Monday, August 26, 2024

MTAALAMU BINGWA WA NYONGA NA MAGOTI ATUA DAR.

 



Ashirikiana na wataalamu wazawa upasuaji Mloganzila


Na Mwandishi Wetu


MTAALAMU bingwa wa ubadilishaji wa nyonga na magoti  kutoka hospitali kubwa nchini India ya Yashoda, Dk. Ram Mohan Reddy amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kambi ya matibabu hayo kwa watanzania.


Daktari huyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani atafanya upasuaji huo kwenye kambi ya siku tano itakayofanyika katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila  kuanzia leo Jumatatu hadi tarehe 30.


Aliwasili jana usiku katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo alipokelewa na wafanyakazi wa Global Medicare ambao wameratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili Mloganzila.


 Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro,  alisema wamefurahi kuona amefika salama nchini Tanzania na kwamba ujio wake utakuwa wa manufaa makubwa kwa watanzania wenye matatizo ya nyonga na magoti.


“Tunajua ni mara yako ya kwanza kuja kufanyakazi na madaktari wa hapa Tanzania  kwenye upasuaji wa aina hii lakini tunatarajia watanzania wengi watanufaika na ujio wako kwenye kambi hii ya siku tano itakayoanza katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila,” alisema


Naye Dk. Reddy aliishukuru serikali ya Tanzania na taasisi ya Global Medicare kwa kuratibu vyema safari yake ya kuja nchini Tanzania na aliahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaojitokeza kwenye kambi hiyo.


“Natarajia tunashirikiana vizuri sana na wataalamu wenzangu wa hapa nchini kwenye kambi hii ya siku tano na kwa huduma hii natarajia tutaongeza chachu ya ushirikiano baina ya Tanzania na India na tutabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa aina hii kwa wataalamu na watu wa hapa nchini watakaokuja kusoma India,” alisema


Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove   Mfuko, alisema hivi karibuni kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu huyo Dk. Ram Mohan Reddy.


 


“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma  kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema


“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili  tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka India kupata uzoefu ili tuweze kubadilishana naye uzoefu ili tuboreshe zaidi huduma zetu,” alisema


“Kwa hiyo watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila mapema ili wafanyiwe uchunguzi wa mapema kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti,” alisisitiza Dk. Mfuko.


 

WANAFUNZI WATAKAOFANYA VIZURI SHULE BRLILLIAN KUPELEKWA SERENGETI

 






Picha mbalimbali mahafali ya 14 ya kidato cha nne shule ya sekondari ya  Brilliant ya Kimara Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam yaliyofanyika jana Jumamosi

...............................................

Na  Mwandishi Wetu

Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Dk. Jasson Rweikzia, ametangaza kwamba kwenye mtandao wa shule za St Anne Marie Academy unaominilikia pia shule ya Brilliant ya Kimara Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa shule baada ya wazazi wake kufariki na kushindwa kulipa ada ya kuendelea na masomo.


 


Alitangaza uamuzi huo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya  14 ya kidato cha nne ya shule ya Brilliant iliyoko Kimara Mbezi jijini Dar es Salaam.


 


Mtandao huo unamiliki shule za St Anne Marie Academy, Brilliant, Rweikiza Nursery and Primary na Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani.


 


Dk Rweikiza alisema shule hizo ziliwahi kupoteza wazazi 93 kwasababu mbalimbali na kusababisha baadhi ya wanafunzi kuacha masomo kwa kukosa ada hali ambayo alisema imeilazimu shule hiyo kuwapa msamaha wa ada wanaofiwa.


 


 " Tumekuwa tukipoteza wazazi wengi na mwezi huu pekee tumepoteza wazazi watatu na hali hii imekuwa ikiathiri sana wanafunzi kitaaluma na wengine kuacha shule kwa kushindwa kulipa ada lakini kuanzia sasa hakuna atakayefukuzwa shule kwa kukosa ada baada ya mzazi wake kufariki," alisema


 


 " Kama yuko darasa la kwanza na amefiwa na mzazi wake ataendelea kusoma mpaka darasa la saba na kama ni sekondari ataendelea mpaka kidato cha nne," alisema Dk. Rweikiza


 


Dk. Rweikiza alisema katika mpango wa kuinua taaluma shuleni hapo wameaandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kwa awatakaofanya vizuri kwenye masomo yao na ziara za kimasomo kwenye mbuga mbalimbali za wanyama.


 


Alisema mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atapata sh 600,000 na atakayepata daraja la II atapata Sh 200,000 na kwamba lengo ni kuhakikisha hakuna daraja la nne wala daraja la tatu shuleni hapo.


 


Mkuu wa shule ya Brilliant, Edrick Phillemon alisema wahitimu hao wa kidato cha nne wameandaliwa vizuri kitaaluma na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao na kwamba ana uhakika wa kupata daraja la kwanza na la pili.


 


“Tuna uhakika wa kufanya vizuri kwani ukiangalia historia ya shule ya Brilliant huwa haipati daraja la nne wa daraja 0, mara nyingi tunafaulisha kwa daraja la kwanza na la pili,” alisema


 


 Alisema wanafunzi hao wamewezeshwa kufikia hapo na walimu wenye taaluma na uzoefu wa kutosha huku akimshukuru Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya shule hiyo.

Friday, August 23, 2024

JJAD KAGERA FARMERS YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA BEI NZURI YA KAHAWA

 

Na Mwandishi Wetu


KAMPUNI  inayojihusisha na kilmo cha kahawa  JJAD Kagera farmers imeishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia bei ya kahawa kupanda hadi kufikia shilingi 1,200 mwaka jana mpaka kufikia shilingi 5,300


Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendji wa wa Kampuni hiyo, Dk.  Albert Katagira, mara baada ya uzinduzi wa kongamano na maonyesho ya 21 ya kahawa bora Afrika.


Kongamano hilo lililoandaliwa na Chama cha Kahawa Bora Afrika (AFCA), linatarajiwa kufanyika mwezi wa pili mwakani na linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya washiriki 2,000 ambao ni wadau wa biashara ya kahawa Afrika na maeneo mengine duniani.


Kampuni ya JJAD Kagera Farmers Limited iliyoko wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imekuwa ikiendesha kilimo cha kahawa aina ya Robusta kwenye mashamba yenye ekari 100.


“Zao la kahawa kwa mwananchi wa Kagera sasa limekuwa mkombozi mkubwa na nashukuru sana AFCA kuamua kuleta kongamano na maonyesho ya kahawa Tanzania mwakani, Kongamano ambalo  litatusaidia sana kuongeza mbinu mpya za kulima zao hili na tutapata masomo mengi,” alisema Dk. Katagira


Dk. Katagira alisema serikali ione umuhimu sasa wa kuwakopesha wakulima wa kahawa kwani kuandaa mashamba ya zao hilo kuna gharama kubwa sana.


“Kuendesha mashamba makubwa ya kahawa siyo kazi rahisi kwa hiyo tunaomba serikali ione umuhimu wa kuwa inawakopesha wakulima mikopo midogo midogo ya kulima kahawa ili wakulima wengi wahamasike kulima zao hili,” alisema


Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa (TCB), Primus Kimaryo alisema kongamano la 21 litafanyika mwakani na ni fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa kwani uzalishaji wa kahawa hiyo umekuwa ukiongezeka.


Alisema bodi ya AFCA iliamua kuwa kongamano lao la  mwakani lifanyike  jijini Dar es Salaam na itakuwa fursa ya kipekee kwa wakulima wa kahawa Tanzania kuonyesha kahawa wanayozalisha kwaajili ya kutafuta masoko ya zao hilo.


“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima kutafuta masoko ya kahawa na kuongeza ubora wa kahawa kwasababu bei ya kahawa duniani inazidi kuwa nzuri kwahiyo wanapaswa kuitumia hiyo fursa kuyafikia masoko ambayo ni makubwa,” alisema


Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza alisema  Tanzania itakuwa mwenyeji wa kongamano na Maonyesho ya 21 ya Kahawa Bora za Afrika (Afrika Fine Coffee Conference & Exhibitions) kuanzia 26 – 28 Februari, 2025, jijini Dar es Salaam.


Alisema kongamano na maonyesho haya  ni jukwaa kubwa zaidi la biashara ya kahawa barani Afrika, na huvutia zaidi ya wadau wa kahawa 2,000 kutoka ndani na nje ya Afrika kila mwaka ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wafanyabiashara wa kahawa, wakaangaji wa kahawa na pia wadau kutoka sekta ya umma na binafsi, na wawakilishi wa serikali.


Alisema kongamano na maonyesho haya yanafanyika hapa nchini kwa mara nyingine baada ya kufanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2016.


“ Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa katika sekta ya kahawa na kongamano na maonyesho haya yanadhihirisha ubora wa kipekee wa kahawa za Afrika na pia yanaimarisha dhamira ya nchi za Afica   kukuza ukuaji na ushirikiano katika sekta ya kahawa Africa,” alisema.


“Kauli mbiu ya Kongamano la 21 ni “Kuhuisha ongezeko la Thamani” ambapo kwenye Kongamano patakuwepo na orodha ya wazungumzaji maarufu kimataifa na kikanda. Aidha Maonyesho ya kahawa yatakayofanyika yataoonyesha ubunifu na maendeleo yaliyotokea hivi karibuni katika sekta ya kahawa,” alisema.


Alisema pia  kutakuwepo warsha ambazo zitakuwa na majadiliano yenya tija, kutoa fursa za kipekee za kuonja na kutathmini kahawa  na safari maalum zitakazoandaliwa ili kujifunza kuhusu kahawa.  



Alisema katika kongamano na maonyesho haya kutakuwepo na mashindano ya watayarisha kahawa Africa (Barista Championship) na Mashindano ya kahawa bora katika ukanda wa Afrika ili kuonyesha vipaji na bidhaa bora zaidi za kahawa kutoka kote barani.


Wednesday, August 21, 2024

ZAIDI YA WAVUVI ELFU 11 LINDI KUFIKIWA NA ELIMU YA UVUVI SALAMA

 





NA HADIJA OMARY, LINDI

Zaidi ya wavuvi elfu 11 Mkoani Lindi wanatarajiwa kufikiwa na kupatiwa elimu ya ufahamu juu ya masuala ya bahari ili kuongeza ufanisi na usalama katika shughuli zao za uvuvi.



Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya  uvuvi salama inayoendeshwa na chuo cha Bahari Dar es salaam Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga, amesema  Elimu hiyo ni muhimu kwa wavuvi wa Lindi kwani itawasaidia kufanya shughuli zao kitaalam na kuachana na uvuvi wa mazoea 


Mkuu wa chuo cha Bahari Dar es salaam Dr. Tumaini Guruma Amesema lengo uzinduzi wa kampeni hiyo ni kuleta ufahamu wa  usalama baharini kwa wananchi huku akiweka bayana fursa mbalimbali zitokanazo na uvuvi ni pamoja na ajira kwa vijana


Mkuu wa idara ya kozi za umahiri Deism Mlay amesema kupitia kampeni hiyo kwa kipindi cha siku nne wataalam watapita katika shule, masoko ya samaki kukutana na wavuvi na kuwapatia elimu  ya kozi za usalama baharini, unahodha wa vyombo vya uvuvi pamoja na usalama katika shughuli za uvuvi.

Monday, August 19, 2024

JINSI MFUMO DUME UNAVYOKATISHA NDOTO ZA WANAWAKE KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI LINDI.

 

NA HADIJA OMARY, LINDI.



Mchango wa mwanamke katika jamii ni mkubwa, adhimu na thamani yake haiwezi kufananishwa na  kiwango chochote cha malipo. 



Lakini kwa bahati mbaya mfumo dume unaendelea kuwatenga wanawake na pale wanapopewa fursa  inakuwa ni kwa bahati tu au ni fursa yenye mipaka fulani. 



Hali hiyo imekua ikiathiri sehemu kubwa ya ushiriki wa mwanamke katika kuwania nafasi za Uongozi ambapo miongozni mwa maeneo yalioathiriwa na mfumo huo nchini Tanzania ni Halmashauri ya Manisaa ya Lindi mkoani Lindi.



Kulingana na tafiti zilizotolewa na Mtandao wa jinsia Nchini Tanzania (TGNP) inaonyesha Idadi ya Wabunge wanawake wakuchaguliwa ni 24, Madiwani 204, Wenyeviti wa vijiji ni 246, Wenyeviti wa Mitaa 528, wa vitogoji ni 4,171.



Ukombozi wa mwanamke ni Pamoja na kumpa nafasi ya kujiona mwenye thamani, uwezo, haki ya kuchaguliwa pamoja na haki ya kuwa na  nafasi sawa na mwanaume katika kila sekta ya jamii; ikiwemo siasa, uongozi Pamoja na Umiliki na usimamizi wa rasilimali.



Hali halisi ni kwamba hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi, za kuchaguliwa au kuteuliwa, wakati Lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu la 2015/2025 linataka wanawake washiriki kikamilifu na kwa tija na fursa sawa katika uongozi na ngazi zote za maamuzi katika siasa, uchumi na Maisha kwa ujumla.



Fatina Ramadhni ni miongoni mwa wanawake aliekumbana na changamoto ya mfumo Dume ambapo licha ya kugombea katika nafasi ya uwenyekiti wa mtaa na kushinda kwa kishindo lakini Mume wake alimfanya kushindwa kutangazwa mshindi na kuhudumu katika nafasi hiyo.



Fatina alisema baada ya mchakato mzima wa uchaguzi kukamilika kisha kupiga kura na baadae kuonekana ana uwezekano mkubwa wa kushinda nafasi hiyo, mume wake alionyesha kutokukubaliana na mke wake na kuamuru nafasi hiyo apatiwe mtu mwingine na si mke wake.



 “Nafasi hiyo ilipatikana vizuri na nilipata nafsi hiyo ya kura kwa vishindo lakini baada ya kupata kura hizo kabla ya kutangazwa ushindi mume wangu alipata taarifa ile, aliingiza mfume dume kwa kusema kwamba mimi sijapata ruhusa kwake yeye hivyo hata kama nimepata kura zote hizo hatakuwa radhi mimi kuwa kiongozi kwa madai kuwa sikupata ridhaa kutoka kwake” 



“hata hivyo aliwashauri waliokuwa wasimamizi wa kura hizo kuniangamizia kura hizo na kutafuta kiongozi mwingine au mwenyekushika madaraka mwingine Zaidi yangu kwa hivyo mimi kwa kweli nilifanyiwa ukatili wa kunyanyaswa katika hili” alieleza Fatina.



Rukia Athumani mkazi wa mtaa wa milola manispaa ya Lindi nae alisema wanawake wengi wanashindwa kugombea nafasi ya uongozi kutokana na mfumo dume uliopo kuanzia ngazi ya familia namna ambavyo unawalea watoto wa kike kutojiamini katika kuweza kuongoza.



“mfano wakati wa malezi kunatofauti kubwa kati ya watoto wa kike na watoto wa kiume mfano hata katika mgawanyo wa majukumu nyumbani utakuta majukumu mengi ya kupika, ama kuhudumia familia anaachiwa mtoto wa kike huku mtoto wa kiume akisalia na majukumu machache hii maana yake nini Baadhi ya familia mtoto wa kike anaandaliwa kuwa mke na sio kiongozi, kwahiyo hii inawafanya wanakuwa wanabaki nyuma na kuona suala la uongozi anatakiwa kuwa mwanaume tu"



Kwa upande wake Ashura Juma mkazi wa Manispaa ya Lindi Alisema wanaume waliowengi wanahofia wanawake zao wakipata nafasi hizo huwenda wanaweza kuwaza kuwazidi kipato na baadae kukengeuka kutokana na kipato chake kuwa kikubwa au kuanzisha mahusiano na wanaume wengine ambao anakutana nao kwenye vikao.



“Ninao mfano mmoja ndugu yangu alikuwa mtumishi kwenye kampuni fulani baada ya kufanya kazi kwa muda kidogo alipoona mke wake anaanza kupendeza mume wake akamuamuru aache kazi kwa kile alichokidai huwenda atakuwa na mahusiano na bosi au mtumishi mwenzie, sasa hebu niambie mtu kama huyo anaweza kumruhusu mkewe agombee ubunge au udiwani hata kama uwezo anao”? alihoji.



Uwepo wa changamoto hiyo ya mfumo dume pamoja na changamoto zingine zinazokwamisha wanawake kutoshiriki kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi unayasukuma mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa maendelea  kutekeleza miradi na mipango kadhaa inayotoa hamasa kwa wanawake na hata vijana kushiriki kugombea nafasi za uongozi



Moja ya mashirika yasio ya kiserikali mkoani Lindi ni shirika la Lindi Regioni Associationi of Non Govermental Organizationis (LANGO) limekuwa likitekeleza mradi wa wanawake na uongozi ambapo kwa mwaka 2019 waliweza kuwafikia wanawake 596 kutoka katika kata za Mchinga, Mbanja na Lindi Mjini



 Afisa programu na Tathimini wa shirika hilo Bishara Mabrouck amesema  progamu hiyo ililenga  kuona mwanamke anashiriki katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi kwamba anapiga kura ama anachaguliwa lakini kubwa Zaidi ni kuona mwanamke anakuwa sehemu ya wanaochaguliwa au anaegombea.



“anavyoshiriki kwenye hizi hatua tatu sauti yake kama mwanamke  inajumuishwa kwenye ngazi mbali mbali za maamuzi na kwamba mwanamke anavyoshiriki kwenye uchaguzi na akachaguliwa tunaamini kwamba maono na fikra za wanawake  zitajumuishwa kwenye mipango kuanzia ngazi za chini za vijiji na hata serikali za mitaa lakini pia kwenye ngazi ya Taifa”



Katika utekelezaji wa program hizo tulikuwa tukiwakutanisha wanawake kwa kuwapa mafunzo yaliyolenga kuwaelewesha hatua za uchaguzi, namna ya kufanya kampeni kwa wale wenye nia ya kugombea, namna ya kuzikabili changamoto za uongozi kwa  kuendesha midahalo ya wanawake  kuwakutanisha wanawake wa kata husika wakijadili pamoja changamoto zinazowafanya wanawake washindwe kugombea katika nafasi hizo.



“Kwenye makongamano na majadiliano hayo zipo changamoto kadhaa ambazo tuliziona ni muhimu kuzifanyia kazi ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na swala la kiuchumi kuanzi katika uchukuaji wa fomu za kugombea pamoja na zoezi zima la uchaguzi, wanawake kutoamininika na jamii, swala la rushwa ya ngono nk.”



“Changamoto nyingine waliyoibaini wakati wa makongamano hayo ni swala la kuhusianisha ushilikina katika mchakato wa uchaguzi ambao imekuwa ikimfanya mwanamke kuhofia kuingia kwa kuwa hatoweza kufanya vitu hivyo, wanawake walio wengi kushindwa kujiamini, na udhalilishaji wakati wa kampeni ”



Michael Mwanga Mkurugenzi wa Lango amesema Bado upo  umuhimu wa kuendelea kuwapambania wanawake ambao wapo katika hali ya chini kutokana na ukweli kwamba bado ipo changamoto kwa wale ambao wamepata nafasi hizo ya kutotambua shida wanazozipata wananchi wa hali ya chini.



“Kumekuwa na shida kwenye siasa ya kwamba wale tunaowapeleka wakagombee na baadae wawe wawakilishi wetu sio kweli kwamba wale wanazisemea shida na mahitaji ya watu wote kwa uhakikia na ndio maana bado tunaendelea kupambana kuwa makundi yote yawepo wakiwepo wanawake wenyewe na hasa wale ambao wanatoka kwenye hali za kawaida kabisa mfano  wafanya biashara, wajasiriamali ”



Makundi haya yanapoingia kwenye nafasi hata ndogo ndogo za uongozi basi waweze kuwa sehemu ya kupambania jamii zao”

Hata hivyo alibainisha kuwa changamoto inakuja pale ambapo bado mifumo iliyopo ya kisiasa bado haijawatambua hawa wanawake wajasiriamali na kuwafanya  wawe wapiga kura pekee.



“hii imedhihirika kwamba hadi sasa jitihada zinazoendelea kufanyika ni za kuwafanya wanawake hawa wajasiriamali wawe wapiga kura tu na sio wa kutoka kwenda kuchukua fomu na kushindana na watu kwa sababu mfume dume tunaouzungumza umeanzia huko kwenye vyama vya siasa ambapo kuna watu tayari wao wamezaliwa kwenye huo mfumo hivyo moja kwa moja tutaendelea kuyaona majina yaleyale tunayoyasikia kwenye siasa siku zote”



Alisema mfumo dume huo umewafanya hata hao wanawake wachache ambao angalau wameweza kupenya na kushika nafasi mbali mbali tayari wameshapitia katik changamoto kadhaa ikiwemo rushwa , matokeo yake hata utendaji kazi wake unategemeana na mtu ambae alimuweka katika nafasi hiyo.



“kwa hivyo mfume dume umeanzia kwenye vyama vyenyewe hata ukitanzama  unaweza kujiuliza ni kwa namna gani vimetengeneza wanawake wa kawaida waweze kushawishika kuingia kwenye uongozi? Wanaingia kwa shida sana na ndio maana wale ambao wenye uwezo unakuta ndo wanaendelea hao hao”



Salama Hamba ni mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake (UWT) kata ya mikumbi amesema ili kuwafanya wanawake wengi waingie kugombea katiki nafasi mbali mbali za uongozi hasa kuanzia katika chaguzi hizi za serikali za mitaa jumuiya imekuwa ikiendelea kuhamasisha wanawake kupitia makongamano mbali mbali ya kisiasa katika ngazi za kata na mitaa.



“ili kuwatia moyo wanawake jumuiya imekuwa ikiwahaidi kuendelea kuwashika mkono na kuwa nao bega kwa bega katika hatua zote za uchaguzi na hii ni katika kuwatia hamasa wanawake wengi wajitokeze kugombea pasipokuwa na woga wowote”



Friday, August 16, 2024

MPANGO WA IMASA WATUA LINDI, BILIONI 3.6 ZATENGWA.

 


LICHA ya zoezi la utoaji wa MIKOPO kwa wanawake, vijana na Watu wenye mahitaji maalumu kusitishwa kwa muda kwa ajili ya uboreshaji, Mkoa wa Lindi imeendelea kutenga fedha hizo ambapo mpaka sasa zimeshatengwa Jumla ya shilingi Bilioni 3.6

Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Lindi kwa niamba ya mkuu wa Mkoa huo wakati wa mafunzo ya uwasilishaji wa program ya uwezeshaji wananchi kiuchumi iliyofanyika huko Manispaaa ya Lindi 


Program hiyo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi imepewa jina la Imarisha uchumi na Mama Samia (IMASA)



Ndemanga Amesema Fedha hizo zimetengwa kutoka kila Halmashauri ambazo zinatolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu .


Amesema kuwa kutokana na dhamira ya serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi katika makundi husika imekuja na mpango wa Imarisha uchumi na Mama Samia (IMASA) ambao katika hatua ya awali imejikita katika kukusanya maoni ya walengwa kuhusu vipaumbele vya mkoa na kuwasajili.


Kwa upande wake katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi Bi. Beng'i M. Issa amesema kuwa madhumuni ya programu hiyo katika hatua ya awali ni kupata takwimu za wananchi kwenye maeneo yao husika na shughuli zao katika maeneo hayo.

 Malengo mengine ni kupata Mahitaji ya kiuchumi kwenye maeneo husika kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Wilaya, kujenga uwezo wa wananchi wote wenye uhitaji kwenye maeneo husika, kutekeleza programu ya kuwezesha wananchi kwenye Mikoa na maeneo yao.



Wakizungumza mara baada ya semina hiyo wajasiriamali kutoka wilaya za Mkoa wa Lindi wameshukuru kwa programu hiyo ambayo inakwenda kuwainua kiuchumi









Thursday, August 15, 2024

OMBI LA WAKILI WA UTETEZI KESI YA WANANDOA KUJERUHI LAGONGA MWAMBA MAHAKAMANI

 

Bharat Nathwani mbele  na mke wake Sangita Nathwani  nyuma kabisa wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kusikiliza kesi inayowakabili ya kumjeruhi jirani yao inayowakabili.

................................................

Na Mwandishi Wetu


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekataa ombi la wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) la kutaka shahidi Kiran Ratilal awasilishe kipande kifupi cha video (clip) kinachoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo ya mchanganyiko wa saruji.


Nathwan na Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


 


Ombi hilo liliwasilishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Aaron Lyamuya na Wakili wa Utetezi Edward Chuwa kwa niaba ya wateja wake, wakati Kiran Lalit Ratilal alipokuwa akiulizwa maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliyoutoa dhidi ya washtakiwa hao.


 


Wakili Chuwa alimuuliza Kiran Lalit Ratilal ambae ni shahidi wa nne katika kesi hiyo, kama ni kweli kwenye ushahidi wake alidai kuwa anayo clip inayoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo hiyo na upo tayari kuitoa,  alidai ni kweli anayo, lakini kwa wakati huo hana.


 


"Kwa hiyo umeomba kuitoa mahakamani kama kielelezo kutokana na maelezo yako uliyoyatoa,"alidai Wakili Chuwa


 


Baada ya Chuwa kudai hivyo, Hakimu Lyamuya alimueleza kuwa shahidi hakuomba kutoa kipande hicho, lakini Wakili Chuwa aliendelea kudai kuwa wanataka itolewe kama ushahidi.


 


Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Nguka alidai kuwa wao hawako tayari kutoa kielelezo hicho, lakini kama Chuwa anataka kufanya hivyo wanaweza kukitoa wao katika utetezi wao kwa kufuata utaratibu.


 


Wakili Chuwa alidai kuwa kama kuna hatua za kufuata yeye hazikumbuki, ndipo Hakimu Lyamuya aliwaeleza kuwa kuna taratibu za kisheria shahidi kutoa kielelezo wakati wa kipindi cha maswali ya dodoso zinatakiwa zifuatwe.


 


"Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake katika shauri la Lilian na Jesus ya mwaka 2018 ilitoa utaratibu, kwa hiyo Chuwa kama ulitaka kufanya hivyo ulitakiwa kufuata taratibu kwenye hiyo rufaa imeonesha hatua kwa hatua,"


 


"Ombi hili linakuja randomly, ombi hili limekataliwa,"alisema Hakimu Lyamuya


Baada ya Hakimu Lyamuya kusema hivyo, Wakili Chuwa alidai kuwa wamemaliza maswali ya dodoso kwa shahidi.


 


Wakili Nguka alimuuliza shahidi baadhi ya maswali ( Re-examination) kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kwa mahakama, alidai upande wa utetezi ulimuuliza sana uhusiano wa mume wake na Hospitali ya Regency, akadai kuwa mume wake sio daktari ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo.


 


Wakili huyo, aliiomba mahakama iwapangie tarehe ya karibu ili walete mashahidi wengine katika kesi hiyo na kudai kuwa wapo tayari kuendelea hata leo.


 


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30, 2024 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.


Wednesday, August 14, 2024

MKUTANO WA MICO HALAL WAIBUA MAMBO KUHUSU UMUHIMU WA BIDHAA ZA HALAL

 


Na Mwandishi Wetu

 

UKUBWA wa soko la bidhaa za Halal duniani umeendelea kuongezeka kutoka Dola trilioni 1.2 miaka 10 iliyopita hadi kufikia dola trilioni 2.29 mwaka jana.

Hayo yamesemwa leo  tarehe 14 Agosti 2024 na mtoa mada Salum Awadh wakati akizungumza kwenye kongamano la pili kuhusu mwenendo, fursa na maendeleo ya soko la bidhaa za Halal duniani wakati wa kongamano hilo ambalo limeandaliwa na MICO Halal International Bureau.

Alisema ongezeko hilo ni kubwa na linaonyesha mwamko mkubwa kwa watu kutumia bidhaa za Halal kwenye maeneo mbalimbali duniani kuanzia kwenye bidhaa na utoaji wa huduma.

Alisema soko la Halal liko kwenye maeneo  kuanzia ya chakula, fedha, dawa, mavazi, vyombo vya habari na  usafiri.

“Fursa la bidhaa za Halal ni kubwa sana hasa ukiangalia waislamu wanawajibika kutumia bidhaa za Halal na hata wasio waislamu wanaweza kutumia bidhaa za Halal,” alisema

Alisema watanzania wanapaswa kutumia ongezeko la matumizi ya bidhaa za Halal kama fursa ya kutengeneza fedha kwani soko lake limeendelea kuongezeka siku hadi siku.

“Kwenye soko la OIC pekee kuna soko kubwa sana kwasababu watumiaji wa bidhaa za Halal ni wengi sana. Soko liko kubwa hapa nchini, liko Afrika na dunia nzima soko lipo ni wananchi wenyewe kuchangamkia fursa,” alisema

Alisema serikali imekuwa ikihamasisha watu kupeleka nyama kwenye masoko ya mataifa ya uarabuni kama United Arab Emirates (UAE) na Saudi Arabia ambazo zimekuwa zikizingatia matumizi ya bidhaa za Halal.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam, Shamim Khan, alipongeza MICO Halal kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litawasaidia wafanyabaiashara kujua namna ya kuzingatia misingi ya Halal kwenye bidhaa zao.

“Nawapongeza sana MICO Halal kwa kuleta hili kongamano kwasababu tulikuwa tunajua maana ya Halal lakini hatuishi kwa kufuata misingi ya Halal kwa hiyo elimu hii itawezesha sisi tuishi kwa kufuata Halal,” alisema

“Lazima tujue unapokwenda supamaketi unanunua kitu kilichofuata Halal kinakuwa kwenye mwonekano gani na kama kimezingatia hasa misingi ya bidhaa za Halal, lazima tujue kitu gani ni halali na kitu gani ni haramu” alisema

Friday, August 9, 2024

MADAKTARI BINGWA KUTOKA INDIA KUFANYA UPASUAJI WA MAGOTI NA NYONGA DAR ES SALAAM.

 


Ni matunda ya ziara ya Rais Samia India

·      Wagonjwa nje ya nchi sasa kumiminika kutibiwa hospitali za Tanzania

Na  Mwandishi Wetu

DAKTARI  bingwa wa upasuaji wa magoti na nyonga kutoka  hospitali maarufu duniani YASHODA iliyoko mji wa Hyderabad nchini India, Dk. Ram Mohan Reddy na wenzake, wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu kwaajili ya kutoa matibabu ya upasuaji wa kibingwa wa magoti na nyonga.


 

Madaktari hao watafanya upasuaji huo  kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji wa magoti na nyonga  wazawa katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili- tawi la Mloganzila ambapo matibabu hayo ya kibigwa yatafanyika.


 

Mkurugenzi mtendaji wa Global Medicare, ambao ni  mawakala wa tiba utalii nchini, Abdulmalik Mollel, alisema madaktari hao watafanya upasuaji wakibingwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la  Mloganzila kuanzia tarehe 26 hadi 28 mwezi huu Agosti 2024.

 
 

Mollel alisema madaktari hao  bobezi  watashirikiana na madaktari bingwa wazawa kwenye kambi hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo madakitari wa ndani kwa kubadilisha uzoefu ambao utawapa ujunzi  zaidi madaktari wenyeji ambao utawawezesha kufanya upasuaji kama huo hata baada ya kuondoka kwa daktari huyo mgeni.


 

“Mwaka jana tulifanya kambi kama hii ya upasuaji na ilikuwa na mafanikio makubwa sana kwasababu kulikuwa na watu zaidi ya 2,300 waliokuwa wanahitaji huduma hiyo  na madaktari wetu walifanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na wale wa nje na tunatarajia daktarin huyu bingwa na bobezi na wenzake katika matibabu ya upasuaji wa nyonga na magoti watawafanyia watu wengi watakao jitokeza mapema nakufanyiwa uchunguzi wa awali,” alisema

 
 

Alisema baada ya uchunguzi wale watakao ngundulika wanahitaji matibabu hayo ya kibingwa ya upasuwaji watafanyiwa.

 
 

Aliongeza kwa kusema, kwa muda mrefu watanzania wenye matatizo ya afya walikuwa wakienda nje ya nchi kwa matibabu lakini baada ya serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya watanzania wengi sasa wamekuwa wakitibiwa  hapa nchini.

 
 

Mollel alisema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye vifaa tiba kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa kama iliyoko kwenye mataifa makubwa duniani na imesomesha wataalamu bobezi ( super specialist)  wa fani mbalimbali kwenye tiba.



 

“Tanzania kwa sasa inavifaa vya kisasa vya kutosha na wataalamu bobezi kama walioko nchini India na kwingineko kwa hiyo sasa ni muda muwafaka madaktaari bobezi wa nje waje hapa nchini kujengeana uwezo (Capacity building)  na wenzao wa ndani ambao wamekuwa wakifanyakazi kubwa sana kwaajili ya Taifa,” alisema  Mollel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL).

 

Alisema huduma za madaktari wabobezi zinazopatikana hapa nchini zimewavutia watu wengi wa nchi jirani kuja kutibiwa hapa nchini badala ya kwenda nchi za nje kufuata tiba kama hiyo ambapo hutumia muda mwingi na gharama kubwa ukilinganisha na kuja hapa nchini.

 


“Kuja kwa madakatri hawa wabobezi ni jambo jema sana kwasababu madaktari wetu watachukua zile teknolojia ambazo zitakuwa hazijafika hapa nchini nasisi kama tuna ujuzi ambao tumewazidi wanachukua  na kwa uwekezaji uliofanywa na serikali katika sekta ya afya Tanzania sasa ni kitovu cha utalii tiba kwa nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la sahara,” alisema Mollel.

 

“YASHODA ni miongoni mwa hospitali kubwa duniani inayopatikana nchini India yenye vitanda 4,000 kwa hiyo inafanya vizuri sana na mwaka jana mwezi wa tano ujumbe wa madaktari bingwa wa Tanzania walienda kujifunza, hivyo basi, wao wana kitu gani tofauti na hivi tulivyonavyo, tulijifunza wana mazingira gani yanayosababisha watu duniani kupendelea kwenda kutibiwa kwao,” alisema
 

 

Aidha, alisema  lengo lilikuwa ni kujifunza yale ambayo yamewafanya wawe bingwa kwenye utalii tiba duniani na kuja kutekeleza nchini yale ambayo wameyafanya yakawapa sifa ya kuwa kitovu cha utalii tiba na kupata wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

 

“Moja ya mafanikio ya ziara tuliyofanya India mwaka jana ni ujio wa madaktari kutoka YASHODA ambayo ni moja ya hospitali tulizotembelea zenye ubora na viwango vya daraja la kwanza duniani na ina madaktari mahiri na wenye mtandao mkubwa duniani kutokana na ubobezi wao,” alisema

 


GLOBAL EDUCATION LINK YATOA VISA 100 KWA WANAOKWENDA KUSOMA NJE YA NCHI

 

Na Mwandishi Wetu


 WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), imetoa Visa 100 kwa kundi la kwanza la wanafunzi wanaotarajia kuanza kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kuanza masomo hayo kuanzia wiki ijayo.


Hiyo inakuja ikiwa zimepita wiki mbili tu tangu matokeo ya kidato cha sita kutoka ambapo mamia ya wanafunzi wa Tanzania wenye kuhitaji kusoma nje ya nchi kupitia GEL wameshaanza kufanya maandalizi ya kuondoka kuanzia wiki ijayo.


Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Global Education Link Abdulmalik Mollel, wakati akigawa Visa 100 kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuondoka wiki ijayo na amezungumza na wazazi na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda nchini humo.


 Mollel alisema lengo la mkutano huo ni kukabidhi Visa, kujadili na wazazi na  wanafunzi kuhusu mambo mengi ya kuzingatia katika maandalizi ya safari yao, kuwakutanisha wazazi na wanafunzi na wawakilishi wa vyuo vikuu ambavyo wanafunzi hao wanatarajia kwenda kusoma pamoja na wanafunzi kujaza nyaraka mbalimbali.


 “Leo tumekutana na wanafunzi hawa kuwapa viza zao ambazo zimekamilika kuwapa bima za afya kuwaeleza tarehe za kusafiri ndege watakazotumia kusafiria, kujua sehemu watakazokaa, watasafiri na nani na watapokelewa na nani,” alisema Mollel


“Wataanza kuondoka kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali duniani kuanzia wiki ijayo na baada ya hapo kila wiki kundi la wanafunzi kuanzia 50 mpaka 70 watakuwa wanaondoka kwenda mataifa mbalimbali,” alisema Mollel.


Mollel aliwataka wanafunzi kuzingatia walichofuata nje ya nchi na kuachana na starehe na badala yake wazingatie masomo na kuhakikisha wanahitimu wakiwa na alama nzuri ili kuwapa moyo wazazi ambao wamejinyima kwaajili yao kuwalipia ada.


Alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa na kawaida ya kufanya mambo ambayo yanasababisha washindwe kumalizia masomo yao hali ambayo inawakatisha tamaa wazazi wao.


“Msiende kunywa pombe wala kwenda klabu za usiku kwasababu kule mnakwenda kufuata elimu. Malizeni masomo mpate kilichowapeleka starehe hata Tanzania zipo,” alisema Mollel


Aiman Mohamed kutoka Mwanza ambaye anatarajia kwenda masomoni nchini India wiki ijayo, alisema anashukuru uratibu uliofanywa na Global Education Link na kumwezesha kupata chuo cha Sharda cha nchini India.


“Kwa dhati kabisa niwapongeza waratibu wa safari yetu Mollel na wenzake kwa namna walivyokuwa karibu nasisi wakati wote wa kuratibu safari na hatimaye mambo yamekuwa mazuri na wiki ijayo tunasafiri kwenda masomoni kutimiza ndoto zetu,” alisema


Rita Nichalaus naye kutoka Mwanza ambaye anatarajia kujiunga na chuo kikuu cha Sharda kilichoko New Delhi India alisema amefurahi kupata elimu ya mambo ambayo wanatakiwa kufanya na ambayo hawatakiwi kuyafanya wanapokuwa masomoni.


“Mwongozo tuliopewa ni muhimu sana kwasababu mwanafunzi anapofika ugenini asipofahamu tabia na tamaduni za wenyeji anaweza kujikuta yuko matatizoni lakini tumeelezwa namna ya kuishi tukiwa huko ni jambo jema na la msingi sana kwetu,” alisema







Tuesday, August 6, 2024

KESI YA WANANDOA KUJERUHI, WAKILI WA SERIKALI AKATAA KESI KUAHIRISHWA.

 

Bharat Nathwani mbele  na mke wake Sangita Nathwani  nyuma kabisa wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam jana kusikiliza kesi inayowakabili ya kumjeruhi jirani yao inayowakabili.

....................................

Na Mwandishi Wetu


UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kujeruhi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wamekataa kuahirishwa kesi kwa madai kuwa wakili wa utetezi anataka kuchelewesha kesi hiyo kwa kudai kuwa anashida ya kiafya.


 


Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliomba pande zote mbili katika kesi hiyo kutumia lugha za kuheshimiana ndani ya chumba cha mahakama kwa sababu kuna watu wanajifunza kutoka kwao.


 


Ombi hilo la kukataa, liliwasilishwa jana Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo, wakati shahidi Kiran Ratilal akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, Edward Chuwa.


 


Mwanga alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kuomba ahirisho la maswali ya dodoso kwa shahidi Ratilal, kwa madai kuwa hawezi kuendelea kwa sababu ya afya yake na pia kuna dawa za kutumia.


 


Baada ya Chuwa kudai hayo, Mwanga alidai kuwa hawawezi kukubali ahirisho kwa sababu, wakili huyo alitakiwa kulisema hilo mapema kabla kesi haijaanza kusikilizwa kuwa ikifika muda fulani waahirishe.


 


"Jamhuri hatuwezi kukubali, wakili alitakiwa kulisema hili mapema anachokifanya ni kutaka kuchelewesha kesi hatuwezi kukubali kuahirisha tunaomba amalize maswali ya dodoso kwa shahidi,"


 


" Mara ya mwisho alisema anaenda Mahakama Kuu, lakini alivyotoka nje alikuwa anazungumza na vyombo vya habari na pia hakusema anaenda kwenye kesi gani,"alidai Wakili Mwanga


 


Hata hivyo, Chuwa alidai kuwa siku hiyo hakusema anakwenda Mahakama Kuu, alidai kuna kazi anakwenda kuifanya na pia alikuwa akizungumza na media saa ngapi?


 


"Naenda kuonana na daktari katika Hospitali Hindul Mandal na siku ya kesi ninaweza kuja na ushahidi hapa mimi nina umri wa miaka 60, nimeomba ahirisho kwa sababu ya ugonjwa,"alidai Wakili Chuwa


 


Hakimu Lyamuya alisema yeye hayuko kwenye nafasi ya kusema kama Wakili ni mgonjwa au sio mgonjwa kwani hali hiyo ni  vile ambavyo mtu mwenyewe anajisikia.


 


"Kwa sababu umesisitiza kwa umri wako wa miaka 60, mahakama inaahirisha kesi hii kwa nafasi ya mwisho ya kufanya maswali ya dodoso ni haki yako, lakini siku ya kesi itakayotajwa inatakiwa ifike mwisho tusiipeleke hii kesi mbali sana,"alisema Hakimu Lyamuya


 


Pia, Hakimu Lyamuya aliwataka watumie lugha ya kuheshimiana pale wanapouliza maswali kwa sababu ni watu wengi wanasikiliza, lakini pia kuna wanafunzi washeria ambao wanajifunza kila kitu kutoka kwao.


 


Hakimu Lyamuya alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kumtuhumu Wakili Mwanga kuwa anamsaidia shahidi, baada ya kupinga shahidi wake kuulizwa swali ambalo tayari alishalijibu.


 


"Mheshimiwa mimi sijamsaidia shahidi kujibu swali bali ninepinga shahidi kuulizwa swali hilohilo ambalo tayari alishalijibu,"alidai Mwanga


 


Kesi imeahirishwa hadi Agosti 15,2024 kwa ajili ya upande wa utetezi kuendelea kumuuliza masawali ya dodoso shahidi.


 


Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam


wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


RAIS SAMIA AACHA ALAMA YA KIPEKEE MOROGORO.

 

Maelfu wanufaika na msaada wa kisheria


Wamshukuru na kutaka huduma ziwe endelevu


 


Na Mwandishi Wetu


RAIS Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Morogoro huku akiacha alama kubwa kwa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na timu ya wanasheria waliosaidia kutoa msaada wa sheria bure kwa maelfu ya wananchi.


Wananchi  wengi walifurahia msaada wa kisheria walioupata kutoka kwa wanasheria wa mpango wa mnsaada wa sheria wa Mama Samia Legal Aid ambao bado wanaendelea kutoa msaada kwenye viwanja vya nane nane mkoani hapa.


Kulikuwa na timu ya wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waliokuwa wakisikiliza kero za kisheria kwenye ziara hiyo na kuzitatua na kulikuwa na timu ingine ya Rais Samia ambayo inaendelea kutoa huduma hiyo katika maonyesho ya nane nane yanayoendelea mkoani Morogoro.


Baadhi ya wananchi wametoa ushuhuda wa namna walivyonufaika na ziara ya Rais Samia kwa huduma za msaada wa kisheria walizopata kwenye ziara hiyo.


Mmoja wa wananchi waliopata msaada wa kisheria kutoka kwa Mama Samia Legal Aid anasema amefurahia mpango huo kwani umekuw mkombozi kwa watu ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili.


“Mpango wa Mama Samia imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi napendekeza kama itampendeza Rais Samia hii isiwe tu kampeni maana kampeni inaisha muda ila ikiwa Taasisi ya kudumu itawasaidia sana wananchi wanyonge ambao wanapambana sana kusaka haki zao kisheria.”


Mkazi mmoja wa mkoani Morogoro  Juma Hamadi ambaye akipata msaada wa kisheria nane nane  alisema alisema  amepata huduma kwa ukarimu wa hali ya juu kwa watumishi wa mpango wa mama Samia na anatarajia matatizo yake ya mgogoro wa shamba yatamalizika.


Anasema wananchi wengi hawana uwezo wa kuweka mawakili kusimamia kesi zao hivyo aliomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kuufanya mpango huo wa msaada wa sheriaa kuwa endelevu.


Mwanaidi Selamani alisema  alitembelea banda hilo la sheria la Mama Samia na amekutana na amepata ufumbuzi wa matatizo yake ya mgogoro wa nyumba ambao ulikuwepo kwa muda mrefu Kibaigwa.


“Hapa kwa msaada wa Rais Samia tunapata msaada wa kisheria bure tunamshukuru Rais Samia huyu mama anawapenda wananchi wake kwa kweli apewe maua yake hii huduma ni mkombozi kwetu,”anasema.


Mkazi wa Morogoro Mjini, Antony Gervas, yeye anasema huduma za msaada wa sheria ziwe endelevu kwani wengi hawana uwezo na kuongeza kuwa katika maonesho ya nanenane amejifunza kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uelewa wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali.


 


“Kwa mpango huu Rais Samia anastahili kupongezwa sana na namshukuru  kwa kampeni hii ambayo imepiga kambi hapa nanenane Morogoro kwasababu itawasaidia wananchi na watanzania kwa ujumla kupata haki zao,”anasema.


 


Naye, Ibrahim Waso mkazi wa Arusha ambaye alihudhuria maonyesho hayo Nane Nane Morogoro  anasema amepata huduma nzuri kwenye banda la kampeni hiyo na amejifunza mambo ya kisheria ya kufuata na kutoa elimu kwa wananchi wenzao wa vijijini.


“Tumepewa namba za kupiga kwa ajili ya msaada wa kisheria tutawapa watendaji wasambaze kwa wananchi ili wanufaike na huduma hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, tunamshukuru sana Rais hakika mama anaupiga mwingi kwa wananchi wake,”anasema.


Mkazi wa  Kihonda Morogoro ,  Jamila Abdalah anasema amefarijika kupata huduma nzuri ambayo hakutegemea kuipa ya elimu ya masuala ya sheria.


“Nampongeza sana Rais kwa kuona umuhimu wa kampeni hii, kweli watu wengi hapa nchini hawana uwezo wa kuweka mawakili  na tunajua mawakili ni ghali lakini ameliona hilo na kuleta kampeni hii ambayo itawasaidia sana watanzania tunashukuru sana,”anasema.  


Kampeni hiyo hadi sasa imewafikia wananchi zaidi ya 490,000 wa mikoa saba na kutatua migogoro iliyokuwa ikiwakabili.


Kampeni hiyo inafanyika kwa miaka mitatu na ilianza mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ikilenga kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza.


WATANZANIA WAHIMIZWA KULA NA KUNYWA BIDHAA ZA KOROSHO

 

NA HADIJA OMARY , LINDI.


Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Ikulu (kazi maalum)  George Mkuchika Amewahimiza watanzania kupenda Kula na kunywa bidhaa za korosho kwani zinavirutubisho vingi vya kupambana na magonjwa pamoja na kufanya uhamasishaji wa  uongezaji wa thamani ya zao hilo.



Mkuchika ametoa Rai hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi, Wadau na wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa maadhimisho ya siku ya Kula na Kula korosho ambayo ni mahusisi kwa ajili ya uhamasishaji wa ulaji na unywaji korosho.


Katika maadhimisho hayo Wananchi Wadau na wakulima wa korosho walijionea bidhaa mbalimbali zitokanazo na korosho kama vile chapati, maandazi, kashata , maziwa ya korosho pamoja na mvinyo.


Amesema ulaji wa  korosho licha ya kumlinda Mlaji na magonjwa lakini pia ni husaidia kukuza uchumi kwa mtu mmoja Mmoja na Soko la ndani .


" Kwa upande wa afya ya Binadamu ukila korosho zilizobanguliwa unakuwa na faida ya kuzuia ugonjwa wa moyo kwa kuzuia shindikizo la damu, ukila korosho unaongeza viini lishe vinavyozuia hatari ya kupata ugonjwa wa kansa pamoja na kuzuia Hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari"




Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele, Dr. Rashid Kidunda  amesema licha ya Mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara kuwa  ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho lakini ni asilimia 10 pekee ya kile kinachozalishwa ndicho kinachotumika kama chakula kwa wakazi wa mikoa hiyo


"Unaweza kuona ni kwa namna gani tupo chini Katika ulaji na unywaji wa korosho kwa hivyo ili kukuza Soko la ndani tuliamua  kuzifanya siku ya tarehe 5 August kila mwaka tuadhimishe siku hii" Amesema Kidunda 


Amesema Nchini Tanzania korosho imeendelea kuwa zao kubwa la kibiashara  Katika kuchangia kipato cha wakulima hasa Katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma 


" Kwa sasa tumeona Mikoa mingine 17 ikiingia Katika kilimo cha zao hilo na sisi kama TARI Naliendele tumepewa jukumu la  kufanya utafiti na kutatua changamoto za wakulima wa zao Hilo" alifafanua 


Kaimu mkurugenzi wa Bodi ya korosho Reveliani  Ngaiza amesema zao la korosho ni zao la kipekee tofauti na mazao mengine kwa kuwa Lina matumizi mengi kuanzia kwenye Majani, Mbegu,  Tawi , shina na hata mzizi wake


" Ukiacha ulaji wa korosho zao la korosho kwa upande wa Majani yanatumika kama Dawa kutibu minyoo tumboni, kuzuwia kuhara , kutoa Gesi tumboni pamoja na kutibu vidonda vya tumbo"


"Lakini ukichukia Jana ukachanganya na gome la mkorosho unapata Dawa ya kutibu ugonjwa wa meno, maganda ya korosho baada ya kubangua yakikamuliwa upatikana kimiminika chakutengeneza wino wa kuandikia kupitia kalamu"







Sunday, August 4, 2024

KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID KUNUFAISHA MAELFU NANENANE.

 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro


WANANCHI wanaopata msaada wa kisheria za mama Samia Legal Aid zinazoendelea kutolewa kwenye maonyesho ya Nane nane mkoani Morogoro wameelezea namna walivyonufaika na huduma hizo.


Wakizungumza mkoani hapa jana, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka huduma hizo kwenye maonyesho hayo ambapo wamesema zimekuwa mkombozi kwao.


Renatha Manda alimshukuru Rais Samia kwa msaada wa kisheria baada ya kusaidiwa na huduma hizo alipokwenda kwenye maonyesho hayo.


“Nilikuwa na tatizo la mirathi nikaenda wakanipa ushauri wa kisheria na kwa kweli nimeridhika na najua suala langu litafika mwisho hivi karibuni,” alisema


Luciani Mwanitu kutoka Nzuguni Dodoma alisema alifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid ambapo amepata elimu kuhusu namna wanavyotoa huduma hizo na alishauri huduma hizo zipanuliwe ili wananchi wengi hasa wa vijijini waweze kufikiwa.


“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuanzisha huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi sana. Nawaomba waisogeze zaidi vijijini ili wananchi wengi zaidi waendelee kunufaika nayo,” alisema


Uwezo Maulid mkazi wa Shinyanga aliyefika kwenye banda hilo alisema amesaidiwa kwenye kesi ya mirathi ya mume wake ambaye alikuwa mtumishi wa umma kwenye manispaa ya Shinyanga Mjini.


“Nimefika hapa wamenipokea vizuri wamenipa mwanasheria wa huko Shinyanga ili aweze kunisimamia kupata haki zangu za msingi mimi mke wa merehemu Seif,” alisema na kuongeza


“Naomba mheshimiwa Rais aweze kunisaidia kwasababu kila ninapokwenda mahakamani naambiwa nirudi nyumbani mtandao umegoma kwasababu siku hizi kesi zinaendeshwa kwa mtandao. Huu ni mwaka wanne tangu mwaka 2021  nilipokonywa hadi nyumba na ndugu wa marehemu,” alisema


Alisema lakini baada ya kufika kwenye banda la mama Samia Legal Aid na kupewa mwanasheria anaamini suala lake litashughulikiwa na kufika mwisho ili aweze kupata haki zake kama mjane wa marehemu mume wake.






Wananchi wakipata huduma za msaada wa sheria bure banda la Mama Samia Legal Aid mkoani Morogoro kwenye maonyesho ya Nane Nane