Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI inayojihusisha na kilmo cha kahawa JJAD Kagera farmers imeishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia bei ya kahawa kupanda hadi kufikia shilingi 1,200 mwaka jana mpaka kufikia shilingi 5,300
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendji wa wa Kampuni hiyo, Dk. Albert Katagira, mara baada ya uzinduzi wa kongamano na maonyesho ya 21 ya kahawa bora Afrika.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Chama cha Kahawa Bora Afrika (AFCA), linatarajiwa kufanyika mwezi wa pili mwakani na linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya washiriki 2,000 ambao ni wadau wa biashara ya kahawa Afrika na maeneo mengine duniani.
Kampuni ya JJAD Kagera Farmers Limited iliyoko wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imekuwa ikiendesha kilimo cha kahawa aina ya Robusta kwenye mashamba yenye ekari 100.
“Zao la kahawa kwa mwananchi wa Kagera sasa limekuwa mkombozi mkubwa na nashukuru sana AFCA kuamua kuleta kongamano na maonyesho ya kahawa Tanzania mwakani, Kongamano ambalo litatusaidia sana kuongeza mbinu mpya za kulima zao hili na tutapata masomo mengi,” alisema Dk. Katagira
Dk. Katagira alisema serikali ione umuhimu sasa wa kuwakopesha wakulima wa kahawa kwani kuandaa mashamba ya zao hilo kuna gharama kubwa sana.
“Kuendesha mashamba makubwa ya kahawa siyo kazi rahisi kwa hiyo tunaomba serikali ione umuhimu wa kuwa inawakopesha wakulima mikopo midogo midogo ya kulima kahawa ili wakulima wengi wahamasike kulima zao hili,” alisema
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa (TCB), Primus Kimaryo alisema kongamano la 21 litafanyika mwakani na ni fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa kwani uzalishaji wa kahawa hiyo umekuwa ukiongezeka.
Alisema bodi ya AFCA iliamua kuwa kongamano lao la mwakani lifanyike jijini Dar es Salaam na itakuwa fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa Tanzania kuonyesha kahawa wanayozalisha kwaajili ya kutafuta masoko ya zao hilo.
“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima kutafuta masoko ya kahawa na kuongeza ubora wa kahawa kwasababu bei ya kahawa duniani inazidi kuwa nzuri kwahiyo wanapaswa kuitumia hiyo fursa kuyafikia masoko ambayo ni makubwa,” alisema
Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza alisema Tanzania itakuwa mwenyeji wa kongamano na Maonyesho ya 21 ya Kahawa Bora za Afrika (Afrika Fine Coffee Conference & Exhibitions) kuanzia 26 – 28 Februari, 2025, jijini Dar es Salaam.
Alisema kongamano na maonyesho haya ni jukwaa kubwa zaidi la biashara ya kahawa barani Afrika, na huvutia zaidi ya wadau wa kahawa 2,000 kutoka ndani na nje ya Afrika kila mwaka ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wafanyabiashara wa kahawa, wakaangaji wa kahawa na pia wadau kutoka sekta ya umma na binafsi, na wawakilishi wa serikali.
Alisema kongamano na maonyesho haya yanafanyika hapa nchini kwa mara nyingine baada ya kufanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2016.
“ Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa katika sekta ya kahawa na kongamano na maonyesho haya yanadhihirisha ubora wa kipekee wa kahawa za Afrika na pia yanaimarisha dhamira ya nchi za Afica kukuza ukuaji na ushirikiano katika sekta ya kahawa Africa,” alisema.
“Kauli mbiu ya Kongamano la 21 ni “Kuhuisha ongezeko la Thamani” ambapo kwenye Kongamano patakuwepo na orodha ya wazungumzaji maarufu kimataifa na kikanda. Aidha Maonyesho ya kahawa yatakayofanyika yataoonyesha ubunifu na maendeleo yaliyotokea hivi karibuni katika sekta ya kahawa,” alisema.
Alisema pia kutakuwepo warsha ambazo zitakuwa na majadiliano yenya tija, kutoa fursa za kipekee za kuonja na kutathmini kahawa na safari maalum zitakazoandaliwa ili kujifunza kuhusu kahawa.
Alisema katika kongamano na maonyesho haya kutakuwepo na mashindano ya watayarisha kahawa Africa (Barista Championship) na Mashindano ya kahawa bora katika ukanda wa Afrika ili kuonyesha vipaji na bidhaa bora zaidi za kahawa kutoka kote barani.
No comments:
Post a Comment