Thursday, October 18, 2018

WAANDISHI WA HABARI ZA KILIMO, SAYANSI, WATUNIKIWA VYETI.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Tekonolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akimkabidhi cheti, Mwandishi wa habari Alex Mathias Sonna kutoka Mtandao wa Fullshangweblog baada ya kushiriki mafunzo ya Waandishi wa habari za Kilimo Sayansi yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Tekonolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akimkabidhi cheti, Mwandishi wa habari Suleiman Msuya, baada ya kushiriki mafunzo ya kuandika habari za Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO), yaliyofanyika New Dodoma Hoteli mkoani Dodoma na kuibuka Mshindi wa Pili katika Mashindano ya uandishi wa habari  juu ya teknolojia hiyo kwa kundi la Waandishi wa habari za magazeti. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Jukwaa la Wazi la Kilimo na Teknolojia Afrika (OFAB) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani, Cornell Alliance For Science na African Agricutural Technology Foundation (AATF). 
Mshindi wa  Kwanza kwa upande wa Waandishi wa Habari za Magazetini Bw. Daniel Mkate kutoka Nipashe akipokea cheti.

 Mshindi wa kwanza wa kuandika habari hizo kwa njia ya redio katika mafunzo hayo, Kemsi Fadhil akipokea cheti.

 
Mshindi wa pili wa kuandika habari za GMO kwa njia ya Televisheni, Vumilia Kondo akipokea cheti.
 

Mshindi wa kwanza wa kuandika habari za GMO kwa njia ya Televisheni katika mafunzo hayo, Doreen Mlay kutoka TBC akipokea cheti.

 Mshindi wa jumla wa kuandika habari za GMO kwa njia ya magazeti katika mafunzo hayo, Rose Milondo akikabidhiwa cheti.
 

 Mwanahabari Dotto Mwaibale akipokea cheti cha ushiriki.

Meza kuu wakati wa utoaji wa vyeti hivyo.

 
Picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mafunzo ya Semina kwa Wandishi wa habari za Kilimo Sayansi iliyofanyika Jijini Dodoma.



MWAMBISI SEKONDARI KIBAHA WALILIA UMEME

Na Omary Mngindo, Kongowe

SHULE ya sekondari ya Mwambisi Forest iliyoko Kata ya Kongowe Kibaha Mji Mkoa wa Pwani, haina huduma ya umeme kwa kipindi cha miaka sita sasa, tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Shule hiyo ambayo inapakana na Hifadhi ya Msitu wa Kongowe mjini hapa (Kongowe Forest) ipo umbali wa mita 100, ambao ni sawa na urefu wa nguzo mbili za umeme ili ufike shuleni hapo.

Hayo yamebainika katika taarifa ya Wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo, iliyosomwa na wanafunzi Leah Samson na Fahad Salimu mbele ya mgeni rasmi Nabii Jofrey, Mwalimu Mkuu Josefu Simba na diwani wa Kata hiyo Idd Kanyalu.

Imeeleza kuwa kukosekana kwa nishati hiyo kunachangia kushindwa kutumika baadhi ya vifaa ambavyo vingesaidia kuboresha taaluma, pia ulinzi wa mali zilizopo shuleni hapo, na kwamba ulipoishia umeme kuna umbali wa mita 100 sawa na nguzo mbili.

"Mbali ya ukosefu wa umeme, changamoto nyingine ni uhaba wa vyumba vya madarasa, viti, meza, jengo la Utawala, ongezeko la wanafunzi, upingufu wa vifaa vya kujifunzia, uzio na idadi ndogo ya walimu wa somo la Baiolojia," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na wahitimu hao, Nabii Jofrey alisema kuwa amepokea changamoto hizo, huku baadhi yake akazitolea majibu hapahapo nyingine akiahidi kuzibeba kwa lengo la kwenda kuzitafutia ufumbuzi.

"Nitatengeneza meza 18 za walimu, nitanunua vitabu nitavyoelekezwa vya kiada pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kufundishia," alisema Nabii Josefu.

Awali mwalimu Simba alisema kwamba shule hiyo pamoja na kuwa ya mfano katika utunzaji wa mazingira, wanaushukuru uongozi wa Hifadhi ya Misitu Kongowe kwa kuwapatia miti na wataalamu wa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Diwani Kanyalu alianza kwa kumshukuru mgeni rasmi kwa kukubali mwaliko huo, huku akieleza kwamba anaimani kubwa kwamba changamoto alizoziahidi atazitekeleza mapema iwezekanavyo.

PROFESA MBARAWA AZINDUA KAMPENI YA UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye chanzo cha Mtawanya, Mtwara Mjini.
.........................


Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa leo amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji Miti kandokando ya vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo la kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.

Profesa Mbarawa amezindua kampeni hiyo kwa kupanda miti nane katika chanzo cha Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kuzitaka Bodi zote za Mabonde tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.

Ametoa agizo hilo kutokana na uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi kwa sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha maji kupungua kutokana na vyanzo vingi kukauka, hali inayoweza  kusababisha ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali.

Na kutaka vyanzo vyote vya maji vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti maalumu inayohifadhi maji na kuagiza wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo waache tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa sheria inaweka bayana kuhusu jambo hilo.

Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009 inayokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza shughuli zote za kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji kilipo na kutaka maeneo yote yawekewe mipaka na vizuizi kuonyesha ukomo wa watu kuingia kwenye vyanzo hivyo.

‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji. Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji. 

Niwatake wananchi watoe ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya uhakika kwa miaka ijayo’’, amezungumza Profesa Mbarawa.

‘‘Kwa kuanza tumepanda miti nane katika chanzo hiki cha Mtawanya, nataka ifikapo Disemba mwaku huu, nikute zaidi ya miti 1,000 kwenye chanzo hiki na zoezi hili lifanyike nchi nzima kwa sababu kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia rasilimali za maji nitalisimamia jambo hili ipasavyo’’, ameonya Profesa Mbarawa.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda amesema ni muhimu zoezi la upandaji miti liwe endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na miti isiyo rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo na kutaka wananchi wazingatie sheria iliyopo kwa hiari, pasipo kutumika nguvu na kuonya kuwa hatavumilia uharibifu wa vyanzo vya maji katika wilaya yake.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Maji hivi karbuni imetoa Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.

Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi 45 ikiwa imeshakamilika na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.



WANAFUNZI WATAKIWA KUWA NA MAADILI MEMA:JAJI MKUU

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wanafunzi  kuwa na maadili mema, kufuata sheria na taratibu za nchi na kuachana na matendo yote yanayokiuka maadili ikiwemo wizi wa mitihani.

Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Jaji Mkuu aliwaambia wanafunzi hao kuwa wizi wa mitihani ni tatizo la kwanza la ukosefu wa maadili katika jamii.

Aliwataka wanafunzi hao kujenge tabia ya kujisomea mambo mbalimbali kwa kuwa karne hii ya ishirini na moja ni karne ya sayansi na teknolojia yenye taarifa nyingi zitakazowasaidia kwa maendeleo yao.

“Karne hii ya ishirini na moja ni tofauti na karne ya ishirini, someni mambo mbalimbali ili mfahamu nchi yenu inakwendaje”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza waisome Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili wafahamu  Tanzania itakuwa ni nchi ya namna gani.

Aidha, Jaji Mkuu pia aliwashauri wanafunzi watakaopenda kuwa wanasheria hapo baadaye kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika jamii kwa kuwa fani ya sheria inahitaji mtu aliye na maadili mema hasa na yule anayechukia na kuvipinga kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.

Hata hivyo alisema kutokusoma sheria hakutawazuia kufahamu sheria mbalimbali za nchi na kuwa karne hii ya ishirini na moja inahitaji fani zote kushirikiana ili kuwa na maendeleo.

Akizungumzia rushwa na uchumi wa nchi, Jaji Mkuu alisema ziko nchi duniani zenye rasilimali nyingi na zimeweza kubadili maisha ya raia wake na wakati huo huo zipo nchi zenye rasilimali nyingi lakini hazijaweza kubadili maisha ya watu wake kutokana na rushwa hivyo aliwataka wanafunzi hao kukataa rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo yao.

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema katika jamii wakiwamo wanasheria wa baadaye.  

Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza ambapo anakagua shughuli za mahakama kwenye Mahakama zilizopo mkoani humo.

MAGAZETI YA LEO 18 OKTOBA 2018