Sunday, December 18, 2016

WANANCHI WOTE WAFANYE MAZOEZI NCHI NZIMA KILA JUMAMOSI YA PILI YA KIALA MWEZI ILI KUEPUKA MAGONJWA.

viungo
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa pili kushoto akishiriki mazoezi ya viungo katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam kushoto ni Rais Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi,wa pili kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa na Naibu wake Dkt. Hamis Kigwangalla kulia .
 wqq
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongea na wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
...................................
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuandaa siku ya mazoezi ya hiari kila ifikapo jumamosi ya pili kila mwezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi Mhe. Samia Suluhu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuandaa utaratibu wa mazoezi pamoja na wananchi kila mwezi ili kuweka jitihada za kukinga magonjwa hayo.

“Watanzania tupende kufanya mazoezi mara kwa mara ili tuweze kuepuka magonjwa yasioambukiza yakiwemo Kisukari, magonjwa ya moyo, saratani ambayo yanasababishwa na mafuta mengi mwilini ”alisema Mhe. Suluhu.

Aidha Mhe. Samia amewaagiza wakuu wa Mikoa na Halmashauri kurudisha viwanja vyote vya michezo vilivyovamiwa ili watu wapate kufanya mazoezi na wasiokua na viwanja watafute maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo.

Mbali na hayo Mhe. Samia amewataka watendaji wa Wizara ya Elimu nchini kuandaa mpango endelevu na viwanja vya michezo kwa wanafunzi ili kuendeleza kampeni hii kuanzia mashuleni kwa ajili ya kujenga msingi bora wa michezo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa asilimia  27 ya vifo vinavyotokea  nchini vinasababishwa na magonjwa yasioambukiza.

Aidha Waziri Ummy ameongeza kuwa mkakati huo ukifanikiwa na kuwafanya wananchi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi utasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi zinazoelekezwa kwenye tiba pamoja na kuokoa maisha ya watanzania wengi kutokana na magonjwa hayo.

Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi amesema kuwa mazoezi ni ya maana sana katika kujenga mwili wa binadamu na nguvu kazi ya taifa kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.

Mbali na hayo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Annastazia Wambura amesema kuna haja ya vifaa vya michezo kushuka bei ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama kwa ajili ya kushiriki michezo.

Aidha Bi. Wambura ametoa onyo kwa mtu au kampuni yeyote kuuza vifaa vya michezo vilivyoandikwa “HAVIUZWI” ili kuweka urahisi wa wananchi kufanya mazoezi kwa wingi nchini.

Kampeni hiyo ya kufanya mazoezi ilioandaliwa na Wizara ya Afya  imezinduliwa rasmi leo ili kupambana na magonjwa yasioambukiza kama vile kisukari, Shinikizo la Damu, uzito uliozidi kiasi , utapia mlo na magonjwa ya moyo.
wqq-sam
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa pili kulia akiwaongoza Rais Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi katikati, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  kulia na Naibu wake Dkt. Hamis Kigwangalla kushoto na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kutembea kutoka viwanja vya leaders hadi Biafra katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
 eq
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katikati akiwaongoza baadhi ya viongozi wa kitaifa na wananchi kufanya mazoezi katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
 weqq
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katikati akiwa katika picha ya pampoja baadhi ya viongozi wa kitaifa na wananchi walioshiriki kwenye uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
 weqw
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa taifa na kamati ya magonjwa yasioambukiza (NCD) walioshiriki kwenye uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasioambukiza nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.


Friday, December 16, 2016

WALIOUZA KIWANJA CHA SHULE WACHUKULIWE HATUA-MAJALIWA

unnamed
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na watumishi wa   serikali na Halmashauri  ya Wilaya ya  Ngorongoro uliopo  kwenye ukumbi wa halmashauri  hiyo iliyopo Wasso  Desemba 15, 2016.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa waadilifu  wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za kisheria walizochukua kwa wahusika.

“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.

Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.

Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.

Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

(mwisho) 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.  


AZAM FC YATAMBULISHA WACHEZAJI WAPYA CHAMAZI.

kikosi-aza
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imetambulisha nyota wapya sita waliosajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo uliofungwa usiku wa kuamkia leo.

Zoezi hilo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Azam FC walikuwemo kwenye zoezi hilo, wakongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu Abdul Mohamed, Meneja wa timu, Phillip Alando, Ofisa Habari, Jaffar Idd pamoja na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Wachezaji wapya waliotambulishwa ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars), kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports), mawinga Enock Atta Agyei (Medeama), Joseph Mahundi, washambuliaji Yahaya Mohammed (Aduana Stars) na Samuel Afful (Sekondi Hasaacas).

Akizungumza wakati akitambulisha nyota hao, Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, alisema kuwa Yakubu ameingia kuziba pengo la Pascal Wawa aliyeondoka baada ya kumaliza mkataba wake huku pia Mpondo akiongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mkabaji baada ya kuondoka kwa wachezaji wawili Michael Bolou na Jean Mugiraneza.

Alisema kuwa wengine walioingia kwenye usajili huo ni washambuliaji Afful na Yahaya ambaye ni mzoefu, wakiziba pengo la Gonazo Ya Thomas na Francisco Zekumbawira walisitishiwa mikataba yao.

Hivyo orodha ya wachezaji wapya wa kigeni wa Azam FC inayotambulika hivi sasa, ni mabeki Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Yakubu, kiungo Mpondo, kiungo mshambuliaji Agyei, washambuliaji Yahaya, Afful.

Aidha Azam FC imewatoa kwa mkopo wachezaji wake saba wa kikosi cha vijana waliojiunga na timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ambao ni Omary Wayne, Joshua Thawe (Friends Rangers), Rajab Odasi, Yohana Mkomola (Ashanti United), Abbas Kapombe, Godfrey Elias (Polisi Dar es Salaam) na Mohamed Sadalah (Mbeya Warriors).

Matarajio makubwa VPL, CAF
Kawemba pia alisema kuwa wanatarajia mabadiliko makubwa kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), katika kucheza mpira, kiwango, matokeo ya uwanjani kutokana na aina ya usajili uliofanywa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zeben Hernandez, kupitia mapendekeo aliyoyatoa kwa uongozi.

“Kwa sababu timu ni ya kwake na mapendekezo kayaweka mwenyewe na usajili kafanya mwenyewe na sasa yupo na ameuona mpira ulivyo hapa nchini,” alisema.

Katika hatua nyingine, bosi huyo alisisitiza kuwa bado malengo yao makubwa ni kutwaa ubingwa wa ligi hiyo na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) pamoja na kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Zeben na matarajio makubwa
Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, akizungumza kwa upande wake alisema kuwa jambo kubwa walilopanga kurejea nalo kwenye mzunguko wa pili ni kubadilisha mpira uliokuwa ukichezwa kwenye mzunguko wa kwanza pamoja na matokeo yaliyokuwa yakipatikana.

“Mimi na benchi langu la ufundi tunatambua ya kuwa Azam FC si timu ndogo ni timu kubwa, malengo ambayo yapo kwa upande wetu ni kubadilisha mpira uliokuwa ukichezwa raundi ya kwanza pamoja na kubadilisha matokeo yaliyokuwa yakipatikana raundi ya kwanza na ndio maana tumeleta wachezaji wa kuongeza nguvu.

“Kikubwa tutajitahidi kadiri iwezekanavyo kuweza kupata ushindi na ikiwezekana si tu kwenye ligi bali hata michuano mingine tunayoshiriki, jitihada tunazofanya kama benchi la ufundi tunaamini ya kuwa Azam FC itafika kwenye sehemu moja nzuri kuliko ambavyo watu wanafikiria,” alimalizia.

LIGI KUU TANZANIA BARA YAREJEA,YANGA UHURU KESHO ‘TFF YATOA ONYO KWA VILABU’

yangaaaaaaaaaaaaaaaaaa
Duru la Pili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Desemba 17 kwa michezo minne kabla ya michezo mingine minne kufanyika siku ya Jumapili Desemba 18, mwaka huu.

Katika mechi za kesho, Mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans SC ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Licha ya kwamba mwenyeji wa mchezo huo ni JKT Ruvu ambayo uwanja wake wa nyumbani mara nyingi huwa ni Mabatini ulioko Mlandizi, lakini kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi Kuu Bara, mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba, Young Africans na Azam FC, hufanyika Uwanja wa Uhuru.

Michezo mingine ya kesho ni Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting ya Pwani itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani ilihali Mwadui ya Shinyanga itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.

Jumapili, Desemba 18, mwaka huu Mbao FC ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Ndanda itakuwa mwenyeji wa Vinara wa Msimamo katika Ligi Kuu ya Vodacom, Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

African Lyon ya Dar es Salaam itaikaribisha Azam FC pia ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru jijijini siku hiyo ya Jumapili wakati Majimaji ya Songea itakuwa Mbeya kucheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limetoa masharti kadhaa likitaka klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kufuata. 

Masharti hayo, ni kwa klabu kutumia makocha wenye sifa kwa mujibu wa kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom. Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) na kwa mujibu wa kanuni hiyo, makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi la Ligi kuu kwa msimu huu wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.

Pia kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza na Pili, masharti ni lazima makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo ambazo zimeanishwa kwenye kanuni za ligi husika.

Kadhalika, tunaagiza klabu kutotumia wachezaji wa kigeni au makocha kama hawana vibali vya ukaazi na kufanya kazi kutoka Idara ya Uhamiaji nchini iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.