Sunday, November 4, 2018

KALEMANI:ILI KUONDOA ADHA YA KUKATIKA UMEME

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akikagua miundombinu ya kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mwakibete, Jijini Mbeya na kuagiza mafundi na wahandisi katika Vituo vyote nchini kufanya ukaguzi wa kila siku kuepusha kukatika Umeme kutokana na hitilafu zinazojitokeza katika Vituo hivyo.
 

Mameneja wote wanaosimamia vituo vya kupoza na kusambaza umeme nchini wametakiwa kufanya ukaguzi ( checkup) wa kila siku asubuhi katika mitambo na mashine zilizopo katika vituo hivyo kuondoa adha ya kukatika umeme kutokana na hitilafu au uharibifu katika vituo hivyo.

Licha ya kuwa vituo hivyo vinafanyiwa ukarabati na ukaguzi wa kila mara au hata baada ya miezi kulingana na utaratibu waliojiwekea.
Hayo yameleezwa na Waziri wa Nishati ,Dkt. Medard Kalemani , wakati wa ziara yake ya kikazi katika Jiji la Mbeya, Novemba 3, 2018, baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Mwakibete na kukagua miradi ya kusambaza umeme katika kijiji cha Nsalaga na Iduda inayotekelezwa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

Alieleza kuwa kumekuwa na changamoto ya kukatika umeme kwa muda mchache katika baadhi ya maeneo na sababu kuu ya ikielezwa kuwa ni hitilafu katika vituo au kuharibika kwa kifaa katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme.

Alifafanua kuwa changamoto hiyo inaepukika na kutoweka kabisa endapo wahandisi na mafundi watakuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa mitambo na mashine zao kila siku asubuhi kubaini tatizo kabla ya kutokea.

Mafundi na wahandisi muwe na tabia ya kufanya ukaguzi na matengenezo ya kila siku asubuhi badala ya kusubiri tatizo litokee, acheni kufanya ukaguzi na matengenezo kwa mazoea, hii itasaidia kufahamu mapema tatizo linazoweza kutokea baadaye na kuondoa usumbufu wa kukatika umeme kwa wananchi hali ya kuwa kuna umeme mwingi nawa kutosha, alisisitiza Kalemani.

Alifafanua kuwa kwa sasa serikali haitaki kuona mtu yeyote anakosa huduma ya umeme kwa muda Fulani kwa sababu tu kumetokea ya hitilafu katika mitambo na mashine katika vituo vya kupoza na kusambaza umeme, badala yake inataka umeme upatikane saa 24 na siku saba kwa wiki kwa kuwa umeme upo wa kutosha na ziada.

Waziri wa Nishati, Dk.Medard Kalemani, (katikati) akipita katika mitaa ya kijiji cha Nsalaga kukagua Miundombinu ya usambazaji wa huduma ya Umeme, unaotekelezwa na Shirika la Umeme,  nchini (Tanesco) ambapo ametoa siku 14,kwa wananchi hao kuunganishwa na huduma hiyo.


WAZIRI LUGOLA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA GEREZA MBIGIRI MKOANI MOROGORO

aziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akionyesha moja ya nyumba ya askari wa Gereza la Mbigiri, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro, ambayo inahitaji matengenezo. Lugolo alifanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo la Kilimo kwa lengo la kupata kero na kuimarisha uzalishaji wa kilimo na ufugaji. Kulia ni askari wa Gereza hilo, Sajenti Lubimbi Sayi. Lugola alifanya kikao na askari na Maafisa wa Gereza hilo na kuwataka kumpa kero zao bila kuwa na woga na hakuna atakaye wanyanyasa.
...........................................
Na Felix Mwagara, MOHA-Morogoro

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka askari pamoja na watumishi mbalimbali waliopo ndani ya Wizara yake wawe huru kuuliza maswali, kusema kero zao zinazowakabili katika vikao vyake na hakuna kiongozi yeyote atakaye wanyanyasa baada ya yeye kuondoka.

Waziri Lugola amesema hayo baada ya kuona baadhi ya watumishi katika ziara mbalimbali anazozifanya nchini, wanakua na woga wa kusema kero zao wakihofia watapata matatizo baada ya yeye kumaliza kikao.

, wakati anapata mambo mengi ambayo yanamsaidia kutatua kero za watumishi wake licha ya kuwa baadhi ya watumishi wanakua na woga wa kusema matatizo yanayowakabili.

Akizungumza katika kikao na askari na Maafisa wa Jeshi la Magereza wa Gereza la Kilimo la Mbigiri, liliopo Wami-Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro, jana, Lugola alisema ili aboreshe utendaji kazi wa Wizara na Idara zake, anahitaji kujua matatizo mbalimbali ya watumishi wake, hivyo katika kikao chake ruksa watumishi kuuliza maswali kwasababu kupitia maswali hayo yanamsaidia sana kutatua kero zao.

“Mimi ndio Waziri wenu, ulizeni swali lolote, toeni kero zenu na hakuna wakuwafuatilia baada ya kikao hiki, hiki ni kikao cha Waziri wenu mmepata nafasi hii ulizeni, niambieni matatizo yenu yanayowakabili ili tuyafanyie kazi,” alisema Lugola.

Pia aliwaambia watumishi hao endapo watapata matatizo baada ya kusema kero zao katika kikao chake, wawe huru kumuambia japo anaamini hakuna chochote kitakacho wakuta maana kikao chake ambacho ni huru.

Lugola aliyasema hayo baada ya baadhi ya askari wa Gereza hilo kuwa na hofu wakati walipokua wanauliza maswali ambapo mmoja wao akitoa kero yake huku akitahadharisha kuwa Waziri huyo amlinde endapo atapata matatizo mara baada ya kikao hicho kumalizika.

“Hivi huwa mnakua karibu na viongozi wenu? Kwa mfano unakuta ukaribu huu wa kukaa hapa kwa kumkaribia Mkuu wa Gereza katika kikao hiki ni wa leo tu kwasababu nipo, lakini baada ya kikao hiki unakuta Mkuu wa Gereza au kiongozi yeyote mkubwa katika Jeshi hafikiwi na askari, hii haiwezekani kuweni karibu na viongozi wenu, waambieni kero zenu na pia nyie viongozi msiwatishe hawa askari wenu, sikilizeni kero zao,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola aliutaka uongozi wa Gereza hilo kuacha malalamiko na badala kutafuta  majibu ya changamoto zinazowakabili na pia wahakikishe wanasimamia nidhamu kwa askari na kutooneana, na pia waendelee kutumia vitendea kazi vilivyopo katika Gereza hilo ili waweze kuongeza uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo, (ACP) Shija Fungwe, alimshukuru Waziri Lugola kwa kufanya ziara katika Gereza lake, na pia maagizo yake aliyoyatoa watayafanyia kazi likiwemo la kuongeza uzalishaji kupitia vitendea kazi walivyonavyo na pia yeye pamoja na askari na Maafisa mbalimbali wa Gereza hilo aliweka wazi kuwa wanaishi vizuri, kwa ushirikiano na pia wapo huru kuzungumza naye kuhusu jambo lolote la utendaji kazi.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufanya ziara katika Gereza letu, tunakuahidi kufanyia kazi maagizo yako uliotupa na pia tutaendelea kutumia vitendea kazi tulivyonavyo ili tuzidi kuboresha, pamoja na kuimarisha uzalishaji wa Gereza hili,” alisema ACP Fungwe.

Waziri Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo ambalo linafanya shughuli za kilimo ya mazao mbalimbali pamoja na ufugaji  wa ng’ombe, kondoo, mbuzi na kuku ambapo kwa ujumla wana mifugo zaidi ya 1000.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimsikikiliza Mkuu wa Gereza la Mbigiri, Mvomero, Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza, (ACP) Shija Fungwe (kulia) alipokua anatoa taarifa ya utendaji kazi wa Gereza hilo la Kilimo. Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo kwa lengo la kupata kero na kuimarisha uzalishaji wa kilimo na ufugaji. Lugola pia alifanya kikao na askari na Maafisa wa Gereza hilo na kuwataka kumpa kero zao bila kuwa na woga na hakuna atakaye wanyanyasa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na askari na Maafisa wa Magereza wa Gereza la Kilimo la Mbigiri lililopo Mvomero, Mkoani wa Morogoro, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Gereza hilo kwa lengo la kupata kero na kuimarisha uzalishaji wa kilimo na ufugaji. Kushoto kwa Waziri huyo ni Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza, (ACP) Shija Fungwe. Lugola aliwataka na askari na Maafisa hao kusema kero zao bila kuwa na woga na hakuna atakaye wanyanyasa.