Saturday, October 8, 2016

WAZIRI WA FEDHA DKT. MPANGO ASEMA TANZANIA ITAENDELEZA KILIMO NA UTALII

jem1
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika Louis Rene Peter Larose (hayupo Pichani), makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington DC, Marekani, kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James.
........................................


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini.

Waziri Mpango ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.

Amesema kuwa kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na  thamani ya mazao ya wakulima.

Kuhusu sekta ya Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.

Eneo jingine alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa haraka.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja na miradi mingine, itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini “Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Mimi nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama kuzidi hadhi ya Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo zikisimamiwa vizuri zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.

Ameitaka Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha malengo yake ya maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba anaongoza kundi la nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.

Mkurugenzi huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na ametoa pole kwa nchi hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.

Ameahidi kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti na kuishauri nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya matetemeko pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa majanga kama hayo.


UJENZI WA MSIKITI BOKO BEACH, MILIONI 3 ZAPATIKANA, INAHITAJIKA MILIONI 550.


 
Diwani wa kata ya Bunju, Kheri Nasoro alipokuwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiri.
....................................................

Harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti katika mtaa wa Boko beach imefanikisha kukusanya milioni tatu na laki mbili, 3,200,000/= ikiwa ni pesa taslimu pamoja na ahadi huku Diwani wa kata ya Bunju Kheri Nasoro, akiwa amechangia kiasi cha shlilingi milioni moja katika ujenzi huo wa Msikiti.
Akizungumza katika Harambee hiyo iliyofanyika katika eneo linalotarajiwa kujengwa msikiti mtaa wa Boko beach Diwani wa kata Bunju Kheri Nasoro amesema atashirikiana na uongozi wa Swafatul mukarama ambao ndio wasimamizi wa ujenzi huo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
Alisema wailsamu wanapaswa kutambua kuwa jambo hilo ni lao  na kwamba kila mmoja ajitolee kulingana na uwezo wake ili kufikia malengo.
Katika harambee hiyo mada za umuhimu wakutoa ziliwasilishwa ambapo Ustadhi, Hashim Rajabu kutoka Masjid Fatmat Zaharaa Boko, alisema waislamu wanapaswa kutambua kuwa kutoa katika njia ya kheri ni kujiwekea akiba ambayo itamsaidia mwenyewe siku ya malipo.
Akinukuu Hadithi ya  Mtume  Muhammad Swalallaahu Alayhi Wasallama, Ustadhi, Hasim alisema ''Mwenye kujnga msikiti, Mwenyezimungu atamjengea nyumba peponi'' hivyo aliwataka waislamu kukimbilia kheri hiyo kwaajili ya kutengeneza Akhera yao.
Nae Ustadhi Omari Jumakutoka masjid Rrahmani Tegeta, alisema swala la kutoa katika njia ya Mwenyezimungu linahita imani na wala si kipato kikubwa kama ambavyo wengi wanadhani.
Ustadhi Omari alitolea  mfano wa baadhi ya  matajiri wanaodhamini mashindano warembo na michezo ya mpira kwa gharama kubwa huku wakiwa hawana habari na  dini ya Allaah katika kuipigania.
Aliongeza kwa kusema kuwa swala la kutoa  katika njia ya mwenyezimungu ni  jihadi ndiyo mana katika  aya kadhaa  ndani ya Qurani Mwenyezimungu amesema kupigana jihadi kwa mali zenu na nafsi zenu, hii inonesha uzito wa  kutoa hali iliyopelekea  kuwekwa katika darja ya jihadi.
 Aliendelea kwa kusema kuwakila neema  itaulizwa, hivyo muislamu asidhani kwakumiliki kwake fedha anayo fursa ya kutumia anavyotaka, bali anapaswa  kutumia fedha kwa mujibu Allaah anavyotaka kwakuwa  kwake yeye zimepita kama  wakala hivyo ataulizwa namna alivyozitumia.
Akifunga  Harambee  hiyo, katibu wa Swafatul Mukarama Abduli Said Shomari alisema katika siku ya kwanza ya harambee hiyo wameweza kukusanya kiasicha shilingi mioni 3  na laki  mbili ikiwa fedha taslimu pamoja na ahadi.
Katibu huyo ametoa wito kwa waislamu kuendelea  kuchangia ujenzi huo wa  msikiti ambao utagharimu shilingi  milioni mia tano na arubaini na saba, laki moja themanini na nne mia sita na tano, hadi kukamilika kwake, 547,184,615/=
 Aidha, alitaja namba kwa watakaokuwa tayari kuchangia wanaweza kuchangia kupitia tigo pesa 0673 976336, Airtel money 0682982111, au akaunti benki, 003140405030001 Benki  ya Amana, akauti zote hizo zinajulikana kwa jina la Masjid Swafatul-Mukarama.

Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa namba  0784070891 katibu wa Bodi amba 0713422774 Mwenyekiti namba 0713326287.

Friday, October 7, 2016

MWANAFUNZI WA TASUBA AZAWADIWA CHETI NA HUNDI KUTOKA BODI YA FILAMU TANZANIA.

unnamed
Bodi ya Filamu Tanzania leo imemkabidhi cheti na hundi yenye thamani ya shilingi Laki Mbili mwanafunzi Omary Maganga aliyefanya vizuri kwenye masomo ya filamu na runinga kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA).

     Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ofisi za bodi hiyo ambapo Afisa Uhusiano na Mawasiliano Abuu Kimario alimkabidhi cheti hicho na hundi kwa niaba ya Katibu Mtendaji Joyce fisoo.

     Baada ya kukabidhiwa zawadi zake bwana Maganga aliishukuru Bodi hiyo ya filamu kwa kutambua juhudi za wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo yao. Pia ameziasa taasisi zingine za Serikali na zisizo za kiserikali kuwatambua wanafunzi wanaofanya vizuri kwani kwa kufanya hivyo kunaongeza morali na ushindani.

     Wakati huo Afisa Uhusiano na Mawasiliano Abuu Kimario kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa bodi hiyo ametoa ahadi ya kuendelea kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo yenye uhusiano na tasnia ya filamu.

Kwa sasa Bodi ya Filamu Tanzania iko kwenye utekelezaji wa programu ya kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya tasnia ya filamu nchini. Program hii ilianzishwa ikiwa na lengo la kukuza ubora wa filamu za Kitanzania.

MADEREVA WA MAGARI YABEBAYO MCHANGA WAITISHIA TANROADS PWANI

MADEREVA wa matipa ya mchanga ,wanaotumia barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro, wamefanya mgomo baridi ,kulalamikia wakala wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani,unaowakamata kutokana na kutofunga mchanga vizuri na kuwapiga faini ya sh.500,000.

Madereva hao waliweka mgomo huo katika eneo la Tamco ambapo ndipo watendaji wa wakala huo walikuwa wakiwasimamisha kwa ajili ya kukagua wale waliojaza mchanga hali inayosababisha kuchafua miundombinu ya barabara.

Dereva Martine Magari na Emmanuel Shao,walisema ni kweli wapo madereva wasiofunga vizuri maturubai ya magari yao lakini tatizo kubwa ni kukosa elimu ya kufunga kwa ubora.

Shao aliziomba idara ama mamlaka husika kutoa elimu juu ya sheria mbalimbali kwani inakuwa sio rahisi kuelewa sheria zote zinazotungwa bila kupatiwa elimu ya kutosha.

“Unaona fuso dogo kama lile,huwezi amini ni sh.500,000 kikweli ni kubwa ,sasa unakuta tunalalamika kutokana na kwamba hatujui lolote kuhusu sheria zao”
“Halafu hatujafundishwa kufunga hooks wanavyotaka wao wakala wa barabara,kila mtu anaufungaji wake lakini endapo watatuelewesha vizuri haina shida.

“Sasa wao wanapanda juu ya gari na kuchokonoa  chokono matokeo yake ndio inakuwa shida ,mchanga unamwagika”alisema Shao.

Magari aliutaka wakala huo kukagua kwa macho na sio kupekenyua maturubai kwa kuingiza mikono kwani kwa kufanya hivyo ni lazima mchanga mwagike.

“Madereva pia wamekasirika kwa hilo huwezi kukagua hadi uingize mikono ,kwakuwa mikono inasababisha mchanga kumwagika halafu unatozwa hela yote hiyo”alifafanua Magari.

Kwa mujibu wa kaimu meneja TANROADS mkoani Pwani,injinia Yudas Msangi,alisema wapo kwenye operesheni ya kukagua magari ,kwa kufuata sheria ya barabara ya mwaka 2007 namba 13 kifungu namba 46C, inayokataza kuchafua barabara.

Alieleza kuwa hakuna anaewaonea madereva hao ,kwani wanatambua vilivyo kuhusu sheria hiyo na mara kwa mara huwa wakielimishwa kuacha tabia ya kuzembea kufunga mchanga vizuri.

Injinia Msangi alisema,wanatoa muda hadi jumatatu ijayo zoezi hilo litaendelea ili kudhibiti uchafuzi huo wa miundombinu ya barabara.
Alisema wanatakiwa wasijaze mchanga kwakuwa unaathiri matairi ya magari mengine yanayopita,kusababisha ajali ,kufukia mifereji na kufuta alama za barabarani na hatimae kuipa mzigo wakala huo.

Injinia Msangi alisema lengo ni kuacha kumwagwa mchanga na kufunga matipa ya mchanga kwa ubora ili kuepusha matatizo na kuiondolea hasara TANROADS.

Aliwataka madereva wa matipa ya mchanga kuacha kudharau sheria zilizopo ili kuepuka migongano isiyo na tija.

Awali kamanda wa usalama barabarani,Abdi Issango ,alifika eneo la tukio na kuzungumza na madereva hao ,uongozi wa tanroads mkoa,akiwemo kaimu meneja,msaidizi wake pamoja na meneja wa barabara mkoa mama Urio.

Alisema ni kweli madereva wengi wamekuwa hawafungi vizuri mchanga kwa kutumia kifungio(hooks)kwenye maturubai ili kuzuia mchanga usimwagike.

Hata hivyo kamanda Issango,alisema kwa kushirikiana na wakala wa barabara mkoani humo,wameamua kutoa muda ili kurekebisha mapungufu yaliyopo ambapo kuanzia jumatatu atakaekiuka maelekezo yaliyotolewa atalipa faini ya sh.500,000.

Akizungumzia kiwango cha faini kinacholalamikiwa,alieleza kila idara ina sheria zake, kwa usalama barabara ukikiuka sheria adhabu yake ni sh.30,000 lakini kwa Tanroads ni 500,000  na kutoingia kwenye mizani faini zake huwa ni mil.2 .

Baada ya kamanda huyo kuzungumza na pande hizo mbili ,madereva hao walitawanyika na kuridhia maelekezo waliyopatiwa sambamba na kukubaliana kuanza kwa zoezi hilo wiki ijayo.