Thursday, November 2, 2023
Wednesday, November 1, 2023
UTAFITI WA GST WAONGEZA KASI YA UKATAJI LESENI MTWARA
Serikali kupitia Taasisi ya Jilolojia na Utafiti wa Madini (GST) imefanya utafiti wa awali na kuainisha madini yanayopatikana katika Mkoa wa Mtwara hatua iliyosaidia wananchi kukata leseni ya utafiti na kujihusisha uchimbaji wa dhahabu ambao unawapatia kipato hasa katika maeneo ya Nanyumbu na Masasi mkoani humo.
Hayo yameelezwa leo Novemba Mosi 2023, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt, Steven Kiruswa, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu swali namba 38 la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Tunza Issa Malapo aliyeuliza ni lini Serikali itafanya utafiti wa uwepo wa Madini Mkoani Mtwara.
Katika majibu yake, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia GST imefanya utafiti wa awali na kuainisha madini yapatikanayo katika Mkoa wa Mtwara.
“Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa madini hayo ni kinywe; vito aina ya ruby, sapphire, rhodolite, amazonite na green tourmaline; metali aina ya dhahabu, shaba, manganese na chuma; madini ya viwanda kama marble na chokaa. Aidha, madini mengine ni mchanga wenye madini mazito yaani heavy minerals kama rutile, titanium, ilmenite, zircon na magnetite.” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mhe. Malapo aliyetaka kujua kama wananchi wa Mtwara wanafahamu kuhusu uwepo wa madini hayo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa baada ya kufanya utafiti huo, GST ilitoa mrejesho kupitia Afisa Madini Mkoa Mtwara na kukabidhi machapisho ya madini kwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara.
Ameongeza kuwa wananchi wamepata mwamko wa kukata leseni za utafiti na uchimbaji ikilinganishwa na kipindi kabla ya utafiti hasa katika madini kama graphite lakini pia maeneo yenye dhahabu yamepelekea wananchi kujihusisha uchimbaji ambao unawapatia kipato hasa katika maeneo ya Nanyumbu na Masasi.
KIKWETE: SERIKALI ITALINDA VIJANA WAPATE AJIRA KWA VIGEZO VYA UTAALAMU NA SI UZOEFU KAZINI.
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema serikali itahakikisha inawalinda vijana kwenye soko la ajira kwa kuhakikisha ajira zao za kwanza kwenye utumishi zinazingatia vigezo vya utaalamu wa kada husika na sio uzoefu kazini.
Kikwete amesema hayo leo Jumatano Novemba 01, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ngwasi Kamani aliyehoji kigezo cha kutakiwa uzoefu katika kuomba kazi kwa vijana waliohitimu vyuo kuwa ni ubaguzi kwa vijana wanaoanza kuomba ajira.
"Ajira za serikali zinatekelezwa kwa kuzingatia sera ya menejimenti na ajira ya mwaka 2008. Kwa mujibu wa aya ya 4 kifungu cha 2 (i) inaelekeza kwamba ajira ya kwanza hususani kwa wale wanaoajiriwa kwa cheo cha kuanzia kwenye miundo ya serikali itafanyika kwa kuzingatia vigezo vya utaalamu bila kujali uzoefu isipokuwa kama ajira husika itahitaji kuwa na uzoefu. Suala la uzoefu lipo kwenye madaraja ambayo si ya kuingilia kazini kama nafasi za waandamizi, viongozi au kada ambazo uzoefu ni sifa za msingi kuingia kama vile udereva ambao mtumishi lazima ajue kuendesha gari kwa viwango vilivyowekwa." Amesema Kikwete.
Akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge Kamani aliyetaka kujua kauli ya serikali kwa waajiri wa sekta binafsi wanaoendelea kutumia kigezo cha uzoefu kutangaza ajira pamoja na serikali kuwatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu wote wanaojitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma, Naibu Waziri Kikwete amesema serikali kupitia kwa ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia vigezo vinavyotakiwa katika soko la ajira huku wakiendelea kutoa maelekezo ya mara kwa mara kuzingatia hilo.
"Pamoja na utaratibu wa kawaida wa kwenye soko la ajira, lakini kwenye sekta binafsi kinachoangaliwa ni tija ili mtu apate faida kwenye jambo lake lakini serikali itaendelea kusimamia utoaji wake wa ajira." Amesema.
Sambamba na hilo, Kikwete alikamilisha majibu yake hayo bungeni kwa kusema kwasasa serikali inaendelea kukamilisha sheria na muundo wa utumishi ambao utawatambua vijana wote wanaojitolea ili waweze kuingia kiurahisi katika soko la ajira.
ASKOFU BAGONZA: KUWENI NA TABIA YA KUANDIKA HISTORIA ZENU MKIWA HAI.
![]() |
Na Alodia Babara.
Karagwe.
Askofu wa kanisa la kiinjili la kirutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe Benson Bagonza ameisihi jamii ya watanzania kuwa na tabia ya kuandika mambo yao wakiwa bado wako hai badala ya kusubili waandikwe na watu wengine baada ya kuwa wameaga duniani.
Askofu Bagonza ameyasema hayo Oktoba 31, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha mzee Clement Nsherenguzi (87) mkazi wa kata ya Bugene wilaya ya Karagwe.
Bagonza amesema kuwa, baadhi ya watu wanaogopa kuandika historia zao wakiwa bado wako hai badala yake wanasubili kuandikwa na watu wengine, jambo ambalo siyo jema kwani wanapoandika wenyewe inatoa mwanya mpana kwao kipi waandike na kipi wasiandike.
Anatolea mfano wa aliyekuwa katibu muhtasi wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere aliyejulikana kwa jina la Joan Wicken ambaye alisha kufa na kabla ya kifo chake alipanga kuandika historia ya hayati baba wa Taifa kwa kutumia kumbukumbu mbalimbali zilizokuwa zinahifadhiwa (dayaries) lakini akasita na kusema historia hiyo itaandikwa baada ya miaka 30.
"Maisha yetu kama wanadamu ni kitabu, lakini kile kitabu kina mambo yaliyoandikwa na ambayo hayajaandikwa na mengine hayaandikiki, nilipewa mwaliko kwenda mjini London kuzindua kitabu cha hayati baba wa Taifa sikwenda lakini kitabu hicho kilizinduliwa siku ya Nyerere day Oktoba 14, 3023 na kitabu hicho kilipangwa kuandikwa na aliyekuwa katibu muhtasi wake kutokana na kumbukumbu mbalimbali za hayati Julius Kambarage Nyerere lakini alisita na kusema kiandikwe baada ya miaka 30 alisubili watu wengi waliomfahamu baba wa Taifa watoweke" amesema askofu Bagonza
Bagonza amesisitiza upendo na amani miongoni mwa wanajamii na kuwataka kuacha chuki, kwani kufanya hivyo wataongeza miaka ya kuishi kama mzee Nsherenguzi
Aidha mzee Clement Nsherenguzi (87) ametaja lengo la kuzindua kitabu hicho chenye sura 19 na kurasa 163 kuwa ni kuweka kumbukumbu za maisha yake na vitu alivyofanya kwa faida ya jamii na kizazi chake na kimechapishwa 2023 na Tanzania Educational Publishers Ltd (TEP).
Kwa upande wake rafiki wa mzee Nsherenguzi ambaye pia ni mkurugenI wa kampuni iliyochapisha kitabu hicho Pius Ngeze amesema kuwa, wazo la kuandika kitambu lilitolewa na Hope binti yake mzee Nsherenguzi na kukubaliwa kisha mzee huyo alianza kuandika na hatimaye kitabu hicho kikazinduliwa jana.



























































