Sunday, October 16, 2016

ATEMBEA KWA MIGUU SIKU 21 ILI KUMUONA WAZIRI MKUU DODOMA BAADA YA KUNYNG'ANYWA SHAMBA LAKE.

ah
Mkazi wa Kilindi, Tanga Angela Basso  , aliyetembea kwa miguu kwa muda wa siku 21  pamoja na Watoto wake Janeth Peter (9) na Happy Peter (7) kuja  Mkoani Dodoma kuonana na Waziri mkuu ili kupeleka malalamiko yake ya kudhulumiwa mashamba yake ya  hekari 30 na kuchomewa nyumba.
.........................................


MKAZI wa Kilindi mkoani Tanga, Angela Basso, akiwa na watoto wake wawili Happy(7) na Janeth Peter(9), amelazimika kutembea kwa miguu kwa siku 21 hadi mkoani Dodoma kwa lengo la kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili amsaidie kurudishiwa hekari 30 za mashamba yake aliyozoporwa.

Basso alifika mjini Dodoma akiwa na watoto wake hao, ambapo alisema aliona ni vyema kwenda Dodoma kuonana na Waziri Mkuu kutokana na kuporwa mashamba na kuchomewa nyumba yake katika kijiji cha Kwendigole wilayani Kilindi na wanaume wawili ambao waliojitokeza kwa nyakati tofauti wakidai ni maeneo yao.

Alisema alipita hatua zote zinazotakiwa kuomba mashamba, ambapo awali alipatiwa  hekari 10 na kijiji na akazifanyia shughuli za kilimo na kujenga nyumba yake ya kuishi, lakini baada ya kwenda kujifungua alikuta mazao yamefyekwa na yeye kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.

Mwanamke huyo alisema baada ya kunyang’anywa alifikisha malalamiko yake kuanzia uongozi wa kijiji hadi wilayani na baadaye akapatiwa eneo jingine la hekari 20, lakini alijitokeza mtu mwingine na kudai eneo hilo ni mali ya kanisa, licha ya kumiliki kihalali eneo la Hembekali.

“Nilikwenda kushtaki kwa serikali ya kijiji, kata na baadaye kwenda kwa mkuu wa wilaya ambako iliamuliwa nirudishiwe mashamba yangu, lakini hawakufanya hivyo mwisho wa siku nikafukuzwa kabisa kuishi kwenye eneo hilo,” alisema Basso.

Mwanamke huyo alisema baada ya kutimuliwa alianza kuishi maisha yake kituo cha mabasi Muheza na baadaye alifukuzwa kituoni hapo kwa madai watu hawaruhusu kulala ama kuishi hapo na ndipo akaamua kuanza safari ya Dodoma baada ya kusikia Waziri Mkuu amehamia Dodoma.

Akisimulia machungu ya safari yake, Basso alisema akiwa njiani walikuwa wakila mahindi ya kukaanga na maji ya kunywa na kulala porini muda mwingine giza linapowakuta katikati ya pori.

“Naomba kusaidiwa jamani nimeanza kufuatilia tangu mwaka 2012 lakini bila mafanikio jambo ambalo limechangia familia yake kusambaratika kutokana na kukosa pa kuishi huku watoto wangu hawa wakikosa elimu kwa kutangatanga,”alisema Mwanamke huyo.

Basso aliomba Serikali itende haki ili yeye aweze kupata haki yake ya kurejeshewa mashamba yake na kurudi katika eneo hilo ili watoto wake wawili wapate nafasi ya kusoma.

Mwanamke huyo alisema kwa sasa amekuwa kama mkimbizi kutokana na kukosa hana mahali pa kuishi huku mumewe naye akiikimbia familia yake baada ya kuporwa ardhi hiyo ambayo ilikuwa kama kitega uchumi chao.

TAMKO LA WAZIRI UMMY MWALIMU KUHUSU HUDUMA ZA MATIBABU KWA WATU WENYE ULEMAVU NA WASIO NA UWEZO.

ummy-mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu anapenda   kutoa ufafanuzi kuhusu Tamko la Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kuhusu makundi ya wananchi wanaostahili kupata msamaha wa matibabu.

Aidha, baadhi ya Vyombo vya habari vimenukuu maelezo  ambayo yametolewa na mwenyekiti wa SHIVYAWATA kuhusu  Makundi yanayostahili kupata msamaha wa Matibabu nchini.

Kutokana na Maelezo hayo, napenda kutoa ufafanuzi ufuatao;  Sera ya Afya ya Mwaka (2007) inatambua kuwa wapo wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzifikia huduma za Afya  wakiwemo  watu Wenye Ulemavu.

Aidha, Kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu  Na.9/2010 ambayo, pamoja na mambo mengine, Sheria inabainisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wana haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za Afya.

Kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Afya (2007) na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu(2010) Wizara yangu inatambua na  itaendelea kuhakikisha kwamba Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kugharamia  huduma za Matibabu wanapatiwa Msamaha wa Matibabu katika Ngazi zote kuanzia Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Mikoa na Hosptali za Rufaa.

Pia kwa kutambua umuhimu wa huduma ya Afya kwa Wananchi wote, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika mchakato wa kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo Watu Wenye Ulemavu kupata Kitambulisho cha Bima ya Afya.

Hatua hii itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu Wenye Ulemavu katika kuzifikia huduma za Afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.

Naomba kuchukua fursa hii kuwahakikishia ndugu zangu Wenye Ulemavu kuwa wanayo haki ya kupata huduma za matibabu katika ngazi zote.

Aidha, Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha  makundi maalum  wakiwemo watu Wenye Ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za Matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika  vituo  vyote vya kutolea huduma za afya.

Natoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za  Mitaa kuwatambua Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha Kitengo cha Huduma za Ustawi wa Jamii katika  vituo vya kutolea huduma za Afya ili viweze kuwatambua  na kutoa msamaha kwa watu wenye ulemavu wasio na uwezo ili  waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu wa fedha.

Aidha,  ni marufuku kwa Mtumishi yeyote wa Sekta ya Afya kuonesha vitendo vyovyote vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu Wenye Ulemavu wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za  afya. 

Mtumishi atayethibitika kuonesha kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za Afya kwa kufanya vitendo vya vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maaalum ikiwemo  watu wenye ulemavu  atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Vile vile, ninawataka watoa huduma wote kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu wanapofika  hospitali. Wapatiwe huduma haraka ili kuwapunguzia usumbufu kutokana na mahitaji yao ya kimwili.

Kama ambavyo tumefanya kwa Wazee niwaagiza kila kiongozi ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya kwanza watu wenye ulemavu tukijifunza kwa jinsi tulivyofanya na kufanikiwa katika eneo la kuhudumia wazee.

Watu wenye ulemavu ni wenzetu, watoto wetu, ndugu na jamaa zetu. Tuwahudumie kwa upendo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine.

Imetolewa na
MHE. UMMY A. MWALIMU (Mb.)
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto.
15/10/2016

Saturday, October 15, 2016

KIJANA ANAEDAIWA KUWA NI PANYA ROAD AUWAWA DAR ES SALAAM.

Wananchi wakiangalia mwili wa kijana anayedaiwa kuwa ni wa kundi la kihalifu la panya road aliyeuawa baada ya kufanya uhalifu maeneo ya Mbagala Zakhem Dar es Salaam leo. Katika tukio hilo vijana wengine wawili walipoteza fahamu kutokana na kipigo cha wananchi.
...............................


WANANCHI wa Mbagala sabasaba wamemuua kwa kumshambulia kwa mawe na kisha kumchoma moto kijana mmoja anayedaiwa kuwa ni mharifu wa kundi la panya road ambaye alikuwa na wenzake zaidi ya 15 ambapo wawili kati yao walipoteza fahamu kutokana na shambulio hilo.

Tukio hilo la kushambuliwa kwa panya road hao lilitokea majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mbagala Sabasaba baada ya vijana hao kukurupushwa walipokuwa wakikimbia walipokuwa wakifanya uhalifu maeneo ya sabasaba Magengeni na Mbagala Zakhem.

Polisi waliofika eneo la tukio walilazimika kutumia risasi za moto kuwatawanya wananchi ili waweze kuuchukua mwili wa kijana huyo ambaye hakufahamika jina lake.

Akizungumza na mtandao wa www.habari za jamii.com mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Khalfan alisema usalama wa wananchi upo mashakani kufuatia kundi hilo la panya road.

“Hawa panya road walikuwa zaidi ya 15 wakitokea Mbagala Zakhem ambako walikuwa wakikimbizwa na wananchi baada ya kufanya uhalifu na walipofika hapa Sabasaba walizingirwa na wananchi ambapo watatu kati yao walianza kushambuliwa na mmoja kupoteza maisha baada ya kuchomwa moto ” alisema.

Alisema vijana wawili kati yao walijeruhiwa vibaya na kupoteza fahamu lakini wenzao wengine walifanikiwa kukimbia kuelekea maeneo ya Yombo Dovya huku wakiahidi kurudi kulipiza kisasa kufuatiwa kuuawa kwa mwenzao.

Mkazi mwingine wa Mbagala kwa Mangaya aliyejitambulisha kwa jina la Seif Mwarami alisema vijana hao wataendelea kuuawa na wananchi kwa kuwa kila wanapokwenda kutoa taarifa polisi hawachukuliwi hatua yoyote badala yake uachiwa na kurudi mitaani kuendeleza uhalifu wao” alisema Mwarami.

Aliongeza kuwa kutokana na kuwa na umri mdogo wanashindwa kupelekwa kwenye mahakamani kutokana na kulindwa na sheria ya utoto jambo linalowatia hasira wananchi na kuamua kujichulia hatua mkononi na kuanza kuwaua.

Alisema vijana hao wamekuwa wakitokea maeneo ya Kitunda, Moshi Baa na Yombo kwenda kufanya uhalifu maeneo ya Mbagala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Gilles Muroto alipopigiwa simu  ili kuzungumzia tukio hilo alisema alikuwa kwenye mkutano hivyo apigiwe baadae.

Hata hivyo jeshi la polisi mara kadhaa limekuwa likikataa kuwepo kwa kundi hilo la Panya Road likieleza kuwa wao wanawahesabu kama walivyo wahalifu wengine wa matukio ya ujambazi na mengine.