Monday, July 11, 2016

BILIONI 1.3 ZAKUSANYWA DARAJA LA KIGAMBONI NDANI YA MIEZI 2.


 


Jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimekusanywa kutoka Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam kupitia tozo mbalimbali zinazolipwa na vyombo vya usafiri vinavyopita darajani hapo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Prof. Godius Kahyarara wakati akieleza mapato yaliyopatikana kwenye daraja hilo tangu lilipofunguliwa rasmi Mei 14 mwaka huu.

Prof. Kahyarara alisema kuwa fedha hizo zimekusanywa kupitia tozo za magari yakiwemo magari binafsi, magari ya abiria, magari ya mizigo, pikipiki na bajaji zinazopita darajani hapo kila siku. Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa Daraja la Nyerere, Bw. Gerald Sondo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa daraja wana mpango wa kuboresha huduma za malipo ili watumiaji wa daraja hilo waweze kulipa tozo kwa kutumia kadi za kielektroniki.

“Hivi karibuni tunatarajia kuanzisha mfumo wa malipo kwa kutumia kadi za kielektroniki ambapo madereva wa vyombo vya usafiri watakuwa wanatumia kulipa tozo pindi wanapopita darajani” alisema Sondo.

Aliongeza kuwa mfumo huo utapunguza changamoto ya kupokea pesa taslimu mkononi kwa wanaokusanya mapato darajani hapo, hivyo kuondoa usumbufu wa chenji na kuimarisha usalama wa fedha hizo. Aidha, Bw. Sondo alieleza kuwa mfumo huo pia utawawezesha watumiaji wa daraja hilo kulipa tozo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ya kufanya miamala ya fedha kupitia benki na mitandao mbalimbali ya simu.

Alisema kuwa kwa sasa idadi ya magari, pikipiki na bajaji zinazopita darajani hapo ni kati ya elfu 8 hadi elfu 10 kwa siku na wanalipa tozo kulingana na aina ya chombo cha usafiri. Kwa upande wa waenda kwa miguu na waendesha baiskeli hawalipi gharama yoyote wanapopita kwenye daraja hilo.

Akieleza kuhusu usalama wa daraja na watumiaji wake, Bw. Sondo alisema kuwa ulinzi ni wa uhakika kwa saa 24 kila siku kwani kuna askari wa kutosha pamoja na kamera zinazosaidia zoezi hilo. Pia alisema kuwa wanaandaa kanuni za matumizi ya daraja ikiwemo faini za uharibifu, uchafuzi wa mazingira, matumizi mabaya ya njia na lugha za matusi.

VIPANDE VYA MENO YA TEMBO 666 VYAKAMATWA.






Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna Diwani Athuman akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijiji Dar es Salaam leo, kuhusu Jeshi la Polisi kutokubali kuona kundi la watu wachache linatishia usalama wa maisha ya raia na mali zao, Wote watakaobainika kuwa ni wahalifu watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. 


 JESHI la Polisi  nchini kwa kishirikiana na Ofisi za Interpol Kanda ya Kusini Mwa Afrika imefanya operesheni  na kukamata vipande vya meno ya Tembo 666 vyenye uzito wa Kilogram 1279.19 vyenye thamani zaidi ya a Sh. Biloni Nne.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa  Jeshi  la Polisi (CP), Diwani Athuman wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, amesema kuwa vipande hivyo vya tembo yamehusisha watu tisa  kati yao mmoja ni Raia wa Guinea na mwingine ni Raia wa Uganda.

Amesema kuwa katika operesheni Usalama  III wameweza kukamata  vitu mbalimbali kutokana na taarifa za kiitelijensia zilizokusanywa wakati wa matayarisho ya operesheni ya Usalama III, ambapo waliweza kukamata mitambo ya 18 ya kutengenezea gongo pamoja na  lita  za gongo  960  zimekamatwa.

Athuman amesema katika Operesheni  hiyo wameweza kukamata watuhumiwa 265  ambapo baada ya uchunguzi wataobainika  kuhusika na  vitendo vya kihalifu watafikishwa mahakamani mara moja ikiwa namna au nyingine katika kufankisha vitendo vya kihalifu.

Kamishina Othman amesema ametoa rai kwa wanunuzi wa magari nje ya nchi kuwasiliana na ofisi za Interpol za ndani au nje ya nchi magari yanakotoka kwa uchunguzi kabla ya kuyanunua ili kuondoa usumbufu wa kukamatwa mara kwa mara katika operesheni  kama hizi.

Amesema kutokana na operesheni hiyo jeshi la polisi halitakubali kuona kundi la watu wachache linalotishia usalama maisha raia wema na  mali zao na wataobainika kufanya hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria bila kusita.







Sunday, July 10, 2016

TANZANIA YAPATA DOLA MILIONI 500 KUTOKA INDIA KWAAJILI YA MIRADI YA MAENDELEO.



 
India imeipatia Tanzania dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina nchi hizi mbili.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia mgeni wake, Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi.

“Tunaishukuru India ambayo imeonyesha utayari wa kushirikiana nasi kiuchumi katika kilimo, TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,” amesema Rais Magufuli.Rais Magufuli pia amesema ushirikiano wetu na India utatoa fursa kwa Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani katika ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na wafanyabiashara takriban 50 ambao wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.

“India ni mdau wetu mkubwa wa  kibiashara  na uhusiano huu umekuwa ukikua kwani mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani ya  dola za kimarekani milioni 187 mwaka 2005 hadi dola bilioni 1.29 mwaka 2015,”alisema Rais Magufuli.Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha kwa nchi ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua kipato cha wananchi.

Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na miradi ya India ikiwemo mradi unaojulikana kama Making India, mradi ambao unatumia malighafi zinazopatikana nchini na kutumia nguvu kazi ya nchini ambao utapunguza tatizo  la ajira katika Taifa la Tanzania.

Amebainisha kuwa India iko tayari kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya gesi ikizingatiwa kuwa aina mbali mbali za gesi zinazidi kugunduliwa hapa nchini. Katika suala la gesi India iko tayari kutoa utaalamu na wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India , Mhe. Narendra Modi ameishukuru Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na akaahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.Amesema India italeta watu wake, utaalaamu na teknolojia yake kwa Tanzania, jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni kati India na Tanzania.

Waziri Mkuu huyo amemaliza ziara yake ya kiserikali  ya siku mbili nchini na kuondoka kuendelea na ziara katika nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.

INDIA NA TANZANIA ZASINI MIKATABA YA MIRADI YA MAENDELEO.


 


 Serikali ya India na Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.

Mikataba hiyo imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokua akifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mikataba wa kwanza uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Aidha, mkataba wa pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu dola  za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali.

“Lengo letu ni kusaidiana  na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri Modi.

Waziri Modi aliongeza kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha  ajira 54,176.

Baadhi ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na  mashine ya vipimo vya ugonjwa wa kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.

Katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.

Katika masuala ya viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu  zitakazotibu   magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

“India inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.

Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.