Tuesday, March 28, 2017

NAPE AKABIDHI OFISI KWA MWAKYEMBE MJINI DODOMA.

 
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakikabidhiana hati za makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
.........................
Aliyekuwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye leo amekabidhi rasmi ofisi kwa Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika makabidhiano hayo yaliyohudhuriwa na watendaji wakuu wa Wizara, Mhe. Mwakyembe ameahidi kuwa licha ya kukabidhiwa ofisi, anaamini kuwa Mhe. Nnauye bado ni mdau mkubwa wa sekta za Wizara  na kuwa anategemea kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwake.

Aidha Waziri Mwakyembe ameahidi kuendeleza yote mazuri yaliyo anzishwa na Mhe. Nnauye katika kuimarisha ufanisi wa Wizara na kuhakikisha inakuwa ni moja ya Wizara za mifano nchini. Amesisitiza kuwa katika kipindi kifupi alichokaa Wizarani, Mhe. Nnauye alianzisha mabadiliko makubwa na watu wameanza kuifahamu vizuri Wizara.

Kwa upande wake Mhe. Nnauye amemshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana kubwa ya kusimamia Wizara kwa kipindi cha miezi 15 huku akiwa ndio kwanza amekuwa mbunge katika awamu yake ya kwanza.Aidha Mhe. Nnauye ameahidi kuendela kushirikiana na Wizara kwa ukaribu kwani ni kweli yeye ni mdau mkubwa wa sekta za wizara hii.

“Heshima aliyonipa Mhe. Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumuunga mkono katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini,” alisema Mhe. Nnauye. Aidha alisisitiza kuwa, tofauti na maneno ya mitandaoni, yeye atabaki kuwa mtiifu kwa Rais, Serikali na chama chake.


Pia amewashukuru watendaji wote wa Wizara kwa kumpa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote alichofanya nao kazi na kuwaomba kutoa ushirikiano huo huo kwa Waziri wa sasa Mhe. Mwakyembe.

Monday, March 27, 2017

MAAFISA HABARI HARAKISHENI KUTOA TAARIFA ZA SERIKALI KWA UMMA

ABASII
MAAFISA Habari na Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutoa taarifa kwa haraka zaidi kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili kusaidia kutangaza Mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.

Hayo yamesemwa jana Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza na maafisa habari na TEHAMA katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).

Dkt. Abbas alisema kuwa mara baada ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa Habari wana wajibu wa kuweka taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati kwa kuwa malengo ya tovuti hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za Serikali.

“Tukifungua tovuti hizi tunapaswa kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la upashanaji wa habari na taarifa za miradi ya  Serikali isisubiri tena michakato, isipokuwa kama kutatokea suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi kutoka katika ngazi za juu katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi

Aliongeza kuwa, taaluma ya habari katika zama za sasa inahitaji ubunifu mkubwa katika kuisemea Serikali kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha umma badala ya kutumia njia za kawaida na za kila siku.

“Katika maeneo yetu ya kazi tuna vituo vya redio na televisheni ambazo zinawahitaji Viongozi wetu kufanya nao mahojiano maalum kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali, ni wajibu wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha tunaisemea Serikali” alisema Dkt. Abbasi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima utendaji kazi wa kila Afisa Habari katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Mikoa na Wilaya na Mikoa ili kuona ni namna gani ameweza kutoa taarifa za Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.

“Katika kipindi hiki Serikali ya Awamu ya tano imetekeleza na inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya umeme vijijini (REA), na ujenzi wa miundombinu mingine kwa kutumia fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kueleza wananchi utekelezaji wa miradi hiyo” alisema Dkt. Abbasi.

Alisema kuwa ili taarifa hizo za utekelezaji wa mafanikio hayo ya Serikali ziweze kuwafikia wananchi, ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano kujenga na kuimarisha mtandao wa mawasiliano baina yao pamoja na  watendaji wengine katika maeneo yao ya kazi.

Aliongeza kuwa ubunifu ni siri nyingine ya mafanikio katika suala la upashanaji wa taarifa za Serikali, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuwa mbunifu badala ya kulalamika kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili katika maeneo yao ya kazi ikiwemo ufinyu wa bajeti na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi.

Mafunzo hayo ya wiki moja yalishirikisha mikoa na Halmashauri za Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Dar es salaam, Pwani na Dodoma.

Friday, March 24, 2017

KIINGILIO TAIFA STARAS NA BOTSWANA 3,000.

Taifa-Stars-of-Tanzania-

Taifa Stars – timu ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa mwaka 2017 inaingia uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya kalenda ya FIFA.

Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeatangaza kushusha bei ya kiingilio kwa watu watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.

“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio vya bei ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia gharama kidogo kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,” ameagiza Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu watakaoketi Majukwaa Maalumu – VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi VIP “B” na “C” watalipia Sh 10,000.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake aliwathibitishia Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.

“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu.

Kwa upande wa Peter Buffler – Kocha Mkuu wa Botswana, alisema kwamba anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa kikosi cha Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu. Mchezo ambao pia ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.


SERENGETI BOYS WAPATA CHANJO YA MANJANO.

KIMOOOOOOOOOOOOOO
Timu ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys leo Machi 24, wamefanyiwa chanjo ya ugonjwa wa manjano (yellow fever) kabla ya kuanza safari ya kwenda Morocco, Cameroon na Gabon.

Timu hiyo imefuzu kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17. Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Mei 14 mwaka huu na mapema mwezi ujao itasafiri kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.

Kambi hiyo itakuwa ni ya mwezi mmoja (Aprili 5 hadi Mei 1, 2017) kabla ya kuwa na kambi ya wiki moja huko Cameroon (Mei mosi hadi Mei 7, mwaka huu) na baadaye itafanya kambi nyingine Gabon (Mei 7 mpaka Mei 13) angalau kwa wiki moja kabla ya kuanza fainali hizo Mei 14, mwaka huu.