Monday, April 9, 2018

WATUMISHI DARASA LA SABA KURUDISHWA KAZINI

HALMASHAURI RUDISHENI ASILIMIA 20 VIJIJINI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwang, akifungua semina ya siku moja iliyowashirikisha Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze pamoja na wakuu wa Idara ambayo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Lugoba.
......................................................
Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo imetakiwa kurudisha asilimia 20 ya mapato yake katika serikali za vijiji ili kuziwezesha serikali za vijiji kujiendesha.

Akifungua semina ya siku moja katika ukumbi wa shule ya Sekondari Lugoba, iliyowashirikisha Madiwani wa Halmashuri ya Chalinze pamoja na wakuu wa idara ambayo imelenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji, Muu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga amesema serikali za vijiji zinahitaji kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji hivyo ni muhimu Halmashauri ikarudisha vijijini asilimia 20 ya mapato yake ambayo ipo kisheria.

Aidha, amewataka madiwani na wakuu wa idara katika Halmashauri hiyo kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa mipaka yake bila ya kuingiliana

Alisema zipo Changamoto kadhaa katika utendaji wa Madiwani pamoja na wakuu wa idara ikiwemo kila mmoja kutojua mipaka yake ya kazi hali inayopelekea muingiliano wa majukumu huku madiwani wakithubutu kutoa maazimio kwa watu ambao kisheria hawana mamlaka nao.

Aliongeza kuwa, semina hiyo itawajengea uwezo na kuacha kutumia muda mwingi kwenye vikao hali inayopelekea kupoteza muda wa kuwatumikia wananchi na hilo linatokana na kutojua namna bora ya uendeshaji wa vikao na kutozingatia muda katika kutekeleza majukumu.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka watendaji katika idara ya mipango kuacha kuelekeza miradi ya maendeleo kwenye kata moja kwasababu ya ukaribu na diwani wa kata husika na kusema kuwa jambo hilo litasababisha chuki baina ya wananchi na Diwani wo, Diwani na Diwani lakini pia wananchi wataichukia Serikali kwa kutowapelekea miradi katika maeneo yao.

Mkurugenzi wa Halmashuri  ya Chalinze Edes Lukoa amesema semina hiyo itawajengea uwezo wa kiutendaji wakuu wa idara pamoja na madiwani ili kila mmoja ajue mipaka yake kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma na maadili ya viongozi.

Kwa upande wao Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze wamesema semina hiyo itawasidia jinsi ya kuendesha vikao vyao ambavyo sasa watatumia muda mfupi na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo.
  Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwang, (katikati) kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Edes Lukoa na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatimu.


 
Picha chini na juu ni Madiwani wa Halmashuri ya Chalinze pamoja na wakuu wa idara wakifuatilia hutuba ya Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo wakati akifungua semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Madiwani na Wakuu wa idara katika Halmashauri ya Chalinze.
     
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwang, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Madiwani wa Halmashuri ya Chalinze.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwang, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara wa Halmashuri ya Chalinze.
  
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwang, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na uslama ya wilaya ya Bagamoyo.

TAARIFA KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI 2018.

Ndugu Wanahabari,

Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu Kuanzia Januari hadi kufikia tarehe 31 Machi 2018, jumla ya wagonjwa 1448, wametolewa taarifa, na kati ya hao 27 wamepoteza maisha.

Kwa kipindi cha Januari wagonjwa 365 na vifo 9 walitolewa taarifa, Februari wagonjwa 996 na vifo 18 na Machi wagonjwa 87 bila kifo. Mwenendo wa takwimu hizi za ugonjwa wa Kipindupindu zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa na vifo imepungua kwa kiasi kikubwa. Aidha, Mkoa wa Dodoma umeongoza kwa kipindi cha Januari hadi Machi kwa kuripoti jumla ya wagonjwa 583 kati ya 1,448 walioripotiwa nchi nzima sawa na asilimia 40.3%, ikifuatiwa na Ruvuma 374 (25.8%), Rukwa 276 (19.1%), Iringa 88 (6.1%), Morogoro 56 (3.9%), Songwe 37 (2.6%), Kigoma 25 (1.7%) na Manyara 9 (0.6%).

Kwa mwezi Machi 2018, jumla ya wagonjwa 87 bila kifo wametolewa taarifa, ambapo ni pungufu kubwa sawa na asilimia 91.3% ukilinganisha na mwezi Februari 2018 ambapo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 996 na vifo 18. Kwa mwezi Machi mikoa na halmashauri ambazo zimeendelea kutoa taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini ni Dodoma (Mpwapwa-35, Chamwino-15, Dodoma Mjini-6, Kongwa-5), Ruvuma (Nyasa-18, Mbinga-5), Rukwa (Sumbawanga Vijijini-5), na Iringa (Kilolo-2).

Ukilinganisha idadi ya wagonjwa waliotolewa taarifa mwezi Februari na ule wa mwezi Machi, mikoa imeweza kufanikiwa kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa. Mfano mkoa wa Morogoro umefanikiwa kudhibiti kikamilifu kutoka wagonjwa 56 mwezi Februari na kutokuwa na wagonjwa wowote mwezi Machi. Mikoa mingine iliyofanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa sehemu kubwa katika kipindi cha mwezi mmoja ni Iringa (punguzo la asilimia 97.7%), Rukwa (punguzo la asilimia 96.1%) na Ruvuma (punguzo la asilimia 92.7%). Mkoa wa Dodoma pia umefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa takribani asilimia 83% katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wizara inatoa pongezi kwa Mikoa kwa jitihada mbalimbali walizozichukuwa kudhibiti ugonjwa huo ambayo imepelekea kupunguza kwa sehemu kubwa kuenea kwa ugonjwa huu katika kipindi cha mwezi wa Machi.

Ndugu Wanahabari,

Ingawa takwimu hizi zinaonyesha kuwa ugonjwa umepungua, bado uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu na kupata maambukizi mapya ni tishio hata kama ni Halmashauri moja tu itakuwa na wagonjwa wa Kipindupindu. Tishio hili inaongezeka katika msimu huu wa mvua ambapo inaweza kuongeza kasi ya kuenea kwa maambukizi ya Kipindupindu. Hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia ugonjwa huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa.

Ni dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi mbalimbali na jamii kwa ujumla ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu.  Wizara inasisitiza kuwa wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali za kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye Halmashauri na Mikoa. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.

Ndugu Wanahabari,

Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, Mikoa, hasa iliyotoa taarifa kipindi cha Januari hadi Machi, pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu.  Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:

1.     Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunayoishi.

2.     Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, 
baada ya kutumia choo, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.

3.     Kunywa maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa.

4.     Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu Kipindupindu.

5.     Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.

6.     Kutotiririsha maji   taka ovyo
Vile vile, Wizara inasisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye Halmashauri na Mikoa yote nchini,

1.     Utoaji wa taarifa sahihi za ugonjwa wa Kipindupindu na kwa wakati kwa kufuata miongozo iliyopo.

2.     Usimamizi wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa ni pamoja na;
    • Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
    • Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
    • Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
1.     Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
    • Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
    • Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.
Hitimisho

Wizara kwa ukaribu itaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Kipindupindu nchi nzima. Aidha, Wizara inawashukuru wadau wote wa sekta mbalimbali, wataalamu na watumishi, waandishi wa habari na wananchi kwa michango yao mbalimbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Asanteni sana

Wednesday, April 4, 2018

JUMUIYA YA WAZAZI BAGAMOYO YACHANGIA UJENZI WA SHULE MBWEWE.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa kushoto akimkabidhi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno, fedha taslimu pamoja vifaa vya ujenzi kwajili ya shule ya msingi Voda iliyopo kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
..............................
Jumuiya ya wazazi wa CCM wilaya ya Bagamoyo imeadhimisha sherehe za wazazi kwa kujitolea Damu katika kituo cha Afya Lugoba Halmashauri ya Chalinze pamoja na kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Voda iliyopo kata ya Mbwewe.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa amesema wameamua kuadhimisha sherehe hizo katika kufanya shughuli zenye kuleta tija kwa jamii ikiwa ni pamoja kutoa damu ili kuunga mkono juhudi za kuchaangia damu salama ambazo zitawasaidia wananchi wenye uhitaji.

Aidha, Mlawa alisema pamoja na hilo maadhimisha hayo yanakwenda sambamba na wiki ya upandaji miti kitaifa ambapo jumuiya hiyo imeweza kupanda miti kadhaa katika kituo cha Afya Lugoba.

Wakati huohuo Jumuiya wazazi wa CCM wilaya ya Bagamoyo wameweza kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi katika shule ya msingi Voda iliyopo kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze.

Alisema miongoni mwa vifaa hivyo vya ujenzi walivyovitoa na kumkabidhi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadani Maneno ni pamoa na Saruji mifuko 50, Mabati 100, na Matofali 200.

Alisema Elimu ni kitu muhimu katika jamii hivyo kila mmoja anapaswa kuchangia katika elimu ili kuunga mkono juhudi za serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo imekuja na sera ya elimu bure kwa watu wote.

Alisema, serikali haiwezi kutekeleza mambo ya maendeleo bila wananchi kutoa ushirikiano hivyo alimuomba Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani kuwahamasisha wazazi, wananchama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuchangia mambo mbalimbali ya elimu ili watoto wapate elimu bora  

Aliongeza kwa kusema kuwa Jumuiya ya wazazi ni kioo katika jamii hivyo imeanza kuonyesha njia na wengine wafuate na hatimae kufikia lengo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa pwani Ramadhani Maneno amemtaka Mtendaji kata wa Mbwewe kuwa na mahusiano mazuri na wananchi ili ajue ni changamoto gani zinazowakabili kushindwa kuwapeleka watoto shule ili kuongeza idadi ya wananfunzi katika shule hiyo.

Alisema viongozi katika kila ngazi wanapaswa kuwa karibu na wananchi ili kutoa suhirikiano wa mambo mbalimbali hata yale yanayohusu maendeleo ya kijamii.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Pwani alisema viongozi wa CCM kazi yao ni kuhakikisha ilani ya chama hicho inatekelezwa ipasavyo ili kuondoa kero mbalimbali za wananchi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya jumuiya ya wazazi ni

WAZAZI TUKO IMARA KUSIMAMIA MAADILI MEMA YA TAIFA LETU.
  
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno, akizungumza katika shule ya msingi Voda kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
 
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa akitoa damu katika kituo cha Afya Lugoba ili kuunga mkono mpango wa taifa wa kuchangia damu salama.

 
Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Bagamoyo, Aeshi Rajabu, akitoa damu katika kituo cha Afya Lugoba ili kuunga mkono mpango wa taifa wa kuchangia damu salama.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatimu, akitoa damu katika kituo cha Afya Lugoba ili kuunga mkono mpango wa taifa wa kuchangia damu salama.
 
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Bagamoyo Aboubakary Mlawa (kushoto) Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo (katikati) Kombo Kamote, na Kulia ni Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Bagamoyo, John Francis(Bolizozo)

ZAIDI YA BILIONI MOJA ZAOKOLEWA BAGAMOYO MALIPO YA EPZA.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj Maid Mwanga akizungumza na wananchi wa kata za Kiromo na Zinga katika kijiji cha Kondo ambapo alitoa taarifa ya kamati yake iliyohakiki majina ya wanaostahiki kulipwa kupisha EPZA.
................................................
Jumla ya shilingi Bilioni moja, milioni mia tatu sitini na moja elfu, laki tatu na arubaini na nne na mia nne 1.361,344,400 zimeokolewa katika malipo ya EPZA Bagamoyo ambazo zingelipwa kwa watu hewa.

Hayo yamebainika katika kamati maalum aliyoiunda Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga ili kuhakiki majina yanayopaswa kulipwa kwa wananchi walio ndani ya eneo maalum la uwekezai Bagamoyo EPZA.

Katika Taarifa iliyosomwa kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kondo kata ya Zinga wilayani Bagamoyo, katibu wa kamati hiyo Mkaguzi msaidi wa Jeshi la zima moto Henry Mwaluseke alisema watu 124 wamebainika kuwa wangelipwa malipo yasiyostahiki yenye umla Bilioni 1.361,344,400.

Alisema watu hao ni wale ambao tayari maeneo yao yamelipwa na mamlaka ya bandari ambapo majia na maeneo yao yamejirudia katika malipo ya EPZA wengine ni wale ambao wamefanyiwa tathmini zaidi ya maeneo mawili huku namba ya uthamini ikiwa ni moa  na maina mengine ni yale ambayo yaliyoandikwa mmiliki asiyekuwepo (Absent  owner)  huku taarifa zake za malipo zikiwepo.

Aidha, miongoni mwa kasoro zilizobainika ni pamoja na kutokuwepo kwa fomu namaba moja ambayo inaonyesha mali na kiasi anacholipw muhusika jambo ambalo linaleta utata juu ya kiasi halali kinachopaswa kulipwa kwa wahusika.

Kamati hiyo pia ilibani mapungufu yaliyofanywa na mthamini ambapo makaburi ya wenyeji wa maeneo hayo hayakuthaminiwa hivyo kupendekeza uthamini ufanyike kwa makaburi ili wahusike wahamishe makaburi ya ndugu zao.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ametoa agizo kwa Mkuu wa polisi wilaya ya bagamoyo na Kamanda wa TAKUKURU wilaya kuhakikisha wanawatafuta wanaohusika na fomu namba moja ili watoe maelezo ya kwanini fomu hiyo haijawafikia wananchi mpaka sasa.

Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni, 40, 971,477,100/ kwa wananchi wanaopisha maeneo maalum ya uwekezaji EPZA ambapo wananchi 695 wamefanyiwa tahmini ya kulipwa fedha hizo kati yao 124 wamegulika kuwa ni hewa na kuokoa shilingi Bilioni 1,361,344,400 ambazo wangelipwa walipwaji hewa.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj Maid Mwanga akipokea taarifa ya kamati aliyoiunda kuhakiki majina ya wanaostahiki kulipwa kupisha EPZA.
Sehemu ya wananchi wa kata za Kiromo na Zinga wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo akitoa taarifa ya kamati ya uhakiki wa majina ya wanaostahiki kulipwa kupisha EPZA.

Monday, April 2, 2018

WAZIRI MKUU AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUILINDA AMANI


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua  Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwenye ukumbi wa Msekwa  mjini Dodoma Machi 31, 2018
  ..........................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini popote walipo wahakikishe wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwa ni pamoja na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 31, 2018) kwenye Mkutano Mkuu wa BAKWATA uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu wasaidizi wa Mufti wakasimamia suala hilo.

“Dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku ndio maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake mkubwa katika amani ya nchi yetu. Niwaombe viongozi wangu popote mlipo muilinde amani yetu”

Waziri Mkuu amesema amani ni miongoni mwa neema kubwa sana kwa binadamu na ndio maana wote wanamtambua Mwenyezi Mungu, hivyo wasiruhusu mtu au kikundi chochote kujaribu kuchafua na kuharibu amani iliyopo nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wahakikishe kuwa chombo hicho kinaendelea kuwaunganisha waislamu bila ya kujali makabila yao, rangi zao au madhehebu yao.

Waziri Mkuu amesema Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar bin Zubeiry ambaye ndiye kiongozi wa Waislamu nchini mara zote amekuwa akisisitiza jambo hilo na kuwataka waislamu popote walipo watambue kuwa hicho ni chombo chao.

“Ni muhimu sana kwa ninyi wasaidizi wa Mufti mlio kusanyika hapa muhakikishe mnalisimamia hili katika maeneo yenu. Katika hili napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko pamoja Mheshimiwa Mufti kutekeleza nia hiyo njema.”

Amesema ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ni kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kusikiliza maoni, ushauri na  mapendekezo yeyote kutoka kwa viongozi wa dini . ‘Milango iko wazi saa zote ‘

Ameongeza kuwa yeye si mtaalamu sana kama walivyo Masheikh hao lakini anakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani sura Al Imran aya ya 103 yanayosema “ Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote na wala msifarakane”

Mkutano huo umehudhuriwa na  Sheikh Mkuu wa Mufti wa Tanzania Sheikh Zubeir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Masheikh na viongozi wa BAKWATA wa mikoa na wilaya zote Tanzania.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zubeiry wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma kufungua mkutano wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Machi 31, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) baada ya kufungua mkutano wao kwenye ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma, Machi 31, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.