Thursday, July 7, 2016

WANANCHI BAGAMOYO, WAMPONGEZA MKUU WA WILAYA KWA KUSIMAMIA AMANI NA UTULIVU KIPINDI CHA SIKUKUU.



Wananchi wa Bagamoyo wamempongeza mkuu wa wilaya ya hiyo, Alhaji, Majid Hemed Mwanga kwa mikakati mizuri iliyosaidia kuondoa vurugu katika sikukuu ya Eid el fitri ya mwaka huu.

Wakizungumza na bagamoyokwanza blog, kwa nyakati tofauti mjini Bagamoyo, wananchi hao walisema kuwa ni jambo la kupongeza kwa ulinzi na usalama namna ulivyoimarishwa katika mji wa Bagamoyo hasa katika kipindi hiki cha sikukuu ya Eid elfitri.

Walisema mwaka huu sikukuu imekuwa nzuri kwakuwa mji wa Bagamoyo umekuwa tulivu huku wananchi wakitembea bila ya bugudha yoyote ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo kumekuwa na tabia ya makundi kutoka nje ya Bagamoyo ambao hufika Bagamoyo na kufanya fujo za aina mbalimbali ikiwemo kupora watu, kuwadhuru na kuharibu mali za watu



Miraji Nambole, mkazi wa Bagamoyo alisema Hali hiyo imetokana na juhudi za mkuu wa  wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga ambae ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya, ambapo alitangaza kuwa  atakaefanya fujo atachukuliwa hatua za kisheria.
 

Nae Hamadi Athumani, alisema kuwa kila kitu kinawezekana endepo kitawekewa mikakati na mipango thabiti ya utekelezaji na kuongeza kuwa, katika hili serikali ya wilaya imejipanga na  imefanikiwa ambapo wananchi wameweza kufarahia sikukuu bila ya vurugu yoyote.




Kwa upande wake Diwani wa kata ya Dunda Dicksoni Makamba, alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano uliopo kati ya mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, ambae ni mkuu wa wilaya na vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika wilaya hiyo.

Aliseme utekelezaji wa majukumu yoyote unahitaji ushirikiano na kwamba hata mafanikio hayo ya kuzuia fujo katika mji wa Bagamoyo yamepatikana kutokana na ushirikiano.

Hata hivyo aliwashukuru wananchi wa Bagamoyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha amani na utulivu vinachukua nafasi yake.

Kata ya Dunda ndiyo inayopokea wageni wengi siku za siku za sikukuu kwakuwa kata hiyo ipo katika ufukwe wa Bahari ya Hindi ambayo watu wengi hupenda kutembelea.

Siku moja kabla ya sikukuu ya Eid elfitri, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Hemed Mwanga alitoa onyo kwa yeyote atakaesababisha fujo katika kipindi cha sikukuu huku magari ya abiria yanayoingia Bagamoyo kutakiwa kuwa na vibali vya kuingia Bagamoyo hali iliyosaidia kuondoa msongamano wa makundi yenye kuleta fujo siku za sikukuu katika mji wa Bagamoyo.



IDI PILI BAGAMOYO, MJI UMEKUWA TULIVU.




Diwani wa kata ya Dunda, Mh. Diksoni Makamba akielezea namna walivyofanikisha kudhibiti fujo, mjini Bagamoyo, Kata ya Dunda ndiyo inayopata wageni wengi siku za sikukuu kwakuwa ndiyo kata yenye ufukwe wa Bahari na kumbi za starehe ikiwemo ukumbi wa CCM.

Mgambo wakidhibiti Bodaboda zisitembee hovyo kwenye msongamano wa watu.

Watu waliokuwa Beach wanatoka bila ya kulazimishwa baada ya muda uliotangazwa kutoka huko kutimia ambao ni saa 12 jioni.

Kwa utulivu watu wanatembea mjini Bagamoyo Idi pili.

WAKURUGENZI WATEULIWA, NI WA HALIMASHAURI ZA MAJIJI 5, MANISPAA 21,MIJI 22, NA WILAYA 137 ZA TANZANIA BARA.


RAIS, DKT. JOHN MAGUFULI, AMPONGEZA MUFTI WA TANZANIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, alipokuwa akihutubia Baraza la Eid el fitri katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ali kwa juhudi zake za kuwaunganisha waislamu wote na kupanua uwigo wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutoa huduma za kijamii na ameahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itaunga mkono juhudi hizo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 06 Julai, 2016 wakati akihutubia Baraza la Eid el-Fitr kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililofanyika kitaifa katika viwanja vya Karimejee Jijini Dar es salaam.

Dkt. Magufuli amesema kitendo cha kuwaunganisha waislamu wote katika Baraza la Eid el-Fitr kinafungua ukurasa mpya na ni moja ya hatua muhimu za kuimarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wa makundi mbalimbali pamoja na watanzania wengine waisio waislamu.

Aidha Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na BAKWATA katika kuimarisha taasisi zake zinazotoa huduma za kijamii na kulinda mali zake akisema serikali itahakikisha mali zote za waislamu zinakuwa salama na kwamba wote waliodhulumu mali za waislamu watazirejesha.

Awali akisoma taarifa, Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaji Suleiman Said Lolila amesema BAKWATA inakusudia kupanua huduma za kijamii kwa lengo la kuwahudumia wananchi ikiwemo kujenga chuo kikuu Mkoani Dodoma na pia amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuondoa umasikini huku akimtaka asikatishwe tamaa na wachache watakaoudhika kwa kuguswa na hatua zinazochukuliwa.

Nae Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuongoza bila ubaguzi amewataka watanzania kuungana na juhudi za serikali kupinga matendo maovu ikiwemo rushwa na ufisadi na pia amelaani ndoa za jinsia moja akisema ni kinyume na maadili ya dini.

Baraza la Eid el-Fitr pia limehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, mabalozi na wabunge.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
06 Julai, 2016


Sheikh mkuu wa Tanzania Muft Aboubakari Zubeir bin Aliy kushoto, wakizungumza jambo na Rais, Dkt. John Magufuli katika viwanja vya Karimjee wakati wa Baraza la eid el fitri.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, katikati akifurahia jambo wakati wa Baraza la eid el ftri lililofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

SWALA YA EID JANA KATIKA MSIKITI WA MBWENI MASAITI.

Ilikuwa jana katika msikiti wa Mbweni masiti, wakati wa maandalizi ya swala ya Eid.

Imamu wa Msikiti wa Mbweni Ustaadhi, Zubeir Saidi Chungulu, katika maandalizi ya swala ya eid hapo jana.

Wednesday, July 6, 2016

HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA LEO BAGAMOYO, SIKU YA IDI MOSI.



Wananchi wa Bagamoyo wakiwa katika ufukwe wa Bahari ya Hindi leo idi mosi.


Gari zote ziliegeshwa hapa kwa wale wanaokwenda ufukweni (Beach) kwa malipo ya shilingi 3,000.


Diwani wa kata ya Dunda Mh. Diksoni Makamba akiangalia usalama wa magari yaliyoegeshwa akishirikiana na vijana wake.

Pikipiki zote ziliegeshwa hapa kwa wale waliokwenda ufukweni na walitozwa kati ya shilingi elfu moja na elfu mbili.






Wananchi wakielekea ufukweni kwajili kufurahia sikukuu ya idilfitri.


Kikosi cha uokoaji na zima moto kikiwa kando ya Bahari ya Hindi kuangalia usalama.


Usafi ulizingatiwa piya viliwekwa vifaa vya kutupia taka ili uchafu usizagae hovyo.

Umati wa watu ukielekea Beach ya Bagamoyo kwa amani na utulivu siku ya Idi mosi.