Monday, August 19, 2024

JINSI MFUMO DUME UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WANAWAKE KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI LINDI.

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.



Mchango wa mwanamke katika jamii ni mkubwa, adhimu na thamani yake haiwezi kufananishwa na  kiwango chochote cha malipo. 



Lakini kwa bahati mbaya mfumo dume unaendelea kuwatenga wanawake na pale wanapopewa fursa  inakuwa ni kwa bahati tu au ni fursa yenye mipaka fulani. 



Hali hiyo imekua ikiathiri sehemu kubwa ya ushiriki wa mwanamke katika kuwania nafasi za Uongozi ambapo miongozni mwa maeneo yalioathiriwa na mfumo huo nchini Tanzania ni Halmashauri ya Manisaa ya Lindi mkoani Lindi.



Kulingana na tafiti zilizotolewa na Mtandao wa jinsia Nchini Tanzania (TGNP) inaonyesha Idadi ya Wabunge wanawake wakuchaguliwa ni 24, Madiwani 204, Wenyeviti wa vijiji ni 246, Wenyeviti wa Mitaa 528, wa vitogoji ni 4,171.



Ukombozi wa mwanamke ni Pamoja na kumpa nafasi ya kujiona mwenye thamani, uwezo, haki ya kuchaguliwa pamoja na haki ya kuwa na  nafasi sawa na mwanaume katika kila sekta ya jamii; ikiwemo siasa, uongozi Pamoja na Umiliki na usimamizi wa rasilimali.



Hali halisi ni kwamba hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi, za kuchaguliwa au kuteuliwa, wakati Lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu la 2015/2025 linataka wanawake washiriki kikamilifu na kwa tija na fursa sawa katika uongozi na ngazi zote za maamuzi katika siasa, uchumi na Maisha kwa ujumla.



Fatina Ramadhni ni miongoni mwa wanawake aliekumbana na changamoto ya mfumo Dume ambapo licha ya kugombea katika nafasi ya uwenyekiti wa mtaa na kushinda kwa kishindo lakini Mume wake alimfanya kushindwa kutangazwa mshindi na kuhudumu katika nafasi hiyo.



Fatina alisema baada ya mchakato mzima wa uchaguzi kukamilika kisha kupiga kura na baadae kuonekana ana uwezekano mkubwa wa kushinda nafasi hiyo, mume wake alionyesha kutokukubaliana na mke wake na kuamuru nafasi hiyo apatiwe mtu mwingine na si mke wake.



 “Nafasi hiyo ilipatikana vizuri na nilipata nafsi hiyo ya kura kwa vishindo lakini baada ya kupata kura hizo kabla ya kutangazwa ushindi mume wangu alipata taarifa ile, aliingiza mfume dume kwa kusema kwamba mimi sijapata ruhusa kwake yeye hivyo hata kama nimepata kura zote hizo hatakuwa radhi mimi kuwa kiongozi kwa madai kuwa sikupata ridhaa kutoka kwake” 



“hata hivyo aliwashauri waliokuwa wasimamizi wa kura hizo kuniangamizia kura hizo na kutafuta kiongozi mwingine au mwenyekushika madaraka mwingine Zaidi yangu kwa hivyo mimi kwa kweli nilifanyiwa ukatili wa kunyanyaswa katika hili” alieleza Fatina.



Rukia Athumani mkazi wa mtaa wa milola manispaa ya Lindi nae alisema wanawake wengi wanashindwa kugombea nafasi ya uongozi kutokana na mfumo dume uliopo kuanzia ngazi ya familia namna ambavyo unawalea watoto wa kike kutojiamini katika kuweza kuongoza.



“mfano wakati wa malezi kunatofauti kubwa kati ya watoto wa kike na watoto wa kiume mfano hata katika mgawanyo wa majukumu nyumbani utakuta majukumu mengi ya kupika, ama kuhudumia familia anaachiwa mtoto wa kike huku mtoto wa kiume akisalia na majukumu machache hii maana yake nini Baadhi ya familia mtoto wa kike anaandaliwa kuwa mke na sio kiongozi, kwahiyo hii inawafanya wanakuwa wanabaki nyuma na kuona suala la uongozi anatakiwa kuwa mwanaume tu"



Kwa upande wake Ashura Juma mkazi wa Manispaa ya Lindi Alisema wanaume waliowengi wanahofia wanawake zao wakipata nafasi hizo huwenda wanaweza kuwaza kuwazidi kipato na baadae kukengeuka kutokana na kipato chake kuwa kikubwa au kuanzisha mahusiano na wanaume wengine ambao anakutana nao kwenye vikao.



“Ninao mfano mmoja ndugu yangu alikuwa mtumishi kwenye kampuni fulani baada ya kufanya kazi kwa muda kidogo alipoona mke wake anaanza kupendeza mume wake akamuamuru aache kazi kwa kile alichokidai huwenda atakuwa na mahusiano na bosi au mtumishi mwenzie, sasa hebu niambie mtu kama huyo anaweza kumruhusu mkewe agombee ubunge au udiwani hata kama uwezo anao”? alihoji.



Uwepo wa changamoto hiyo ya mfumo dume pamoja na changamoto zingine zinazokwamisha wanawake kutoshiriki kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi unayasukuma mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa maendelea  kutekeleza miradi na mipango kadhaa inayotoa hamasa kwa wanawake na hata vijana kushiriki kugombea nafasi za uongozi



Moja ya mashirika yasio ya kiserikali mkoani Lindi ni shirika la Lindi Regioni Associationi of Non Govermental Organizationis (LANGO) limekuwa likitekeleza mradi wa wanawake na uongozi ambapo kwa mwaka 2019 waliweza kuwafikia wanawake 596 kutoka katika kata za Mchinga, Mbanja na Lindi Mjini



 Afisa programu na Tathimini wa shirika hilo Bishara Mabrouck amesema  progamu hiyo ililenga  kuona mwanamke anashiriki katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi kwamba anapiga kura ama anachaguliwa lakini kubwa Zaidi ni kuona mwanamke anakuwa sehemu ya wanaochaguliwa au anaegombea.



“anavyoshiriki kwenye hizi hatua tatu sauti yake kama mwanamke  inajumuishwa kwenye ngazi mbali mbali za maamuzi na kwamba mwanamke anavyoshiriki kwenye uchaguzi na akachaguliwa tunaamini kwamba maono na fikra za wanawake  zitajumuishwa kwenye mipango kuanzia ngazi za chini za vijiji na hata serikali za mitaa lakini pia kwenye ngazi ya Taifa”



Katika utekelezaji wa program hizo tulikuwa tukiwakutanisha wanawake kwa kuwapa mafunzo yaliyolenga kuwaelewesha hatua za uchaguzi, namna ya kufanya kampeni kwa wale wenye nia ya kugombea, namna ya kuzikabili changamoto za uongozi kwa  kuendesha midahalo ya wanawake  kuwakutanisha wanawake wa kata husika wakijadili pamoja changamoto zinazowafanya wanawake washindwe kugombea katika nafasi hizo.



“Kwenye makongamano na majadiliano hayo zipo changamoto kadhaa ambazo tuliziona ni muhimu kuzifanyia kazi ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na swala la kiuchumi kuanzi katika uchukuaji wa fomu za kugombea pamoja na zoezi zima la uchaguzi, wanawake kutoamininika na jamii, swala la rushwa ya ngono nk.”



“Changamoto nyingine waliyoibaini wakati wa makongamano hayo ni swala la kuhusianisha ushilikina katika mchakato wa uchaguzi ambao imekuwa ikimfanya mwanamke kuhofia kuingia kwa kuwa hatoweza kufanya vitu hivyo, wanawake walio wengi kushindwa kujiamini, na udhalilishaji wakati wa kampeni ”



Michael Mwanga Mkurugenzi wa Lango amesema Bado upo  umuhimu wa kuendelea kuwapambania wanawake ambao wapo katika hali ya chini kutokana na ukweli kwamba bado ipo changamoto kwa wale ambao wamepata nafasi hizo ya kutotambua shida wanazozipata wananchi wa hali ya chini.



“Kumekuwa na shida kwenye siasa ya kwamba wale tunaowapeleka wakagombee na baadae wawe wawakilishi wetu sio kweli kwamba wale wanazisemea shida na mahitaji ya watu wote kwa uhakikia na ndio maana bado tunaendelea kupambana kuwa makundi yote yawepo wakiwepo wanawake wenyewe na hasa wale ambao wanatoka kwenye hali za kawaida kabisa mfano  wafanya biashara, wajasiriamali ”



Makundi haya yanapoingia kwenye nafasi hata ndogo ndogo za uongozi basi waweze kuwa sehemu ya kupambania jamii zao”

Hata hivyo alibainisha kuwa changamoto inakuja pale ambapo bado mifumo iliyopo ya kisiasa bado haijawatambua hawa wanawake wajasiriamali na kuwafanya  wawe wapiga kura pekee.



“hii imedhihirika kwamba hadi sasa jitihada zinazoendelea kufanyika ni za kuwafanya wanawake hawa wajasiriamali wawe wapiga kura tu na sio wa kutoka kwenda kuchukua fomu na kushindana na watu kwa sababu mfume dume tunaouzungumza umeanzia huko kwenye vyama vya siasa ambapo kuna watu tayari wao wamezaliwa kwenye huo mfumo hivyo moja kwa moja tutaendelea kuyaona majina yaleyale tunayoyasikia kwenye siasa siku zote”



Alisema mfumo dume huo umewafanya hata hao wanawake wachache ambao angalau wameweza kupenya na kushika nafasi mbali mbali tayari wameshapitia katik changamoto kadhaa ikiwemo rushwa , matokeo yake hata utendaji kazi wake unategemeana na mtu ambae alimuweka katika nafasi hiyo.



“kwa hivyo mfume dume umeanzia kwenye vyama vyenyewe hata ukitanzama  unaweza kujiuliza ni kwa namna gani vimetengeneza wanawake wa kawaida waweze kushawishika kuingia kwenye uongozi? Wanaingia kwa shida sana na ndio maana wale ambao wenye uwezo unakuta ndo wanaendelea hao hao”



Salama Hamba ni mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake (UWT) kata ya mikumbi amesema ili kuwafanya wanawake wengi waingie kugombea katiki nafasi mbali mbali za uongozi hasa kuanzia katika chaguzi hizi za serikali za mitaa jumuiya imekuwa ikiendelea kuhamasisha wanawake kupitia makongamano mbali mbali ya kisiasa katika ngazi za kata na mitaa.



“ili kuwatia moyo wanawake jumuiya imekuwa ikiwahaidi kuendelea kuwashika mkono na kuwa nao bega kwa bega katika hatua zote za uchaguzi na hii ni katika kuwatia hamasa wanawake wengi wajitokeze kugombea pasipokuwa na woga wowote”



No comments:

Post a Comment