Friday, October 19, 2018

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YATANGAZA UJIO WA MVUA KUBWA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua, kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Aprili, 2019,  jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utabiri, Samwel Mbuya akifuatilia. 
.......................................


MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua, katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Aprili, 2019.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi amesema Mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara.

Alisema maeneo ya mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku vipindi vingi vya mvua vikitarajiwa nusu ya kwanza ya msimu wa Novemba, Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili, 2018/19 na kupungua nusu ya pili ya msimu huo.

“Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2018 katika mikoa ya Kigoma na Katavi na wiki ya tatu na ya nne katika maeneo mengine yaliyosalia. Mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019 katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua,” alisema Dk. Kijazi.

Aidha, kutokana na mvua za vuli katika maeneo hayo ametoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa.

Aliongeza kuwa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori Katika kipindi cha mvua za ‘Msimu’ (Novemba hadi Aprili) 2018/19, hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharage na mtama, yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama.

“…Magonjwa ya wanyama na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na ile ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi,” aalisisitiza katika taarifa yake.



WAZIRI MWIJAGE AZINDUA KIWANDA CHA VILAINISHI KIGAMBONI.



 Waziri wa Viwanda,  Biashara na Uwekezaji,  Charles Mwijage akifungua kitambaa ikiwa ni ishara ya kuzindua Kiwanda cha vilainishi katika wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Na Selemani Beta

Waziri wa Viwanda,  Biashara na Uwekezaji,  Charles Mwijage amezitaka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). kuliangalia kwa jicho la karibu soko la vilainishi hapa Nchini kwani hivi sasa soko hilo limekuwa na bidhaa ambazo hazikidhi ubora unaokubalika.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda kipya cha vilainishi cha Lakes Lubes, kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mwijage alisema kwa muda mrefu sekta hiyo imekuwa kama imesahaulika kiasi ambacho kumekuwa na malalamiko toka kwa wananchi juu ya uwepo wa vilainishi visivyokidhi ubora

“Niseme kwakweli soko linabidhaa ambazo hazina ubora, wakati mwingine kukiri sio dhambi lakini niwahakikishie kuwa tunajipanga kuliangalia soko hili ili kuwa na bidhaa zenye viwango vinavyokubalika lakini pia kudhibiti uingizaji wa vilainishi holela hautakuwa na nafasi” Alisema

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kiwanda hicho, Mwijage alisema kiwanda hicho kimekuja wakati muafaka na kinaenda sambambana sera ya Muheshimiwa Rais ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda.

“Kwa aslimia kubwa sera ya viwanda inalenga kuongeza ajira kwa wananchi wetu, Zaidi ya 75% inalenga ajira na zingine 25 ndiyo hapo mambo mengine ikiwamo kodi.
Nikiangalia hapa mnasema mtaajiri watu Zaidi ya 250, hilo ni jambo jema na kwakweli mmeunga mkono jitihada za Mh. Magufuri’ Aliongeza.

Ataka waajiri kuwaajari watumishi wao

Katika hatua nyingine, Waziri Mwijage amewataka waajiri Nchini kuacha kuwanyanyasa wafanyakazi wao badala yake wajikite kuboresha maslahi yao ili waweze kuwaombea kwa Mwenyezimungu biashara zao ziweze kunawiri.

Mwijage amesema maslahi ya mfanyakazi yakiboreshwa hata ugumu wa maisha nao utapungua na hapo ndipo mfanyakazi atatumia muda wake kujituma kwamoyo wake wote kuleta mafanikio katika viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bw. Khaled Hassan Mohamedi amemshauri waziri Mwijage kuzuia uingizaji holela wa vilainishi kwani hivi sasa vilainishi vyote vinapatikana katika kiwanda hicho.


Mohamed alisema viwanda vya ndani vyakutengeneza vilainishi vya mitambo vina uwezo wa kuzalisha vilainishi hivyo kwa ubora wa hali ya juu.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 45,000 za vilainishi vya aina zote na tayari wameshapata vibali kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali.

“Wenye magari na mitambo wanalalamikia vilainishi visivyo na ubora sasa sisi tumekuja na bidhaa ambayo watumiaji wa vyombo vya moto wataifurahia na tutatoa waranti kama mtu chombo chake kitaharibika  kwa kutumia vilainishi vyetu tutamfidia,” alisema Mohamed.

Alisema malighafi za kutengeneza vilainishi hivyo watakuwa wanatoa nchi za Urusi, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu na kwamba Lake Lubes imewekeza Dola za Marekani milioni 4.5.

Alisema kiwanda hicho kinatarajia kuwa nafursa za ajira zipatazo 250 na mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 39, kati yao 34 ni wazawa na raia wa kigeni watano na kwamba wanatarajia kuendelea kupunguza raia wa kigeni ili wabaki Watanzania pekee.

Mkuu wa wilaya akaribisha wawekezaji

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Bi Sara Msafiri amewataka wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kigamboni wajitokeze kwani bado Kigamboni inahitaji wawekezaji vitu mbalimbali.

DC BAGAMOYO AWAONYA WATUMISHI WA SERIKLI.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa katika kikao na wawekezai na wafanayabiashara Bagamoyo.
......................

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa amewataka watumishi wa serikali wilayani humo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia Kanuni, Maadili na kujituma zaidi katika kuiletea wilaya maendeleo na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwenye kikao kilichowajumuisha wadau wa maendeleo wilayani Bagamoyo wakiwemo wawekezaji wenye viwanda, wafanya biashara, pamoja na wakuu wa idara lengo likiwa ni kuangalia ni mambo gani yanayokwamisha kufikia malengo kwa wawekezaji na wafanya biashara ndani ya wilaya hiyo.

Alisema Maendeleo hayapatikani kama hakuna ushirikiano kati ya watendaji wa serikali na wawekezaji au wafanyabiashara ambao uwepo wao unasaidia ajira kwa wananchi, na kulipa kodi itakayofanya maendeleo yenye manufaa kwenye jamii.

Kawawa alisema hataki kuona mtendaji wa serikali anafanya kazi kwa mazoea kwa kudharau watu wanaohitaji msaada wake katika kufanikisha jambo na kuonya kuwa mtunishi atakaebainika kukwamisha maendeleo Bagamoyo atamchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia vivutio vilivyopo Bagamoyo ambavyo vinaweza kuingizia wilaya mapato kwa wageni, aliwataka watendaji wa idara ya mambo ya kale kubuni mbinu zitakazowavutia watalii wa ndani na nje ya nchi kufika Bagamoyo kujionea mambo mbalimbali ya kihistoria ili serikali nayo iongeze mapato.

Alisema si vyema kuweka sheria kandamizi kwa watalii kwani kufanya hivyo kutapelekea kupunguza watalii na kupunguza mapato ya serikali yanayotokana na watalii.

Awali wakichangia mada katika mkutano huo, wawekezaji na wafanyabiashara wametaja changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kufikia malengo yao ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa maji ya uhakika na umeme wa uhakika hali inayopelekea kuzorota kwa uzalishaji huku wengine wakishindwa kabisa kuanza uzalishaji.

Kwa upande wao wafanyabiashara wamelalamikia kodi zinazokadiriwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuwa hayazingatii uhalisia wa biashara husika hivyo hukadiriwa kodi kubwa inayopelekea wafanyabiashara kushindwa kulipa na hatimae kufunga biashara.

Walisema ni vyema makadirio ya kodi yakafanywa kwa uhalisia wa biashara husika ili watu wengi waweze kuendesha biashara na kulipa kodi kuliko ilivyo sasa biashara nyingi zimefungwa kwasababu ya madeni makubwa yasiyolipika.

Kufuatia malalamiko hayo wakuu wa vitengo vya DAWASA, TANESCO na TRA wamepata nafasi ya kujibu hoja zilizowasilishwa  ambapo Meneja wa DAWASA Bagamoyo alisema katika kuhakikisha tatizo la maji linaondoka katika wilaya ya  Bagamoyo DAWASA inaendelea na mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji katika maeneo ya mji wa Bagamoyo lenye ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita.

Alisema Tenki hilo litakapokamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya, Bagamoyo mjini na ukanda maalum wa ewekezaji EPZA.

Nae Meneja wa TANESCO wilaya ya Bagamoyo Daniel Kyando alisema kutokana na miundombinu iliyopo TANESCO Bagamoyo ina uwezo wa kuhudumia megawatts 22 ambapo mpaka sasa Bagamoyo umeme unaotumika ni megawatts 9 tu.

Akizungumzia swala la kukatika kwa umeme katika mji wa Bagamoyo, kyando alisema hiyo inatokana na matengenezo yanayofanywa na mafundi katika kuimarisha miundombinu hasa katika kipindi cha mvua.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo, Farence Mniko alisema TRA Bagamoyo inaendele kushirikiana na wafanyabiashara ili kuhakikisha kila mmoja analipa kodi inayomstahiki.

Akizungumzia swala la wafanyabiashara wenye madeni makubwa na kupelekea kufunga biashara zao, Meneja Mniko aliwataka wafanyabiashara hao kufika ofisi za TRA ili kuona namna bora ya kulipa madeni hayo au kusamehewa ikiwa watakidhi vigezo vya kusamehewa baada ya kujaza fomu ya msamaha.
  
Meneja wa TANESCO wilaya ya Bagamoyo Daniel Kyandoakizungumza katika mkutano huo.
 
Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo, Farence Mniko akizungumza katika mkutano huo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Mfaume Kawawa (katikati) akiwasikiliza  wawekezai na wafanayabiashara Bagamoyo katika kikao alichokiitisha hivi karibuni katika Hoteli ya Green Park.



Wawekezai, wafanayabiashara na wakuu wa idara wilayani Bagamoyo, wakiwa katika kikao cha pamoja alichokiitisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa.

MAGAZETI YA LEO 19 OKTOBA 2018.