwa, Wanasheria wa Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wataanza kupitia mikataba ya wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini ili kuchukua hatua za kuwawajibisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa kusuasua.

Aliyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa, Wilaya na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.

“ Yako baadhi ya maeneo ambayo Wakandarasi hawafanyi vizuri kama vile Mtwara, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Shinyanga, Singida, Tabora (Kaliua, Uyui, Urambo), Dodoma na Tanga (Wilaya ya Korogwe, Mkinga na Pangani), ambao utekelezaji wao katika mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza, wako chini ya asilimia 20,” alisema Mgalu.

Naibu Waziri alitoa agizo kuwa, wakandarasi katika maeneo hayo wahakikishe kuwa, wanafanya kazi kwa kasi na ufanisi ikiwemo kuweka magenge mengi ya kazi, uwepo vifaa na wasimamizi wa miradi wa kutosha ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na Serikali na pia kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kusambaza umeme vijijini.

Kuhusu hali ya usambazaji umeme vijijini, Mgalu alisema kuwa, kuanzia Januari mwaka 2017 hadi sasa jumla ya vijiji 1,098 vimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Mradi wa Makambako-Songea, Mradi wa Backbone na miradi ya umeme iliyo nje ya gridi.

Hivyo kwa ujumla alisema kuwa, hadi sasa jumla ya vijiji 5,493 vimesambaziwa umeme nchini na vijiji vilivyosalia ni 6,775 ambavyo vinaendelea kusambaziwa umeme kupitia REA III mzunguko wa kwanza na wa pili.

Aidha, Naibu Waziri wa Nishati, aliwakumbusha wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa miradi husika inaleta tija kwa jamii kwa kuunganisha nishati hiyo katika sehemu mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii kama vituo vya afya na katika shughuli zinazokuza uchumi wa wananchi kama vile mashine za kusaga na kukoboa nafaka au sehemu za biashara.

Vilevile, Naibu Waziri wa Nishati aliwakumbusha wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kuhusu kutekeleza agizo la Serikali la kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila Wiki na kununua vifaa vya umeme vinavyozalishwa hapa nchini. 

Hata hivyo, alisema kuwa viwanda vinavyozalisha vifaa hivyo chini ya ubora unaotakiwa vitaanza kuchukuliwa hatua kwani vinachelewesha kazi ya usambazaji umeme nchini.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati katika kikao hicho, Haji Janabi alitoa pongezi kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme na kuwa na ari ya kufanya kazi, usiku na mchana.

Aidha alitoa wito kwa watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi kufanya kazi kwa bidii kama ilivyo kwa viongozi hao wa Wizara na kuwa wabunifu. Alisema kuwa, baada ya kikao kazi hicho, Wizara na Taasisi zitatekeleza ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri na kusimamia miradi ya usambazaji umeme vijijini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.




Baadhi  ya watendaji wa REA na TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA, TANESCO na Wizara ya Nishati wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

Tuesday, December 11, 2018

BENKI KUU YATAJA FAIDA YA DHAMANA ZA SERIKALI KWA MAENDELEO YA TAIFA.

Mshauri  wa Benki Kuu ya Tanzania BoT tawi la Dodoma akifafanua jambo katika semina hiyo inayoendelea jijini Dodoma.
..................................

WATANZANIA wameshauriwa kushiriki kikamilifu katika minada ya dhamana za Serikali kwani faida zake ni kubwa kwa Taifa ikiwamo kufanya shughuli za maendeleo kwa kutumia fedha zake za ndani.

Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Alexander Ng’winamila wakati akiwasilisha mada katika mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na fedha yalioandaliwa na BoT kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari za fedha na uchumi.

Akizungumza wakati akitoa mada inayohusu uwekezaji katika dhamana za Serikali; faida zake kwa Taifa na wawekezaji ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye midana ya dhamana za Serikali.

Amesema ametoa ombi kuendelea kuhamasisha kutolewa kwa elimu kwa umma ili waweze kushiriki kikamilifu na hatimaye kuifanya serikali iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa fedha za ndani.”Ombi letu kwa vyombo vya habari tunaomba muendelee kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye dhamana za Serikali.

Kuna faida nyingi na mojawapo ushiriki wao utawezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani badala ya kwenda kukopa nje ya nchi,”alisema.

Akifafanua zaidi zinazopatikana kwenye dhamana za Serikali ni kusaidia Serikali kugharamia bajeti iwapo kutakuwa na upungufu wa kibajeti, kupata fedha za kuendeshea miradi ya maendeleo , kusimamia ujazi wa fedha katika uchumi, husaidia kudhibiti mfumuko wa bei , huchagia uwepo wa soko la upili na husaidia kuhamasisha utafutaji wa mitaji kwa taasisi zingine.

Pia amesema hutoa fursa za uwekezaji ,hivyo kuwepo kwa ushindani katika uwekezaji mbalimbali na kusaidia kupatikana kwa riba zinazoaminia na soko huku akieleza kwa mwananchi wa kawaida faida
za kushiriki ni nyingi kwani ni sehemu salama kutokana na ukweli kwamba Serikali haitarajiwi kukiuka mategeo ya wadai wake wakati wa malipo.

Ametaja faida nyingine dhamana za Serikali zinahamishika hivyo mwekezaji anaweza kuuza muda wowote.Pia dhamana za Serikali zinaweza kutolewa kama dhamana kwa ajili ya mikipo na faida nyingine ni kwamba dhamana za Serikali zina kiwango cha faida inayoridhisha.”Tunaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye
dhamana za Serikali kwa maendeleo ya Taifa letu.”

Kuhusu midana ya dhamana za Serikali amesema ipo ya aina mbili ambapo kuna mnada wa muda mfupi ambao ni wa mwaka mmoja na mnada wa dhamana za Serikali wa muda mrefu ambao unaanzia miaka miwili mpaka miaka 20.

Pia amesema ili mwekezaji aweze kushiriki katika minada ya dhamana za Serikali ni lazima awe na akaunti ya uwekezaji katika dhamana za Serikali na kwamba ufunguzi wa akaunti ya dhamana za Serikali hufanyika kupitia kwa mawakala walioidhinishwa ambao huwasilisha.

“Wakati wa kufungua akaunti kuna taarifa muhimu ambazo zinahitaji zikiambatanishwa na kitambulisho halali kinachotambulika na mamlaka za nchi pamoja na namba ya mlipa kodi(TIN) ”amefafanua. 

Ng’winamila amesema fomu za kujiunga zinapatikana kupitia mawakala waliopo nchini pamoja na kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua unapozungumzia dhamana za Serikali kwa lugha rahisi ni kwamba Serikali inakopa kwa wananchi wake.
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha Benki Kuu ya Tazania Bw. Alexander Nw’winamila akitoa mada ya uuzaji wa Hati Funagani na Amana za Serikali katika semina ya waandishi wa habari za Fedha na Uchumi inayofanyika jijini Dodoma katika tawi la Benki Kuu ya Tanzania BoT Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo hayo.
Bi. Zalia Mbeo Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki (BoT) akitoa mchango wake katika semina hiyo kuhusu mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mada zinazotolewa na wataalam wa Benki Kuu ya Tanzania.
Vick Msima Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki akifuatilia mjadala katika semina hiyo.
Mwanablog kutoka Fullshangweblog Bwana John Bukuku akiwa katika semina hiyo.
Meneja Kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania BoT akitoa mada kuhus hatua za kuimarisha usimamizi wa Taasisi za fedha.Bw. Nassor Omary.
Baadhi ya wanahabari wakijadiliana jambo katika semina hiyo.

TIF. YAJENGA MSIKITI KIJIJI CHA BITUNDU BUKOBA.

Msikiti mpya uliojengwa na Taasisi yaThe Islamic Foundation (TIF)  kitongoji cha kakashule kijiji cha bituntu halmashauri ya wilaya Bukoba mkoani Kagera,

Msikiti wa zamani uliokuwa unatumika na waumini wa dini ya kiislamu kitongoji cha kakashule kijiji cha bituntu halmashauri ya wilaya Bukoba mkoani Kagera.
..................................................
Na Allawi Kaboyo- Bukoba.

Waumini wa dini ya kiislam katika kitongoji kakashule kijiji cha bituntu halmashauri ya wilaya Bukoba mkoani Kagera, wameishukuru taasisi ya THE ISLAMIC FOUNDATION (TIF) yenye makao yake makuu mjini Morogoro, kwa kuwajengea nyumba bora ya kumuabudia mola wao kulinganisha na nyumba waliokuwa wakiitumia siku za nyuma.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya kukabidhiwa msikiti iliyofanyika desemba 07 mwaka huu 2018, waumini hao wameonyesha kufurahishwa na neema hiyo waliyoletewa katika maeneo yao huku wakiwaombea kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) viongozi waliofadhili uwepo wa msikiti huo ambapo awali walikuwa wakitumia msikiti ulikuwa sio salama kwao hasa kipindi cha mvua na kuwafanya wakati mwingine kushindwa kufanya ibaada kabisa.

"Ni miaka saba sasa tumekuwa tujikokota kujenga msikiti na kufanikiwa kuupata msikiti huu wa nyasi ambao hata hivyo imekiwa changamoto kwa nyasi zilizotumika kuezekea kuondolewa na upepo na kupelekea matundu makubwa" alisema mmoja wa waumini was msikiti huo.

Kwaupande wake mkurugenzi wa taasisi ya THE ISLAMIC FOUNDATION (TIF) mkoani kagera Sheikh Hamdani Kagaruki akawataka waislamu kuutumia msikiti huo kwaajili ya ibaada na wala sio kwa mambo mengine na kueleza kazi ambazo zinaendelea kufanywa na taasisi hiyo mkoani hapa ukiwemo ujenzi wa visima vya maji na miradi mingine ya kijamii katika maeneo mbalimbali.

"Niwaombe ndugu zangu waislamu msikiti huu usiwe wakufungwa bali utumike kwaajili ya ibaada na sio mambo mengine yanayokwenda kinyume na maamrisho ya mola wetu, taasisi yetu inaendelea kujenga msikiti mingi ndani ya mkoa wetu kikubwa tuzidishe dua kwa kuwaombea viongozi wetu ili wazidi kutufadhiri" alisema mkurugenzi huyo.

Katika juhudi za kuendeleza dini tukufu ya kiislamu na kuhakikisha inaenea, taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) imekuwa ikijenga misikiti katika maeneo mbalimbali katika mkoa wa Kagera na hapa tunashuhudia uzinduzi wa msikiti mpya na mzuri unaowafanya waumini wa maeneo haya kufanya ibada kwa amani

MBUNGE WA KIBAHA MJINI ACHANGIA MILIONI MBILI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI WA VIZIWAZIWA.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza na baadhi ya wananchi wa mitaa miwili ya Sagale pamoja na viziwaziwa hawapo pichani wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
.......................................................


VICTOR MASANGU,KIBAHA

WAKAZI zaidi ya 2500 kutoka mitaa miwili ya Sagale na Viziwaziwa katika halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani  kwa sasa  bado wanakabiliwa na changamoto ya  kupata  magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuumwa na  matumbo kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.

Wakazi hao wanakabiliwa na hali hiyo kwasababu ya kuwalazimu kutumia maji machafu ya visima ambayo  sio salama kwa afya zao kutokana na kuchangia na wanyama mbali mbali pamoja na wadudu.

Hayo yamebanishwa na wananchi wakati wakizungumza katika mahojiano maalumu mara baada ya kutembelewa na  Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ikiwa ni ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi kwa lengo la kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

Baadhi ya wakazi hao akiwemo  Yakimu Musa pamoja na Kili Mussa walisema  kwamba kwa kipindi cha miezi sita  sasa wamekuwa wakiteseka usiku na mchana kwa ajili ya  kutembea umbari mrefu kutafuta maji ya visima ambayo hata hivyo sio salama kabisa kwa matumizi ya binadamu.


Naye Diwani wa kata ya Viziwaziwa Mohamed Masoud alibainisha kwamba hapo awali walikuwa wanapata maji kupitia mradi ujulikanao kwa jina la Savi lakini kutokana na kudaiwa deni la kiasi  cha shilingi milioni 6 walikatiwa huduma ya upatikanaji wa maji hayo na ndipo wananchi wake wakaanza kupata usumbufu mkubwa wa kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.


Katika kuliona  hilo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo na kusikiliza kero za wananchi ameahidi kulivalia njuga suala hilo kwa kuwakutanisha viongozi wa mamlaka zinazohusika ambapo pia  amechangia kiasi cha shilingi milioni 2  kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji  inarejeshwa  kwa wananchi katika hali yake ya kawaida ili kuwaondolea adha waliyokuwa wanaipata.

“Kwa kweli mimi kama Mbunge wenu nia yangu ni kuhakikisha tunashirikiana na nyinyi katika kuzitatua changamoto mbali mbali ambazo zinawakabiliwa katika Nyanja tofauti na kikubwa katika mtaa huu wa mikongeni kitu kikubwa ni suala la maji ambalo limetokana na deni ambalo mlikuwa mnadaiwa kwa hiyo mimi nitaendeleo kuchangia zaidi na pia nitawakutanisha wahusika  katika mamlaka zinazohusika kulitafutia ufumbuzi,”alisema Koka.

WANANCHI hao wa mtaa wa Sagale pamoja na mtaa wa viziwaziwa Wilayani Kibaha mnamo mwaka 2013 waliamua kuanzisha mradi maalumu wa kusambaza huduma ya maji  kwa ajili ya kuondokana na kero  hiyo lakini  kutokana na kuibuka kwa changamoto ya kudaiwa deni hilo  mradi huo  uliweza kusimama  mwaka huu na kupelekea  usum ufu mkubwa kwa wakazi hao.
Diwani wa kata ya Viziwaziwa  Mohamed Masoud akifafanua jambo kwa wananchi wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini katika mitaa ya ya Viziwaziwa na Sagale (PICHA NA VICTOR MASANGU)

WAKUU WA MIKOA WAPONGEZA UJENZI WA RELI YA KISASA (STANDARD GAUGE)

Wakuu wa mikoa nchini wameipongeza serikali  kwa ujenzi wa Reli ya kisasa  (standard Gauge) na kusema kuwa, huo ni mradi utakaoleta manufaa katika mapinduzi ya kiuchumi hasa wakati huu serikali inavyojikita katika uchumi wa viwanda.

Wakiongea na Mwandishi wa habari hizi mara baada ya kukagua Mradi huo ambapo wameanzia Morogoro hadi Dar es Salaam wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Reli Tanzania (TRC) Bwana Masanja Kadogosa.

Wamesema fursa nyingi zitapatikana mara baada ya kukamilika kwa Mradi huo mkubwa hapa Tanzania na nchi jirani.

Akizungumzia Mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kwa sasa ujenzi huo unaenda kwa kasi ambapo baadhi ya maeneo tayari wameanza kuweka miundombinu ikiwemo ya mataruma na nguzo za umeme.

Kadogosa alitoa wito kwa wananchi walio jirani na Mradi huo kutoa ushirikiano wa kutosha katika kulinda miundombinu hiyo ambayo ni chachu ya kuleta maendeleo ikiwemo upatikanaji wa ajira. 
Wakuu wa mikoa wakipata maelezo kuhusu ujenzi wa Reli ya kisasa

MAGAZETI YA LEO DESEMBA 11, 2018.

RUVU DARAJANI WALILIA MAZAO YAO

Baadhi ya wakulima katika bonde la Ruvu, kijiji cha Ruvu Darajani kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wakionesha miche ya mipapai iliyokatwa katwa katika mashamba yao, PICHA NA OMARY MNGINDO.
...........................................................


Na Omary Mngindo, Ruvu

WAKULIMA katika Kijiji cha Ruvu Darajani, Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameiomba Serikali kuingilia kati vitendo vinavyofanywa na watu wanaojiita wanatoka ofisi inayosimamia bonde la Ruvu wilayani humo, kwa kufyeka mazao waliyoyapanda. 

Wakizungumza na waandishi wa habari katika mashamba yao, wakazi wakijitambilisha kwa majina ya Ally Jeki,  Zaynabu Kikande  Shayo, Ally Jeki na Said Swaiba, walisema kuwa mwishoni mwa wiki wamevamiwa na watu hao waliokatakata mazao kwenye mashamba yao. 

Swaiba alisema kuwa siku ya tukio watu hao walipofika waliwachuku vijana wakaelekea nao kwenye mashamba hayo, kisha kuanza zoezi la kukata mazao pasipokushirikisha viongozi wa Kijiji, kitendo walichokieleza ni cha uonevu, huku wakiomba serikali ikemee jambo hilo. 

"Tunalima bustani nje ya mita 60 wanaodai ni mali yao, lakini cha kusikitisha hivi karibuni wamekuja kuivamia, wamekata mazao yetu ambayo wengi wetu tunayategemea kuendesha familia zetu, wengine tunasomesha kupitia kilimo hiki," alisema Swaiba.

Nae Samir Shayo alilalamika mipapainyake kukatwa baa watu hao ambao walipofika waliambatana na askari waliokuwa na silaha za moto,  kitendo kilichowaogopesha wananchi hao. 

"Kama mnavyoona, shamba langu lipo mbali na mita za 60 lakini hata kama wamechukua mita 100 bado wsingefika hapa, lakini wameamua kutufanya kitendo kibayabsana,  tunaomba serikali ikemee vitendo hivi vya kibabe," alisema Samir. 

Kwa upande wake Mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Ruvu Ramadhani Natamani alisema kwamba mwezi wa nne mwaka huu walifika ofisini kwao wakawaeleza wanataka kuweka mipaka ya kuonesha mwisho wa kulimwa, lakini hawakuonekana tena 

"Cha kusikitisha Mtendaji wa Kijiji alipotaka kuwasogelea wajue kinachoendelea, aliambiwa asiwasogelee eneo walilokuwa wanakata mazao ya wakulima,  tunaomba uongozi wa Mkoa uingiliekati suala hili, " alisema Mnyamani.
 
Sehemu ya miche ya mipapai iliyokatwa katwa katika mashamba ya wakulima wa bonde la Ruvu kijiji cha Ruvu Darajani kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, PICHA NA OMARY MNGINDO.