Tuesday, August 16, 2016

VYAMA VYA MICHEZO NCHINI WAMETAKIWA KUIGA MFANO WA AATanzania.

Katibu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja.



Vyama vya michezo nchini vimeaswa kuthamini na kutoa shukrani baada ya kumaliza mashindano kwa lengo la kuimarisha ushirikiano pamoja na kuwapa moyo wanamichezo na wadhamini wa mashindano.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi na vyeti kwa washiriki, wadhamini na waandishi wa habari waliofanya vizuri katika kupiga picha na kuandika habari za Mashindano ya Magari yaliyofanyika Julai 8 hadi 10 wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kusimamiwa na Taasisi ya Automobile Association Tanzania (AATanzania).

“Vyama vingine vya michezo nchini vinapaswa kuiga mfano wa AATanzania wa kutoa shukrani baada ya mashindano, hili ni fundisho kubwa, wanapaswa kuthamini na kutambua msaada wa kufanikisha mashindano yeyote wanayoyaandaa” alisema Kiganja.

Katibu huyo aliongeza kuwa, yanafanyika mashindano ya michezo mbalimbali nchini yakiwa lengo la kuburudisha na kuelimisha jamii, ni wajibu wao kuiga mfano uliouoneshwa na AATanzania wa kutoa shukrani baada ya mashindano.

Naye Rais wa AATanzania Bw. Nizar Javan ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na BMT ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashindano hayo yaliyofanikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Bw. Nizar aliongeza kuwa mashindano hayo yaliisha salama bila ya kutokea ajali yeyote hatua ambayo inaendana na kauli mbiu yao inayosema “Usalama kwanza”.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Afisa Mnadhimu Kikosi cha Usalama Barabarani (SACP) Fortunatus Musilimu amewashukuru AATanzania kusimamia, kuandaa na kufanikisha mashindano hayo ambayo yamezingatia usalama wa washiriki wa mashindano na magari yaliyotumika.

Katika kuitangaza Tanzania kupitia mchezo wa magari, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Zamaradi Kawawa amewasihi waandaaji wa mashindano hayo kuebdelea kuhamasisha wachezaji wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi na kushiriki mashindano hayo, hatua ambayo itasaidia kuongeza ushindani na kuitangaza Tanzania Kimataifa kwa kuwa mchezo huo unashirikisha mataifa malimbali.

Waandishi wa habari waliopata vyeti na zawadi kwa kuuhabarisha umma juu ya mashindano hayo ni pamoja na Mohamed Ugassa kutoka gazeti la The Guardian, Jimmy Tara wa ITV, Brown Msyani kutoka gazeti la Citizen, Timzoo Kalugira na Michael Maluwe kutoka Azam Tv, Nasongelya Kilyinga gazeti la Daily News na Miguel Suleyman ambaye ni wandishi wa habari wa kujitegemea.

Pamoja na waandishi hao, wadau waliopewa zawadi kwa kutambua mchango wao katika kufanikisha mashindano hayo ni Jeshi la Polisi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo Tanzania na Hoteli ya Southern Sun.

Mashindano hayo ya magari yaliyofanyika nchini yanatambuliwa na Shirikisho la Michezo ya Magari Duniani (FiA) ambayo AATanzania ni mwanachama.

TANZANIA INA VIVUTIO VINGI KATIKA HIFADHI ZA TAIFA.



 
Huyu ni aina mojawapo ya chura ambaye hapatikani mahali popote duniani isipokuwa katika Hifadhi ya Mazingira asili ya Mkingu ambaye ni mojawapo ya kivutio cha utalii katika hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii)

Baadhi ya sehemu za kuvutia katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo ni njia mojawapo inayotumiwa na watalii kwenda kijiji cha Maskati kuangalia vivutio vya Utalii vinavyopatikana katika Hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii).

Maporomoko Lusingizo yenye mita zaidi ya 50 yaliyoko katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo ni mojawapo ya kivutio cha Utalii katika Hifadhi hiyo, Hadi hivi sasa kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha umeme katika kivutio hicho cha utalii. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii).
.....................................................................................................


Hifadhi asili ya Mkingu ipo wilaya ya Muvemero Mkoani Morogoro. Hifadhi hii ni eneo muhimu sana kiutalii kutokana na upekee wake wa maisha ya viumbe, mimea pamoja na maisha ya binadamu kiujumla.

Hifadhi hii ina ukubwa wa hekta 26, 334 na imezungukwa na vijiji vitano ambavyo vipo ndani ya kata sita na tarafa mbili.

Tangu kuanzishwa kwake Hifadhi hii mwaka 2016, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) imekuwa ikihudumia hifadhi hii kutokana na kuwa na mimea na viumbe ambavyo ni vivutio pekee vya Utalii nchini ambavyo havipatikani mahali popote duniani.

Mhifadhi Mkuu wa Mazingira asili ya Mkingu, Bw. Abeid Kindo anasema kutokana na sifa hizo za kipekee zinazopatikana katika Hifadhi hiyo imekuwa na umuhimu wa aina mbili ambao ni umuhimu wa kidunia na umuhimu wa kitaifa, Katika umuhimu wa kidunia upo katika viumbe, mimea na wanyama.

Anasema hifadhi hii ina wanyama wenye uti wa mgongo 392 kati ya hao 32 hawapatikana mahali popote duniani isipokuwa ni Mkingu tu yaani ni endemic species. Aidha , alisema kuna vyura na ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo tu.

Bw. Kindo anasema kuwa hifadhi hiyo imejaliwa kuwa na wanyama wanaotambaa 42 kati ya hao 14 hawapatikanimahali popote duniani isipokuwa Mkingu tu pamoja na aina ya ndege 214 kati ya hao ni aina nne ndio wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Mbali na hiyo, Anasema kuwa ndani ya hifadhi kuna msitu unaotumika kwa masuala ya mila za Waluguru kuwa eneo hilo ni zuri sana amabalo nalo ni kivutio cha utalii ndani ya msitu huo

Mbali ya kupatikana kwa wanyama na mimea katika Hifadhi hiyo Bw, Kindo anaeleza kuwa kuna pango la Malolo ambalo wenyeji wa Mkindo wana historia kubwa ya pango hilo ambalo wenyeji hawataweza kusahau kwani kuna mwanaume mmoja aliiba mke wa Mtu akaishi naye ndani ya pango hilo kwa muda wa miaka 3 bila kujulikana kijini. Pango hilo lina vyumba mithili ya nyumba iliyojengwa.

Pia anasema kuwa nadni ya hifadhi hiyo kuna pango ambalo ukikaa nje kuna upepo unaotoka ndani unapuliza hiyo ni ishara tosha kuwa humo ndani ndani kuna uhai. Anabainisha kuwa hifadhi hiyo ina jiwe lenye alama za nyayo za binadamu, kwato za mifugo ikiwa hiyo ni ishara tosha kuwa maisha ya kale ya binadamu yalianzia ndani ya hifadhi hiyo. .

Aliongeza kuwa mbali ya mapango ndani ya hifadhi hiyo , kuna maporomoko Lusingizo yenye mita zaidi ya 50 , hadi hivi sasa kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha umeme katika kivuto hicho cha utalii.

Pia kuna magofu ya kale ya Wajerumani ambayo waliishi ndani ya hifadhi kabla vita vya pili vya dunia na baada ya kuondoka kwa Wajerumani ilikuwa shule ya msingi ya kijiji cha Mafuta, na baada ya eneo hilo likatangazwa kuwa hifadhi , Shule ile ilitolewa na kujengwa kijijini.

Bw. Kindo anasema licha ya hifadhi hiyo kuwa na vivutio lukuki bado imekuwa ikitembelewa na idadi ya watalii isiyoridhisha licha kwa mwaka jana wameweza kupata watalii 75 kutoka Ujerumani,

‘’Tokea mwaka jana hadi hivi sasa tumeweza kuibua vivutio saba vya utalii na tunaendelea kufanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha tunakuwa na vivutio vingi vya utalii ili tuweze kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi ‘’.alisema Bw. Kindo

Aidha,Alisema Hifadhi hiyo ndio chanzo cha mto Wami, mto Ruvu na Mto Mkingu ambapo maji hayo yamekuwa yakitumika katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo,uvuvi,mazalia na makazi ya mimea na wanyama bila kusahau maji hayo ndiyo hutumika kuwanyesha wakazi wa Dare s Salaam na mikoa ya jirani

Amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali wasisubili watafiti kutoka nje ya nchi kwenda kufanya tafiti katika Hifadhi hiyo badala yake wao wawe mstari wa mbele katika kuvumbua vitu vingi ambavyo vinapatikana katika hifadhi hiyo