Wednesday, August 10, 2016

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUHUBIRI MADHARA YA UJANGIRI KWA TAIFA.







Wito huo umetolewa leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam.

Waziri Maghembe amesema kuwa Viongozi wa dini wakiongeza neno juu ya ujangili wa wanyama hao itasaidia roho za waumini kujua umuhimu wa wanyama hao na kuwatendea mema kwani nao wana haki ya kuishi kama viumbe wengine.

“Katika ibada zetu za jumapili na ijumaa tujitahidi kutoa mahubiri na dua kwa jamii ili kufikisha ujumbe juu ya kuwalinda wanyama hawa na kupambana na ujangili ndani ya nchi yetu”, amesema Waziri huyo.

Aidha amesema kuwa idadi ya tembo mwaka 1990 hadi 1994 walikuwa takribani laki tatu na nusu(350,000), mwaka 2009 walikuwa 45,000 na mwaka jana idadi ya tembo hao walikuwa 55,000 hivyo jamii kwa ujumla imetakiwa kuwalinda wanyama hao.

Mbali na hayo Waziri Maghembe alizitaja faida za wanyama kuwa ni pamoja na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 15.5 na kuweza kutoa ajira takribani Watanzania milioni moja katika Sekta ya Utalii na kusaidia katika mzunguko wa uotaji wa baadhi ya mbegu.

Kwa upande wake Mwandishi wa Kitabu hicho Mchungaji Christosiler Kalata amesema kuwa lengo la kuandaa kitabu hicho ni kuwaelemisha na kuitaka jamii kutunza uumbaji wa Mwenyezi Mungu wakiwemo wanyama.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WILDAID Peter Knights ambao ni wadhamini wa kitabu hicho, ameipongeza Serikali ya China kwa jitihada zake za kupiga marufuku biashara ya uuzaji wa meno ya Tembo hatua hiyo imesaidia kulinda wanyama hao. 

TAMASHA LA DAR FESTIVAL MWEZI SEPTEMBA, LITALENGA KUTANGAZA UTAMADUNI WA KI TANZANIA.



Pichani kati ni Mratibu wa tamasha la Dar  Festival, Faridi Faraji akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani),jijini Dar es Salaam juu ya  tamasha hilo litakalofanyika  mwezi huu katika viwanja  vya viwanja vya leaders club na siku ya pili ndani ya viwanja vya Makumbusho jijini Dar.Kulia ni Diwani wa Kata ya Ilala na kushoto ni  mmoja wa Waratibu wa tamasha hilo, Shaban Kapilima.
.................................................................................................

Na Sara Zuberi


Mratibu wa Tamasha la Dar  Festival, Faridi  Faraji amesema kuwa tamasha hilo jipya litalenga kutangaza na kudumisha utamaduni wa Tanzania,na kuwa tamasha hilo litahusisha michezo ya kiasili kama Bao,Karata ambalo litaenda sambamba na burudani nyingine za ngoma za asili na maonesho ya baadhi ya tamaduni za makabila ya Tanzania.

" Pia tunategemea kuwa na mashindano ya kucheza ,vichekezo na maonyesho ya Muziki kutoka kwa baadhi ya Wasanii" alisema Faridi.

Amesema kuwa kutokana na utafiti inaonyesha watu wengi wamekuwa wakikosa matukio kama haya na, hivyo wanatarajia tamasha hilo litapokelewa kwa furaha kubwa na Watanzania watajitokeza kwa wingi kwani litahusisha watu wa rika mbalimbali.

Akifafanua zaidi faida ya tamasha hilo, Faridi amesema kuwa tamasha hilo litaendeleza umoja wa Watanzania, Burudani kwa Watanzania, kuwakumbusha Watanzania utamaduni wao, kutangaza utamaduni wa Watanzania samnbamba na kusaidia Serikali kupitia sekta ya utalii ili kuongeza pato la taifa.

Faridi ametoa wito kwa wanahabari kulitangaza tamasha hilo ili wadau wajitokeza kwa kulidhamini,hivyo kwa pamoja watakuwa wamesaidia  kudumisha utamaduni wetu na kuisaidia serikali yetu kutunza utalii.




Tuesday, August 9, 2016

MWIGULU NCHEMBA ATEMBELEA KAMBI YA WAKIMBIZI MKOANI KATAVI.



Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Mh.Mwigulu Nchemba leo amewasili mkoani Katavi,na kufanya ukaguzi kwenye kambi ya wakimbizi ya Katumba ambako kulikuwepo na zoezi la uhakiki wa waliokuwa wakimbizi kutoka Burundi na baadae kuamua kuwapa Uraia wa Tanzania mwaka 2009.

Katika ukaguzi huo Mh.Mwigulu amesema kuwa zoezi la uhakiki linafanyika ili kuchunguza mienendo yao na uwepo wao kwenye eneo la Kambi,amesema kuwa kumekuwepo na taarifa za baadhi ya ndugu zetu ambao wamekuwa wakijihusisha na watu waovu,kufanya vitendo vya kibaguzi na kutoka nje ya kambi zao na kwenda nchi jirani bila kibali.

Mh.Mwigulu amesema kuwa mbali ya kambi ya Katumba,pia ametembelea kambi ya Mishamo na kuviagiza vyombo vya usalama na kupitia Seririkali za mitaa kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na vitendo hivyo,amaesema na kuongeza kuwa Tanzania haina tabia za kibaguzi"moja kati ya sifa kubwa ya nchi yetu ni kushinda vita dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote tangu tulipopata uhuru" ,alisema Mh.Mwigulu.

"Natoa rai kwa raia wote tuliowapa kibali cha kufanya kazi,kuishi na kuwa raia wa nchi yetu, waache kujihusisha na vitendo viovu na vya kibaguzi.Hatutawavumilia watu ambao tumewakaribisha kwa nia njema hapa nchini na baadae wahatarishe usalama na amani ya nchi yetu",alisema Mh.Mwigulu.

Mwigulu alibainisha pia kuwa amekutana na Askari wa jeshi la polisi na idara zake zote na pia ametembelea gereza la mpanda ikiwa ni ziara ya kupata uhalisia wa changamoto zinazokabili jeshi la polisi,Magereza,Uhamiaji na zimamoto kwa kila mkoa,ambapo tayari kwa majawabu ya kudumu.