Sunday, December 31, 2017

SUBIRA MGALU ATOA AGIZO KWA TANESCO.



 Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wilayani Bagamoyo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya siku mbili aliyoianza jana Tarehe 30 Desemba 2017 na leo Tarehe 31 Desemba 2017.
...........................
Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka mameneja wa Tanesco mikoa na wilaya kote nchini kuwaunganishia umeme wananchi wakaokuwa wameomba na kukamilisha malipo yao ndani ya siku saba tu.

Agzo hilo amelitoa wilayani Bagamoyo alipokuwa katika ziara ya kukagua mradi wa kusambaza umeme vijijini REA awamu ya tatu unaotekelezwa nchi nzima.

Alisema kila meneja wa TANESCO anatakiwa kuhakikisha kuwa, wateja wote waliojaza fomu na kukamilisha malipo yao wanatakiwa kuunganishwa umeme ndani ya siku saba tu ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wa kusubiri kuunganishiwa umeme kwa muda mrefu.

Aidha, alisema kufuatia agizo hilo atafanya ziara kwenye ofisi za TANESCO nchi nzima ili kuona idadi ya wananchi walioomba na kulipia huduma ya umeme na idadi ya waliounganishwa na kwamba meneja atakaeshindwa kutekeleza hilo anapaswa kutoa maelezo juu ya kwanini mteja hakuunganishiwa umeme ndani ya siku saba toka kulipia kwakwe.

Naibu waziri huyo wa Nishati amewataka Wananchi waliopo kwenye vijiji vinavyopitiwa na mradi wa kusambaza umeme vijijini REA wametakiwa kutumia fursa ya mradi huo kuchukua fomu na kulipia gharama ya shilingi elfu ishirini na saba tu ili waunganishiwe umeme kupitia REA awamu ya tatu.

Alisema Serikali imewathamini wananchi wake kwa kuwepelekea mradi wa kusambaza umeme vijijini REA ili kila mwananchi apate huduma hivyo ni matarajio ya serikali kuona fursa hiyo inatumika vizuri.

 Kwa upande wao wabunge wa jimbo la Bagamoyo na Chalinze wamempongeza Naibu waziri huyo wa kwanza mwanamke katika wizara ya nishati kwa kujali wananchi na kuwatembelea vijijini.

Dkt. Shukuru Kawambwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo amesema kufika kwa naibu waziri huyo vijijini kutampunguzia maswali anayoulizwa na wananchi kuhusu vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme.

Nae mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema wananchi wanajenga imani na serikali yao ya awamu ya tano hasa pale wanpoona kiongozi kama Naibu waziri anawatembelea na kusikiliza vilio vya wananchi
Alisema mfumo huo unawafanya wananchi kuimanini serikali yao hasa pale ilani ya chama Cha mapinduzi inatekelezwa kwa vitendo.

Wakati huo huo Naibu waziri wa Nishati huyo amewahakikishaia wananchi wa Kijiji cha Kongo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, kuwa watapata umeme katikati ya januari 2018 ili kuwaondolea kero ya kukosa umeme katika kijiji hicho kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Katika hatua nyingine Naibu waziri wa nishati ambae ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani amechangia shilingi laki mbili kwaajili ujenzi wa ofisi ya CCM katika kijiji cha Kongo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo.

Mradi wa kusambaza umeme vijijini REA awamu ya tatu mzunguuko wa kwanza unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2019 kwa kufikisha umeme katika vijiji 3559 ambapo REA awamu ya tatu mzunguuko wa pili unatarajiwa kuanza kutekelezwa 2019-2021 ili kutekeleza lengo la serikali la kuvipatia umeme vijiji vyote 7873 vilivyobaki ifkapo mwaka 2021.


 Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wilayani Bagamoyo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya siku mbili aliyoianza jana Tarehe 30 Desemba 2017 na leo Tarehe 31 Desemba 2017.
Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akitoa maelekezo kuhusu nguzo za umeme zilizokaa kwa muda mrefu katika kijiji cha Kongo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo.
Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akipokea na kusoma mabango yaliyowasilishwa kwake na wananchi wa kijiji cha Kongo kata ya Yombo Halmashauri ya Bagamoyo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani wakilalamikia kukosa umeme kwa zaidi ya miaka 40 sasa licha ya kuwa kijiji hicho ndicho chenye mtambo maji wa Ruvu chini.

Naibu  Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akisikiliza maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Msimamizi wa Miradi ya umeme vijijini REA Mkoa wa Pwani Mhandisi Mohamed Sauko (Kushoto) kushoto mwa Naibu waziri ni Meneja wa TANESCO wilaya ya Bagamoyo Daniel Michael Kyando, na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa.

Monday, December 25, 2017

RC PWANI ATEMBELEA KIWANDA CHA BETRI KIBAHA.


Mkuu wa Mkoa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo  jana Jumapili Tarehe 24 Desemba 2017. amekgua kazi ya ujenzi wa kiwanda cha kampuni ya China Boda Technical Group Ltd inayojenga kiwanda cha kutengeneza betri za magari katika Plot No 21 TAMCO Industrial Estate, Kibaha, Mkoa wa Pwani. 

Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani amefanya ziara hiyo ili kukagua kasi ya ujenzi na kupokea changamoto zozote wanazokabiliana nazo ili kuona namna ya kushirikiana nao katika kuzitatua ili kufikia malengo.

Katika ziara hiyo amefurahishwa na kasi ya ujenzi inavyoendelea na kusema kuwa ni ya kuridhisha.

Aidha alipata fursa ya kuwasiliana kwa simu na Kandarasi wa Ujenzi huo ambaye amemuhakikishia kwamba ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo atakuwa amekamilisha kazi ya ujenzi kama mkataba wake unvyoonesha. 

Alisema licha ya kazi nzuri inayoendelea katika kiwanda hicho bado kuna kazi kubwa ya ujenzi wa barabara kuingia kwenye kiwanda yenye upana wa meta 15 ambayo inatakiwa kujengwa na NDC kulingana na makubaliano ya Mkataba. 

Aliongeza kuwa, ili kukamilisha ujenzi Kiwanda hicho, kuna michoro ya ujenzi wa majengo mbalimbali inayotakiwa kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ili ujenzi wa miundombinu hiyo ianze mara moja.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ameahidi kushughulikia changamoto hizo mapema iwezekanavyo ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.

Kazi hiyo ya ujenzi inatakiwa ikamilike kabla ya mvua za masika zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Machi, 2018 ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kipindi cha mvua.

Sunday, December 24, 2017

NAIBU WAZIRI NISHATI ASHANGAZWA NA TATIZO LA UMEME BAGAMOYO.



Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ameshangazwa na tabia ya kukatika umeme mara kwa mara katika wilaya ya Bagamoyo hali ya kuwa Serikali imeshaweka mikakati ya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika.

Naibu waziri huyo aliyasema hayo mjini Bagamoyo alipokuwa akifunga maonesho ya wajasiliamali katika viwanja vya shule ya msingi Mbaruku.

Alisema Serikali imeshaweka mikakati ya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika nchi nzima ili kuenda sambamba na mahitaji katika kuelekea kuwa nch ya viwanda.

Aliongeza kuwa katika mikakati iliyowekwa na serikali iliwahusisha mameneja nchi nzima ili nao waeleze changamoto zinazowakabili na hatimae kuzipatia ufumbuzi ili kuondokana na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.

Aliongeza kwa kusema kuwa, ujenzi wa viwanda, wajasiliamali kujikwamua kiuchumi na maendeleo kwa ujumla vyote hivyo vinategemea upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kufikia malengo.

Alisema kutokana na mikakati hiyo anashangaa kuona mapaka sasa bado kuna tatizo la kukatika umeme Bagamoyo jambo ambalo lilipaswa kuisha.
Alimuagiza meneja wa TANESCO wilaya ya bagamoyo kuhakikisha

anashughulikia changamoto zinazomkabili ili kuondoa tatizo hilo ili kuepuka kuwapa hasara wananchi ambao wanategemea umeme katika kuzalisha na kuhifadhi bidhaa mbalimbali.

Naibu waziri huyo alikuwa na ziara katika wilaya ya Bagamoyo ambapo alipata nafasi ya kuongea na wananchi katika kitongoji cha sanzale kata ya Magomeni na baadae kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo katika Uwanja wa shule ya msingi Mbaruku. 

Aidha, aliwasikiliza wananchi wa kitongoji cha Sanzale ambao hawajafikiwa na huduma ya umeme na kuwahakikishia kuwa Mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu utawafikia ili nao wapate huduma hiyo ya umeme.

Naibu waziri huyo ameridhishwa na hali ya ujenzi wa nyumba za kuishi zilizojengwa katika kitongonji cha Sanzale na kuahidi kutatua tatizo la umeme.

SUBIRA MGALU APONGEZA WANAWAKE BAGAMOYO.


Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu ambae pia ni naibu waziri wa Nishati, (katikati) akiangalia bidhaa ya unga wa viazi vitamu unaotengenezwa na wajasilimali wanawake Bagamoyo wakati wa kufunga maonesho hayo yaliyofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Mbaruku, wa kwanza kulia ni katibu tawala wa wilaya ya Bagamoyo,Erica Yegela , wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, fatuma Latu na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis.
...........................................

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu amepongeza jukwaa la Uwezeshaji Wanawake wilayani Bagamoyo kwa hatua waliyopiga katika kujikwamua kiuchumi.

Subira Mgalu aliyasema hayo leo jumapili Desemba 24 2017 wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali yaliyoandaliwa na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo katika viwanja vya shule ya msingi Mbaruku.

Alisema Jukwaa hilo limepiga hatua hivyo ni jukumu la serikali kuunga mkono juhudi hizo ili wanawake waweze kujikwamua kupitia fursa mbalimbali zilizoandaliwa na serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Mbunge huyo wa viti maalum Mkoa wa Pwani ambae pia ni naibu waziri wa Nishati alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo kuhakikisha anaunga anashirikiana na wanawake hao ili waweze kufikia malengo yao.
Alisema kwa sasa Bagamoyo kuna fursa nyingi za kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kuanza mwezi januari ambapo mahitaji ya vitu mbalimbali yataongezeka.

Aidha, alitoa wito kwa wajasiliamali hao wanawake kujiwekea malengo ya kuzalisha bidhaa malighafi ambazo zitahitajika kwenye viwanda vinavyojengwa wilayani Bagamoyo ili wanawake wajasiliamali wafaidike kupitia maendeleo ya viwanda.

Alisema vipo viwanda kadhaa ambavyo vinahitaji malghafi kutoka kwa wajasiliamali hivyo ni vyema wanawake wakatumia fursa hiyo kujua ni aina gani ya bidhaa zinazohitajika, ubora wake na namna ya kuzalisha.
Aliongeza kwa kusema kuwa dhamira ya Rais John Magufuli ni kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini na badala yake kuwasogezea fursa ili waweze kuzitumia kubadilisha maisha yao.

Alisema kwa Bagamoyo fursa nyingi zimeshandaliwa na utekelezaji wake tayari umeshaanza ikiwemo ujenzi wa viwanda vya aina mbalimbali.

Subira Mgalu alimtaka Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi bagamoyo kutafuta namna ya kupata wafadhili watakaowezsha katika utekelezaji wa miradi ya wanawake haku yeye akiahidi kushirikiana nao.

Nae mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa alisema wananchi wa Bagamoyo kwa sasa wanapaswa kutumia fursa zilizopo ili kujiongezea kipato.

Alisema ni vyema wakaunganisha nguvu kwenye vikundi ili wafaidike na asilimia tano zinazotolewa na Halmashauri kwaajili ya kinamama na vijana.

Akizungumza mbele ya mgeni rasmi mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Devis alisema anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuonesha kuthamini kwa wananchi wa hali ya chini na kufanya juhudi za kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Teddy alitoa shukrani kwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na Mbunge wa jimbo la Bagamoyo kwa namna walivyotoa ushirikiano ili kufanikisha maonesho hayo ambayo ni njia ya kuwakomboa wanawake kiuchumi.

Alisema kupitia maonesho hayo wajasiliamali wengi wamefaidika kwa kujua fursa mbali mbali ambazo wakizitumia wanaweza kupiga hatua.
  Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis akimkaribisha mgeni rasmi  katika kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyoandaliwa na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo.
  Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis (kushoto) akimkabidhi zawadi Mgeni rasmi Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu, (Kulia).

Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu ambae pia ni naibu waziri wa Nishati, akiwa ameshika kikaango cha asili cha kupikia Mboga katika moja ya banda la wajasiliamali wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali mjini Bagamoyo leo Tarehe 24 Desemba 2017.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Omari Latu, akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyofanyika uwanja wa shule ya msingi Mbaruku. 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya wajasiliamali Bagamoyo yaliyofanyika uwanja wa shule ya msingi Mbaruku.