Friday, November 10, 2023
Thursday, November 9, 2023
MAKONDA ATOA MAAGIZO KWA MAWAZIRI, KAGERA
Na Alodia Babara
Bukoba.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, ametoa maagizo mbalimbali kwa Mawaziri wa wizara nne hapa nchini ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuwapigia simu mawaziri hao na kutoa majibu ya changamoto na kutatua changamoto hizo.
Mawaziri waliopigiwa simu ni pamoja na waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, Waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun, waziri wa uchukuzi Makame Mbarawa na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa.
Makonda ametoa maagizo hayo leo Novemba 9, 2023 wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara akiongea na wananchi mkoani Kagera uliofanyika uwanja wa mashujaa Mayunga.
Moja ya changamoyo zilizotajwa ni pamoja na ujenzi wa soko kuu, kingo za mto Kanoni, ujenzi wa stend kuu, uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Bukoba, tatizo la nida maeneo ya mipakani na ujenzi wa barabara za lami.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akijibu kuhusu changamoto za ujenzi wa soko kuu, stend kuu na kingo za mto Kanoni amesema kuwa maagizo ya katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Makonda ameyapokea na kufanyia utekelezaji haraka, mwezi Desemba 2023 atafika mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua maeneo itakapotekelezwa miradi hiyo
Akijibia changamoto ya vitambulisho vya NIDA kwa upande wa wananchi waishio mipakani waziri wa mambo ya ndani Hamad Massaun amesema kuwa, swala la vitambukisho vya NIDA katika maeneo hayo wizara inalifanyia kazi ili kuharakisha zoezi na wale wenye haki ya kupata kadi za NIDA waweze kuzipata.
Amesema wameanza mkakati wa kutembelea mikoa iliyopo maeneo ya mpakani kwa kuanza na mkoa wa Mara na baadaye watakwenda Kagera.
Makonda amewataka Askari wa usalama barabarani wote nchini kutowaonea waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na badala yake watumie sheria wanapowakamata na kuwakuta na makosa.
HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAVUKA MALENGO UKUSANYAJI WA MAPATO
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imevunja rekodi ya kukusanya kiwango katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuaniza Julai mpaka Septemba 2023
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Bagamoyo Mhe. Halima Okashi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo tarehe 09 Novemba 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.
Akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani Mkuu huyo wa Wilaya aliwapongeza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 kuanzia Julai mpaka Septemba 2023.
Katika kipindi hicho Halmashauri imekusanya zaidi ya shiling bilioni 1 sawa na asilimia 27.7 ambapo ni asilimia 2.7 zaidi ya malengo waliyojiwekea ya asilimia 25.
"Niwapongeze Madiwani wa Kata zote pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato kwenye taarifa yenu inaonyesha mapato yaliyopatikana ni asilimia 27.7 ambapo malengo yalikuwa ni asilimia 25 hivyo hongereni sana kwa ongezeko hilo la asilimia 2.7" alisema Bi Halima Okashi
Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliwataka Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kuongeza ubunifu zaidi ili kuweza kupata wigo wa kuongeza mapato utakaopelekea uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo akipokea pongezi hizo kwa niaba ya Baraza la Madiwani Mhe. Mohamedi Usinga aliahidi kuendelea kuboresha vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuboresha mapato kwenye Halmashauri hiyo.
Wednesday, November 8, 2023
WANUFAIKA MRADI WA KLIC WATAKIWA KUTUNZA VIFAA VYA TEHAMA-TET
Na Andrew Chale,Dar es Salaam.
Shule zote nchini zilizonufaika na vifaa vya mradi wa KOREAN E-LEARNING IMPROVEMENT COOPORATION(KLIC) ulio chini ya Ofisi ya Elimu ya Gwangju Metropolitan ya nchini Korea ya Kusini, wenye lengo la kuboresha elimu nchini katika eneo la TEHAMA, wametakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri , kiusahihi na kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utafiti,Habari na Machapisho waTaasisi ya Elimu Tanzania(TET), Bw. Kwangu Masalu leo tarehe 8/11/2023 katika shule ya Sekondari Kimbiji iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam katika ziara ya ujumbe wa watu kutoka korea ulipofika shuleni hapo kwa ajili ya kugawa vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia masomo pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo ya namna ya kuvitumia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo .
Mwakilishi wa walimu waliopo kwenye ziara hiyo kutoka nchini Korea Kusini, Bwana.Kim Chi Gon ameeleza kuwa , wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanakuza utumiaji wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini na kwani kwa sasa ulimwengu umebadilika sana hasa katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Twidike Ntima ameeleza kwamba shule hiyo kuwa moja ya shule za mfano wa kupata vifaa vya TEHAMA ni jambo kubwa ambapo imesaidia sana kwa walimu kuweza kufanya kazi kwa urahisi na kuwa endapo masuala ya TEHAMA yataendelea kusambaa nchi nzima basi wanafunzi nchini na walimu wataweza kupiga hatua katika masuala ya elimu.
Naye Mkuu wa shule hiyo Bi. Joyce Ndaona amesema kuwa kwa sasa walimu wa shule hiyo wamepata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa nchini Korea ya Kusini ambapo wameweza kupata ujuzi wa kurahisishiwa kazi hasa katika eneo la ufundishaji na kuwapa nafuu wanafunzi kutumia TEHAMA kwenye ujifunzaji tofauti na awali.
Hata hivyo ugeni huo wa walimu na wanafunzi ukiwa katika shule hiyo ya Kimbjiji, uliweza kujionea namna wanafunzi wanavyoonesha uelewa katika masomo yao ambapo waliweza kuonesha utaalamu wao kupitia masomo ya fikizia na Uchoraji na baadae wanafunzi hao kuweza kufanya mafunzo kwa vitendo.
WAFANYABIASHARA MKURANGA, KIBITI WAMSIFU SAMIA UHURU WA BIASHARA.
Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
WAFANYABISHARA wilayani Mkuranga na Kibiti, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuliza dhorobu ya hali ya biashara nchini.
Wamesema kwenye wilaya hizo biashara zinafanyika kwa amani na utulivu bila usumbufu tofauti na miaka ya nyuma.
Wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwenye mkutano kati ya wafanyabishara wa wilaya hizo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) inayoendelea mkoani Pwani yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wafanyabishara.
Mfanyabiashara Hassan Mbwana Kambangwa, amesema wafanyabiashara kwa asilimia kubwa wilayani humo wananufaidika sana tangu kuingia kwa utawala wa Rais Samia.
Amesema "Kimsingi namshuruku Rais Samia kwa kutuletea ugeni uliotupa fursa ya kuzungumza changamoto zinazotukabili, lakini sisi tangu kuingia kwa utawala huu wa Mama Samia tunafaidika nao kwa asilimia kubwa."
Mfanyabiasha huyo ametolea mfano wa mambo wanayofaidika nayo kuwa ni mikopo, uhusiano mazuri na halmashauri lakini pia taasisi mbalimbali za kifedha ziko huru kuwasaidia wafanyabiashara.
Amesema serikali imezingatia suala la amani na utulivu na kwa mikoa mingi ilikua inapata changamoto nyingi lakini hapa wilaya ya Mkuranga wafanyabiashara wako huru na wanafanyabiashara bila bugudha.
"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan tunafanyabiashara kwa amani lakini pia tunashukuru ujio huu wa leo umefanya tuweza kufunguka yale ambayo yako ndani ya moyo na tunaamini mtayafikisha," Kambangwa.
Naye mfanyabishara Wilaya ya Kibiti, Salim Juma, amempongeza Rais Samia kwa kuona sekta ya wafanyabishara ni sehemu ya uchumi wa Taifa na kuamua kuungana kwa pamoja kutatua kero zao.
"Ili kuwa na ustawi tumefanikiwa kumpa Rais Samia, ambaye ameona umuhimu wetu na kutambua mchango wetu ndio maana leo viongozi mpo hapa," amesema Juma.
Mwisho























































